Friday, September 11, 2015

DR. JOHN POMBE MAGUFULI NA UWEZO WAKE WA KULETA MABADILIKO CHANYA



Tujadiliane kwa HOJA na Sababu

Kuelekea uchaguzi Mkuu 2015  mabadiliko ni miongoni mwa mambo yanayochukua nafasi kubwa katika kampeni na ilani za vyama vya siasa. Hoja nyingi zinatolewa hususani katika dhana ya mabadiliko ya mfumo au kiongozi au yote mawili yaani mfumo na uongozi. Kwa bahati mbaya watanzania hawaelezwi mahusiano kati ya mfumo na viongozi. Mbaya zaidi wengi wetu tumeporwa uwezo wa kutafakari kutokana na kuzamishwa kwenye mahaba kwa wagombea au vyama vya siasa.

Kwa kuwa bado kuna siku zaidi ya arobaini ni vyema tukawatafakari baadhi ya wagombea wa nafasi ya uraisi ambao ndio hasa wanachuana vikali katika kampeni zinazoendelea.  Yapo mambo kadhaa yanayoweza kutuongoza katika kuwapima wagombea na sera zao. Moja, ni kutafakari kama inatosha kuwa mashabiki wa matamko tu yenye kushawishi juu ya kuleta mabadiliko  kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wameendelea kuwalaghai wananchi kipindi hiki cha kampeni za uchanguzi mkuu 2015.

Muhimu sana ni  kupima nia na zaidi sana uwezo wa  kiongozi husika kutafsiri madhui ya ahadi zake katika vitendo.  Hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba  wameibuka wanasiasa wanaotoa matumaini hewa kwa wananchi kwa kusema tu yale ambayo wananchi wangependa kusikia. Ni jambo jema kuwajengea wananchi matumaini lakini ni hatari pia kuwalaghai wananchi kwa mambo ambayo kiongozi husika sio tu yeye mwenyewe hayaamini au hana uwezo wala dhamira ya dhati kutimiza. Maswali mawili ni muhimu kuulizwa katika hili, moja ni mfumo gani unaolengwa kubadilishwa ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa watanzania? Je viongozi husika wanavyo vigezo, uwezo  na uzoefu katika kujenga mifumo endelevu?

Edward Lowasa na dhana ya mabadiliko ndani ya UKAWA

Tukianza  na kambi  ya UKAWA inayowakilishwa na Edward Lowasa, tukivipima vyama vya siasa vinavyounda UKAWA kwa mifano na kutafuta vielelezo vya kimfumo inaonekana  dhahiri kuwa  aidha hakuna kabisa mifumo bali haiba (personalities)  au kuna baadhi ya viashiria vya kuwepo kwa mfumo lakini kutoka na kujengwa kwenye misingi dhaifu mifumo hii imekuwa sio endelevu. Pengine kwa kutambua udhaifu huu UKAWA imefungua milango kupokea baadhi ya  wanasiasa ambao wamewahi kuongoza nchi yetu katika nafasi kubwa za uongozi kama ile ya Waziri Mkuu. Hawa ni pamoja na Edward Lowasa ambae ndio mgombe uraisi na Fredrick Sumaye .

Hata hivyo  ukiwauliza au hata ukijaribu kutafuta na kupima jambo gani la kimfumo waliwezakulifanya katika nafasi zao?  Kinachojitokeza ni aidha viongozi hawa hawakuwa na uelewa sahihi wa masuala ya kimfumo hivyo kushindwa kufanya uchambuzi sahihi wa matatizo ya kimfumo na kuyapatia majawabu ya kiutendaji. Mara nyingine  walidandia miradi ya maendeleo na kuisukuma kwa mabavu bila kuweka misingi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kujenga  taasisi imara  kutekeleza na kusimamia sekta husika mambo hayo licha ya kuwa mazuri yaligeuka kusongwa na changamoto nyingi.

