Saturday, April 25, 2015

MIAKA 51 YA MUUNGANO: HUU NI WAKATI MUAFAKA WA KUWEPO HAKI ZA WANAWAKE KIKATIBA

Katiba Inayopendekezwa imefuta misingi ya usawa kati ya wanawake na wanaume

Hivi karibuni nilipata wasaa wa kuonana na watetezi wa haki za binadamu, watetezi hawa wanawake na wanaume kutoka asasi za kiraia walinialika kujadiliana nao juu ya mchakato wa Katiba. Katika vikao viwili tulikaa pamoja, sote tulikubaliana kila mwenye uelewa au msimamo kuhusu Katiba Inayopendekezwa apewe fursa kuusema na asizongwe. Wote tulikubaliana kwamba utofauti wa mawazo ni afya kwa hakika na hasa pale wote wenye misimamo wanapojenga hoja zao kwa sababu za msingi na zenye mashiko.

Nilijielekeza kuelewa hoja zao, hasa za wale ambao wanasema Katiba Inayopendekezwa imelinda haki za wanawake, nilisikiliza kwa dhamira ya kuelewa na kujifunza kutoka kwao. Baada ya mjadala niligundua kwamba wanawake walikuwa na hoja kadhaa ambazo kwa maelezo yao zilifanikiwa kuingia katika Katiba Inayopendekezwa, na kwa mantiki hiyo wanawajibika kuipigia chapuo Katiba Inayopendekezwa.

Kabla ya kufafanua namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imelitizama suala la haki za wanawake ni vema nikagusia kwa sehemu dhana ya Mahitaji ya Kimkakati ya jinsia au kwa kiingereza “Strategic Gender Needs”.

Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia na Katiba

Mahitaji ya kimkakati ya jinsia au “Strategic Gender Needs” ni yale ambayo wanawake na wanaume huyahitaji ili kubadilisha nafasi zao katika jamii, mahitaji haya yanajumuisha mgawanyo wa madaraka kijinsia, mamlaka na udhibiti wa rasilimali, fursa sawa kwa wanawake na wanaume, haki za kipato sawa kwa kazi sawa kati ya wanawake na wanaume, Mageuzi ya kikatiba, kisheria na kimfumo ambayo yanatambua nafasi muhimu ya wanawake pamoja na wanaume kwa usawa katika kuleta maendeleo ya jamii. Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ndio humlinda mwanamke dhidi ya utegemezi, umasikini, kunyanyaswa, unyonyaji au “exploitation” na kuwekwa nje ya mfumo wa kufanya maamuzi.

Mara zote Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia kwa maana ya “Strategic Gender Needs” ndio huwa ufunguo kwa Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au kwa kiingereza “Practical Gender Needs”. Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au “Practical Gender Needs” hujumuisha yale mambo ya kawaida na yanayoshikika ambayo mtu wa kawaida huyahitaji wakiwemo wanawake. Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia yanajumuisha mahitaji ya msingi katika maisha ya siku hadi siku kama vile upatikanaji wa maji, huduma za afya na ajira. Kupatikana kwa mahitaji ya kawaida ya jinsia kwa mwanamke huwa hayamwondoi mwanamke katika nafasi yake ya utegemezi, unyonyaji na kutokuwa maamuzi juu ya rasilimali zake mwenyewe.

Swali langu muhimu kwa wanawake wote, dada zangu, shangazi zangu na mama zangu wote wenye mapenzi mema na kuona utu wa mwanamke unaheshimiwa, haki za wanawake zinatolewa, zinatunzwa, zinahifadhiwa na kuheshimiwa, Je Katiba Inayopendekezwa na bila kuweka misimamo ya kisiasa imezingatia Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia au “Strategic Gender Needs”?

Katiba Inayopendekezwa inapaswa kupimwa ni kwa kiwango gani imetizama na kujumuisha Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo kwayo mahitaji ya kawaida ya jinsia hupatikana. Tunapoweza kuhakikisha uwepo wa mahitaji ya kimkakati katika Katiba, huu huwa msingi wa kuona utolewaji haki za wanawake.

Kama Katiba Inayopendekezwa imejaribu kuweka Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia pasina kuweka misingi kwa mahitaji ya kimkakati ni kazi bure kwasababu haki za wanawake zitabakia kuwa kiini macho. Kama haki za wanawake hazikubainishwa ipasavyo katika Katiba Inayopendekezwa bado mwanamke wa Tanzania ataendelea kuwa tegemezi, fukara na ushiriki wake kwenye nyanja za utoaji maamuzi zitabakia kutegemea utashi na fadhila kutoka kwa viongozi wa juu.

Tuitazame Katiba Inayopendekezwa kwa jicho la Rasimu ya Warioba

Rasimu ya Warioba Katiba Ibara ya 47(1)(b) ilisema “Kila mwanamke ana haki ya kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili”. Rasimu ililenga kujenga msingi wa kumpa mwanamke udhibiti wa rasilimali zake na kumlinda na ukatili ambao huja kama sehemu ya kumpora rasilimali alizo nazo. Mfano mzuri ni mwanamke wa kijijini na mkulima, anayelima kwa jembe la mkono na kupata mazao yake, je ni mara ngapi mwanamke huyu huwa na mamlaka juu ya wakati gani mazao yatauzwa, na yatauzwa kwa bei gani na pesa ikipatikana je mwanamke huyu huipangia matumizi yake mwenyewe?

Ukienda kwenye Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 masharti ya 47(1)(b) kutoka katika Rasimu yamefutwa, huwa najiuliza msingi wa kufuta masharti yale ya Rasimu ni upi?.

