Saturday, May 23, 2015

TAFAKURI YANGU YA UONGOZI NA MCHAKATO WA NDANI WA CCM KUPATA WAGOMBEA: TUJIREKEBISHE



Mungu ametupa akili, busara na hekima, kisha akatupa ufahamu, fikra na uwezo wa kuunda taasisi ili zitusaidie kuturatibu, kutuwezesha na kutusaidia. Kwa ufahamu aliotupa Mungu, akatuwezesha kuchagua na kuteua kutoka miongoni mwetu watu wa tofauti, watu wasiojipenda wenyewe, watu wenye uwezo mkubwa na maono, watu wapole, wenye uhalali katika jamii wa kuonya na kukemea ili hawa wawe viongozi wetu.

Uongozi ni dhamana, ni jukumu zito, mtu uongozi hupewa na watu, hubarikiwa na hata kulazimishwa, uongozi huwa hautafutwi kwa udi na uvumba. Katika dini zote na jamii za watu katika historia viongozi walitengenezwa, hata wale waliozaliwa katika mnyonyororo wa uongozi iliwapasa kulelewa kiuongozi. Ilimpasa mtu awaye kiongozi, kuhakikisha kwamba anawaleta watu wake pamoja, masikini na matajiri, wakulima na wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

Kiongozi anapaswa kuwa msingi imara wa umoja wa kitaasisi, jamii na Taifa kwa ujumla. Kiongozi anayeanza na mpasuko na si umoja, kiongozi anayeanza na chuki na si upendo, viongozi wanaoanza na makundi na si taasisi kwanza, tafsiri yake si njema, si afya na ni muendelezo wa nyufa katika taasisi yoyote ile.

Chama cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni kitatoa utaratibu na mchakato wa kumpata mgombea wa Urais kupitia CCM. Tukumbuke tena, CCM ndio chama kilichopo madarakani sasa, hivyo inapaswa kuonesha mfano, CCM inapaswa kuwa kioo, najua CCM imejikwaa wakati mwingine kwa makusudi na wakati mwingine kwa bahati mbaya. Sifa kubwa ya uongozi thabiti ni kuonesha uongozi pale ambapo watu ndani ya taasisi au kwa ujumla Taasisi inapojikwaa. Kuonesha uongozi kunaweza kuwa katika namna nyingi, mojawapo ni kwa hali yoyote kuukumbatia ukweli pasina kuathiri menejimenti ya siasa

Uongozi ni kuonesha kutokuvunjika moyo, kutokukata tamaa, kujikwaa sio kuanguka, na kama CCM imetetereka bado inaweza kuamka tena na kuthibitishia umma wa watanzania kwamba misingi ya kusimamia maadili na miiko ya viongozi bado iko imara kama ilivyo misingi ya CCM ambayo kwayo iliasisiwa.

Labda nitolee mfano wa mambo kadhaa ambayo kwa makusudi baadhi ya wana CCM wamesaidia kuteteresha CCM. Mosi, namna ambayo chama ambacho ndio kimeshika mamlaka ya nchi na serikali kimeshughulikia masuala ya ubadhirifu wa mali ya umma, kumekuwa na tuhuma kadhaa wa kadhaa katika miaka 10 iliyopita. Tumeona uwajibikaji, lakini CCM ingeweza kufanya vizuri zaidi ili kurudisha imani ambayo inaonekana dhahiri kutetereka miongoni mwa wananchi. Uongozi wa CCM unapaswa kuwa mkali zaidi kwa wale wanaokwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa CCM. Urafiki ni jambo jema, lakini misingi ya CCM inapaswa kuwa juu ya urafiki wakati wowote.

Wengi wenu, viongozi wa CCM mlikuwepo kipindi cha Mwalimu Nyerere na kwa hakika wengi wenu ni mashahidi wa namna alitenda kama Kiongozi. Hivi kuna kipindi kigumu kama miaka ya 80 mwanzoni? Kipindi kile ambacho ajira rasmi ziliporomoka kwa karibu asilimia 80, matatizo ya njaa na kutetereka kwa uchumi wa nchi. Mwalimu alikuwa mkali kweli kweli, lakini pia alikuwa kama baba, alikuwa msikivu na mpole, kama Kiongozi mkuu ndio mwenye dira, ndiye anayetupa hamasa kupiga makasia katika Bahari iliyochafuka ili tuelekee uelekeo sahihi na salama, ambaye kupitia kwake watu walipaswa kuyaona matumaini, walipaswa kuiona Tanzania njema.

Mnakumbuka vikao vya Karimjee vya kuokoa uchumi wa Taifa letu miaka ya 80 katikati, nafasi ya Mzee Kawawa ya menejimenti ya siasa au “political management” katika vikao pale hali ilipochafuka. Hali ilipokuwa tete, na hasira ziko juu, Mzee Kawawa kwa busara na hekima zake alijua namna ya kutukwamua na hali ikapoa, kisha Mwalimu akaahirisha kikao mpaka siku inayofuata, hiyo ndio ilikuwa CCM.

Leo hii nidhamu ya baadhi ya wana CCM na viongozi imeshuka, nasikia hata kuzomeana kumo katika vikao. Kuheshimia miongoni mwa viongozi ndio msingi mkubwa wa kujengeana imani na kuaminiana. Viongozi wasioaminiana, hawaheshimiani, viongozi wasioheshimiana hawapendani, na viongozi wasiopendana hawazungumzi kwa uwazi na ukweli. Tunapofika hapo, taasisi ya chama iko mashakani, uongozi wa nchi kutoka katika chama unawekwa rehani.

Zamani ilikuwa tunasema zidumu fikra za Mwenyekiti, usemi huu haukuwa wa bahati mbaya, ni kwamba Kiongozi alilitizama Taifa na akatuhamasisha kupiga juhudi kuelekea kule wananchi wetu wanapaswa kuwa, nikizungumza kwa nahau, kule kwenye nchi ya maziwa na asali. Leo hii fikra za Mwenyekiti si jambo tena, inaweza isiwe kama kipindi kile cha zamani, lakini sidhani kama Mwenyekiti anapewa heshima yake kama Kiongozi. Kuhusu ubadhirifu wa mali za umma, akaja na falsafa ya “kujivua gamba”, hii imeshindwa kabisa na kubaki kuwa mzaha, wana CCM hawakusimama bega kwa bega na Mwenyekiti wao. Kushindwa kwa falsafa hii kukapelekea pia kushindwa kutoa msukumo uliostahili wa kushughulikia ubadhirifu katika serikali na vyombo vyake.

Pili, ni Mchakato wa Katiba, huu umekuwa ni dhihaka kwa watanzania. Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ndiye Mkuu wa Nchi alianzisha mchakato wa kuandikwa Katiba mpya kwa maslahi ya Taifa la Tanzania na Wananchi wake. Nini kilitokea katika kusimamia fikra yake hii adhimu na adimu kwa Taifa letu? Mzaha kabisa. Wako waliomhoji, ninaposema kumhoji simaanishi katika namna ya heshima ya kutaka taarifa au maelezo kutoka kwa Kiongozi wako, bali katika namna ya kiburi, dharau na ujuvi usio na tija kwa CCM na kwa Taifa.

Kilichotokea ni Mwenyekiti kukosa kuungwa mkono katika CCM katika jambo ambalo lililokuwa na maslahi kwa Taifa. Naikumbuka dhamira yake, nayakumbuka maono yake, nayasoma maandiko yake, nasikiliza hotuba zake, kwa hakika kilichokuja kuwa Katiba Inayopendekezwa hakiakisi dhamira ile ya awali. Hapa CCM lazima mjirekebishe, na iwe sasa na si baadaye, na mfanye upesi maana mkichelewa chelewa mtakuta mtoto si wenu. Ile tabia ya ninyi kulalama kila kona ya nchi huku mkiwasema watendaji wa serikali muiache, ninyi hampaswi kulalama, mnapowalaumu kwanini hili na lile halijatokea na wao wanawashangaa ninyi ambao mko wengi bungeni na mmeshika madaraka ya serikali, mnapaswa kutoa uongozi.

Kitu kibaya kabisa ni pale ambapo Kituo cha Demokrasia (TCD) kilipopiga hatua ya kuwa na “Makubaliano na Rais” juu ya kuokoa mchakato wa Katiba na kutoka na mapendekezo ya kutuvusha katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na CCM ikapuuza juhudi hii kubwa. Ninyi mnajua CCM iliwakilishwa na Kiongozi wa juu kabisa, Makamu wa Mwenyekiti, Mhe. Phillip Mangula, na yeye hajawahi kukana kuwa sehemu ya mchakato wa TCD, haipendezi pale ambapo Makamu wa Mwenyekiti hajakana matokeo halafu Katibu wa Itikadi na Uenezi aje aseme chama hakiko huko. Vitendo kama hivi Wananchi na wanachama wanavitizama kwa ukaribu sana, vitendo vinavunja mioyo ya Wananchi na wanachama.

Leo ni tarehe 24 Mei, kama CCM haitachukua uamuzi wa haraka kutoa uongozi katika Mchakato wa Katiba na Uchaguzi Mkuu, hii haitakuwa ishara nzuri ya chama kuimarika na kukua kiuongozi. Hebu tufuatilia kalenda hii, Tume ya Uchaguzi imesema itamaliza kuandikisha wapiga kura Julai 16, kisha litafuata zoezi ya uhakiki wa orodha kwa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine itakuwa imemaliza au inamalizia zoezi la uhakiki. Ikumbukwe pia kwa desturi Bunge huvunjwa mwezi wa Julai, na imekuwa desturi kwamba kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani huanza kwenye tarehe 20 Agosti mpaka siku ya uchaguzi ambayo huwa wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba.

Mpaka leo, hakuna mswada wowote wa kurekebisha Katiba ya Mwaka 1977 ambao kuna fununu au ambao imejulikana kwamba utapelekwa Bungeni ili kutekeleza “Makubaliano ya Rais na TCD”. Sitaki kusema kwamba tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu bila marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kwa maana hata si kila dalili ya mawingu huleta mvua.