Mbaya zaidi viongozi hawa na wengine wanaofanana nao walitumia nafasi zao kujinufaisha wenyewe ikiwa ni pamoja na kujenga mitandao ya kukwapua fedha za umma kwa maslahi yao binafsi na washirika wao. Kinachopaswa kuogopwa sana na Watanzania ni ile hulka ya viongozi hawa kutaka kujilimbikizia mali kwa namna yeyote ile. Hawa ni miongoni mwa viongozi  ambao wamediliki hata kusema kuwa wakichaguliwa kuongoza nchi hii watatengeneza kundi la aina  fulani ya matajiri ambao wataendesha uchumi wa taifa letu.

Swali la kujiuliza ni kama huu ni mkakati wa kimfumo na je haya ndio mabadiliko ambayo Watanzania watarajie? Hii ni dhana hatari inayolenga kuchochea kuongezeka kwa tabaka la maskini na matajiri. Ni muhimu kutambua kuwa matajiri kazi yao kubwa ni kutengeneza faida kutokana na mitaji yao. Haishangazi kuona kuwa matajiri hawa wanaotajwa na mmoja wa wagombea wa uraisi kuwa ni “marafiki” zake wamekuwa wakifadhili harakati za mgombea huyo kuingia madarakani kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita. Jambo jingine la kujiuliza ni Je kwa uwekezaji huu matajiri hawa wanatarajia kuvuna nini? Wasiwasi wangu ni kwamba chondechode mgombea huyu asijekuwa ameweka rehani rasilimali za nchi hii na ikiwa ni pamoja na maisha ya watanzania ili tu atimize ndoto yake ya kuwa raisi wa inchi.

Rai yangu ni kwamba Watanzania tufungue fahamu zetu kipindi hiki cha kampeni na kupima wagombea na hoja  zao pasipo ushabiki na ushawishi mwepesi. Naelewa vyema haja ya kufanya mabadiliko lakini tujiulize ni mabadiliko ya aina gani tunahitaji. Haifai kabisa kumkubali mgombea hana kabisa vigezo vya kuleta mabadiliko eti tu kwa sababu tunataka mabadiliko. Mgombea ambae hana uwezo wala uthubutu wa kukemea ufisadi  hatufai kabisa hasa kwa kuzingatia hulka za kifisadi ambazo zimeshamiri katika jamii yetu sio tu kwenye sekta ya umma bali hata sekta binafsi. Ni nani asiefahamu kuwa ufisadi uwe mkubwa au mdogo ni kikwazo kikubwa katika maendeleo na ustawi ya nchi yetu.

Je ni mara ngapi tumesikia mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA akiweka bayana  mkakati wa kupambana na ufisadi? Ni nani asietambua kuwa ajenda ya mapambano dhidi ya ufisadi ndio iliyowafanya wananchi wengi kuvutiwa na sera za CHADEMA hususani chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho Dr. Wilbroad Slaa?  Tujiulize kwanini vita  dhidi ya ufisadi sio tena hoja kubwa kwa CHADEMA na UKAWA mara tu baada ya kumpitisha Edward Lowasa kupeperusha bendera ya chama hich na umoja huo katika nafasi ya urais kwenye uchanguzi Mkuu.

Zaidi sana tujiulize ni kwa nini Edward Lowasa anapata kigugumizi kukemea ufisadi? Tumhoji atawezaje kutekeleza ahadi zake lukuki za mabadiliko bila kuwa na haki na uthubutu wa kukemea ufisadi? Atahakikishaje huduma za jamii zinapatika kwa wananchi wote, elimu burekwa wote mpaka chuo kikuu, na kuongeza tija kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji bila kudhibiti mianya ya ufisadi? Au anaikwepa vita dhidi ya ufisadi kwa sababu anajua ni kupitia ufisadi pekee hasa kwa njia ya manunuzi na mikataba feki ndio anaweza kulipa hisani kwa marafiki zake wanaoendelea kufadhiri mradi wake wa kuingia Ikulu. Nachelea kusema kuwa kwa Edward Lowasa uraisi ni mradi wakunenepesha mitaji ya matajiri wanaojiita marafiki zake ambao sasa wamekaa mkao wa kula. Sioni dalili za mabadiliko chanya yanayowezakutokana na kiongozi wa aina hii kwenye nchi yetu kwa kuzingatia muktaza tulionao kijamii, Kisiasa na kiuchumi.