Ukiendelea kusoma Ibara ya 47(2) ya Rasimu ya Warioba inasema “Mamlaka za nchi zitaweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara hiiikiwa ni pamoja na kukuza utu, heshima, usalama na fursa za wanawakewakiwemo wajane”. Ibara hii ilikuwa ina lengo la kutoa maelekezo kwa mamlaka za nchi kutekeleza masharti yaliyoainishwa katika Ibara hii. Ieleweke pia masuala ya maendeleo ikiwemo suala la jinsia kwa asili ya Nchi yetu sio jambo la Muungano.

Kwa uelewa huu ndio maana Rasimu ya Warioba iliona Katiba itoe maelekezo kwa Mamlaka za Nchi ambazo ziko tatu ambazo ni (i) Mamlaka ya Mambo ya Muungano ambayo chombo cha utendaji ni Serikali ya Muungano, (ii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na (iii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara au Tanganyika. Warioba alijua kwamba kuna masuala ya Haki za Wanawake ambayo kila Mamlaka ingeweza kuyashughulikia kwa sehemu, nafasi na mamlaka yake. Huu ulikuwa msingi mkubwa wa kuhakikisha tunalinda Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo yangepelekea kutolewa kwa haki za wanawake raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanapatikana Tanzania Bara na Zanzibar.

Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 imeyafuta na hivyo haina masharti ya Rasimu yaliyomo katika Ibara ya 47(2) ambayo ukiacha kutoa maelekezo ya utendaji lakini pia kitaalamu ni masharti wezeshi au kwa kiingereza huitwa “enabling provision”. Najiuliza dhambi ya masharti yale ambayo baada ya kuwasikiliza Wananchi na hasa wanawake na zaidi wanawake wajane walio ona ingefaa yawepo kikatiba.

Ili ujue Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanawake wanakubwa sehemu ya wanufaikaji wa Katiba Mpya na Bora na inayotokana na maoni ya Wananchi. Ukisoma Ibara ya 54 inaeleza kuhusu usimamizi wa haki za binadamu na ukiendelea na kusoma Ibara ya 54(1)(a) inaeleza “Katika kutafsiri masharti ya Sura hii ya Haki za Binadamu, Mahakama au chombo kingine chochote cha kufanyauamuzi kitazingatia mambo yafuatayo:- haki ya usawa, utu na uhuru wa mtu binafsi”. Kwa kiingereza haki ya usawa ndio huitwa “equality principle”, kwamba tunapozitoa haki, lazima tuangalie je wanawake wapo? Je wanaume wapo?

Na neno “Utu” ni kuhusu masikini na matajiri wa Taifa letu, tunapogawana keki ya Taifa je nani waanze kula, matajiri au masikini? Rasimu ya Warioba ilipendekeza katika Katiba misingi hii ya kuzingatiwa, Katiba Inayopendekezwa imeifuta yote katika Ibara ya 65, na ukiisoma Ibara hii utagundua haina masharti ya 54(1)(a). Najiuliza dhambi ya masharti haya ilikuwa nini? Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia hayawezi kuwapo kama msingi huu umefutwa.

Rasimu ya Warioba katika Ibara yake ya 113 ilieleza bayana kwamba uwakilishi katika chombo cha kutunga sheria kwa maana ya Bunge uwe nusu wanawake na nusu wanaume. Warioba alitizama mbali kwamba kwa namna ambavyo jamii yetu imejengwa katika mfumo dume ufike wakati wa kubadili fikra na kuwa na chombo cha kutunga sheria ambacho kinazingatia uwakilishi unaojengwa katika kuheshimu misingi ya usawa wa kijinsia.

Warioba alijua kwamba wakulima wengi nchini ni wanawake, alijua pia kwamba wahanga na wanufaikaji wa mfumo wa afya nchini ni wanawake na kwa mantiki hiyo watu ambao wako kwenye sehemu na nafasi nzuri ya kuwasilisha mawazo ya watanzania ni wanawake sambamba na wanaume. Na sisi kama watu ambao Rais alitupa dhamana ya kufanya kazi na Mzee Warioba tulijiridhisha kwamba hata katika Bunge wanaolala wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea ni wanaume na sio wanawake.

Warioba ni kama alibashiri kwamba iwapo tungekuwa na Bunge ambalo lingekuwa na uwakilishi uliosawa kati ya wanawake na wanaume ndani ya muda mfupi watanzania wangetambua wanawake wana uwezo tena hata zaidi ya wanaume na ingewajengea imani kwamba hata uongozi wa nchi ungeweza kuaminiwa kwa mwanamke.

Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 129 imefuta masharti yaliyokuwemo katika Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 113(3) yaliyosema “Katika kila Jimbo la Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamme”. Huu ulikuwa msingi wa kuhakikisha kuna usawa wa jinsi na jinsia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Sijaelewa msingi wa kufutwa kwa msingi huu ambao ungepelekea kuzingatiwa kwa asilimia 100 kwa Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo yangewakomboa mamilioni ya wanawake ambao wanakumbana na unyanyasaji uliojengwa fikra za wengi katika Taifa letu.

Ukisoma Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 193(3)(b) ilizungumzia majukumu ya Tume Huru ya Uchaguzi kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuna uwakilishi unaozingatia jinsi. Tafsiri ya Ibara hii ni kwamba kama Tume Huru ya Uchaguzi ikija katika Jimbo na hakuna mgombea mwanamke basi ujue uchaguzi hakuna na vivyo hivyo kinyume chake. Ukiisoma Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 220(3) utagundua ni kipengele cha “uwakilishi unaozingatia jinsi” ndicho pekee kilichofutwa. Nawauliza nyote dhambi ilikuwa nini hata kufuta jukumu hili la Tume Huru ya Uchaguzi?


