Saturday, April 23, 2016

SALAMU ZANGU KUTOKA MUSOMA

                                Hapa nikila kiapo cha nafasi ya Madaraka ya Mkuu wa Wilaya
                                Hapa nikisaini kiapo
                                Hapa nikitoa neno kwa umma wa wana Musoma na watendaji wa Halmashauri
                                                Picha ya pamoja, Mkuu wa Mkoa Mhe. Magesa Mulongo na Wakuu wa Wilaya wenzangu wa Mkoa wa Mara

SALAMU ZANGU KUTOKA WILAYA YA MUSOMA

Ndugu zangu wapendwa na watanzania, nawasalimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa kibali. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini, kunipa heshima na dhamana ya kuwa Msaidizi wake katika nafasi ya madaraka ya utumishi na uongozi kama Mkuu wa Wilaya ya Musoma.

Wilaya ya Musoma ina maeneo mawili ya kimamlaka kwa maana ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Musoma na yenye zaidi ya wakazi 360,000. Dhamana hii niliyopewa na Mhe. Rais, inanilazimu kuhakikisha ustawi wa watanzania waishio Wilaya ya Musoma unaimarika, dhamana hii inakwenda sambamba na kuhakikisha Serikali (Kuu, Manispaa na Halmashauri) tunaenenda katika namna ambayo inakuza na kuongeza tija kwa maisha ya wananchi tuliopewa dhamana ya kuwahudumia na kuwaongoza.

Nimeupokea Uteuzi wa Mhe. Rais kwa furaha na heshima kubwa, Nimewaahidi wakazi wa Musoma kuifanya Musoma MFANO wa Kuigwa katika kila nyanja, ni lazima tushirikiane, tushauriane, tusaidiane na kuelekezana katika namna ambayo ni ya UWAZI na inazingatia misingi ya UKWELI, HAKI, UMOJA, UWAJIBIKAJI na UADILIFU.

Kwa kipindi cha mwezi hivi nitapotea ili kujifunza na kuielewa Musoma, kuwafahamu na kuwajua watumishi wenzangu katika Wilaya ya Musoma.

Hapo awali nalipata heshima na fursa ya kuaminiwa dhamana ya uongozi katika ngazi ya Kitaifa kama Kamishna wa Tume ya Katiba. Kazi ya Ukamishna wa Tume ya Katiba, ilinipa fursa ya kuiona Tanzania, kuielewa Tanzania, kuijua misingi ya kuanzishwa nchi yetu. Kazi ya Katiba ilinipa fursa ya kutembelea Nchi nzima na kuzijua kero, changamoto, shida, manung'uniko, lakini pia nilijua fursa adhimu mbalimbali zilizopo katika nchi yetu. Nalipata bahati ya kukaa Mkoa wa Mara kwa miezi miwili ikiwemo Wilaya ya Musoma. Kazi ya Katiba ilinipa fursa ya kuiona Tanzania katika jicho la Uongozi wa Nchi lakini pia kusikiliza matakwa, matamanio na matarajio ya wananchi wenzangu wa Tanzania. Nilipata fursa ya kufanya kazi na viongozi waliopo madarakani katika ngazi ya Taifa na viongozi wastaafu na hakika nimejifunza mengi na ninaendelea kujifunza mengi zaidi kutoka kwa viongozi hawa. Wamenifunza juu ya Misingi ya Taifa, Katiba, Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo, Utamaduni na desturi za Serikali na Mamlaka za Nchi.

Mheshimiwa Rais ameniamini na kuniongeza fursa ya kuifahamu Nchi yangu kwa kukaa na wananchi wetu kila siku kama mtu mwenye nafasi ya madaraka (dhamana) ya kushirikiana na wananchi kutatua changamoto zao na kuhakikisha dhamira na ndoto ya Mheshimiwa Rais ambayo ameelekezwa na watanzania inatimia na kuwa hakika kweli.

Mimi nahisi kupendelewa kipekee, Mkoa wa Mara na hasa Musoma ndio Muasisi wa Taifa hili alizaliwa na kukulia, lakini pia wazee wangu wa nguvu ninaowapenda kupitiliza (hawa ni kama nimpendavyo Mzee Polepole) wamezaliwa katika Mkoa huu, Mzee wa Nguvu Mhe. Joseph S. Warioba, Mzee wa Nguvu Joseph W. Butiku na Balozi Marwa. Hili linanipa mguso wa kipekee sana kujituma na kuuishi utume wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa kujitoa maisha yake kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Kwa hili Nakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipendelea 
Kama kazi ya Tume ilikuwa Darasani, Hapa niko Maabara, kufanya majaribio na utekelezaji wa elimu niliyoipata shule na kutoka kwa malezi na maongozi ya viongozi ambao nimepitia mikononi mwao.
Mpaka sasa nimetambua hakika hakuna kazi nyingine kwa wakati huu ambayo itaniweka karibu na wananchi na kuwaelewa kama nafasi ambayo Mheshimiwa Rais amenipa dhamana ya kumsaidia.
Kwa msaada wa Mungu hakuna kero ambayo hatutaitatua, hakuna changamoto ambayo hatutafanyia kazi na hakuna kero ambayo hatutaishughulikia.