Iko bayana kwamba hatuwezi kufanya kura ya maoni mwaka huu, kwa kalenda niliyoieleza hapo juu, Kura ya Maoni inataka siku 30 za kampeni, kati ya leo na Oktoba hakuna siku 30 za bure ambazo hazitaingilia ratiba ya uchaguzi mkuu. Katika hili lazima CCM ioneshe uongozi, mkishindwa katika hili, mimi nitaendelea kupenda misingi ya kuanzishwa CCM ila heshima ya viongozi wetu katika chama na chama kama taasisi itakuwa inakaribia ukingoni. Tusifike huko.

Viongozi wetu, wenye dhamana katika CCM nawaombea mkaongozwe na hekima ya kiMungu. Mkawatazame viongozi wenye nia ya kushika hatamu ya Taifa letu kwa macho ya kiMungu na si vinginevyo.

Mkifanya maamuzi mabaya, mtaivuruga CCM, wanachama na watanzania watahuzunika sana, mtatuachia matatizo, leo hii sura ya CCM haijatukuka katika kiwango chake, watu wetu wana maswali zaidi kuliko majibu.

Nihitimishe kwa kusemea siasa za makundi CCM, wala tusijaribu kujitoa ufahamu, Makundi yalitetemesha CCM Mwaka 1995 bahati nzuri alikuwepo Mwalimu Nyerere akasaidia. Makundi yalitikisa chama mwaka 2005 na bahati mbaya athari zake ziko hata leo. CCM haiwezi kumudu mwendelezo wa siasa za makundi zisizo na tija, uzoefu unaonesha CCM inadhoofika kutokana na makundi haya.

Wana CCM wanapaswa kuchagua hivi leo kwamba watakitazama chama na kukiimarisha ama sivyo wana CCM waamue kufuata uelekeo wa siasa za mihemko ya makundi na wale wote watumiao mbinu mbaya za makundi ambayo mwishowe yatakivuruga Chama cha Mapinduzi.

Saturday, May 16, 2015

SERIKALI IKISEMA “NDIYO” UJUE KUNA SABABU YA KUSEMA HAPANA


Pale tunapokuwa na maswali mengi zaidi kuliko majibu na hekaya za mbio za sakafuni

Ni dhahiri sasa kwamba serikali imejipambanua moja kwa moja kwamba inaunga mkono Katiba Inayopendekezwa. Serikali imekwenda mbali zaidi na kutoa maelekezo kwa wananchi kwamba wakati ukifika waipigie kura ya “Ndiyo” Katiba Inayopendekezwa. Huenda mnashtuka, ndiyo, kwani hamkufuatilia Sherehe za Miaka 51 ya Muungano wetu mwezi uliopita. Shamra shamra na jumbe za maadhimisho zilijinasibu na hamasa ya kuipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa. Ilikuwa bayana kwamba haikuwa bahati mbaya, maadhimisho ya Muungano ni sherehe za kitaifa na zinaandaliwa, kuratibiwa na kuendeshwa na serikali, kwa mwenzangu na mimi ujumbe ulifika bayana kabisa.
Labda nirejee msingi wa utawala wa nchi yetu Tanzania, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 na ndio Katiba inayotumika sasa inasema katika Ibara yake ya 8 inasema “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo - (a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii; (b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; (c) Serikali itawajibika kwa wananchi; (d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii”.
Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, maneno haya ni maneno mazito kabisa, na kwa lugha nyingine, cheo kikubwa kabisa cha msingi katika Taifa letu ni raia (citizen), huyu ndio mwananchi mtanzania. Imesemwa pia, kwamba “Serikali ni watu” na kwa hakika watu wenyewe ndio kwa ujumla wao huitwa raia wa Jamhuri ya Muungano, na wananchi wa Taifa letu.
Serikali hupaswa kutenda sawasawa na matakwa ya watu yanayozingatia maslahi mapana ya Taifa letu. Sifa kubwa ya serikali bora tangu kuasisiwa kwa Taifa letu imekuwa ni ile ambayo ni sikivu kwa wananchi. Usikivu huu wa serikali sio ni matokeo ya utashi pekee, la hasha, bali ni msingi ambao sisi kama Taifa tumekubaliana kuujenga na kuuweka katika Katiba kwamba “Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii pamoja na Serikali itawajibika kwa wananchi”
Unapoanza kuona serikali inatenda lwake, mbali na wananchi wanataka nini, tunapaswa kujihoji tunakotoka, tuliko na tunakokwenda kwa maana ya namna tunaishi na kusimamia misingi muhimu ya Taifa letu.
Sisi kama Taifa tumekubaliana kwa pamoja kwamba tutaandika Katiba Mpya na ili kuhitimisha mchakato wa huu, sisi raia tutaamua kama ipite ama isipite kwa kuifanyia uamuzi wa Kura ya Ndio au Hapana. Kifungu cha 35 cha sheria ya Kura ya Maoni kimeliweka sharti hili bayana kabisa. Kila raia ana haki ya kuamua ama apige kura ya NDIO au kura ya HAPANA, sisi raia na taasisi zetu za kiraia vikiwemo na vyama vya siasa na taasisi za kidini tunashiriki kujadiliana kwa hoja na sababu. Kuna maeneo tunakubaliana na kuna maeneo tunahitaji mjadala zaidi, na tunaendelea kufanya hivyo.
Wajibu wa serikali katika mchakato huu ni uwezeshwaji, uraghibishi au “facilitation”, na ndio maana kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni serikali kwanza ilituundia Tume ya Katiba, kisha serikali ikatuundia Bunge Maalum na hatimaye serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatuendeshea kura ya maoni. Hakuna wajibu mwingine kisheria ambao serikali imepewa juu ya mchakato huu isipokuwa kuuwezesha kifedha, kwa kutoa rasilimali watu na vitendea kazi kila inapobidi.
Wakati wa Bunge Maalum, kidogo serikali ilijisahau, ikajikuta inapanga na kupangua hoja na kidogo kidogo tukaanza kuona kumbe viongozi wetu katika serikali wana msimamo katika mchakato huu. Mimi sina tatizo la kimsingi kama viongozi wetu wa kuchaguliwa wakiwa na msimamo na hii ni kuanzia kwa Mhe. Rais, Mawaziri, Wabunge, Madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji. Hawa najua tunaweza kuhojiana nao kwa hoja, sababu na ushahidi na nina uhakika inapokuja kwenye suala la maoni ya Katiba Mpya, wananchi nao wanajua walisema nini, kwahiyo sina shaka.
Tatizo langu ni kuingiza Serikali jumla jumla, hilo ni kosa, ni kosa kubwa sana, na ndio maana nahoji, Kama serikali ikisema NDIO nani wa kupinga? Ninapata moyo mkuu wakati huu kwasababu najua viongozi wetu wa kisiasa wengi wao wana lao jambo na wanatumia kila mbinu kupitisha masuala ambayo yatalinda maslahi yao. Mbinu hizi wanazotumia viongozi wetu wa kisiasa zinajumuisha kuitumia “machinery” au taasisi ya serikali kwenye kupenyeza ushawishi wao wa kutafuta kura za NDIO, hilo ni kosa.
Mimi kama raia, nasema HAPANA kwa tabia hii isiyofaa, serikali inapaswa kutokuwa na upande au “neutral” na nitoe rai kwa wanasiasa kuacha kutumia “machinery” ya serikali kwa manufaa binafsi, ni makosa makubwa. Na kama tabia hii itaendelea mimi, hata kama nitabaki peke yangu, nitaendelea kuikemea kuwa ni mbaya na isiyofaa na nitaongeza jitihada za kuwaeleza watanzania kwamba Katiba Inayopendekezwa imelinda viongozi na imepora haki za wananchi.
Leo niendelee na uthibitisho wa namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa inawalinda viongozi na ndio maana wanaipigia chapuo. Usikubali ee mwananchi, Katiba Mpya Bora itatusaidia kudhibiti matumizi mabaya ya baadhi ya viongozi wetu.
Utolewa, usimamizi, uhifadhi na udumishwaji wa haki za binadamu ni jukumu la serikali pamoja na umma wa watanzania. Haki za binadamu zikichezewa, watu wetu wataendelea kunyanyaswa pasina heshima ya utu wao, kuwa mafukara katika nchi yao wenyewe yenye utajiri wa kila namna. Ili kuhahakisha haki za binadamu zinatunzwa, zinatolewa, zinahifadhiwa, zinalindwa na kuheshimiwa na watu na kwa watu wote, Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili ijulikanayo kama Rasimu ya Warioba iliweka masharti yafuatayo;-
Ibara ya 210(1) inahusu Kazi na Majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu, “(i) kutembelea magereza, vituo vya polisi au mahali penginepopote ambapo mtu au watu wanazuiliwa kwa madhumuniya kutathmini na kukagua hali za watu anaozuiliwa katikasehemu hizo na kutoa mapendekezo yatakayowezeshakurekebisha kasoro zilizopo;
(j) kutoamapendekezoyanayohusiananasheriailiyokwi shatungwa au inayokusudiwa kutungwa, kanuni, aumambo ya kiutawala ili kuhakikisha zinakidhi
viwango vyakimataifa na kikanda vya haki za binadamu;
(k) kuwasilisha taarifa na maoni huru kwenye vyombo na taasisiza kimataifa na za kikanda kuhusu hali ya haki za binadamunchini pale inapobidi;
(l) kuihamasisha Serikali kutia saini na kuridhia mikataba aumakubaliano ya kimataifa yanayohusu haki za binadamu,kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa haki za binadamu zilizomo kwa mujibu wa Katiba hii, Katiba za NchiWashirika, sheria za nchi na mikataba au makubaliano yakimataifa ambayo Jamhuri ya Muungano inawajibika nayo; na
(m) kwa kupitia Serikalini, kushirikiana na wawakilishi waUmoja wa Mataifa, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Umojawa Nchi za Afrika, Jumuiya ya Madola na taasisi nyinginezenye mahusiano baina yao, miongoni mwao au ya kikanda na taasisi za nchi nyingine katika maeneo ya hifadhi naukuzaji wa haki za binadamu”.
Ibara ya 210(2) ikaweka Masharti yafuatayo;- “Tume ya Haki za Binadamu itakuwa na mamlaka maalum kama ifuatavyo: (a) kumuita mtu yeyote mbele ya Tume na kumtaka awasilishembele yake nyaraka zozote, kumbukumbu au kitu chochotekilicho katika mamlaka yake kinachohusiana na jambolinalochunguzwa na Tume; (b) kumtaka mtu yeyote kutoa taarifa anayoifahamu kwa Tumejuu ya jambo linalochunguzwa na Tume; (c) kusababisha mtu yeyote anayekiuka maagizo au taratibu zaTume kufunguliwa mashtaka ya jinai mahakamani”.
Masharti haya yote yaliyokuwamo kwenye Rasimu ya Warioba yamefutwa na hayamo katika Katiba Inayopendekezwa. Najiuliza dhamira ya waandishi wa Katiba Inayopendekezwa ilikuwa ni ipi? Na Najiuliza dhamira ya Serikali kutulazimisha kupigia Kura ya NDIO kwa Katiba Inayopendekezwa ilhali ikijua kuna mapungufu yote hayo ni ipi.
Mwisho kabisa nitoe RAI kwa Tume ya Uchaguzi, kwamba tarehe ya Kura ya Maoni ni jambo linalopaswa kuwa bayana, tusigeuze tarehe ya Kura ya Maoni kama siku ya kurudi Masiha, kwa maana haijulikani siku wala saa. Sifa moja kubwa ya utawala bora na wenye ufanisi ni “predictability” hali ya kuwa bayana na mambo ya baadaye.
Leo ni tarehe 17 Mei 2015, bado tunaandikisha wapiga kura mpaka mwezi wa saba. Bunge huenda litavunjwa mwezi wa saba na baraza la wawakilishi mwezi wa nane. Kampeni za Uchaguzi Mkuu ni zaidi ya siku 60, kwa maana kwamba kampeni zitaanza mwishoni mwa mwezi wa Agosti na kumalizika wiki ya mwisho ya Mwezi Oktoba. Sasa kweli kabla ya Uchaguzi Mkuu unaona hapo Kura ya Maoni ikifanyika? Haiwezekani! Haya tuangalie marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 ili tuvuke Uchaguzi Mkuu bila tashwishwi, mpaka leo hakuna mswada wa sheria wa marekebisho ya Katiba na Bunge la bajeti litaendelea hadi karibu na mwisho wa mwezi wa Juni.
Je ukitizama unaona nini mbele? Ninaona muda hautoshi, ninaona busara inahitajika zaidi hasa kuhusu Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu ni lazima. Tafakari na tujadiliane.
WASAMBAZIE NA WENGINE na USISAHAU ku-LIKE Humphrey Polepole