Ni miaka 51 ya Muungano, unadhani bado wanawake wanatakiwa kupewa nafasi za uongozi kwa mbinu za miaka ya 70, kwa maana ya viti maalum na kwa kusubiri utashi na fadhila za viongozi wakubwa? Je wanawake hawastahili haki sawa na wanaume? Nimeandika nikiwa kama mwanaume anayethamini nafasi muhimu ya wanawake katika ujenzi wa Taifa letu na anaye amini kwamba Taifa hili haliwezi kupiga hatua kama tutaendelea kuwahadaa wanawake, wapenzi wetu, dada zetu, shangazi zetu, mama zetu na bibi zetu. Niwatakie Miaka 51 ya kusherehekea Muungano wetu. Muungano wa Haki na Heshima Udumu Milele.!

Saturday, April 18, 2015

KUHUSU MAADILI YA VIONGOZI, KATIBA INAYOPENDEKEZWA IMEPUUZA KILIO CHA WENGI JUU YA UADILIFU WA VIONGOZI

Mhe. Rais na Makamu wa Rais wakipata picha ya pamoja na wajumbe wapya wa Tume ya Maadili
Kudhoofisha maadili ya uongozi ni sawasawa na madaraka pasina udhibiti

Maadili na uwajibikaji wa viongozi wa Umma

Tanzania, kama ilivyo nchi nyingine za Kiafrika, ina changomto za kiuwajibikaji na wananchi wametoa mawazo yao wakati wa mchakato kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya. Wananchi walizungumzia changamoto za uwajibikaji kwa viongozi wa umma na wakatoa sababu na mantiki ya kuunda mfumo thabiti wa uwajibikaji.

Uwajibikaji ni dhana pana, inahusu utaratibu endelevu wa udhibiti na uwekaji wa mipaka katika matumizi ya madaraka. Vilevile, ina maana ya kuwepo utaratibu wa kuwalazimisha wenye madaraka kufanya wanayotakiwa kuyafanya na kuacha kufanya wasiyotakiwa kuyafanya na ya kujibu maswali au hoja zinazohusiana na matumizi ya madaraka aliyopewa. Kwa mantiki hii, uwajibikaji unamaanisha pia kipengele cha adhabu kwa wale wanaotumia madaraka ya umma vibaya. Kwa hiyo, dhana ya uwajibikaji inahusu masuala yafuatayo: kwanza, uwepo wa mfumo wa udhibiti wa madaraka; pili, uwepo wa utaratibu wa kuwalazimisha wale walio na madaraka kutekeleza wajibu wao na kuwazuia kukiuka wajibu wao; na tatu, kuwepo utaratibu wa kuwaadhibu wenye madaraka pale wanapokosea.

Kwa upande mwingine, maadili maana yake ni kanuni au misingi inayoelekeza ni kitu gani kibaya au kisichofaa au kizuri au kinachofaa. Misingi hii inaweza kujengwa katika utamaduni wa jamii husika. Vilevile, misingi hiyo inaweza kuandikwa na kwa kanuni ya maadili. Kwa maneno mengine na hasa kwa hali ilivyo katika nchi yetu sasa na hata kwa vizazi vijavyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka masharti mahususi ya maadili ya viongozi katika Katiba kama sehemu ya kujenga utamaduni wa kikatiba wa kuendelea kudhibiti matumizi ya madaraka.

Kuna aina nyingi za uandishi wa Katiba, moja ni ile ambayo kitaalamu huitwa “instrumentalist approach” Katiba hizi huwa hazijipambanui sana, kwa asili yake huwa zinaweka misingi na kujenga taasisi, huwa fupi na maeneo mengi huja kufanyiwa kazi na sheria zitakazotungwa na Bunge. Aina ya pili ni ile inayoitwa “Programmatic approach” ambayo huwezesha uandishi wa Katiba za mfano wa Katiba ya uhuru wa Taifa la Ireland. Ni Katiba ambayo huweka bayana ndoto, malengo makuu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali na sera za kitaifa ambazo kwa ujumla wake katika Katiba hutanabaisha dira ya nchi.

Katiba ambazo ni programmatic huweka ndani yake pia masharti mahususi juu ya misingi ya Taifa, misingi juu ya maadili ya Taifa, misingi ya maadili ya viongozi sambamba na utaratibu wa uwajibikaji kwa viongozi wa umma. Moja ya changamoto kubwa katika taifa lolote lile ni namna gani Taifa linaweza kuwa na mfumo wa kikatiba ambao unawazuia viongozi wa Serikali kuyatumia madaraka ya umma vibaya.

Mwanafalsafa wa Uskochi David Hume katika Karne ya 18, alipata kunena haya, “tunapotengeneza mfumo wa Serikali katika Katiba na kuweka udhibiti na urari wa madaraka ni vizuri kuzingatia kuwa kila mtu siyo mwaminifu na kwamba binadamu yeyote katika matendo yake mengi huwa hana malengo mengine isipokuwa kutafuta manufaa binafsi. Hume anaendelea kusema ni lazima kuweka utaratibu wa kuyadhibiti madaraka hayo ili mtu huyo aweze kutoa ushirikiano wake katika masuala ya umma. Anaonya kuwa tusipofanya hivyo tutajisifu kuwa tuna katiba lakini kumbe hatuna usalama wa mali na uhuru wetu isipokuwa tu kwa matakwa ya watawala au viongozi wetu, na jambo linapotolewa kwa utashi wa viongozi na hasa katika mambo ya msingi kama hatutakuwa na usalama kabisa. Kwa ujumla, mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa madaraka wanayopewa viongozi ni lazima yadhibitiwe kikatiba; haifai kumwamini mtu kwa sababu ni vizuri kila mtu achukuliwe siyo mwaminifu au kwa kimombo anasema “every man ought to be supposed a knave”.

