Saturday, April 4, 2015

RAI YANGU: FURSA ILIYOBAKI NI MAREKEBISHO YA KATIBA YA MWAKA 1977

Mhe. John Cheyo akiutangazia umma wa watanzania makubaliano ya Mhe. Rais na TCD
Katika wiki hii inayoisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeutangazia umma wa watanzania kwamba hakutakuwa na Kura ya Maoni tarehe 30 Aprili kama ilivyotangazwa hapo awali. Tume imesema badala yake zoezi la uandikishwaji wa Wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR litaendelea hadi mwezi julai mwaka huu. Tarehe ya Kura ya Maoni itatangazwa hapo baadaye baada ya Tume ya Taifa ya uchaguzi kukubaliana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Nitakuwa mnyimi wa shukrani nisiposema kupitia kwenu Tume ya Taifa ya Uchaguzi, asante serikali kwa kutegua kitendawili hiki chepesi. Naomba ieleweke kwamba huu sio ushindi wala isiingizwe siasa hapa bali ni uthibitisho kwamba tunapaswa tuseme kweli hata kama tunatetemeka kwa woga. Serikali ni watu na watu wenyewe ndio sisi, inapaswa kutusikiliza hasa pale tunapozungumza masuala yenye masilahi kwa taifa letu.

Tanzania itajengwa na wenye uthubutu wa kusema kweli na kuisimamia kweli. Nirudie tena, kupitia Tume ya Uchaguzi, Asante serikali, asante wadau wote na asante wananchi wa Tanzania kwa mshikamano wenu. Nawasihi watanzania wenzangu kwa ujumla wenu, tusiiache serikali yetu inapokosea au inaposhindwa kuyatazama mambo kwa upana wake, wao (viongozi wetu) ni binadamu pia, tunapaswa kuwakumbusha, kuwashauri na kama hawasikii basi tuwasumbue tena na tena mpaka watakaposikia hoja zetu chetu.

Wale ambao mmepewa dhamana ya kuwashauri viongozi wetu, fanyeni hivyo kwa unyenyekevu, weledi na uzalendo mkubwa. Viongozi wetu hufanya maamuzi kwa kuzingatia vipawa vya alivyowakirimu Mungu, weledi wao, mitazamo na dira za kiuongozi, lakini ukweli unabaki palepale kwamba nafasi ya watumishi wa umma katika kuwasaidia kiweledi na kitaalamu ni ya muhimu kabisa. Mtumishi mtaalamu ambaye hatoi ushauri sahihi na hasemi kweli ni janga katika utumishi wa umma na umma wa watanzania na anaweza kuwa chanzo cha kupotosha viongozi wetu.

Lakini pia viongozi wengine huwa wabishi na wenye kiburi, kwa hali ilivyo sasa tusichoke kuendelea kuwaambia hatari ya maamuzi yasiyo sahihi katika mustakabali wa Taifa letu na kama ni wale wako katika dhamana ya wananchi basi tusubiri Wananchi waamue hatima yao

ANGALIZO

Nimemsikia Mhe. Mbunge mmoja ambaye kauli zake kwa uzoefu wangu huwa zinatimia na huja na kauli hizo mwishoni mwishoni kabisa na huwa zinafanyiwa kazi moja kwa moja. Kama mtakuwa watu wa kufuatilia mwaka juzi (2013) kwenye kikao cha kuelekea mwisho wa mwaka alitoa pendekezo ambalo lilifanyiwa kazi ipasavyo licha ya kwamba lilikuwa kinyume na usanifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Nimemsikia sikia magazetini kwamba ameomba mwongozo juu ya hoja kwamba Bunge la Jamhuri lipitishe hoja kwamba Katiba Inayopendekezwa ifanywe ya Mpito ili tuvuke Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Na akaendelea kusema kwamba Katiba Inayopendekezwa imesheheni mambo ambayo watu wamekuwa wakiyadai. Mheshimiwa Mbunge atakuwa ameshindwa kufahamu namna ambavyo mchakato wa Katiba mpya katika ngazi ya Bunge Maalum ulivurugika na kwamba mpaka leo Taifa limegawika kisiasa, kidini na baina ya Bara na Zanzibar. Haitaki elimu kubwa kujua Katiba Inayopendekezwa imetugawa watanzania na imepoteza sifa ya kuwa ishara ya Umoja wetu.