Sunday, May 10, 2015

TUJIKUMBUSHE HOJA YA SHIRIKISHO LENYE SERIKALI TATU


Kumekuwa na kuchanganya mambo katika majadiliano yetu katika kila kona juu ya suala la shirikisho ambalo limetajwa katika ibara ya kwanza ya Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Warioba na suala la muundo wa serikali tatu katika Jamhuri ya Muungano lililomo katika Sura ya Sita ya Rasimu ya Warioba. Imefikia hatua sasa wapo wanaodhani ukizungumzia shirikisho maana yake ni serikali tatu na ukizungumzia serikali mbili umekataa shirikisho. Mtizamo huo sio sahihi kama nitakavyoeleza baadaye.

Pili inaelekea kuwa wapo watu ambao wana mzio (allergy) na neno “Shirikisho” na hivyo kulichukia na kulipa maana hasi ambayo siyo sahihi. Kwa watu hao kwao neno shirikisho wamelipa maana ya kubuni ya kifo cha Muungano. Mtizamo huo  sio sahihi na ni mtizamo potofu kabisa. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa kufa kwa Miungano duniani na dhana ya shirikisho. Kwani ipo Miungano ya Serikali moja ambayo ilikufa katika kipindi kifupi sana kama ule wa Misri na Syria na ipo Miungano ya shirikisho ambayo inadumu mpaka leo kama vile Ethiopia, Nigeria, Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Marekani na India.

Tatu kuna dhana potofu kuwa shirikisho na muungano wa serikali tatu unaopendekezwa katika Rasimu ya Warioba utahamasisha utaifa wa Tanganyika. Dhana hiyo pia ni potofu kwani zipo nchi zenye muungano wa serikali moja kwa sababu ya kulazimisha kufuta utambulisho wa upande mmoja wa Muungano huo leo baada ya zaidi ya miaka hamsini ya Muungano wao upande ule ambao ulizikwa utambulisho wake unadai sasa utaifa wake. Nchi hiyo ni Jamhuri ya Cameroon ambayo ni muungano wa serikali moja  wa iliyokuwa “French Cameroon” na “British Cameroon” zilizoungana mwaka 1961. Hali hiyo imechambuliwa vizuri sana na  Verkijika G. Fanso katika makala yake “Anglophone and Francophone Nationalism in Cameroon” [The Round Table (1991) 350, 281 – 296] na pia katika makala ya Piet Konings na Francis G. Nyamnjoh  “The Anglophone Problem in Cameroon” [The Journal of Modern African Studies, 35, (1997), 207 – 229]

Nilianza kwa kusema kuwa suala la shirikisho na suala serikali tatu hayahusiani ingawa yanaingiliana. Mjadala wa aina ya Muungano wa Tanzania umekuwa na ubishani mkubwa kwa miaka mingi. Je Muungano huu ni serikali moja yaani “Unitary State” au ni wa shirikisho yaani “Federation”?.Wapo wanazuoni maarufu wa sheria hapa Tanzania na wanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao wamechambua Muungano huu wa sasa wa serikali mbili na kuhitimisha kuwa ni wa mfumo wa Shirikisho. Hii ina maana hata sasa tuna shirikisho la serikali mbili. Kwa hali hiyo basi Rasimu ya Warioba ilipendekeza tutoke kwenye shirikisho la serikali mbili la sasa na kwenda katika shirikisho la serikali tatu.

Miongoni wa wanazuoni hao ni Profesa P.B. Srivastava ambaye alifundisha sheria za Katiba (Constitutions and Legal Systems of East Africa) na Sheria za Utawala (Administrative Law) katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika miaka ya 1980 ndiye aliyechambua kwa kina muungano wa Tanzania na kuhitimisha kuwa ni wa aina ya shirikisho katika Mhadhara wake wa Kiprofesa (Professorial Inaugral Lecture) wake alioutoa Machi 1982 iitwayo “The Constitution of the United Republic of Tanzania 1977:Some Salient Features – Some Riddles”.

Miaka minane baadaye, yaani mwaka 1990,  msomi mwingine Profesa Issa Gulamhussein Shivji, ambaye kwa miaka yote kabla ya hapo alikuwa akijihusisha na Sheria za Kazi (Labour Law) alitoa Mhadhara wa Kiprofesa (Professorial Lecture)  wake uitwao “The Legal Foundation  of the Union in Tanzania’s Union and Zanzibar Constitutions” naye alihitimisha kuwa Muungano wa sasa wa Tanzania ni wa mfumo wa shirikisho kama nitavyofafanua baadaye.

Wanasiasa wa CCM ambao walisema kuwa Muungano wa sasa ni shirikisho ni Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Msimamo huo uliungwa mkono na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika hotuba iliyotolewa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Brigedia – Jenerali Ramadhan Haji Faki mwaka 1983 alipojibu hoja ya ushauri kuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Moringe Sokoine aliposhauri Chama cha Mapinduzi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina mamlaka juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. [Zanzibar Government: A Reaction to Prime Minister Ndugu Sokoine’s Advice to the Party to Restructure the Government given to the Party and Government Leaders Tabled by the Chief Minister to the House of Representatives, Zanzibar Printing Press, 1983, p. 5). Msimamo huo pia uliungwa mkono na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Wolfgang Dourado.

Msimamo huo wa Mzee Jumbe kuwa muundo wa Muungano ni shirikisho ulileta kuchafuka kwa hali ya hewa wakati wa mjadala wa Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Pamoja na Mwasisi wa Muungano na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutofautiana na Mzee Jumbe, kama ilivyoelezwa katika Randama ya Rasimu ya Warioba katika ukurasa wa tatu, nanukuu:

“Kwa mujibu wa kumbukumbu za kikao cha halmashauri ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi katika mkutano wa tano ambao ulikuwa maalumu uliofanyika Dodoma Januari 24-30, 1984, Mwalimu Nyerere alitamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa Shirikisho lakini ukiangalia kutoka Tanzania Bara ni serikali moja. Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi aliyesema kuwa Muungano wa Tanzania umeunda shirikisho (Federation) na sio serikali moja (Unitary State).

Mfumo wa Shirikisho unaopendekezwa katika Rasimu ya Warioba unaendeleza hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Nchi na ni Dola moja lenye mamlaka kamili yenye serikali tatu, shirikisho hili linatokana na muungano wa hiari wa Tanganyika na Zanzibar ambazo zilikuwa Jamhuri zenye mamlaka kamili kabla ya kuungana tarehe 27 Aprili 1964”

Msimamo huo wa Mwalimu Nyerere kuwa kwa upande wa Zanzibar Jamhuri ya Muungano ya Muungano ina sura ya shirikisho inafanana kwa kiasi fulani na uchambuzi wa mtaalam nguli Mwingereza wa masuala ya katiba Professor S.A. de Smith ambaye katika kitabu chake kiitwacho Constitutional and Administrative Law, 2nd Edition, 1973, p.33 anasema kwamba:

“Tanzania is part federation, since Zanzibar has exclusive fields of competence both in theory and in practice, but for political reasons the term ‘federal’ does not appear in the constitution and in as much as it implies a degree of disunity as well as diversity.”