Maadili katika Rasimu ya Warioba ukilinganisha na Katiba Inayopendekezwa

Rasimu ya Katiba Toleo la Pili ilijaribu kwa mara ya kwanza baada ya marekebisho makubwa yaliyofanyika mwaka 1984 kwa Katiba ya Mwaka 1977 yaliyoigeuza kwa sehemu Katiba ya Mwaka 1977 kuwa “programmatic”. Licha ya marekebisho hayo bado Katiba ya mwaka 1977 haikuwa imejipambanua ipasavyo ili kuendana na mahitaji ya wakati, yaliyohitaji misingi ya maadili na uwajibikaji pamoja na uanzishwaji wa taasisi huru za kusimamia maadili na uwajibikaji wa viongozi wa umma.

Wengi wenu mtakuwa mlishuhudia kile kilichokuja kuwa maarufa miongoni wa mitandao ya kijamii kama sinema ya Baraza la Maadili. Iliitwa sinema kwasababu watuhumiwa waliopata kuhojiwa katika baraza letu la Maadili chini ya Jaji Msumi hawakuonekana kuitetemekea Mamlaka ile ambayo ndio ina dhamana ya kuwawajibisha viongozi wanaokwenda kinyume na maadili ya uongozi. Hata pale waandishi walipomhoji mwenyekiti wa Baraza juu ya hatima ya viongozi wale, aliishia kusema wakimaliza kazi watapeleka taarifa kwa mamlaka za juu. Swali ambalo wananchi wamekuwa wakijiuliza ni vipi pale ambapo wanaohojiwa ni viongozi na watumishi kutoka mamlaka ya juu? Je utekelezwaji wa mapendekezo ya Baraza utazingatiwaje katika mazingira hayo?, haya si maneno yangu ninayasikia huku na huko.

Tunaposema kwamba Katiba Inayopendekezwa imetupilia mbali masharti mahususi kuhusu maadili ya uongozi, hebu tutizame mfano huu;- Ibara ya 15 ya Warioba ilisema “Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli zakiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuriya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitiakwa Katibu Mkuu wa Wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikaliinayohusika, akiainisha: (a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa zawadi; na
(d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo”. Kifungu cha pili cha Ibara hii kinasema “Neno “zawadi” kama lilivyotumika katika Ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani atakachopewa Kiongoziwa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma. (3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na
mambomengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.

Katiba Inayopendekezwa imeiboresha Ibara hii na kuandika Ibara ya 29(2)(a) ambayo kwa jumla inasema “Kwa madhumuni ya Katiba hii, Bunge litatunga sheria itakayoweka, pamoja na mambo mengine: (a) tafsiri ya neno zawadi, aina, thamani, kiwango na uhifadhi wa zawadi ambayo kiongozi anapokea wakati akitekeleza
majukumu yake.

Nikitazama kwa kina maboresho hayo utagundua masharti ambayo wananchi walikuwa wanayapendekeza kuwa yawepo katika Katiba kama masharti mahususi, Katiba Inayopendekezwa imeyatupilia mbali na kuacha ombwe hilo kufanyiwa kazi na Sheria zitakazotungwa na Bunge. Ikumbukwe hata wabunge ni viongozi na masharti haya kikatiba yangewawajibisha hata wao na kama yasingefutwa basi wangelazimika kutunga sheria ambazo misingi yake imo katika Katiba tofauti na mtindo wa uandishi wa Katiba Inayopendekezwa ambao unawapa viongozi nguvu za kutumia utashi wao kutunga masharti ya kuwawajibisha na kuwadhibiti viongozi wao wenyewe. Kwa maneno mengine misingi ya kuwadhibiti viongozi wetu na namna wanatumia madaraka yao inapaswa iwekwe kwenye Katiba na wananchi na si viongozi waje kujitungia masharti ya kuwadhibiti wao wenyewe, hawatatenda.

Warioba alisema katiba Ibara ya 16 kwamba “Kiongozi wa umma - (a) hatafungua au kumiliki akaunti ya benki
nje ya Jamhuriya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na (b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namnaau mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma”.

Ukiitizama Katiba Inayopendekezwa namna ambavyo imeiboresha Ibara hii katika Ibara ya 29(2) inasomeka kama ifuatavyo “Kwa madhumuni ya Katiba hii, Bunge litatunga sheria itakayoweka, pamoja na mambo mengine: (b) masharti ya kufungua akaunti za nje kwa kiongozi wa umma.

Hivi kweli ukisoma Ibara za 15 na 16 za Rasimu ya Warioba, je uboreshwaje wake ni kama ulivyowekwa katika Ibara ya 29(2) ya Katiba Inayopendekezwa? Tafakarini kwa kina kabla ya kusema Katiba Inayopendekezwa ni Bora Afrika.

Warioba alisema katiba Ibara ya 21(3) kwamba “Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosaya: kimaadili; (b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; au (c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu washeria za nchi au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi waumma.