Wapo wanaosema eti kwa sababu ajenda ya ufisadi ipo ndani ya Ilani ya CHADEMA ambayo pia inanadiwa na UKAWA, hivyo ikitokea Edward Lowasa akashinda atalazimishwa na ilani hiyo kukemea ufisadi. Wachambuzi hawa wanawezakuwa sahihi endapo wafanya tathmini ya taswira ya uraisi anaoutamani Edward Lowasa na ukweli kwamba ataapishwa kama Edward Lowasa.  Hasa kwa kuzingatia Katiba ya sasa ni dhahiri kwamba atakapoingia tu madarakani sioni kama CHADEMA watakuwa tena na nguvu ya kumdhibiti.

Tusisahau pia kuwa ni CHADEMA na UKAWA ndio walimbembeleza Edward Lowassa kujiunga nao na ni dhahiri kwamba sharti ambalo aliwapatia ni kumpitisha yeye kugombea uraisi. Kana kwamba haitoshi kampeni za mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA zinafadhiliwa kwa asilimia kubwa na Edward Lowassa na Marafiki zake. Maana yake ni kwamba watakapoanza kutaka kudhibiti utekelezaji wa mradi wake wa kunenepesha mitaji ya mafisadi waliofadhili safari yake kuingia Ikulu atawauliza swali dogo tu mnategemea nitalipaje madeni ya kampeni za uchaguzi? Kwa kuufahamu ukweli wa mkataba kati ya viongozi wa CHADEMA/UKAWA na Edward Lowasa lakini pia kwa madaraka makubwa atakayokuwanayo kama raisi wakati huo hawataweza kumdhibiti. 

Wapo wanaoweka imani kwenye uwezekano wa kubadilisha katiba ili pamoja na mambo mengine kupunguza madaraka ya raisi. Ufahamu wangu juu ya uwezo wa watu binafsi kufanya mabadiliko na kiwango   cha mabadiliko huchangiwa sana na historia ya muhusika na kundi/kizazi/tabaka anakotoka. Kwa mfano mara nyingi wazee ni hawapendi madiliko hasa yale yanayokinzana na matakwa yao. Simuoni mzee Edward Lowasa katika umri wake eti anatakakuleta mabadiliko ya kasi hasa ukizingatia yeye ukiacha majanga ya kisiasa aliyokutana nayo yupo katika tabaka la matajiri.

Dkt. John Pombe Magufuli na Mabadiliko ndani ya CCM

Watanzania wengi bila kujali itikadi na nafasi zao wamewahi ama  kusikia, kukiri, au kuthibitisha kwa vitendo kuwa  Dkt. Magufuli ni kiongozi shupavu, mwenye dira na uwezo wa kubadili mifumo  na utendaji  katika sekta mbalimbali. Hii inathibitika wazi pale watu wanapoamua kufanya tathmini sahihi ya utumishi wa kiongozi huyu kwa kuangalia  utendaji wake na mafanikio yaliyofikiwa na sekta au taasisi ambazo Dkt Magufuli amewahi kuzisimamia.  Hapa ni vigumu kupinga ukweli kwamba Dkt magufuli ndiye aliyeleta mabadiliko na maboresho katika sekta ya Ujenzi hususani wa miundo mbinu ya barabara.

Maeneo mengine ambayo Dkt Magufuli ameacha  mbegu ya maboresho ni  katika sekta ya ardhi pamoja na ile ya mifugo na uvuvi  licha ya kuzitumikia sekta hizi kwa muda mfupi kabla ya kurejea tena kwenye sekta ya Ujenzi. Taswira ya sasa ya sekta ya ujenzi ambayo sio tu kwamba ina mifumo bayana na thabiti licha ya changamoto kadhaa, sekta hii inasimamiwa na taasisi madhubuti ambazo zinalenga kutafsiri dira na mikakati ya sekta katika uhalisia na vitendo.