Kwa kiswahili akimaanisha “Tanzania kwa sehemu ni shirikisho kwa sababu Zanzibar ina mamlaka yake kamili ya ndani kinadharia na kivitendo lakini kwa sababu za kisiasa neno shirikisho halionekani katika Katiba huku hali hii ikionesha kiwango cha utengano pamoja na utofauti” (Tafsiri ni yangu).

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” katika ukurasa wa 15, alipata kusema “Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi Moja mifumo ya kawaida mifumo ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na Nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja.

Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana basi nchi hizo huwa huru. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, Serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”

Muundo wa Shirikisho, ambao ni tofauti na muundo wa serikali moja. Katika muundo huu, nchi zinapoungana kunakuwa na ngazi mbili za serikali, yaani serikali ya muungano au shirikisho na serikali za washirika. Serikali ya Muungano inakuwa na mamlaka kwa masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya muungano, wakati serikali za washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba kushughulikia mambo yote yasiyo ya muungano.

Sababu nyingine ya kuendelea kupendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu ni uhalisia kwamba Muundo wa Shirikisho utaendelea kuhifadhi asili, taswira na hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa kwa mujibu wa Kifungu cha 2 cha Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933 unaohusu Haki na Majukumu ya Nchi (the Montevideo Convention on Rights and Duties of States) unaosema na ninanukuu “the federal state shall constitute a sole person in the eyes of international law” inayomaanisha nchi yenye muundo wa shirikisho katika sheria za kimataifa ni nchi na dola moja.

Katika mfumo huu, kwa kawaida mamlaka ya mwisho au mamlaka kamili (sovereignty) yanabaki katika serikali ya shirikisho. Kama nilivyosema, utambulisho wa nchi katika mahusiano ya kimataifa na vyombo vya ulinzi na usalama hubaki katika serikali ya shirikisho. Sifa nyingine ya shirikisho ni kuwa mwananchi anatawaliwa na serikali mbili ilihali katika muundo wa muungano wa serikali moja mwananchi anatawaliwa na serikali moja pekee. Muungano wa Tangannyika na Zanzibar siku zote umekuwa na sura mbili. Kwa wananchi wa Zanzibar wamekuwa katika shirikisho tangu mwaka 1964 kwa sababu wanatawaliwa na serikali mbili (serikali ya muungano na serikali ya Zanzibar). Kwa upande wa Tanzania Bara kuna sura ya muungano zaidi kwa sababu kuna serikali moja kwa maana serikali ya Tanzania Bara au Tanganyika haipo.

Sababu nyingine ya kupendekeza muundo wa shirikisho ni kukuza demokrasia kwa maana ya kutoa mamlaka zaidi kwa nchi washirika kujiamulia mambo yao wenyewe. Hii inatekeleza madai ya miaka mingi ya Zanzibar kuwa na Shirikisho la Serikali Tatu tangu wakati wa Mzee Aboud Jumbe Mwinyi na baada ya hapo ambalo liliungwa mkono na watu wengi akiwemo Profesa Issa Gulamhussein Shivji. Hoja hiyo ya Prof. Issa Shivji kuunga mkono madai ya Zanzibar ya kuanzishwa kwa mfumo wa shirikisho lenye serikali tatu limo katika kitabu chake kiitwacho “Pan-Africanism or Pragmatism?: Lessons of the Tanganyika – Zanzibar Union (2008 ukurasa 250 anaposisitiza kuwa;

“A demand for a three government federation, greater autonomy for Zanzibar, reduction in union matters, from Zanzibar was a demand for the right to self-determination, a democratic demand” [ yaani, madai ya shirkisho la serikali tatu na kupunguzwa kwa mambo ya muungano yanayotolewa na Zanzibar ni madai ya haki ya kujiamulia mambo yao na ni haki ya kidemokrasia Uk. I.G. Shivji, Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika- Zanzibar Union,2008, P. 250]
 
Pia, Chini ya mfumo wa Muungano wa Shirikisho, ugawaji wa madaraka huwekwa kwenye Katiba kiasi kwamba katika hali ya kawaida serikali ya muungano haiwezi kuingilia na kunyang’anya madaraka ya serikali za washirika bila ya kufuata utaratibu uliyowekwa kwenye Katiba. Nchi ambazo zimeimarika katika mfumo huo ni pamoja na Marekani, Kanada, India, Brazil, Ujerumani, Uswisi, Australia, Nigeria na Ethiopia. Mfumo wa Shirikisho unawezesha nchi washiriki kuwa na nguvu kubwa ya kushughulikia maslahi ya pamoja huku kila moja ikiwa na mamlaka ya kushughulika masuala yasiyo ya pamoja. Mfumo huu unawapa washirika wa Muungano fursa ya kuhifadhi utambulisho wao wa kihistoria.

Sababu nyingine muhimu ya kupendekeza muungano wa shirikisho la serikali tatu ni kuweka bayana mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano zilizobainishwa na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano  ya Mwaka 1977 katika Ibara ya 4, 34, 64 na 102. Mamlaka hizo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara.  Hoja hii inatiliwa nguvu na Msomi Maarufu wa Masuala ya Katiba Professor Srivastava, kwamba:

 “The United Republic envisages a triangular system with Tanzania Mainland and Zanzibar forming two corners of the base and the United Republic constituting the vortex. Accordingly, there are three jurisdictional areas territory-wise and subject-wise for the operation of governmental powers, both legislative and executive, which necessitate existence of three governments, namely, Government of United Republic, Government of Tanzania Mainland and Government of Zanzibar corresponding to three jurisdictions.


[Tafsiri yangu: Jamhuri ya Muungano ni mfumo wa serikali tatu, Tanzania Bara na Zanzibar zikiwa ni nguzo za pembeni na Jamhuri ya Muungano ikiwa ni kilele chake: Hivyo, kuna mamlaka tatu kieneo na kimatumizi ya madaraka ya kiserikali, kibunge ambayo yanalazimu kuwe na serikali tatu: yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar] { B. P. Srivastava, 'The Constitution of the United Republic of Tanzania 1977 - Some Salient Features, Some Riddles' Eastern Africa Law Review 11-14 (1978-81}, 73-127, at pp.79-80.}

Saturday, April 25, 2015

MIAKA 51 YA MUUNGANO: HUU NI WAKATI MUAFAKA WA KUWEPO HAKI ZA WANAWAKE KIKATIBA

Katiba Inayopendekezwa imefuta misingi ya usawa kati ya wanawake na wanaume

Hivi karibuni nilipata wasaa wa kuonana na watetezi wa haki za binadamu, watetezi hawa wanawake na wanaume kutoka asasi za kiraia walinialika kujadiliana nao juu ya mchakato wa Katiba. Katika vikao viwili tulikaa pamoja, sote tulikubaliana kila mwenye uelewa au msimamo kuhusu Katiba Inayopendekezwa apewe fursa kuusema na asizongwe. Wote tulikubaliana kwamba utofauti wa mawazo ni afya kwa hakika na hasa pale wote wenye misimamo wanapojenga hoja zao kwa sababu za msingi na zenye mashiko.

Nilijielekeza kuelewa hoja zao, hasa za wale ambao wanasema Katiba Inayopendekezwa imelinda haki za wanawake, nilisikiliza kwa dhamira ya kuelewa na kujifunza kutoka kwao. Baada ya mjadala niligundua kwamba wanawake walikuwa na hoja kadhaa ambazo kwa maelezo yao zilifanikiwa kuingia katika Katiba Inayopendekezwa, na kwa mantiki hiyo wanawajibika kuipigia chapuo Katiba Inayopendekezwa.

Kabla ya kufafanua namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imelitizama suala la haki za wanawake ni vema nikagusia kwa sehemu dhana ya Mahitaji ya Kimkakati ya jinsia au kwa kiingereza “Strategic Gender Needs”.

Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia na Katiba

Mahitaji ya kimkakati ya jinsia au “Strategic Gender Needs” ni yale ambayo wanawake na wanaume huyahitaji ili kubadilisha nafasi zao katika jamii, mahitaji haya yanajumuisha mgawanyo wa madaraka kijinsia, mamlaka na udhibiti wa rasilimali, fursa sawa kwa wanawake na wanaume, haki za kipato sawa kwa kazi sawa kati ya wanawake na wanaume, Mageuzi ya kikatiba, kisheria na kimfumo ambayo yanatambua nafasi muhimu ya wanawake pamoja na wanaume kwa usawa katika kuleta maendeleo ya jamii. Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ndio humlinda mwanamke dhidi ya utegemezi, umasikini, kunyanyaswa, unyonyaji au “exploitation” na kuwekwa nje ya mfumo wa kufanya maamuzi.

Mara zote Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia kwa maana ya “Strategic Gender Needs” ndio huwa ufunguo kwa Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au kwa kiingereza “Practical Gender Needs”. Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au “Practical Gender Needs” hujumuisha yale mambo ya kawaida na yanayoshikika ambayo mtu wa kawaida huyahitaji wakiwemo wanawake. Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia yanajumuisha mahitaji ya msingi katika maisha ya siku hadi siku kama vile upatikanaji wa maji, huduma za afya na ajira. Kupatikana kwa mahitaji ya kawaida ya jinsia kwa mwanamke huwa hayamwondoi mwanamke katika nafasi yake ya utegemezi, unyonyaji na kutokuwa maamuzi juu ya rasilimali zake mwenyewe.

Swali langu muhimu kwa wanawake wote, dada zangu, shangazi zangu na mama zangu wote wenye mapenzi mema na kuona utu wa mwanamke unaheshimiwa, haki za wanawake zinatolewa, zinatunzwa, zinahifadhiwa na kuheshimiwa, Je Katiba Inayopendekezwa na bila kuweka misimamo ya kisiasa imezingatia Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia au “Strategic Gender Needs”?