Katiba Inayopendekezwa imeyafuta kabisa masharti haya, kwa msingi huu tusishangae kiongozi anayetuhumiwa kwa masuala tajwa hapo juu akaendelea kutoa huduma kwa wananchi ilhali tukijua mzizi wa tatizo uko kwa kiongozi au mtumishi huyo wa umma.

Katiba Inayopendekezwa inapokuja katika suala la Maadili kwakweli haijawatendea haki watanzania, hasa katika kipindi hiki ambapo taifa letu limepitia katika kufichuka kwa tuhuma na kashfa za ufisadi mkubwa katika taasisi zetu za serikali tena karibu katika ngazi zote.

Labda kabla ya kuwaacha niwape mfano wa mwisho, Ukiangalia Tume ya Maadili na uwajibikaji utagundua kwa sababu ambazo hazieleweki masharti mengi na muhimu yaliyokuwa sehemu ya majukumu ya Tume ya Maadili kwa Rasimu ya Warioba yamefutiliwa mbali katika Katiba Inayopendekezwa. Rejea masharti ya ibara ya 203(2)(b), (e) hadi (o) ya Rasimu ya Tume, juu ya majukumu ya Tume ya maadali yauongozi.Ukisoma kifungu cha 231 cha Katiba Inayopendekezwa masharti hayo yamefutwa.

Hakika Katiba Inayopendekezwa itaturudi nyuma kabisa katika uandishi bora wa Katiba Barani Afrika, lakini fursa ya kuirekebisha kabla haijawa rasmi mpya iko pale pale ukirejea kifungu cha 35(3) na (4) cha Sheria ya Kura ya Maoni.

Karibu kutoa Maoni



Monday, April 13, 2015

TCD MSIPOLISEMEA HILI LA MAREKEBISHO YA KATIBA YA 1977, MTAPOTEZA HESHIMA YENU

Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu hivi hivi

Kuahirishwa kwa Kura ya Maoni

Wiki iliyopita nilieleza furaha yangu baada ya serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuahirisha Kura ya Maoni iliyokuwa ifanyike tarehe 30 Aprili, kitendo cha serikali ni cha kiungwana licha ya kwamba kimekuja kwa kuchelewa sana. Serikali kwa ukubwa wake na taasisi zake lukuki ambazo nyingine zimepewa hata dhamana ya kutumia intelijensia kuyaelewa mambo na kutoa ushauri stahiki kwa viongozi wetu, hatukutarajia tupige kelele kwa miezi mitano kusema Kura ya Maoni haiwezekani mwaka 2015, na hasahasa mwezi wane. Sote tulijua bado hatukuwa na vifaa (BVR) vya kuwaandikisha watu, sote tulijua tunatumia mfumo mpya kuwaandikisha watu na hivyo kutarajia sintofahamu kadhaa wa kadhaa, sote tulijua sheria ya Kura ya Maoni ilikuwa imeweka utaratibu na masharti ya kuzingatiwa kabla ya kwenda kwenye zoezi la Kura ya Maoni, na sote tunajua masharti hayo na utaratibu kwa kiasi kikubwa haukuwahi kufuatwa.

Zaidi ya yote, kila mtu anajua kwamba mpaka mwezi wa pili kwenda wa tatu na hata leo bado tunaendelea kugawa Katiba Inayopendekezwa kwa umma wa watanzania. Na sote tunafahamu kwa serikali yetu imechapa nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa ambayo ni wastani wa Katiba Inayopendekezwa moja inapaswa kusomwa na watu kati ya 12 hadi 13. Katiba Inayopendekezwa moja kusomwa na watu 12 au 13, tafsiri yake ni kwamba, wewe ambaye hujapata kuiona Katiba Inayopendekezwa kuna wenzake 11 au 12 ambao wakimaliza kusoma ndipo na wewe itafika zamu yako, kuwa mvumilivu maana sasa una muda wa kutosha.

Ilikuwa bayana pia kwamba tusingeweza kwenda kwenye Kura ya Maoni tukiwa tumegawika kabisa, kisiasa na kiimani. Kura ya Maoni ingeendeleza mpasuko ambayo kuuziba ingetugharimu zaidi kama Taifa. Na kama ambavyo utakuwa umefuatilia, dini zote mbili zina madai na kwa msingi huo, zote hazijaridhika na zote zilishajipanga kupiga kura ya Hapana. Kwa maneno mengine tarehe 30 Aprili angekuwa ni mtu basi angeshakuwa mhanga wa mpasuko wa kijamii na kwa maana hiyo tokeo lolote la Aprili 30 lingekuwa limepasua Taifa kuliko kutujenga.

Nyote mmeshuhudia kwamba kuelekea Kura ya Maoni Aprili 30 ambayo sasa imeahirishwa tulikuwa tayari na mpasuko mkubwa wa kisiasa, vyama vikubwa vilikuwa vimesusia kushiriki katika zoezi la Kura ya Maoni. Kuna baadhi ya watu walichukulia mzaha kwamba hata wakisusia kama vyama itakuwa kazi bure iwapo watu watajitokeza na kushiriki katika Kura ya Maoni. Baadhi ya watu hawa walienda mbali zaidi na kuhamasisha kwamba watu wapuuze msimamo wa vyama kususia na badala yake wakashiriki Kura ya Maoni. Mimi kwa mfano chama changu hakikususia, na nilikuwa nimejiandaa kwenda kupiga kura ya Hapana na vivyo hivyo nikajaribu kulisemea hili kwamba kuna tofauti kubwa kati ya msimamo wa chama kama taasisi na haki ya mwananchi kushiriki katika shughuli za umma ikiwemo kupiga kura ya maoni.