Akiwa Naibu wa waziri wa ujenzi katika serikali ya awamu ya tatu, ni Dkt. Magufuli ndie alibadilisha mfumo wa kutegemea wahisani kwa asilimia miamoja katika sekta ya ujenzi wa barabara.Mfumo huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Ujenzi, takribani asilimia sabini (70%) ya miradi yote ya ujenzi wa barabara inchini inajengwa kwa kutumia fedha za serikali. Ni asilimia thelasini pekee ya miradi yote ya ujenzi inafaddiliwa na wahisani. Swali la kujiuliza ni je nini kimefanikisha utelekezaji wa mfumo huu? Hapa ndipo unawezakuona uwezo na uzoefu wa kiongozi katika kubadili mfumo kwa kujenga taasisi zinazotakiwa ili kusimamia na kuendeleze mfumo.  Ni Dkt. John Pombe Magufuli ndie alieanzisha harakati za maboresho katika usimamizi, utekelezaji na uendelezaji wa sekta ya ujenzi nchini.

Kiongozi huyu amesimamia kuanzishwa kwa taasisi kadhaa muhimu katika sekta ya ujenzi ambazo ni pamoja na Mfuko wa barabara (Road Funds) ambao mapato yake yameongezeka kutoka shilingi bilioni 73.08 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 751.7 mwaka 2014/15. Taasisi nyingine ni pamoja na Wakalawa barabara (TANROADS) inayosimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja. Pia zipo taasisi kama Wakala wa Majengo Tanzania (TBA); Board ya Usajili wa Wahandisi (ERB); Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRD na Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB). Taasisi zote hizi zinalenga kutelekeza majukumu tofauti lakini yanayotegemeana katika ustawi wa sekta ya ujenzi. Hapa unaweza kuona mantiki ya ujenzi wa mfumo sio hisia wala propaganda.

Mifano hii michache ni kielelezo cha uzoefu, dhamira na upeo, na umakini wa kiongozi katika  kuchambua, kuamua na kusimamia mambo miradi ya maendeleo. Ni mgombea Dkt. John Pombe Magufuli ndie ambae amembanua wazi dhamira na mikakati yake kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Huyu sio tu kwamba anasema dhahiri kwamba  atafungua mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi lakini pia uzoefu katika wizara alozitumikia una akisi dhamira hii.


Ni vigumu kupinga ukweli kwamba hatua ambayo nchi yetu imefika inahitaji kiongozi ambae sio tu anapenda kusema kile ambacho watanzania wanapenda kusikia bali kile watanzania wanachohitaji yaani Kiongozi mwenye uwezo wa kurejesha uadilifu, uaminifu na uchapa kazi katika sekta zote.

NI SAWA TUNATAKA MABADILIKO: JE NI YA MAGUFULI AU LOWASSA??


Tutafakari kwa Hoja na Sababu

Wagombea Urais wa CCM, Dr. John Magufuli na mwenzake wa CHADEMA Ndg Edward Lowassa wanakubaliana jambo moja kubwa: Haja ya kuwa na mabadiliko katika nchi yetu. Wagombea wote wameahidi kila mmoja kuwa iwapo atashinda ataleta mabadiliko. Tulinganishe sasa na kupima aina ya mabadiliko ambayo yanaweza kutokea iwapo mmojawapo atachaguliwa kuwa Rais wa nchi yetu.

Kulingana na historia ya utendaji wake katika wizara alizokabidhiwa na ahadi anazotoa mgombea wa CCM, Dr. John  Magufuli, chini ya Urais wake inaonekana  utawala wa sheria na nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma itatamalaki.  Magufuli anajulikana zaidi kwa Watanzania kuwa ni mtu anayesimamia sheria hata pale zinapogusa maslahi ya wakubwa zake. Watanzania watakumbuka jinsi Magufuli alivyoweza kurudisha magari yaliyokuwa yameporwa kinyemela  na vigogo wa serikali enzi za utawala wa Benjamin Mkapa.