Katiba Inayopendekezwa inapaswa kupimwa ni kwa kiwango gani imetizama na kujumuisha Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo kwayo mahitaji ya kawaida ya jinsia hupatikana. Tunapoweza kuhakikisha uwepo wa mahitaji ya kimkakati katika Katiba, huu huwa msingi wa kuona utolewaji haki za wanawake.

Kama Katiba Inayopendekezwa imejaribu kuweka Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia pasina kuweka misingi kwa mahitaji ya kimkakati ni kazi bure kwasababu haki za wanawake zitabakia kuwa kiini macho. Kama haki za wanawake hazikubainishwa ipasavyo katika Katiba Inayopendekezwa bado mwanamke wa Tanzania ataendelea kuwa tegemezi, fukara na ushiriki wake kwenye nyanja za utoaji maamuzi zitabakia kutegemea utashi na fadhila kutoka kwa viongozi wa juu.

Tuitazame Katiba Inayopendekezwa kwa jicho la Rasimu ya Warioba

Rasimu ya Warioba Katiba Ibara ya 47(1)(b) ilisema “Kila mwanamke ana haki ya kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili”. Rasimu ililenga kujenga msingi wa kumpa mwanamke udhibiti wa rasilimali zake na kumlinda na ukatili ambao huja kama sehemu ya kumpora rasilimali alizo nazo. Mfano mzuri ni mwanamke wa kijijini na mkulima, anayelima kwa jembe la mkono na kupata mazao yake, je ni mara ngapi mwanamke huyu huwa na mamlaka juu ya wakati gani mazao yatauzwa, na yatauzwa kwa bei gani na pesa ikipatikana je mwanamke huyu huipangia matumizi yake mwenyewe?

Ukienda kwenye Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 masharti ya 47(1)(b) kutoka katika Rasimu yamefutwa, huwa najiuliza msingi wa kufuta masharti yale ya Rasimu ni upi?.

Ukiendelea kusoma Ibara ya 47(2) ya Rasimu ya Warioba inasema “Mamlaka za nchi zitaweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara hiiikiwa ni pamoja na kukuza utu, heshima, usalama na fursa za wanawakewakiwemo wajane”. Ibara hii ilikuwa ina lengo la kutoa maelekezo kwa mamlaka za nchi kutekeleza masharti yaliyoainishwa katika Ibara hii. Ieleweke pia masuala ya maendeleo ikiwemo suala la jinsia kwa asili ya Nchi yetu sio jambo la Muungano.

Kwa uelewa huu ndio maana Rasimu ya Warioba iliona Katiba itoe maelekezo kwa Mamlaka za Nchi ambazo ziko tatu ambazo ni (i) Mamlaka ya Mambo ya Muungano ambayo chombo cha utendaji ni Serikali ya Muungano, (ii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na (iii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara au Tanganyika. Warioba alijua kwamba kuna masuala ya Haki za Wanawake ambayo kila Mamlaka ingeweza kuyashughulikia kwa sehemu, nafasi na mamlaka yake. Huu ulikuwa msingi mkubwa wa kuhakikisha tunalinda Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo yangepelekea kutolewa kwa haki za wanawake raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanapatikana Tanzania Bara na Zanzibar.

Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 imeyafuta na hivyo haina masharti ya Rasimu yaliyomo katika Ibara ya 47(2) ambayo ukiacha kutoa maelekezo ya utendaji lakini pia kitaalamu ni masharti wezeshi au kwa kiingereza huitwa “enabling provision”. Najiuliza dhambi ya masharti yale ambayo baada ya kuwasikiliza Wananchi na hasa wanawake na zaidi wanawake wajane walio ona ingefaa yawepo kikatiba.

Ili ujue Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanawake wanakubwa sehemu ya wanufaikaji wa Katiba Mpya na Bora na inayotokana na maoni ya Wananchi. Ukisoma Ibara ya 54 inaeleza kuhusu usimamizi wa haki za binadamu na ukiendelea na kusoma Ibara ya 54(1)(a) inaeleza “Katika kutafsiri masharti ya Sura hii ya Haki za Binadamu, Mahakama au chombo kingine chochote cha kufanyauamuzi kitazingatia mambo yafuatayo:- haki ya usawa, utu na uhuru wa mtu binafsi”. Kwa kiingereza haki ya usawa ndio huitwa “equality principle”, kwamba tunapozitoa haki, lazima tuangalie je wanawake wapo? Je wanaume wapo?

Na neno “Utu” ni kuhusu masikini na matajiri wa Taifa letu, tunapogawana keki ya Taifa je nani waanze kula, matajiri au masikini? Rasimu ya Warioba ilipendekeza katika Katiba misingi hii ya kuzingatiwa, Katiba Inayopendekezwa imeifuta yote katika Ibara ya 65, na ukiisoma Ibara hii utagundua haina masharti ya 54(1)(a). Najiuliza dhambi ya masharti haya ilikuwa nini? Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia hayawezi kuwapo kama msingi huu umefutwa.

Rasimu ya Warioba katika Ibara yake ya 113 ilieleza bayana kwamba uwakilishi katika chombo cha kutunga sheria kwa maana ya Bunge uwe nusu wanawake na nusu wanaume. Warioba alitizama mbali kwamba kwa namna ambavyo jamii yetu imejengwa katika mfumo dume ufike wakati wa kubadili fikra na kuwa na chombo cha kutunga sheria ambacho kinazingatia uwakilishi unaojengwa katika kuheshimu misingi ya usawa wa kijinsia.

Warioba alijua kwamba wakulima wengi nchini ni wanawake, alijua pia kwamba wahanga na wanufaikaji wa mfumo wa afya nchini ni wanawake na kwa mantiki hiyo watu ambao wako kwenye sehemu na nafasi nzuri ya kuwasilisha mawazo ya watanzania ni wanawake sambamba na wanaume. Na sisi kama watu ambao Rais alitupa dhamana ya kufanya kazi na Mzee Warioba tulijiridhisha kwamba hata katika Bunge wanaolala wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea ni wanaume na sio wanawake.

Warioba ni kama alibashiri kwamba iwapo tungekuwa na Bunge ambalo lingekuwa na uwakilishi uliosawa kati ya wanawake na wanaume ndani ya muda mfupi watanzania wangetambua wanawake wana uwezo tena hata zaidi ya wanaume na ingewajengea imani kwamba hata uongozi wa nchi ungeweza kuaminiwa kwa mwanamke.

Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 129 imefuta masharti yaliyokuwemo katika Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 113(3) yaliyosema “Katika kila Jimbo la Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamme”. Huu ulikuwa msingi wa kuhakikisha kuna usawa wa jinsi na jinsia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Sijaelewa msingi wa kufutwa kwa msingi huu ambao ungepelekea kuzingatiwa kwa asilimia 100 kwa Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo yangewakomboa mamilioni ya wanawake ambao wanakumbana na unyanyasaji uliojengwa fikra za wengi katika Taifa letu.

Ukisoma Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 193(3)(b) ilizungumzia majukumu ya Tume Huru ya Uchaguzi kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuna uwakilishi unaozingatia jinsi. Tafsiri ya Ibara hii ni kwamba kama Tume Huru ya Uchaguzi ikija katika Jimbo na hakuna mgombea mwanamke basi ujue uchaguzi hakuna na vivyo hivyo kinyume chake. Ukiisoma Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 220(3) utagundua ni kipengele cha “uwakilishi unaozingatia jinsi” ndicho pekee kilichofutwa. Nawauliza nyote dhambi ilikuwa nini hata kufuta jukumu hili la Tume Huru ya Uchaguzi?


Ni miaka 51 ya Muungano, unadhani bado wanawake wanatakiwa kupewa nafasi za uongozi kwa mbinu za miaka ya 70, kwa maana ya viti maalum na kwa kusubiri utashi na fadhila za viongozi wakubwa? Je wanawake hawastahili haki sawa na wanaume? Nimeandika nikiwa kama mwanaume anayethamini nafasi muhimu ya wanawake katika ujenzi wa Taifa letu na anaye amini kwamba Taifa hili haliwezi kupiga hatua kama tutaendelea kuwahadaa wanawake, wapenzi wetu, dada zetu, shangazi zetu, mama zetu na bibi zetu. Niwatakie Miaka 51 ya kusherehekea Muungano wetu. Muungano wa Haki na Heshima Udumu Milele.!

Saturday, April 18, 2015

KUHUSU MAADILI YA VIONGOZI, KATIBA INAYOPENDEKEZWA IMEPUUZA KILIO CHA WENGI JUU YA UADILIFU WA VIONGOZI

Mhe. Rais na Makamu wa Rais wakipata picha ya pamoja na wajumbe wapya wa Tume ya Maadili
Kudhoofisha maadili ya uongozi ni sawasawa na madaraka pasina udhibiti

Maadili na uwajibikaji wa viongozi wa Umma

Tanzania, kama ilivyo nchi nyingine za Kiafrika, ina changomto za kiuwajibikaji na wananchi wametoa mawazo yao wakati wa mchakato kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya. Wananchi walizungumzia changamoto za uwajibikaji kwa viongozi wa umma na wakatoa sababu na mantiki ya kuunda mfumo thabiti wa uwajibikaji.

Uwajibikaji ni dhana pana, inahusu utaratibu endelevu wa udhibiti na uwekaji wa mipaka katika matumizi ya madaraka. Vilevile, ina maana ya kuwepo utaratibu wa kuwalazimisha wenye madaraka kufanya wanayotakiwa kuyafanya na kuacha kufanya wasiyotakiwa kuyafanya na ya kujibu maswali au hoja zinazohusiana na matumizi ya madaraka aliyopewa. Kwa mantiki hii, uwajibikaji unamaanisha pia kipengele cha adhabu kwa wale wanaotumia madaraka ya umma vibaya. Kwa hiyo, dhana ya uwajibikaji inahusu masuala yafuatayo: kwanza, uwepo wa mfumo wa udhibiti wa madaraka; pili, uwepo wa utaratibu wa kuwalazimisha wale walio na madaraka kutekeleza wajibu wao na kuwazuia kukiuka wajibu wao; na tatu, kuwepo utaratibu wa kuwaadhibu wenye madaraka pale wanapokosea.