Watu huenda kupiga kura kama raia wa Tanzania, na hushiriki zoezi la kupiga kura kama haki yao ya kimsingi na haijalishi watu hawa ni wanachama wa chama cha siasa au la. Chama cha Siasa kama taasisi inayotambuliwa kisheria (rejea Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258), kina uongozi, kina utaratibu wa kufanya uamuzi kupitia vikao na kadharika,chama kinaweza kutoa msimamo, kufanya uamuzi na uamuzi huo usiingiliwe na uhuru wa raia mmoja mmoja kutumia haki zake katika Jamhuri yetu. Kwahiyo vyama vikisema tunasusia Kura ya Maoni hilo ni tatizo na wa kulitatua sio wananchi bali ni vyama kukaa na kutatua matatizo yaliyopo miongoni mwao.

Makubaliano ya Rais na TCD

Juzi juzi hapa nikapata kusikia jamaa yangu mmoja ambaye alisemalo mara nyingi huwa ama huwa lina wakilisha msimamo, huyu jamaa ni kama mpishi, mpishi akikwambia leo hakuna nyama ni maharagwe usimbishie maana yeye anakaa jikoni kila wakati, anajua. Katika mazungumzo anaonesha kana kwamba hakuna kitu kama Makubaliano ya Rais na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Watu kama hawa huwa sio wa kupuuzwa hata kidogo, lakini kubwa ni kwamba yeye namshukulia kama mwakilisha fikra, na mimi nawaeleza ninyi wanachama wa TCD. Napenda kuwaeleza kwamba Tanzania na watanzania waliona mwanga kupitia ninyi, waliwaamini na kuwaheshimu, nawasihi enendeni kwa moyo huyo.

Naomba niwakumbushe, siku Mhe. Cheyo anasoma Makubaliano ya Rais na TCD, kushoto kwake aliketi Mhe. Dovutwa na kushoto kwa Mhe. Dovutwa aliketi Mhe. Philip Mangula. Kwa ishara hii ya umoja na mshikamano wa TCD, tusaidie watanzania kuvuka kipindi hiki chenye changamoto nyingi. Ninyi (viongozi na wanachama wa TCD) mnajua fika, na ninajua mnajua na mko katika nafasi ya kujua ukweli wa mambo kwamba hatuwezi tena kuwa na Kura ya Maoni mwaka huu. Kinyume na fikra hiyo ni kujaribu kulazimisha mambo halafu mwishowe tuharibu kila kitu, na ninauhakika miongoni mwenu kuna wazee wenye hekima na wenye hofu ya Mungu, mnajua fika kwa joto la kisiasa lilipo sasa hivi kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, kimsingi haiwezekani tena kuchomeka Katiba Inayopendekezwa ili ipigiwe Kura ya Maoni.

Juzi waziri mmoja wa zamani akaandika katika mitandao ya kijamii, kulikoni katika chama cha Mapinduzi, mbona kimya mpaka sasa kuhusu kinyang’anyiro cha watangaza nia ya Urais kupitia CCM ilhali kila kitu kinapaswa kuwa kimekamilika ifikapo mwezi Mei. Swali la makusudi kutoka kwa mwanasiasa huyu maarufu, ni ishara inayotuonesha uzito wa hali ilivyo kisiasa nchini, huku kwenye CCM peke yake kuna hali ngumu, kuna joto mithiri ya tanuruni, bado kwenye vyama vinavyoboresha mawazo (wengine wanaita vyama vya upinzani) vinyang’anyiro bado. Katika ngazi za ubunge, wabunge wa sasa pamoja na watangaza nia za ubunge wote akili zinawapaa kujaribu kuwapa maneno matamu matamu ya lala salama au maneno matamu ya kufunga uchumba kwa miaka mingine mitano au mwanzo mpya wa miaka mitano.

Kama kwenye Urais na Ubunge watu hawalali mpaka kieleweke, kwenye udiwani, vikumbo ni zaidi katika ngazi ya kata. Sasa nikuulize unadhani Taifa liko katika akili iliyotulia ya kuipigia Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa kwa maana viongozi wetu waongoza kampeni ambao wengi ni wanataka kuendelea kushikilia majimbo au wametingwa na kutangaza nia pamoja na wananchi raia mmoja mmoja ambao saizi tunatathmini nani abaki na nani asirudi na kwanini abaki na kwanini asirudi. Hivi kweli ukituongezea na Katiba Inayopendekezwa si utatuvuruga?

Kibaya zaidi, kitendo chochote cha kuchanganya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu itakuwa ni dhambi kubwa kuliko, tutageuza Mchakato wa Katiba na Katiba Inayopendekezwa kuwa ajenda ya uchaguzi, hilo litavuruga maana ya Katiba isiyopasualiwa kisiasa katika ya ndio na hapana zinazohamasishwa kwa minajiri ya siasa zetu ambazo mara nyingi huwa hazina maslahi ya umma mpana wa watanzania.

TCD, nawasihi tena, kutaneni na jadilini, huyu Rais wetu ni muungwana na msikivu, mkimweleza kwa hoja hizi na zenu nzuri zaidi atawaelewa na twaweza kuona Bunge lijalo tukijadili marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 ili tuvuke salama katika Uchaguzi Mkuu. Msipofanya hivyo, viongozi wangu wa CCM, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI, TLP na UDP kama sehemu ya TCD, mtapoteza imani yenu mbele ya umma wa watanzania. Nawasihi fanyeni hili kwa maslahi ya Taifa na zaidi tumsaidie Mhe. Rais amalize na Uchaguzi kwa mara ya kwanza usio na tashwishwi wala waa na huo utakuwa sehemu ya utumishi wake uliotukuka kwetu na sisi kwa hakika tutamkumbuka ikiwemo pamoja na mchakato wa Katiba ambao tutaendelea nao mwakani. Na wala msihofu, tukifanya marekebisho, lazima tutatunga na masharti yatokanayo na masharti ya mpito na mojawapo ya kazi za kikatiba kwa Rais ajaye na Serikali yake ni kuendelea na Mchakato wa Katiba, sio utashi bali ni takwa la kikatiba.