Kwa upande wa  Ndg. Edward Lowasa, iwapo  atachaguliwa kuwa Rais, kuna uwezekano mkubwa kukawa na utawala unaotegemea hisia za Rais na ‘marafiki’ zake  badala ya utawala wa sheria. Utendaji wake wa nyuma unaonyesha wazi kuwa Lowassa kama kiongozi ni mtu anayeamini matashi yake binafsi bila kuzingatia utawala wa sheria. Watanzania watakumbuka kuwa March 2006, akiwa waziri mkuu, Lowassa alimfukuza kazi mhandisi wa Manispaa ya Temeke bila kumpa nafasi ya kujitetea na tena mbele ya waandishi wa habari na kundi la wananchi waliokuwepo katika tukio la kuporomoka jengo la Chang’ombe Village.  

Hivi karibuni, wakati anazindua kampeni zake, Lowassa alitoa ahadi kuwa ikiwa atashinda atamuchia huru Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya aliyefungwa maisha jela kwa kwa kosa la  kubaka na kulawiti watoto katika hukumu iliyotolewa na mahakama ya hakimu mkazi kisutu mwaka 2004. Kesi hiyo ilipelekwa katika mahakama ya rufaa mwaka 2010 na Mahakama ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya chini. Tena, mwaka 2013, jopo la majaji wa mahakama ya rufaa watatu likijumuisha Jaji Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Msati walifanya mapitio ya mahakama hiyo na kuwaona wafungwa hao kuwa wana hatia.

Ikumbukwe kuwa sheria za Tanzania zinamyima Rais mamlaka ya kusamehe watu waliofungwa kwa makosa ya kubaka na kulawiti. Kwa kutamka kuwa atawachia wazi wafungwa hao,bila ya kusema chochote juu ya wale watoto waliolawitiwa na kubakwa na haja ya kufuata utawala wa sheria nchini ni dhahiri kuwa katika utawala wa  Lowassa utawala wa sheria utawekwa kando na matashi ya watawala ndio yatakuwa yanaongoza nchi. Hili linadhibitishwa na ahadi nyingine  ya  Lowassa  kuwa  akiwa Rais, watuhumiwa wa kesi za ugaidi waliokamatwa huko Zanzibar wataachiwa huru kwa amri ya Rais. Ikumbukwe kuwa kwa sasa dunia iko kwenye vita dhidi ya ugaidi na ugaidi ni hatari kubwa na thahiri kwa maisha ya  wananchi na mali zao.

Wagombea wote wameahidi kupambana na ufisadi na rushwa iwapo watachaguliwa kushika nafasi ya Urais. Magufuli ameahidi wazi kuwa ataleta  mabadiliko katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia masuala hayo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa rushwa itaweza kudhibitiwa katika utawala wake ukizingatia kuwa katika harakati zake zote hakuungwa mkono na genge la mafisadi kama ilivyozoeleka kwa siasa za CCM tangu mwaka 2005 ilipotekwa na genge la wanamtandao.

Hali hii itamfanya aweze kutawala bila kuwa na  deni la kulipa fadhila kwa mtu yeyote. Uzoefu wa siku za karibuni unaonyesha kuwa rushwa na ufisadi mkubwa unasababishwa na kujaza ‘marafiki’ katika nafasi muhimu za maamuzi. Kujaza marafiki hasa waliokufadhili kwenye harakati za uchaguzi kunafanya mifumo ya uwajibkaji katika nchi iwe na ganzi ya kufanya kazi dhidi ya marafiki hao.

Kwa upande wake Lowassa hajaeleza atafanya nini bayana katika kupambana na rushwa zaidi ya kusema atashughulikia rushwa. Kama ambavyo ilibainishwa na waziri mkuu mstaafu na mpambe wa Lowassa katika harakati za Urais, Fredrick Sumaye,  katika viwanja vya jangwani, Lowassa ndiye mwasisi wa ‘mtandao’ uliomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005. Kundi hili lilimjumisha pia Rostam Azizi na Laurence Masha ambao leo hii ndio pia ndio wanaongoza mikakati ya Lowassa. Rushwa katika mikataba ya aina mbalimbali na hata ukwapuaji wa fedha za umma kupitia maskandali mbalimbali kama EPA, Richmond  na Dowans ulifanyika kama njia ya kulipa deni la fadhila wakati wa uchaguzi. Kama tulivyogusia hapo juu, ni vigumu kuchukua hatua dhidi ya marafiki na maswahiba.