Kuhusu Kauli yake, Napenda kusema yafuatayo;-

1) Kauli yake ipuuzwe na Wabunge wote, wa CCM na wote wa vyama vya upinzani

2) Katiba Inayopendekezwa ni mbaya na haifai na ni zao la mchakato ambao mwishoni ulishindwa kujenga muafaka wa Kitaifa, hakuzingatia maridhiano na haukupata kuwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa vyama vya siasa na wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba.

3) Bunge la Jamhuri ya Muungano halina mamlaka wala uhalali wa kuijadili Katiba Inayopendekezwa, hivyo hoja ya kwamba Bunge la Jamhuri liipitishe Katiba Inayopendekezwa kuwa ni ya Mpito haipo, haina mashiko na ina nia ya kuendeleza migogoro ya kisiasa inayotugawa Wananchi na isiyo na tija kwa Taifa letu.

YANAYOTAKIWA KUFANYWA HARAKA

1) Mchakato wa kuandaa mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kuzingatia Ibara ya 98, ili ifanyiwe marekebisho madogo ya 15 yatakayojumuisha mambo ambayo Mhe. Rais alikubaliana na Kituo cha Demokrasia (TCD). Mambo haya ni pamoja na (i) Matokeo ya Urais kuwa ni zaidi ya asilimia 50 ya kura zote halali zilizopigwa na kuhesabiwa, (ii) Matokeo hayo yaweze kuhojiwa Mahakamani kama kuna tashwishwi, (iii) Uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na (iv) Uwepo wa Mgombea Huru.

2) Tuushirikishe umma wa watanzania katika kutoa maoni yao kwa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 kwa kiasi cha kutosha, Serikali na Bunge watuongoze kufanikisha hili.

Naendelea kusema kama isingekuwa Rais Kikwete, tusingepata mchakato ambao Wananchi walishiriki ipasavyo katika awamu ya kwanza ya maoni ya Wananchi, awamu ya pili ya Mabaraza ya Katiba. Awamu ya tatu ya Bunge Maalum ilishindwa kujenga muafaka na kusababisha mpasuko wa kisiasa na zoezi lililobaki yaani awamu ya nne ya Kura ya Maoni ambayo mpaka sasa na kwa mapenzi mema ya Taifa letu haiwezi kufanyika tena mwaka huu labda tusifanye Uchaguzi Mkuu.

KUHUSU WALE WENYE FIKRA OVU

Nimeanza kusikia watu mbalimbali hasahasa vijana wadogo wadogo tu ambao wameanza kusema hakujawahi kuwa na makubaliano baina ya Mhe. Rais na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Na wengine wasomi kabisa wameanza kusema kama mmekosa Katiba Mpya sasa, sahauni marekebisho ya 15 ya Katiba ya 1977. Watu hawa hawa hawaitakii mema nchi yetu.

Niwaulize unadhani tutaweza kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila Tume Huru ya Uchaguzi, tukisema ndio, basi tutakuwa tunamkanusha hata Rais ambaye alisema tunapaswa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi katika uchaguzi ujao. Kama mtasema hapana basi mjiulize dhamira zenu ni zipi na hapa nitawauliza vyama vyote vya upinzani, je kelele zenu zimekuwa za debeshinda?

Chama cha Mapinduzi kitajijengea heshima kubwa kama kitatoa uongozi ili tufanye Marekebisho ya 15 ambayo uchaguzi huu ukipita salama, hatutakuwa tena na lawama zisizo na msingi na sintofahamu inayotokana kupotea kwa imani ya vyama vya upinzani kwa chombo cha kikatiba kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

RAI YANGU KWENU

Kama mnataka tumshukuru Rais Kikwete kwa kutuanzishia mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambao msingi na usanifu wake ulikuwa Wananchi kutoa maoni yao basi tuna budi ya kuunga mkono na kukumbusha kwa sauti kubwa ili waliopewa dhamana watuletee mswada wa sheria ya kurekebisha Katiba ya Mwaka 1977 ili kwa muda mchache uliobaki turekebisha Katiba na kuunda vyombo vinavyopaswa kuundwa.

Wanaopuuza rai yangu wanataka Rais Kikwete amalize utumishi wake kwetu bila kuhakikisha misingi ya mpito ambayo itaimarisha demokrasia yetu, na misingi wa misingi hii ni Marekebisho ya 15 ya Katiba ya Mwaka 1977. Kwa maneno mengine mbadala wa kutokuwa na Katiba Mpya ni Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 Hima Hima watanzania.

No comments:

Post a Comment