SABABU 15 WIKI HII ZA KUSEMA
HAPANA KWA KATIBA INAYOPENDEKEZWA
Katiba Mpya inapaswa kuwa Mpya kweli kweli na si
vinginevyo
1. Uhuru
wa Mkuu wa Jeshi la Polisi
Rasimu ya Warioba
ilipendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi atekeleze kazi zake kwa uhuru, bila woga, upendeleo
wala chuki na kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria za nchi. Masharti
haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa
2. Tume
ya Utumishi wa Jeshi la Wananchi
Tume ya Warioba
ilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi ya Jeshi la
Ulinzi la
Wananchi
wa Tanzania itakayokuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya utumishi katika
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katiba Inayopendekezwa imefuta
masharti haya licha ya wapiganaji wetu kupendekeza utaratibu wa kusimamia
maslahi yao Kikatiba.
3.
Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi
Kutakuwa
na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itakayokuwa na jukumu la kusimamia
utumishi wa Jeshi la Polisi. Katika uajiri wa askari wa Jeshi la Polisi, Tume
ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itazingatia kanuni na misingi ya utumishi
iliyoainishwa katika Katiba hii
4.
Misingi ya utendaji wa Jeshi la
Polisi
Rasimu ya Warioba
ilipendekeza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi la Jamhuri
ya Muungano litazingatia (a) viwango vya juu vya kitaaluma na nidhamu miongoni
mwa wafanyakazi wake; (b) ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu; (c) kanuni za
uwazi na uwajibikaji; na (d) kukuza mahusiano na jamii. Warioba akaendelea
kusema, Jeshi la Polisi, katika kutekeleza majukumu yake, litashirikiana na
vyombo vinavyohusika na kupambana na uhalifu vya Nchi Washirika katika kufanya
uchunguzi na kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi.
Misingi hii yote
imefutwa na Katiba Inayopendekezwa
5.
Kuhusu Sifa ya Kielimu kwa Mbunge
Rasimu
ya Warioba ilipendekeza sifa mojawapo ya kuwa mbunge ni kuwa na elimu
isiyopungua kidato cha nne na ajue kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au
kiingereza. Baadhi ya sababu za kuunga mkono pendekezo hili ni pamoja na
maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na Changamoto zilizoko katika sekta za
uchumi, elimu na utandawazi ipo haja ya Mbunge kuwa na elimu ya kutosha kuweza
kukabiliana na Changamoto zinazosababishwa na mabadiliko haya.
Katiba
Inayopendekezwa inapendekeza sifa mojawapo ya kuwa Mbunge ni kujua na kusoma
lugha ya Kiswahili au kiingereza. Pendekezo hili liko mbali kabisa na chini ya
kiwango cha maoni ya watumishi wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma.
6. Nafasi
za Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu Kikatiba
Rasimu ya Warioba
ilipendekeza kuweko na nafasi kikatiba za Makatibu Wakuu watakaoteuliwa na Rais
kutoka miongoni mwa watumishi waandamizi katika utumishi wa umma kama
watakavyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma. Kila Katibu Mkuu atakuwa kiongozi na Mtendaji
Mkuu wa Wizara ya Serikali aliyopangiwa na Rais na atashika nafasi ya madaraka ya
Katibu Mkuu na kutekeleza majukumu yake kama itakavyoainishwa katika sheria za
nchi.
Rais anaweza, kwa
mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma, kumteua mtumishi mwandamizi katika
Utumishi wa Umma kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Kila Katibu Mkuu atakuwa mshauri wa mwisho kwa Waziri kwa masuala yote
ya utendaji na atatoa ushauri kwa Baraza la Mawaziri katika vikao na Kamati
zitakazoitishwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri. Katibu Mkuu au Naibu Katibu
Mkuu hatashika madaraka yake hadi awe ameapa mbele ya Rais kiapo cha utii na
uaminifu au kiapo kingine chochote kinachohusu utendaji wa kazi zake
kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Katiba Inayopendekezwa imefuta
masharti haya na kudhoofisha ujenzi wa utumishi wa umma kikatiba.
