Saturday, April 23, 2016

SALAMU ZANGU KUTOKA MUSOMA

                                Hapa nikila kiapo cha nafasi ya Madaraka ya Mkuu wa Wilaya
                                Hapa nikisaini kiapo
                                Hapa nikitoa neno kwa umma wa wana Musoma na watendaji wa Halmashauri
                                                Picha ya pamoja, Mkuu wa Mkoa Mhe. Magesa Mulongo na Wakuu wa Wilaya wenzangu wa Mkoa wa Mara

SALAMU ZANGU KUTOKA WILAYA YA MUSOMA

Ndugu zangu wapendwa na watanzania, nawasalimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa kibali. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini, kunipa heshima na dhamana ya kuwa Msaidizi wake katika nafasi ya madaraka ya utumishi na uongozi kama Mkuu wa Wilaya ya Musoma.

Wilaya ya Musoma ina maeneo mawili ya kimamlaka kwa maana ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Musoma na yenye zaidi ya wakazi 360,000. Dhamana hii niliyopewa na Mhe. Rais, inanilazimu kuhakikisha ustawi wa watanzania waishio Wilaya ya Musoma unaimarika, dhamana hii inakwenda sambamba na kuhakikisha Serikali (Kuu, Manispaa na Halmashauri) tunaenenda katika namna ambayo inakuza na kuongeza tija kwa maisha ya wananchi tuliopewa dhamana ya kuwahudumia na kuwaongoza.

Nimeupokea Uteuzi wa Mhe. Rais kwa furaha na heshima kubwa, Nimewaahidi wakazi wa Musoma kuifanya Musoma MFANO wa Kuigwa katika kila nyanja, ni lazima tushirikiane, tushauriane, tusaidiane na kuelekezana katika namna ambayo ni ya UWAZI na inazingatia misingi ya UKWELI, HAKI, UMOJA, UWAJIBIKAJI na UADILIFU.

Kwa kipindi cha mwezi hivi nitapotea ili kujifunza na kuielewa Musoma, kuwafahamu na kuwajua watumishi wenzangu katika Wilaya ya Musoma.

Hapo awali nalipata heshima na fursa ya kuaminiwa dhamana ya uongozi katika ngazi ya Kitaifa kama Kamishna wa Tume ya Katiba. Kazi ya Ukamishna wa Tume ya Katiba, ilinipa fursa ya kuiona Tanzania, kuielewa Tanzania, kuijua misingi ya kuanzishwa nchi yetu. Kazi ya Katiba ilinipa fursa ya kutembelea Nchi nzima na kuzijua kero, changamoto, shida, manung'uniko, lakini pia nilijua fursa adhimu mbalimbali zilizopo katika nchi yetu. Nalipata bahati ya kukaa Mkoa wa Mara kwa miezi miwili ikiwemo Wilaya ya Musoma. Kazi ya Katiba ilinipa fursa ya kuiona Tanzania katika jicho la Uongozi wa Nchi lakini pia kusikiliza matakwa, matamanio na matarajio ya wananchi wenzangu wa Tanzania. Nilipata fursa ya kufanya kazi na viongozi waliopo madarakani katika ngazi ya Taifa na viongozi wastaafu na hakika nimejifunza mengi na ninaendelea kujifunza mengi zaidi kutoka kwa viongozi hawa. Wamenifunza juu ya Misingi ya Taifa, Katiba, Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo, Utamaduni na desturi za Serikali na Mamlaka za Nchi.

Mheshimiwa Rais ameniamini na kuniongeza fursa ya kuifahamu Nchi yangu kwa kukaa na wananchi wetu kila siku kama mtu mwenye nafasi ya madaraka (dhamana) ya kushirikiana na wananchi kutatua changamoto zao na kuhakikisha dhamira na ndoto ya Mheshimiwa Rais ambayo ameelekezwa na watanzania inatimia na kuwa hakika kweli.

Mimi nahisi kupendelewa kipekee, Mkoa wa Mara na hasa Musoma ndio Muasisi wa Taifa hili alizaliwa na kukulia, lakini pia wazee wangu wa nguvu ninaowapenda kupitiliza (hawa ni kama nimpendavyo Mzee Polepole) wamezaliwa katika Mkoa huu, Mzee wa Nguvu Mhe. Joseph S. Warioba, Mzee wa Nguvu Joseph W. Butiku na Balozi Marwa. Hili linanipa mguso wa kipekee sana kujituma na kuuishi utume wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa kujitoa maisha yake kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Kwa hili Nakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipendelea 
Kama kazi ya Tume ilikuwa Darasani, Hapa niko Maabara, kufanya majaribio na utekelezaji wa elimu niliyoipata shule na kutoka kwa malezi na maongozi ya viongozi ambao nimepitia mikononi mwao.
Mpaka sasa nimetambua hakika hakuna kazi nyingine kwa wakati huu ambayo itaniweka karibu na wananchi na kuwaelewa kama nafasi ambayo Mheshimiwa Rais amenipa dhamana ya kumsaidia.
Kwa msaada wa Mungu hakuna kero ambayo hatutaitatua, hakuna changamoto ambayo hatutafanyia kazi na hakuna kero ambayo hatutaishughulikia.

Nitaendelea kutumia fursa hii kuendelea kujenga uwezo wa vijana wenzangu katika uongozi maana sasa tumepata "kisa mafunzo"

Kipekee nimshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Magesa Mulongo, ananipa ushirikiano, maongozi, maelekezo, ushauri na amenipa uhuru wa kutenda na kujiamini au kimombo "to exercise leadership". Yeye ana upeo Mkubwa na Uzoefu, na hakika uwepo wake Mkoa wa Mara unatosha kutupa hamasa ya kumsaidia kufikia Mara ambayo ni Mkoa wa Mfano kwa Tanzania.

Niwashukuru Wakuu wa Wilaya wenzangu wa wilaya zote za Mkoa wa Mara, upendo mlionionesha mpaka leo hakika umenifanya nisiikose (nisi-imiss) Dar es Salaam, ninyi ndio ndugu zangu kiutumishi na kiuongozi, nitashirikiana nanyi, nitajifunza kwenu na nitawaomba ushauri kila mara.

Kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Musoma, nina maelekezo ya kuwahudumia kwa kauli mbiu na falsafa ya HAPAKAZITU!!

Mungu awabariki

Mimi Rafiki yenu Mpendwa