Nitaendelea kutumia fursa hii kuendelea kujenga uwezo wa vijana wenzangu katika uongozi maana sasa tumepata "kisa mafunzo"

Kipekee nimshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Magesa Mulongo, ananipa ushirikiano, maongozi, maelekezo, ushauri na amenipa uhuru wa kutenda na kujiamini au kimombo "to exercise leadership". Yeye ana upeo Mkubwa na Uzoefu, na hakika uwepo wake Mkoa wa Mara unatosha kutupa hamasa ya kumsaidia kufikia Mara ambayo ni Mkoa wa Mfano kwa Tanzania.

Niwashukuru Wakuu wa Wilaya wenzangu wa wilaya zote za Mkoa wa Mara, upendo mlionionesha mpaka leo hakika umenifanya nisiikose (nisi-imiss) Dar es Salaam, ninyi ndio ndugu zangu kiutumishi na kiuongozi, nitashirikiana nanyi, nitajifunza kwenu na nitawaomba ushauri kila mara.

Kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Musoma, nina maelekezo ya kuwahudumia kwa kauli mbiu na falsafa ya HAPAKAZITU!!

Mungu awabariki

Mimi Rafiki yenu Mpendwa

Tuesday, March 29, 2016

KUHUSU MCC KUSITISHA MSAADA WA MCC 2 NA SHUGHULI ZAKE TANZANIA: MTIZAMO



Nianze na nukuu hizi mbili kuntu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere- Mwenyezi Mungu amrehemu.

“Democracy is not a bottle of Coca-Cola which you can import. Democracy should develop according to that particular country”. June 1991 in Rio De Janeiro, Brazil

"Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza. Demokrasia lazima ikue na kuendelezwa kulingana na nchi husika". Juni 1991 Rio De Janeiro, Brazil (Tafsiri ni yangu)

“No nation has the right to make decisions for another nation; no people for another people”. From ‘A Peaceful New Year’ speech, Tanzania, January 1968

"Hakuna Taifa lina haki ya kufanya maamuzi juu ya Taifa lingine; wala watu juu ya watu wengine ". Hotuba ya Amani ya Mwaka Mpya, Tanzania, Januari 1968 (Tafsiri ni yangu)

Hili la Marekani na uamuzi wa MCC ni jambo la mpito na haliwezi kuua mahusiano yetu na Marekani. Tanzania na Marekani zinashirikiana kwa mambo mengi na MCC ni sehemu tu tena ni eneo jipya la ushirikiano. Uamuzi huu ni jaribio kwa uhuru wa Taifa letu. Hakuna namna nyingine ila kushinda hili kama tulivyoshinda mengine huko nyuma. Kwa wale ambao wameuona umri watakumbuka namna tulivunja uhusiano na Ujerumani Magharibi 1964 pale walipotaka kuwa na kauli hasi dhidi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Tulivunja uhusiano na Ujerumani Magharibi baada ya kutaka kuingilia Uhuru wa Mataifa Mawili huru yaliyoamua kuungana na kuunda Nchi Mpya ambayo leo tunajivunia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 1965 Tulivunja uhusiano na Uingereza kufuatia na kitendo cha wazungu wachache kujitangazia Uhuru (Unilateral Declaration of Independence) kule Rhodesia na uingereza kukaa kimya na kushindwa kuchukua hatua stahiki.

Tulivunja Uhusiano na Uingereza kuieleza Dunia kwamba Uhuru wa nchi za Afrika ni kipaumbele muhimu kwa Tanzania.  Jambo tunalopaswa kufahamu ni kuwa MCC 2 toka mwanzo imekuwa ni mtihani  dhidi ya uhuru wetu. Napenda ieleweke kwamba kipindi hiki kilichotokea sio kuvunjika kwa uhusiano wetu na Marekani bali taasisi ya MCC ndio imesitisha msaada wao kwetu, lakini mahusiano yetu na marekani bado yako pale pale, na si Marekani au Tanzania inayoweza kuugharimu uhusiano wetu.

MCC 1 ilikuwa ni chambo cha kutuvuta na tulipewa bila masharti tena hela nyingi dola milioni 698 na ni fedha tulizopewa moja kwa moja na kupewa uhuru wa kuamua tuzitumieje. Tanzania ilitakiwa kuainisha maeneo kisha wao wanatoa hela. Ndio maana miradi kama ile barabara ambazo hazikuwa zikipata ufadhili kwa kuwa hazikuonekana ni za kiuchumi na miradi ya maji ya Morogoro na kwingineko iliingizwa humu na kupata ufadhili. MCC 2 sio hivyo. Kwenye MCC 2 walengwa wakubwa ni sekta binafsi ya Marekani, hapa kuna mtego hapa, hapa ni biashara hapa.