7. Kamati
Maalum ya Makatibu Wakuu
Rasimu
ya Warioba ilipendekeza kuwepo kikatiba kwa Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu itakayoongozwa
na Katibu Mkuu Kiongozi ambayo itakuwa na majukumu ya kuchambua na kulishauri
Baraza la Mawaziri juu ya masuala mbalimbali kabla ya kuwasilishwa na kufanyiwa
uamuzi na Baraza hilo na itatekeleza majukumu mengine kama itakavyopangiwa na
Baraza la Mawaziri.
Katiba
Inayopendekezwa imefuta msharti hayo yote mahususi licha ya kwamba huu ulikuwa
wakati muafaka wa kuiimarisha sekta ya utumishi wa umma Kikatiba ili iendelee
kutuhudumia wananchi ikiwa na ari, kujiamini na kutenda kwa weledi pasina ya
kuvurugwa na mara kadhaa na wanasiasa wabaya.
8.
Uhuru wa Habari na vyombo vya Habari
Katiba
Inayopendekezwa imeweka masharti “pokonyezi” (claw-back clauses) kwenye ibara
ya Uhuru wa Habari na vyombo vya Habari. Rasimu
ya Warioba inatoa wajibu kusambaza habari na taarifa kwa wananchi. Katiba Inayopendekezwa
inatoa wajibu wa kusambaza habari na taarifa sahihi na za ukweli
kwa wananchi.
Kuweka
maneno taarifa sahihi na za ukweli ni kuminya haki hii, Katiba inapasa kuweka
msingi na sheria ingetoa ufafanuzi. Kuwekwa hapa masharti haya kutapelekea
kutumika ndivyo sivyo. kuzingatia miiko ya taaluma ya uandishi na utangazaji wa
habari ni suala la sheria na kanuni, na ikumbukwe ulimwengu wa leo hautegemei
pekee wanataaluma wa habari kutoa habari, kifungu hiki kitaminya haki hii. Kwa
kuweka maneno haya katika masharti ya ibara hii, Uhuru wa Habari na vyombo vya
Habari uko mashakani kabisa
9.
Haki ya Elimu na Kujifunza
Wananchi
walipendekeza kutolewa kwa elimu bora ya msingi bure na bila vikwazo ikiwemo
kupata elimu bora inayotolewa nje ya utaratibu wa umma kwa gharama nafuu.
Masharti yafuatayo
yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa:-
Kila mtu ana haki ya:
§ kupata
fursa ya kupata elimu bora bila ya vikwazo;
§ kupata
elimu bora ya msingi bila ya malipo nainayomtayarisha kikamilifu mwanafunzi ama
kuendelea naelimu ya ngazi inayofuatia au kuweka msingi wa kuanzakujitegemea;
§ kupata
elimu bora inayotolewa nje ya utaratibu wa ummakwa gharama nafuu; na
10.
Haki ya Mtoto
Wananchi
walipendekeza kutolewa ulinzi zaidi kwa haki za mtoto na Rasimu ya Katiba Mpya
Toleo la Pili iliweka masharti yaliyoelekeza Mamlaka ya Nchi kuweka utaratibu
wa Kisheria utakaowezesha utekelezaji na
usimamizi wa haki za mtoto kwa kufuata msingi wa kutoakipaumbele kwa maslahi na
manufaa ya mtoto. Masharti haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa na kufanya
haki zilizowekwa katika Ibara hii kuwa kiini macho.
11. Haki
za watu wenye Ulemavu
Wananchi
na hasa watu wenye ulemavu walipendekeza mamlaka ya nchi kuweka utaratibu wa
sheria utakaowezesha watu wenye ulemavu kushiriki kwenye nafasi za uwakilishi.
Katiba
inayopendekezwa imeondoa jukumu hili na tafsiri yake ni kwamba wawakilishi wa
watu wenye ulemavu wataendelea kuteuliwa pasina ya kuwa na msingi wa kikatiba
na kisheria kuhakikisha watu wenye ulemavu wanawachagua wawakilishi wao tofauti
na sasa.
