Saturday, March 28, 2015

TUJIKUMBUSHE MAONI YA WANANCHI, KATIBA HUANDIKWA NA WANANCHI NA SI VIONGOZI

TUJIKUMBUSHE MAONI YA WANANCHI, KATIBA HUANDIKWA NA WANANCHI NA SI VIONGOZI

Uwajibikaji wa Wabunge

Suala la wabunge kuwajibika katika majimbo yao ya uchaguzi ni moja ya eneo ambalo wananchi wengi walichangia wakati wa utoaji wa maoni ili kupata katiba mpya. Dhana ya uwajibikaji wa wabunge imegawanyika katika mitizamo miwili. Mtizamo wa kwanza ni uwajibikaji wa mbunge kama mwakilishi aliyechaguliwa kuwakilisha mawazo ya wananchi wa jimbo husika. Vilevile, wabunge wanawajibika kwa wananchi wao kwa ahadi walizozitoa wakati wa kampeni. Kwa mtizamo wa pili, mbunge kama sehemu ya Bunge anawajibika kuisimamia na kuishauri serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya katiba na sheria za nchi.

Hali Ilivyo kwa Sasa

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, haijaweka kifungu kinachombana mbunge kuwajibika moja kwa moja katika jimbo lake la uchaguzi kwa wananchi waliomchagua. Utaratibu pekee ambao mwananchi anaweza kuutumia kumwajibisha mbunge ni kupitia chaguzi za wabunge ambazo kwa kawaida hufanyika kila baada ya miaka mitano. Kwa upande mwingine wabunge wanawajibika kwa vyama vyao kwa kusimamia sera na misimamo ya kiitikadi kwa vyama. Hivyo endapo akishindwa kutekeleza wajibu wake, chama kina uwezo wa kumwajibisha mbunge huyo.

Maoni ya Wananchi

Wananchi katika mchakato huu wa kukusanya maoni, wametoa maoni juu ya hoja ya uwajibikaji wa wabunge katika majimbo yao ya uchaguzi kama ifuatavyo:

(a) kuwe na taratibu za kisheria ambazo wananchi wanaweza kuzitumia kumuondoa madarakani mbunge asiyewajibika kwa wapiga kura wake;
(b) wabunge wawajibike kwa vyama vyao vya siasa; na
(c) wabunge wawajibike kwa wapiga kura.

Wananchi waliotoa maoni yao, walipendekeza kuwe na utaratibu wa kumwajibisha mbunge asiyewajibika kwa wapiga kura wake pamoja na kupendekeza mambo yafuatayo:

(i) kuwe na sheria itakayotoa utaratibu kwa wananchi kuweza kumuondoa madarakani mbunge ambaye hawajibiki kwa wapiga kura wake;
(ii) wananchi wapewe uwezo wa kumsimamisha ubunge na kumshitaki mbunge aliyefanya kosa;
(iii) mbunge atoe taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa ahadi alizoziahidi wakati wa kampeni; na
(iv) wabunge ambao hawachangii bungeni na kuwasilisha kero za wananchi wao waondolewe ubunge.

Aidha, wananchi wengine waliopendekeza wabunge wawajibike kwa vyama vyao vya siasa, wametoa sababu kuwa chama ndicho kilichomuweka kugombea katika jimbo la uchaguzi kwa hiyo wananchi wamemchagua kwa sababu ya kukipenda chama hicho.

Wananchi waliopendekeza wabunge wawajibike kwa wapiga kura wao na mbunge asipoteze nafasi yake ya ubunge kwa kuondolewa uanachama wa chama cha siasa kilichompendekeza, wametoa sababu kuwa wananchi waliomchagua wanajumuisha wananchi ambao si wanachama wa chama kilichompendekeza.

Wananchi waliotoa maoni katika hoja ya Uwajibikaji wa Wabunge katika majimbo yao ya uchaguzi, wametoa sababu zifuatazo:

(i) kutoa nafasi kwa wananchi wengine kuweza kuwatumikia wananchi wa jimbo husika badala ya wabunge wasiowajibika;
(ii) kuepukana na wabunge kutoa ahadi zisizotekelezeka wakati wa Kampeni;
(iii) kuleta changamoto za maendeleo kwa mbunge na wananchi wa eneo husika;

(iv) kuboresha utendaji na uwajibikaji wa wabunge; na
(v) kuleta ufanisi na kuwafanya wabunge wasijisahau baada ya kuchaguliwa.