Baada ya CCM kujikomboa kutoka katika makucha ya wanamtandao kwa kuwaondoa wagombea wa kundi hili akiwemo Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea Urais kupitia chama hicho, kundi hilo limeweza ‘kuiteka nyara’ CHADEMA na kupitia kwake vyama vikuu vya upinzani kupitia UKAWA. Lowassa amesema waziwazi kuwa fedha anazogawa kwa wananchi mbalimbali zinatokana na ‘marafiki’ zake. Kwa hiyo, kama atachaguliwa, utawala wa Lowassa utaendeleza utawala wa wanamtandao, na watanzania watarajie kushamiri kwa ufisadi nchini kwa sababu tulizoeleza hapo juu.

Watanzania watakumbuka kuwa kile kinachoonekana kuwa ni ushabiki wa kupindukia kwa Lowassa hauna tofauti na ushbiki uliokuwepo mwaka 2005  kwa Kikwete. Hii inatokana na ukweli kuwa kundi linaloratibu na kuongoza kampeni za Lowassa ni lilile lililofanya kazi hiyo mwaka 2005. Tayari, kuna taarifa zinazosema kuwa wanamtandao wameshagawana nafasi muhimu za uongozi na mikataba katika maeneo manono kama bandari, madini na vitalu vya gesi na mafuta iwapo watafanikiwa kuiteka dola kupitia uchaguzi.

Magufuli ameahidi kuwa ataleta mabadiliko katika utendaji wa watumishi wa umma kwa kuweka mifumo imara ya uwajibikaji. Watu walio karibu na Magufuli wanasema kuwa Magufuli ameahidi kuwa akiwa Rais atawekeana mikataba ya utendaji kazi (Perfomance contracts) na mawaziri wake ambapo kila waziri ataingia kama yeye binafsi na akishindwa kufikia malengo atawajibishwa kwa kuondolewa madarakani. Magufuli ameahidi pia kuwa mafisadi watakaotiwa hatiani watafilisiwa mali zao. 

Kwa upande wake Lowassa amesema kuwa akiingia madarakani atabadilisha mfumo wote wa nchi. Hii ina maana kuwa Lowassa akiwa Rais, taasisi za utawala kama vile Polisi, Jeshi, Utumishi wa Umma na vyombo vingine vitafumuliwa na kuundwa upya na kuwekwa watu wapya. Muhimu hapa ni kukubaliana  kuwa siyo rahisi kwa jambo hilo kufanyika kwa kuwa kama ilivyo duniani kote yeyote atakaye shinda atalazimika kufanya kazi na vyombo hivyo. Mabadiliko yeyote ya utendaji wa vyombo hivyo vitategemea na hulka, tabia na haiba ya Rais. Hakika duniani kote mabadiliko katika nchi huletwa kwa vyombo hivyo kufanya kazi zao ipasavyo kutokana na uongozi na usimamizi dhabiti wa mkuu wa nchi.

Hitimisho


 Haya ni baadhi ya mabadiliko yanaweza kutokea iwapo mmoja wa wagombea wetu watachaguliwa katika nafasi ya Urais. Mabadiliko haya yanaonyesha wazi kuwa uchaguzi ni muhimu sana kwa mustakabali wetu kama mtu mmoja mmoja na kama Taifa. Kwa sababu hiyo, ushabiki na uungwaji mkono wa wagombea lazima uzingatie faida na hasara zake kwa nchi na kwetu binafsi. Ni wakati wa kuwahoji na kuwatathimini wagombea wetu ili siku ya upigaji kura tisije tukafanya kosa litakalotuathiri sisi na vizazi vyetu.  Tathmini hiyo ni muhimu kwa kujua kuwa utendaji kazi wa Rais huakisi na kuathiri utendaji kazi wa serikali na taasisi zote zilizo chini yake. Yaani Rais akiwa fisadi serikali na vyombo vyote chini yake vitakuwa vya kifisadi. La, Rais akiwa mwadilifu na mchapakazi na serikali yake itakuwa vivyo hivyo.