Fursa ya Mjadala

Kilichobaki sasa ni kuendelea kujadiliana kuhusu mchakato wa Katiba, Rasimu ya Warioba, Katiba Inayopendekezwa na tuulizane maswali na kupeana majibu. Kama ilivyo ada wikendi hii Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeandaa Mdahalo wa Katiba huko Mbeya, ni sehemu ya kujadiliana. Na ninawasihi Taasisi ya Mwalimu Nyerere wasiishie hapo, waende na mikoa mingine mingi zaidi maana elimu hii inahitajika sana.

Tunapojiandaa kisaikolojia na Uchaguzi Mkuu

Tuipe Tume ya Taifa ya Uchaguzi ushirikiano wa kutosha wanapoendelea na zoezi la uandikishwaji wapiga kura. Tujitokeze kwa wingi kuandikishwa na kupata vitambulisho vya mpiga kura, bila kitambulisho cha mpiga kura hutaweza kutumia haki yako kufanya uamuzi wa ni nani na nani wapewe dhamana ya kukuongoza katika ngazi ya kata, jimbo na Jamhuri yetu.


Wito, kwa unyenyekevu niwasihi serikali msiwaingilie Tume wanapotenda kazi yao, wapeni uhuru wa kutosha kama ambavyo wanapaswa kuwa. Waacheni ili watanzania kwa muda huu uliobaki wapate huduma ya Tume bila matatizo. Rai yangu kwa vyama vya siasa, jipangeni, pigeni siasa safi, jengeni hoja, toeni sababu na onesheni ushahidi, watu watawaelewa tu, ila achene kuisakama Tume ya Uchaguzi bila sababu, maana hiyo ni tabia mbaya.

Saturday, April 4, 2015

RAI YANGU: FURSA ILIYOBAKI NI MAREKEBISHO YA KATIBA YA MWAKA 1977

Mhe. John Cheyo akiutangazia umma wa watanzania makubaliano ya Mhe. Rais na TCD
Katika wiki hii inayoisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeutangazia umma wa watanzania kwamba hakutakuwa na Kura ya Maoni tarehe 30 Aprili kama ilivyotangazwa hapo awali. Tume imesema badala yake zoezi la uandikishwaji wa Wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR litaendelea hadi mwezi julai mwaka huu. Tarehe ya Kura ya Maoni itatangazwa hapo baadaye baada ya Tume ya Taifa ya uchaguzi kukubaliana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Nitakuwa mnyimi wa shukrani nisiposema kupitia kwenu Tume ya Taifa ya Uchaguzi, asante serikali kwa kutegua kitendawili hiki chepesi. Naomba ieleweke kwamba huu sio ushindi wala isiingizwe siasa hapa bali ni uthibitisho kwamba tunapaswa tuseme kweli hata kama tunatetemeka kwa woga. Serikali ni watu na watu wenyewe ndio sisi, inapaswa kutusikiliza hasa pale tunapozungumza masuala yenye masilahi kwa taifa letu.

Tanzania itajengwa na wenye uthubutu wa kusema kweli na kuisimamia kweli. Nirudie tena, kupitia Tume ya Uchaguzi, Asante serikali, asante wadau wote na asante wananchi wa Tanzania kwa mshikamano wenu. Nawasihi watanzania wenzangu kwa ujumla wenu, tusiiache serikali yetu inapokosea au inaposhindwa kuyatazama mambo kwa upana wake, wao (viongozi wetu) ni binadamu pia, tunapaswa kuwakumbusha, kuwashauri na kama hawasikii basi tuwasumbue tena na tena mpaka watakaposikia hoja zetu chetu.

Wale ambao mmepewa dhamana ya kuwashauri viongozi wetu, fanyeni hivyo kwa unyenyekevu, weledi na uzalendo mkubwa. Viongozi wetu hufanya maamuzi kwa kuzingatia vipawa vya alivyowakirimu Mungu, weledi wao, mitazamo na dira za kiuongozi, lakini ukweli unabaki palepale kwamba nafasi ya watumishi wa umma katika kuwasaidia kiweledi na kitaalamu ni ya muhimu kabisa. Mtumishi mtaalamu ambaye hatoi ushauri sahihi na hasemi kweli ni janga katika utumishi wa umma na umma wa watanzania na anaweza kuwa chanzo cha kupotosha viongozi wetu.