Kwa upande mwingine, maadili maana yake ni kanuni au misingi inayoelekeza ni kitu gani kibaya au kisichofaa au kizuri au kinachofaa. Misingi hii inaweza kujengwa katika utamaduni wa jamii husika. Vilevile, misingi hiyo inaweza kuandikwa na kwa kanuni ya maadili. Kwa maneno mengine na hasa kwa hali ilivyo katika nchi yetu sasa na hata kwa vizazi vijavyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka masharti mahususi ya maadili ya viongozi katika Katiba kama sehemu ya kujenga utamaduni wa kikatiba wa kuendelea kudhibiti matumizi ya madaraka.

Kuna aina nyingi za uandishi wa Katiba, moja ni ile ambayo kitaalamu huitwa “instrumentalist approach” Katiba hizi huwa hazijipambanui sana, kwa asili yake huwa zinaweka misingi na kujenga taasisi, huwa fupi na maeneo mengi huja kufanyiwa kazi na sheria zitakazotungwa na Bunge. Aina ya pili ni ile inayoitwa “Programmatic approach” ambayo huwezesha uandishi wa Katiba za mfano wa Katiba ya uhuru wa Taifa la Ireland. Ni Katiba ambayo huweka bayana ndoto, malengo makuu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali na sera za kitaifa ambazo kwa ujumla wake katika Katiba hutanabaisha dira ya nchi.

Katiba ambazo ni programmatic huweka ndani yake pia masharti mahususi juu ya misingi ya Taifa, misingi juu ya maadili ya Taifa, misingi ya maadili ya viongozi sambamba na utaratibu wa uwajibikaji kwa viongozi wa umma. Moja ya changamoto kubwa katika taifa lolote lile ni namna gani Taifa linaweza kuwa na mfumo wa kikatiba ambao unawazuia viongozi wa Serikali kuyatumia madaraka ya umma vibaya.

Mwanafalsafa wa Uskochi David Hume katika Karne ya 18, alipata kunena haya, “tunapotengeneza mfumo wa Serikali katika Katiba na kuweka udhibiti na urari wa madaraka ni vizuri kuzingatia kuwa kila mtu siyo mwaminifu na kwamba binadamu yeyote katika matendo yake mengi huwa hana malengo mengine isipokuwa kutafuta manufaa binafsi. Hume anaendelea kusema ni lazima kuweka utaratibu wa kuyadhibiti madaraka hayo ili mtu huyo aweze kutoa ushirikiano wake katika masuala ya umma. Anaonya kuwa tusipofanya hivyo tutajisifu kuwa tuna katiba lakini kumbe hatuna usalama wa mali na uhuru wetu isipokuwa tu kwa matakwa ya watawala au viongozi wetu, na jambo linapotolewa kwa utashi wa viongozi na hasa katika mambo ya msingi kama hatutakuwa na usalama kabisa. Kwa ujumla, mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa madaraka wanayopewa viongozi ni lazima yadhibitiwe kikatiba; haifai kumwamini mtu kwa sababu ni vizuri kila mtu achukuliwe siyo mwaminifu au kwa kimombo anasema “every man ought to be supposed a knave”.

Maadili katika Rasimu ya Warioba ukilinganisha na Katiba Inayopendekezwa

Rasimu ya Katiba Toleo la Pili ilijaribu kwa mara ya kwanza baada ya marekebisho makubwa yaliyofanyika mwaka 1984 kwa Katiba ya Mwaka 1977 yaliyoigeuza kwa sehemu Katiba ya Mwaka 1977 kuwa “programmatic”. Licha ya marekebisho hayo bado Katiba ya mwaka 1977 haikuwa imejipambanua ipasavyo ili kuendana na mahitaji ya wakati, yaliyohitaji misingi ya maadili na uwajibikaji pamoja na uanzishwaji wa taasisi huru za kusimamia maadili na uwajibikaji wa viongozi wa umma.

Wengi wenu mtakuwa mlishuhudia kile kilichokuja kuwa maarufa miongoni wa mitandao ya kijamii kama sinema ya Baraza la Maadili. Iliitwa sinema kwasababu watuhumiwa waliopata kuhojiwa katika baraza letu la Maadili chini ya Jaji Msumi hawakuonekana kuitetemekea Mamlaka ile ambayo ndio ina dhamana ya kuwawajibisha viongozi wanaokwenda kinyume na maadili ya uongozi. Hata pale waandishi walipomhoji mwenyekiti wa Baraza juu ya hatima ya viongozi wale, aliishia kusema wakimaliza kazi watapeleka taarifa kwa mamlaka za juu. Swali ambalo wananchi wamekuwa wakijiuliza ni vipi pale ambapo wanaohojiwa ni viongozi na watumishi kutoka mamlaka ya juu? Je utekelezwaji wa mapendekezo ya Baraza utazingatiwaje katika mazingira hayo?, haya si maneno yangu ninayasikia huku na huko.

Tunaposema kwamba Katiba Inayopendekezwa imetupilia mbali masharti mahususi kuhusu maadili ya uongozi, hebu tutizame mfano huu;- Ibara ya 15 ya Warioba ilisema “Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli zakiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuriya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitiakwa Katibu Mkuu wa Wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikaliinayohusika, akiainisha: (a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa zawadi; na
(d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo”. Kifungu cha pili cha Ibara hii kinasema “Neno “zawadi” kama lilivyotumika katika Ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani atakachopewa Kiongoziwa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma. (3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na
mambomengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.

Katiba Inayopendekezwa imeiboresha Ibara hii na kuandika Ibara ya 29(2)(a) ambayo kwa jumla inasema “Kwa madhumuni ya Katiba hii, Bunge litatunga sheria itakayoweka, pamoja na mambo mengine: (a) tafsiri ya neno zawadi, aina, thamani, kiwango na uhifadhi wa zawadi ambayo kiongozi anapokea wakati akitekeleza
majukumu yake.

Nikitazama kwa kina maboresho hayo utagundua masharti ambayo wananchi walikuwa wanayapendekeza kuwa yawepo katika Katiba kama masharti mahususi, Katiba Inayopendekezwa imeyatupilia mbali na kuacha ombwe hilo kufanyiwa kazi na Sheria zitakazotungwa na Bunge. Ikumbukwe hata wabunge ni viongozi na masharti haya kikatiba yangewawajibisha hata wao na kama yasingefutwa basi wangelazimika kutunga sheria ambazo misingi yake imo katika Katiba tofauti na mtindo wa uandishi wa Katiba Inayopendekezwa ambao unawapa viongozi nguvu za kutumia utashi wao kutunga masharti ya kuwawajibisha na kuwadhibiti viongozi wao wenyewe. Kwa maneno mengine misingi ya kuwadhibiti viongozi wetu na namna wanatumia madaraka yao inapaswa iwekwe kwenye Katiba na wananchi na si viongozi waje kujitungia masharti ya kuwadhibiti wao wenyewe, hawatatenda.

Warioba alisema katiba Ibara ya 16 kwamba “Kiongozi wa umma - (a) hatafungua au kumiliki akaunti ya benki
nje ya Jamhuriya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na (b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namnaau mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma”.

Ukiitizama Katiba Inayopendekezwa namna ambavyo imeiboresha Ibara hii katika Ibara ya 29(2) inasomeka kama ifuatavyo “Kwa madhumuni ya Katiba hii, Bunge litatunga sheria itakayoweka, pamoja na mambo mengine: (b) masharti ya kufungua akaunti za nje kwa kiongozi wa umma.

Hivi kweli ukisoma Ibara za 15 na 16 za Rasimu ya Warioba, je uboreshwaje wake ni kama ulivyowekwa katika Ibara ya 29(2) ya Katiba Inayopendekezwa? Tafakarini kwa kina kabla ya kusema Katiba Inayopendekezwa ni Bora Afrika.

Warioba alisema katiba Ibara ya 21(3) kwamba “Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosaya: kimaadili; (b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; au (c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu washeria za nchi au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi waumma.

Katiba Inayopendekezwa imeyafuta kabisa masharti haya, kwa msingi huu tusishangae kiongozi anayetuhumiwa kwa masuala tajwa hapo juu akaendelea kutoa huduma kwa wananchi ilhali tukijua mzizi wa tatizo uko kwa kiongozi au mtumishi huyo wa umma.

Katiba Inayopendekezwa inapokuja katika suala la Maadili kwakweli haijawatendea haki watanzania, hasa katika kipindi hiki ambapo taifa letu limepitia katika kufichuka kwa tuhuma na kashfa za ufisadi mkubwa katika taasisi zetu za serikali tena karibu katika ngazi zote.

Labda kabla ya kuwaacha niwape mfano wa mwisho, Ukiangalia Tume ya Maadili na uwajibikaji utagundua kwa sababu ambazo hazieleweki masharti mengi na muhimu yaliyokuwa sehemu ya majukumu ya Tume ya Maadili kwa Rasimu ya Warioba yamefutiliwa mbali katika Katiba Inayopendekezwa. Rejea masharti ya ibara ya 203(2)(b), (e) hadi (o) ya Rasimu ya Tume, juu ya majukumu ya Tume ya maadali yauongozi.Ukisoma kifungu cha 231 cha Katiba Inayopendekezwa masharti hayo yamefutwa.

Hakika Katiba Inayopendekezwa itaturudi nyuma kabisa katika uandishi bora wa Katiba Barani Afrika, lakini fursa ya kuirekebisha kabla haijawa rasmi mpya iko pale pale ukirejea kifungu cha 35(3) na (4) cha Sheria ya Kura ya Maoni.