12. Haki
za Wanawake
Wananchi
waliotoa maoni hasa wanawake na wanaume walipendekeza kwa sauti moja kuona haki
za wanawake zinalindwa, zinahifadhiwa, zinatolewa na kutekelezwa kwa wakati na
mamlaka za nchi. Wananchi walipendekeza kuona wanawake wanalindwa dhidi ya
unyonyaji na ukatili. Katiba Inayopendekezwa sio tu imefuta kifungu
kinachomlinda mwanamke dhidi ya unyonyaji bali pia imefuta masharti elekezi
yaliyokuwamo katika Rasimu ya Warioba ambayo yalikuwa yanazielekeza Mamlaka za
nchi kuweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji
wa masharti ya Ibara hii ikiwa ni pamoja na kukuza utu, heshima, usalama na
fursa za wanawakewakiwemo wajane.
13.
Kamati ya Uteuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi
Rasimu ya Warioba
ilipendekeza katika kifungu cha 191 kwamba Asasi za Kiraia zinaweza kupendekeza
kwa Kamati ya Uteuzi majina ya watu wanaofaa kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti
na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake
ya 218 imefuta masharti yaliyotoa fursa kwa asasi za kiraia na asasi zisizokuwa
za kiserikali kupendekeza watu watakaofaa kuhudumu katika Tume Huru ya
Uchaguzi. Kila mtu ataelewa nafasi muhimu kabisa ya Asasi za Kiraia katika
maendeleo ya Taifa letu hasa ukizingatia ni asasi hizi ndizo zinashirikiana na
serikali katika kujenga uwajibikaji na kuimarisha utawala bora nchini.
14.
Ujumbe wa Tume na Kanuni za Maadili ya
Viongozi wa Umma
Rasimu ya Warioba
katika Ibara yake ya 192(4) ilipendekeza kwamba “Mjumbe
wa Tume Huru ya Uchaguzi ambaye atakiukamasharti ya kanuni za maadili atapoteza
sifa za kuendelea kuwa mjumbe”. Masharti haya yaliwekwa kuhakikisha kwamba
wajumbe wanayaishi maadili, miiko na kanuni za utumishi wa umma hasa
ukizingatia uadilifu wa Tume Huru ya Uchaguzi ni kigezo kikubwa cha ujenzi wa
demokrasia imara na makini kwa Taifa letu. Katiba Inayopendekezwa katika Ibara
ya 219 imeyafifisha na kuondoa masharti ya moja kwa moja kama yalivyokuwa
katika rasimu ya Warioba.
15.
Wajibu wa Tume Huru ya Uchaguzi
Rasimu ya Warioba katika ibara 193(3)(b) ilieleza bayana kwamba mojawapo
ya majukumu ya Tume Huru ya Uchaguzi ni pamoja na kuhakikisha kuna ya
uwakilishi unaozingatia jinsi. Masharti haya yanapaswa kusomwa sambamba na
masharti yaliyomo katika Rasimu ya Warioba Ibara ya 113 juu ya uwakilishi wa 50
kwa 50 kati ya Wanawake na Wanaume ambao msingi wake ulikuwa katika ngazi ya
jimbo. Ili ujue Katiba Inayopendekezwa na walioshiriki kuiandika ama kwa kujua
au kwa kutokujua na kwa hila wamefuta masharti ya usawa kati ya wanawake na
wanaume ni pale walipofuta jukumu la Tume kusimamia usawa wa jinsi, ukisoma
Katiba Inayopendekezwa ibara ya 220(3) utagundua masharti hayo hayapo.
KUMBUKA UKISEMA HAPANA MUDA UKIFIKA, NA KWA MUJIBU WA KIFUNGU CHA 35 CHA SHERIA YA KURA YA MAONI, BUNGE MAALUM LITAITISHWA TENA KWENDA KUREKEBISHA MAPUNGUFU HAYA NA KUZINGATIA MAONI YA WANANCHI. MJULISHE MWINGINE HARAKA
NA USIKOSE KUSOMA GAZETI LA RAI ALHAMISI NA MWANANCHI JUMAPILI KWA MAELEZO MAPANA ZAIDI.
No comments:
Post a Comment