Lakini pia viongozi wengine huwa wabishi na wenye kiburi, kwa hali ilivyo sasa tusichoke kuendelea kuwaambia hatari ya maamuzi yasiyo sahihi katika mustakabali wa Taifa letu na kama ni wale wako katika dhamana ya wananchi basi tusubiri Wananchi waamue hatima yao

ANGALIZO

Nimemsikia Mhe. Mbunge mmoja ambaye kauli zake kwa uzoefu wangu huwa zinatimia na huja na kauli hizo mwishoni mwishoni kabisa na huwa zinafanyiwa kazi moja kwa moja. Kama mtakuwa watu wa kufuatilia mwaka juzi (2013) kwenye kikao cha kuelekea mwisho wa mwaka alitoa pendekezo ambalo lilifanyiwa kazi ipasavyo licha ya kwamba lilikuwa kinyume na usanifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Nimemsikia sikia magazetini kwamba ameomba mwongozo juu ya hoja kwamba Bunge la Jamhuri lipitishe hoja kwamba Katiba Inayopendekezwa ifanywe ya Mpito ili tuvuke Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Na akaendelea kusema kwamba Katiba Inayopendekezwa imesheheni mambo ambayo watu wamekuwa wakiyadai. Mheshimiwa Mbunge atakuwa ameshindwa kufahamu namna ambavyo mchakato wa Katiba mpya katika ngazi ya Bunge Maalum ulivurugika na kwamba mpaka leo Taifa limegawika kisiasa, kidini na baina ya Bara na Zanzibar. Haitaki elimu kubwa kujua Katiba Inayopendekezwa imetugawa watanzania na imepoteza sifa ya kuwa ishara ya Umoja wetu.

Kuhusu Kauli yake, Napenda kusema yafuatayo;-

1) Kauli yake ipuuzwe na Wabunge wote, wa CCM na wote wa vyama vya upinzani

2) Katiba Inayopendekezwa ni mbaya na haifai na ni zao la mchakato ambao mwishoni ulishindwa kujenga muafaka wa Kitaifa, hakuzingatia maridhiano na haukupata kuwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa vyama vya siasa na wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba.

3) Bunge la Jamhuri ya Muungano halina mamlaka wala uhalali wa kuijadili Katiba Inayopendekezwa, hivyo hoja ya kwamba Bunge la Jamhuri liipitishe Katiba Inayopendekezwa kuwa ni ya Mpito haipo, haina mashiko na ina nia ya kuendeleza migogoro ya kisiasa inayotugawa Wananchi na isiyo na tija kwa Taifa letu.

YANAYOTAKIWA KUFANYWA HARAKA

1) Mchakato wa kuandaa mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kuzingatia Ibara ya 98, ili ifanyiwe marekebisho madogo ya 15 yatakayojumuisha mambo ambayo Mhe. Rais alikubaliana na Kituo cha Demokrasia (TCD). Mambo haya ni pamoja na (i) Matokeo ya Urais kuwa ni zaidi ya asilimia 50 ya kura zote halali zilizopigwa na kuhesabiwa, (ii) Matokeo hayo yaweze kuhojiwa Mahakamani kama kuna tashwishwi, (iii) Uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na (iv) Uwepo wa Mgombea Huru.

2) Tuushirikishe umma wa watanzania katika kutoa maoni yao kwa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kwa kiasi cha kutosha, Serikali na Bunge watuongoze kufanikisha hili.

Naendelea kusema kama isingekuwa Rais Kikwete, tusingepata mchakato ambao Wananchi walishiriki ipasavyo katika awamu ya kwanza ya maoni ya Wananchi, awamu ya pili ya Mabaraza ya Katiba. Awamu ya tatu ya Bunge Maalum ilishindwa kujenga muafaka na kusababisha mpasuko wa kisiasa na zoezi lililobaki yaani awamu ya nne ya Kura ya Maoni ambayo mpaka sasa na kwa mapenzi mema ya Taifa letu haiwezi kufanyika tena mwaka huu labda tusifanye Uchaguzi Mkuu.

KUHUSU WALE WENYE FIKRA OVU

Nimeanza kusikia watu mbalimbali hasahasa vijana wadogo wadogo tu ambao wameanza kusema hakujawahi kuwa na makubaliano baina ya Mhe. Rais na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Na wengine wasomi kabisa wameanza kusema kama mmekosa Katiba Mpya sasa, sahauni marekebisho ya 15 ya Katiba ya 1977. Watu hawa hawa hawaitakii mema nchi yetu.

Niwaulize unadhani tutaweza kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila Tume Huru ya Uchaguzi, tukisema ndio, basi tutakuwa tunamkanusha hata Rais ambaye alisema tunapaswa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi katika uchaguzi ujao. Kama mtasema hapana basi mjiulize dhamira zenu ni zipi na hapa nitawauliza vyama vyote vya upinzani, je kelele zenu zimekuwa za debeshinda?

Chama cha Mapinduzi kitajijengea heshima kubwa kama kitatoa uongozi ili tufanye Marekebisho ya 15 ambayo uchaguzi huu ukipita salama, hatutakuwa tena na lawama zisizo na msingi na sintofahamu inayotokana kupotea kwa imani ya vyama vya upinzani kwa chombo cha kikatiba kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

RAI YANGU KWENU

Kama mnataka tumshukuru Rais Kikwete kwa kutuanzishia mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambao msingi na usanifu wake ulikuwa Wananchi kutoa maoni yao basi tuna budi ya kuunga mkono na kukumbusha kwa sauti kubwa ili waliopewa dhamana watuletee mswada wa sheria ya kurekebisha Katiba ya Mwaka 1977 ili kwa muda mchache uliobaki turekebisha Katiba na kuunda vyombo vinavyopaswa kuundwa.

Wanaopuuza rai yangu wanataka Rais Kikwete amalize utumishi wake kwetu bila kuhakikisha misingi ya mpito ambayo itaimarisha demokrasia yetu, na misingi wa misingi hii ni Marekebisho ya 15 ya Katiba ya Mwaka 1977. Kwa maneno mengine mbadala wa kutokuwa na Katiba Mpya ni Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 Hima Hima watanzania.