Karibu kutoa Maoni



Monday, April 13, 2015

TCD MSIPOLISEMEA HILI LA MAREKEBISHO YA KATIBA YA 1977, MTAPOTEZA HESHIMA YENU

Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu hivi hivi

Kuahirishwa kwa Kura ya Maoni

Wiki iliyopita nilieleza furaha yangu baada ya serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuahirisha Kura ya Maoni iliyokuwa ifanyike tarehe 30 Aprili, kitendo cha serikali ni cha kiungwana licha ya kwamba kimekuja kwa kuchelewa sana. Serikali kwa ukubwa wake na taasisi zake lukuki ambazo nyingine zimepewa hata dhamana ya kutumia intelijensia kuyaelewa mambo na kutoa ushauri stahiki kwa viongozi wetu, hatukutarajia tupige kelele kwa miezi mitano kusema Kura ya Maoni haiwezekani mwaka 2015, na hasahasa mwezi wane. Sote tulijua bado hatukuwa na vifaa (BVR) vya kuwaandikisha watu, sote tulijua tunatumia mfumo mpya kuwaandikisha watu na hivyo kutarajia sintofahamu kadhaa wa kadhaa, sote tulijua sheria ya Kura ya Maoni ilikuwa imeweka utaratibu na masharti ya kuzingatiwa kabla ya kwenda kwenye zoezi la Kura ya Maoni, na sote tunajua masharti hayo na utaratibu kwa kiasi kikubwa haukuwahi kufuatwa.

Zaidi ya yote, kila mtu anajua kwamba mpaka mwezi wa pili kwenda wa tatu na hata leo bado tunaendelea kugawa Katiba Inayopendekezwa kwa umma wa watanzania. Na sote tunafahamu kwa serikali yetu imechapa nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa ambayo ni wastani wa Katiba Inayopendekezwa moja inapaswa kusomwa na watu kati ya 12 hadi 13. Katiba Inayopendekezwa moja kusomwa na watu 12 au 13, tafsiri yake ni kwamba, wewe ambaye hujapata kuiona Katiba Inayopendekezwa kuna wenzake 11 au 12 ambao wakimaliza kusoma ndipo na wewe itafika zamu yako, kuwa mvumilivu maana sasa una muda wa kutosha.

Ilikuwa bayana pia kwamba tusingeweza kwenda kwenye Kura ya Maoni tukiwa tumegawika kabisa, kisiasa na kiimani. Kura ya Maoni ingeendeleza mpasuko ambayo kuuziba ingetugharimu zaidi kama Taifa. Na kama ambavyo utakuwa umefuatilia, dini zote mbili zina madai na kwa msingi huo, zote hazijaridhika na zote zilishajipanga kupiga kura ya Hapana. Kwa maneno mengine tarehe 30 Aprili angekuwa ni mtu basi angeshakuwa mhanga wa mpasuko wa kijamii na kwa maana hiyo tokeo lolote la Aprili 30 lingekuwa limepasua Taifa kuliko kutujenga.

Nyote mmeshuhudia kwamba kuelekea Kura ya Maoni Aprili 30 ambayo sasa imeahirishwa tulikuwa tayari na mpasuko mkubwa wa kisiasa, vyama vikubwa vilikuwa vimesusia kushiriki katika zoezi la Kura ya Maoni. Kuna baadhi ya watu walichukulia mzaha kwamba hata wakisusia kama vyama itakuwa kazi bure iwapo watu watajitokeza na kushiriki katika Kura ya Maoni. Baadhi ya watu hawa walienda mbali zaidi na kuhamasisha kwamba watu wapuuze msimamo wa vyama kususia na badala yake wakashiriki Kura ya Maoni. Mimi kwa mfano chama changu hakikususia, na nilikuwa nimejiandaa kwenda kupiga kura ya Hapana na vivyo hivyo nikajaribu kulisemea hili kwamba kuna tofauti kubwa kati ya msimamo wa chama kama taasisi na haki ya mwananchi kushiriki katika shughuli za umma ikiwemo kupiga kura ya maoni.

Watu huenda kupiga kura kama raia wa Tanzania, na hushiriki zoezi la kupiga kura kama haki yao ya kimsingi na haijalishi watu hawa ni wanachama wa chama cha siasa au la. Chama cha Siasa kama taasisi inayotambuliwa kisheria (rejea Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258), kina uongozi, kina utaratibu wa kufanya uamuzi kupitia vikao na kadharika,chama kinaweza kutoa msimamo, kufanya uamuzi na uamuzi huo usiingiliwe na uhuru wa raia mmoja mmoja kutumia haki zake katika Jamhuri yetu. Kwahiyo vyama vikisema tunasusia Kura ya Maoni hilo ni tatizo na wa kulitatua sio wananchi bali ni vyama kukaa na kutatua matatizo yaliyopo miongoni mwao.

Makubaliano ya Rais na TCD

Juzi juzi hapa nikapata kusikia jamaa yangu mmoja ambaye alisemalo mara nyingi huwa ama huwa lina wakilisha msimamo, huyu jamaa ni kama mpishi, mpishi akikwambia leo hakuna nyama ni maharagwe usimbishie maana yeye anakaa jikoni kila wakati, anajua. Katika mazungumzo anaonesha kana kwamba hakuna kitu kama Makubaliano ya Rais na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Watu kama hawa huwa sio wa kupuuzwa hata kidogo, lakini kubwa ni kwamba yeye namshukulia kama mwakilisha fikra, na mimi nawaeleza ninyi wanachama wa TCD. Napenda kuwaeleza kwamba Tanzania na watanzania waliona mwanga kupitia ninyi, waliwaamini na kuwaheshimu, nawasihi enendeni kwa moyo huyo.

Naomba niwakumbushe, siku Mhe. Cheyo anasoma Makubaliano ya Rais na TCD, kushoto kwake aliketi Mhe. Dovutwa na kushoto kwa Mhe. Dovutwa aliketi Mhe. Philip Mangula. Kwa ishara hii ya umoja na mshikamano wa TCD, tusaidie watanzania kuvuka kipindi hiki chenye changamoto nyingi. Ninyi (viongozi na wanachama wa TCD) mnajua fika, na ninajua mnajua na mko katika nafasi ya kujua ukweli wa mambo kwamba hatuwezi tena kuwa na Kura ya Maoni mwaka huu. Kinyume na fikra hiyo ni kujaribu kulazimisha mambo halafu mwishowe tuharibu kila kitu, na ninauhakika miongoni mwenu kuna wazee wenye hekima na wenye hofu ya Mungu, mnajua fika kwa joto la kisiasa lilipo sasa hivi kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, kimsingi haiwezekani tena kuchomeka Katiba Inayopendekezwa ili ipigiwe Kura ya Maoni.

Juzi waziri mmoja wa zamani akaandika katika mitandao ya kijamii, kulikoni katika chama cha Mapinduzi, mbona kimya mpaka sasa kuhusu kinyang’anyiro cha watangaza nia ya Urais kupitia CCM ilhali kila kitu kinapaswa kuwa kimekamilika ifikapo mwezi Mei. Swali la makusudi kutoka kwa mwanasiasa huyu maarufu, ni ishara inayotuonesha uzito wa hali ilivyo kisiasa nchini, huku kwenye CCM peke yake kuna hali ngumu, kuna joto mithiri ya tanuruni, bado kwenye vyama vinavyoboresha mawazo (wengine wanaita vyama vya upinzani) vinyang’anyiro bado. Katika ngazi za ubunge, wabunge wa sasa pamoja na watangaza nia za ubunge wote akili zinawapaa kujaribu kuwapa maneno matamu matamu ya lala salama au maneno matamu ya kufunga uchumba kwa miaka mingine mitano au mwanzo mpya wa miaka mitano.

Kama kwenye Urais na Ubunge watu hawalali mpaka kieleweke, kwenye udiwani, vikumbo ni zaidi katika ngazi ya kata. Sasa nikuulize unadhani Taifa liko katika akili iliyotulia ya kuipigia Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa kwa maana viongozi wetu waongoza kampeni ambao wengi ni wanataka kuendelea kushikilia majimbo au wametingwa na kutangaza nia pamoja na wananchi raia mmoja mmoja ambao saizi tunatathmini nani abaki na nani asirudi na kwanini abaki na kwanini asirudi. Hivi kweli ukituongezea na Katiba Inayopendekezwa si utatuvuruga?

Kibaya zaidi, kitendo chochote cha kuchanganya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu itakuwa ni dhambi kubwa kuliko, tutageuza Mchakato wa Katiba na Katiba Inayopendekezwa kuwa ajenda ya uchaguzi, hilo litavuruga maana ya Katiba isiyopasualiwa kisiasa katika ya ndio na hapana zinazohamasishwa kwa minajiri ya siasa zetu ambazo mara nyingi huwa hazina maslahi ya umma mpana wa watanzania.

TCD, nawasihi tena, kutaneni na jadilini, huyu Rais wetu ni muungwana na msikivu, mkimweleza kwa hoja hizi na zenu nzuri zaidi atawaelewa na twaweza kuona Bunge lijalo tukijadili marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 ili tuvuke salama katika Uchaguzi Mkuu. Msipofanya hivyo, viongozi wangu wa CCM, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI, TLP na UDP kama sehemu ya TCD, mtapoteza imani yenu mbele ya umma wa watanzania. Nawasihi fanyeni hili kwa maslahi ya Taifa na zaidi tumsaidie Mhe. Rais amalize na Uchaguzi kwa mara ya kwanza usio na tashwishwi wala waa na huo utakuwa sehemu ya utumishi wake uliotukuka kwetu na sisi kwa hakika tutamkumbuka ikiwemo pamoja na mchakato wa Katiba ambao tutaendelea nao mwakani. Na wala msihofu, tukifanya marekebisho, lazima tutatunga na masharti yatokanayo na masharti ya mpito na mojawapo ya kazi za kikatiba kwa Rais ajaye na Serikali yake ni kuendelea na Mchakato wa Katiba, sio utashi bali ni takwa la kikatiba.

Fursa ya Mjadala

Kilichobaki sasa ni kuendelea kujadiliana kuhusu mchakato wa Katiba, Rasimu ya Warioba, Katiba Inayopendekezwa na tuulizane maswali na kupeana majibu. Kama ilivyo ada wikendi hii Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeandaa Mdahalo wa Katiba huko Mbeya, ni sehemu ya kujadiliana. Na ninawasihi Taasisi ya Mwalimu Nyerere wasiishie hapo, waende na mikoa mingine mingi zaidi maana elimu hii inahitajika sana.