Uzoefu wa Nchi Nyingine Duniani

Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia ililifanyia utafiti suala la haki ya wananchi kuweza kuwawajibisha wabunge wao pale wanaposhindwa kuwajibika na kutekeleza majukumu na ahadi zao majimboni kwa kuangalia uzoefu wa nchi mbalimbali.

Ibara ya 84 ya katiba ya Uganda inatoa mamlaka kwa wananchi ama kundi la watu kuweza kumuondoa madarakani mbunge wao kabla ya muda wake wa kulitumikia bunge kumalizika, iwapo mbunge huyo atashindwa kuwajibika kwa taifa na kundi au wananchi waliomchagua. Malawi walikuwa na utaratibu wa wananchi kuwawajibisha wabunge wao, hata hivyo utaratibu huo ulifutwa mwaka 2006.

Ibara ya 104 ya katiba ya Kenya, pia imetoa mamlaka kwa wananchi ama kundi la watu kuweza kumuondoa madarakani mbunge wao kabla ya muda wake wa kulitumikia Bunge kumalizika, iwapo mbunge huyo atashindwa kuwajibika kwa taifa, kundi au wananchi waliomchagua.

Mapendekezo ya iliyokuwa Tume ya Katiba

Baada ya kuzingatia maoni ya wananchi, sababu za maoni na uzoefu katika baadhi ya nchi duniani, katika hoja ya uwajibikaji wa wabunge katika majimbo yao ya uchaguzi, iliyokuwa Tume ya Katiba ilipendekeza kuwa mbunge atawajibika kwa wananchi na pia kwa chama chake endapo mbunge huyo amependekezwa na chama cha siasa. Tume ilikwenda mbali na kuweka masharti ya haki ya Wananchi kumwajibisha mbunge asiyewajibika ipasavyo katika ibara ya 129.

Katiba Inayopendekezwa haina kabisa masharti hayo kwa maana kwamba Wananchi hawatakuwa na mamlaka ya kumwajibisha mbunge wao hata kama anakwenda kinyume na matarajio yao.

Miiko na Maadili ya Uongozi

Miiko ya uongozi ni jumla ya makatazo ambayo kiongozi wa umma hatakiwi kuyafanya katika dhamana yake kama kiongozi. Kimsingi Miiko ya Uongozi ni kanuni zinazobainisha mwenendo unaofaa na usiofaa kwa viongozi wa umma. Lengo la kuwa na miiko ya uongozi ni kuwafanya waliokabidhiwa madaraka ya uongozi wa umma kuyatumia kulingana na malengo yaliyowekwa ndani ya Katiba, sheria na taratibu na si kwa manufaa binafsi.

Hali Ilivyo kwa Sasa

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haijaweka masharti mahsusi kuhusu miiko ya viongozi. Katiba inaelekeza Bunge la Jamhuri ya Muungano kutunga sheria itakayosimamia misingi ya maadili ya viongozi wa umma kupitia Ibara ya 132(4). Sheria ya maadili ya viongozi wa umma, Sura 398 imeainisha kwa undani miiko ya uongozi. Uhalisia wa sheria hii imekuwa butu na haina meno na imeshindwa kuthibiti viongozi wasio waadilifu na wanaokwenda kinyume na maadili na kanuni za uongozi.

Maoni ya Wananchi

Wananchi katika eneo hili wametoa maoni kama ifuatavyo:
(a) miiko ijulikane kwa viongozi kabla ya kuingia madarakani;
(b) miiko iliyokuwa katika Azimio la Arusha irudishwe;
(c) kuwepo na usawa katika kupata huduma;
(d) kutojilimbikizia mali;
(e) utii na sheria;
(f) viongozi wasitoe wala kupokea rushwa;
(g) viongozi wavae mavazi ya stara;
(h) viongozi wawekewe ukomo wa kumiliki mali;
(i) kiiko iwekwe kwenye katiba;
(j) viongozi watangaze mali zao wanapoingia na wanapoondoka madarakani;
(k) kianzishwe chuo cha maadili ya viongozi;
(l) viongozi wasiwe na mali na fedha nje ya nchi; na
(m) viongozi wasifanye biashara.

Wananchi katika eneo hili la Miiko ya Uongozi wametoa maoni na sababu zifuatazo:

(a) watoto wa viongozi wasipewe nafasi za uongozi kwa upendeleo;
(b) viongozi wasiokuwa waadilifu katika ndoa zao wawajibishwe.
(c) kurudisha heshima katika utumishi wa umma;
(d) kuondoa matabaka ya utajiri na umaskini;
(e) kuongeza ufanisi katika utendaji kazi;
(f) kuondoa rushwa;
(g) kuleta nidhamu na uadilifu;
(h) kuondoa upendeleo kwa familia ya kiongozi;
(i) kuleta usawa;
(j) ni miongoni mwa miiko ya Azimio la Arusha;
(k) kuepusha mgongano wa maslahi kati ya kazi za umma na biashara za viongozi;
(l) kuimarisha uadilifu katika kutekeleza haki za raia;
(m) viongozi wanaishi maisha ya juu sana kuliko wananchi;
(n) kurudisha maadili ya uongozi kama yalivyokuwa katika Azimio la Arusha;
(o) wasiwe wabadhirifu;
(p) wananchi waweze kujiridhisha na uhalali wa mali za viongozi walizozipata wakiwa madarakani; na
(q) mali zilizopatikana kwa ubadhirifu zitaifishwe.

Wananchi waliotaka viongozi wasiwe na mali na fedha nje ya nchi wametoa sababu zifuatazo:

(a) kuzuia ufisadi;
(b) hawana uzalendo;
(c) wanaathiri mzunguko wa fedha nchini;
(d) kukomesha tabia hiyo;
(e) kukuza uchumi wa nchi; na
(f) wanayumbisha uchumi wa nchi.

Wananchi waliotaka viongozi wasifanye biashara, wametoa sababu zifuatazo:

(a) wasiwanyanyase wafanya biashara wa hali ya chini;
(b) wanahujumu mali za umma;
(c) wasijilimbikizie mali;
(d) wasichanganye mambo ya utawala na biashara;
(e) kuondoa mgongano wa maslahi;
(f) ni hatari; na
(g) wanawazuia wengine kujiinua.

Uzoefu kutoka Nchi Nyengine

Iliyokuwa Tume ya Katiba ilifanya utafiti katika nchi mbalimbali kwa lengo la kupata uzoefu katika hoja ya Miiko ya Viongozi. Uzoefu unaonyesha kuwa katika nchi nyingine kama vile Malaysia, Ufilipino, Brazil, Kenya na Afrika Kusini zimeweka masharti ya maadili ya viongozi kwenye katiba zao ili kutatua tatizo la uvunjifu wa maaadili hasa kwa viongozi wa siasa wakiwemo wabunge, mawaziri, makatibu wakuu, Rais, Waziri Mkuu na viongozi wote wa ngazi za juu. Aidha, uamuzi wa kuweka maadili kwenye katiba umetokana na changamoto zinazolikabili taifa husika.

Maadili ya viongozi yanatakiwa yatungwe na wananchi katika mchakato wa kuandika katiba mpya kwani sheria hiyo ikitungwa na viongozi katika serikali na bunge watashindwa kuweka masharti ya kuwabana wao wenyewe na viongozi wa juu katika serikali.

Hivyo basi, katiba nyingi za kisasa zimeamua kutatua tatizo hili kwa kuweka maadili kwenye katiba ambako si rahisi kwa wabunge au viongozi wa ngazi za juu kubadili katiba hiyo kwa manufaa yao hasa kama kutakuwa na zuio.

Kenya imeweka sura moja ya maadili ili kupiga vita rushwa, ufisadi na uvunjifu bayana wa maadili.

Mapendekezo ya iliyokuwa Tume ya Katiba

Kwa kuzingatia maoni ya wananchi na sababu zilizotolewa kuhusiana na hoja ya miiko na maadili ya viongozi wa umma, iliyokuwa Tume ilipendekeza kuwepo kwa masharti mahsusi na usimamizi wa miiko na maadili ya viongozi. Masharti mahususi kuhusu eneo la Maadili na Miiko ya viongozi yaliainishwa katika Rasimu ya Warioba, rejea Ibara za 13 mpaka ibara ya 21 tofauti na Katiba Inayopendekezwa iliyoweka Ibara 4 tu na zenye masharti ya jumla jumla.

Mapendekezo ya Katiba Inayopendekezwa

Katiba Inayopendekezwa imesema hasahasa kwenye eneo la kanuni za maadili ya uongozi wa umma kwamba kanuni hizi zitungiwe sheria ya Bunge, rejea kifungu cha 29(2). Katiba Inayopendekezwa kwa mantiki hiyo imepoka na kufutilia mbali mamlaka ya Wananchi kuamua miiko na kanuni za maadili ambayo viongozi wa umma wanapaswa kuiishi na kuenenda kwayo kikatiba. Katiba Inayopendekezwa inashindwa kujifunza hata kutoka nchi zilizoendelea kimaadili ambazo zimeweka maadili na miiko ya viongozi kwenye Katiba zao.


No comments:

Post a Comment