Tunapojiandaa kisaikolojia na Uchaguzi Mkuu

Tuipe Tume ya Taifa ya Uchaguzi ushirikiano wa kutosha wanapoendelea na zoezi la uandikishwaji wapiga kura. Tujitokeze kwa wingi kuandikishwa na kupata vitambulisho vya mpiga kura, bila kitambulisho cha mpiga kura hutaweza kutumia haki yako kufanya uamuzi wa ni nani na nani wapewe dhamana ya kukuongoza katika ngazi ya kata, jimbo na Jamhuri yetu.


Wito, kwa unyenyekevu niwasihi serikali msiwaingilie Tume wanapotenda kazi yao, wapeni uhuru wa kutosha kama ambavyo wanapaswa kuwa. Waacheni ili watanzania kwa muda huu uliobaki wapate huduma ya Tume bila matatizo. Rai yangu kwa vyama vya siasa, jipangeni, pigeni siasa safi, jengeni hoja, toeni sababu na onesheni ushahidi, watu watawaelewa tu, ila achene kuisakama Tume ya Uchaguzi bila sababu, maana hiyo ni tabia mbaya.

Saturday, April 4, 2015

RAI YANGU: FURSA ILIYOBAKI NI MAREKEBISHO YA KATIBA YA MWAKA 1977

Mhe. John Cheyo akiutangazia umma wa watanzania makubaliano ya Mhe. Rais na TCD
Katika wiki hii inayoisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeutangazia umma wa watanzania kwamba hakutakuwa na Kura ya Maoni tarehe 30 Aprili kama ilivyotangazwa hapo awali. Tume imesema badala yake zoezi la uandikishwaji wa Wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR litaendelea hadi mwezi julai mwaka huu. Tarehe ya Kura ya Maoni itatangazwa hapo baadaye baada ya Tume ya Taifa ya uchaguzi kukubaliana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Nitakuwa mnyimi wa shukrani nisiposema kupitia kwenu Tume ya Taifa ya Uchaguzi, asante serikali kwa kutegua kitendawili hiki chepesi. Naomba ieleweke kwamba huu sio ushindi wala isiingizwe siasa hapa bali ni uthibitisho kwamba tunapaswa tuseme kweli hata kama tunatetemeka kwa woga. Serikali ni watu na watu wenyewe ndio sisi, inapaswa kutusikiliza hasa pale tunapozungumza masuala yenye masilahi kwa taifa letu.

Tanzania itajengwa na wenye uthubutu wa kusema kweli na kuisimamia kweli. Nirudie tena, kupitia Tume ya Uchaguzi, Asante serikali, asante wadau wote na asante wananchi wa Tanzania kwa mshikamano wenu. Nawasihi watanzania wenzangu kwa ujumla wenu, tusiiache serikali yetu inapokosea au inaposhindwa kuyatazama mambo kwa upana wake, wao (viongozi wetu) ni binadamu pia, tunapaswa kuwakumbusha, kuwashauri na kama hawasikii basi tuwasumbue tena na tena mpaka watakaposikia hoja zetu chetu.

Wale ambao mmepewa dhamana ya kuwashauri viongozi wetu, fanyeni hivyo kwa unyenyekevu, weledi na uzalendo mkubwa. Viongozi wetu hufanya maamuzi kwa kuzingatia vipawa vya alivyowakirimu Mungu, weledi wao, mitazamo na dira za kiuongozi, lakini ukweli unabaki palepale kwamba nafasi ya watumishi wa umma katika kuwasaidia kiweledi na kitaalamu ni ya muhimu kabisa. Mtumishi mtaalamu ambaye hatoi ushauri sahihi na hasemi kweli ni janga katika utumishi wa umma na umma wa watanzania na anaweza kuwa chanzo cha kupotosha viongozi wetu.

Lakini pia viongozi wengine huwa wabishi na wenye kiburi, kwa hali ilivyo sasa tusichoke kuendelea kuwaambia hatari ya maamuzi yasiyo sahihi katika mustakabali wa Taifa letu na kama ni wale wako katika dhamana ya wananchi basi tusubiri Wananchi waamue hatima yao

ANGALIZO

Nimemsikia Mhe. Mbunge mmoja ambaye kauli zake kwa uzoefu wangu huwa zinatimia na huja na kauli hizo mwishoni mwishoni kabisa na huwa zinafanyiwa kazi moja kwa moja. Kama mtakuwa watu wa kufuatilia mwaka juzi (2013) kwenye kikao cha kuelekea mwisho wa mwaka alitoa pendekezo ambalo lilifanyiwa kazi ipasavyo licha ya kwamba lilikuwa kinyume na usanifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Nimemsikia sikia magazetini kwamba ameomba mwongozo juu ya hoja kwamba Bunge la Jamhuri lipitishe hoja kwamba Katiba Inayopendekezwa ifanywe ya Mpito ili tuvuke Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Na akaendelea kusema kwamba Katiba Inayopendekezwa imesheheni mambo ambayo watu wamekuwa wakiyadai. Mheshimiwa Mbunge atakuwa ameshindwa kufahamu namna ambavyo mchakato wa Katiba mpya katika ngazi ya Bunge Maalum ulivurugika na kwamba mpaka leo Taifa limegawika kisiasa, kidini na baina ya Bara na Zanzibar. Haitaki elimu kubwa kujua Katiba Inayopendekezwa imetugawa watanzania na imepoteza sifa ya kuwa ishara ya Umoja wetu.

Kuhusu Kauli yake, Napenda kusema yafuatayo;-

1) Kauli yake ipuuzwe na Wabunge wote, wa CCM na wote wa vyama vya upinzani

2) Katiba Inayopendekezwa ni mbaya na haifai na ni zao la mchakato ambao mwishoni ulishindwa kujenga muafaka wa Kitaifa, hakuzingatia maridhiano na haukupata kuwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa vyama vya siasa na wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba.

3) Bunge la Jamhuri ya Muungano halina mamlaka wala uhalali wa kuijadili Katiba Inayopendekezwa, hivyo hoja ya kwamba Bunge la Jamhuri liipitishe Katiba Inayopendekezwa kuwa ni ya Mpito haipo, haina mashiko na ina nia ya kuendeleza migogoro ya kisiasa inayotugawa Wananchi na isiyo na tija kwa Taifa letu.

YANAYOTAKIWA KUFANYWA HARAKA

1) Mchakato wa kuandaa mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kuzingatia Ibara ya 98, ili ifanyiwe marekebisho madogo ya 15 yatakayojumuisha mambo ambayo Mhe. Rais alikubaliana na Kituo cha Demokrasia (TCD). Mambo haya ni pamoja na (i) Matokeo ya Urais kuwa ni zaidi ya asilimia 50 ya kura zote halali zilizopigwa na kuhesabiwa, (ii) Matokeo hayo yaweze kuhojiwa Mahakamani kama kuna tashwishwi, (iii) Uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na (iv) Uwepo wa Mgombea Huru.

2) Tuushirikishe umma wa watanzania katika kutoa maoni yao kwa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kwa kiasi cha kutosha, Serikali na Bunge watuongoze kufanikisha hili.

Naendelea kusema kama isingekuwa Rais Kikwete, tusingepata mchakato ambao Wananchi walishiriki ipasavyo katika awamu ya kwanza ya maoni ya Wananchi, awamu ya pili ya Mabaraza ya Katiba. Awamu ya tatu ya Bunge Maalum ilishindwa kujenga muafaka na kusababisha mpasuko wa kisiasa na zoezi lililobaki yaani awamu ya nne ya Kura ya Maoni ambayo mpaka sasa na kwa mapenzi mema ya Taifa letu haiwezi kufanyika tena mwaka huu labda tusifanye Uchaguzi Mkuu.

KUHUSU WALE WENYE FIKRA OVU

Nimeanza kusikia watu mbalimbali hasahasa vijana wadogo wadogo tu ambao wameanza kusema hakujawahi kuwa na makubaliano baina ya Mhe. Rais na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Na wengine wasomi kabisa wameanza kusema kama mmekosa Katiba Mpya sasa, sahauni marekebisho ya 15 ya Katiba ya 1977. Watu hawa hawa hawaitakii mema nchi yetu.

Niwaulize unadhani tutaweza kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila Tume Huru ya Uchaguzi, tukisema ndio, basi tutakuwa tunamkanusha hata Rais ambaye alisema tunapaswa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi katika uchaguzi ujao. Kama mtasema hapana basi mjiulize dhamira zenu ni zipi na hapa nitawauliza vyama vyote vya upinzani, je kelele zenu zimekuwa za debeshinda?

Chama cha Mapinduzi kitajijengea heshima kubwa kama kitatoa uongozi ili tufanye Marekebisho ya 15 ambayo uchaguzi huu ukipita salama, hatutakuwa tena na lawama zisizo na msingi na sintofahamu inayotokana kupotea kwa imani ya vyama vya upinzani kwa chombo cha kikatiba kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

RAI YANGU KWENU

Kama mnataka tumshukuru Rais Kikwete kwa kutuanzishia mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambao msingi na usanifu wake ulikuwa Wananchi kutoa maoni yao basi tuna budi ya kuunga mkono na kukumbusha kwa sauti kubwa ili waliopewa dhamana watuletee mswada wa sheria ya kurekebisha Katiba ya Mwaka 1977 ili kwa muda mchache uliobaki turekebisha Katiba na kuunda vyombo vinavyopaswa kuundwa.

Wanaopuuza rai yangu wanataka Rais Kikwete amalize utumishi wake kwetu bila kuhakikisha misingi ya mpito ambayo itaimarisha demokrasia yetu, na misingi wa misingi hii ni Marekebisho ya 15 ya Katiba ya Mwaka 1977. Kwa maneno mengine mbadala wa kutokuwa na Katiba Mpya ni Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 Hima Hima watanzania.