Mchakato wa MCC 2 ulipoanzishwa, wafanyabiashara kwa kushirikiana na Maseneta wakaanzisha hoja kuwa kwanini Marekani inatoa fedha kwa ufadhili katika nchi ambazo China ndio wenye kufaidika na fedha hizo? Wakaleta hoja ya kuwa Serikali ya Marekani ifanye jitihada ya kuweka fedha kwa kusaidia Sekta Binafsi ya Marekani kupenya Afrika.

Ukaitishwa mkutano wa US-Africa Summit na agenda kubwa ikawa Power Africa. Katika Power Africa, Marekani ikalichagua eneo la Nishati (si uzalishaji viwanda) kwa kutambua kuwa ndio eneo pekee wanaloweza kushindana na wachina. Wakasema wataelekeza fedha huko kuisaidia Afrika kutatua tatizo la nishati ambalo ndio pembejeo ya viwanda. Wakaweka sharti kuwa fedha hizo na miradi hiyo itatekelezwa na Sekta Binafsi ya Marekani.

Ndio sababu wengi wenu mtakumbuka hata Rais Obama alitangazia dhamira ile pale Ubungo kwenye Mitambo ya Symbion Power na sio kwamba alipenda kwenda kutembea Ubungo. Kuanzia hapo kumekuwepo na shinikizo kubwa sana na masharti magumu na yenye kuhamahama (shifting goal post) kutaka kuibaka sekta ya nishati nchini ikiwemo mageuzi ya TANESCO. Zikaainishwa hatua kadhaa,ambazo utekelezaji wake baadhi ni kisheria na kisera na hivyo haziwezi kwenda kwa deadline walizotaka. Kila bodi ikikutana wanaibua hiki na kile lakini wakisema hela watatoa. Hela hizi zikawa zimeshikiliwa kama chambo ukisogelea zinasogea, ni sawa na ule mchoro wa Mpanda Punda aliyeshika fimbo yenye majani na akiielekeza mbele ya punda, kwamba punda ataendelea kuyafuata majani akidhani atayafikia kumbe ndio anaupiga mwendo. Hatimaye wakasema wanasubiri uchaguzi mkuu jambo ambalo halihusiani na madai ya mwanzoni. Baada ya uchaguzi wakaibuka na suala la Zanzibar.

Hivyo, uamuzi wao wa leo ni uamuzi uliotarajiwa. Pia ni uamuzi wenye madhara kwa sekta binafsi ya Marekani pia ambayo ndio ilikuwa itekeleze miradi hiyo. Kama Taifa ni muhimu kulinda utu na uhuru wetu. Ndio msingi wa sera yetu ya nje toka mwanzo na hata sasa. Tumetofautiana na Marekani katika hili tutapatana katika mengine. Ndio uhai wa maisha ya diplomasia.

Wao nao wanayo hadhira ya wapiga kura wao wanayojaribu kuituliza huko nchini kwao kwa uamuzi huu. Tunapaswa kuheshimu uamuzi wao kama ambavyo wanapaswa kuuheshimu wetu. Hatimaye baadae tutapatana. Marekani inaihitaji Tanzania zaidi na Tanzania inaihitaji Marekani. Marekani inahitaji MCC 2 zaidi hali kadhalika Tanzania inahitaji MCC 2.

Mahusiano ya Tanzania na Marekani hayakuanza na hayataisha na MCC. MCC imeyakuta na itayaacha.

Kama marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ndio kigezo, basi Marekani isingekuwa inatoa zaidi ya Dola Bilioni 3 kila mwaka kwa Egypt iliyo chini ya utawala wa kijeshi kwa sababu ya kuununua ugomvi wa Egypt na Israel na isingetoa kiasi cha dola bilioni 6 kwa Israel kila mwaka kwa yale wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina.

Huu ni wakati ambao Taifa linawaita Wazalendo wake. Wazalendo wasimame na kusema 'Nchi yangu KWANZA, iwe Sahihi au Imekosea" na Makuwadi watashangilia na kusema "si mnaona sasa kiko wapi?".

Huu ni wakati wa kujifunga mikanda na kulinda heshima yetu kama Taifa letu. Tuna vyanzo vya mapato vingi sana ambavyo hatujaanza kukusanya mapato, tuwe wabunifu na tusibweteke na kutegemea mapato yataongezeka maradufu kwa vyanzo vile vile.

Niseme kwa uchache, sababu walizotoa MCC, na ieleweke aliyetoa tamko ni MCC, heri lingetoka tamko hili Wizara ya Mambo ya Nje au Ikulu ya Marekani, moja ni Zanzibar na pili ni Sheria ya Makosa ya Mitandao (Cyber crimes Act).

Sasa hebu tujadili kidogo, hivi kule Zanzibar tulitaka kitokee nini pale ambapo wanasiasa walikuwa hawataki kujadiliana? Tume ile ile ya Uchaguzi ambayo bado ilikuwa na uhalali wa kikatiba na kisheria kuuitisha, kuufuta na kuuitisha tena uchaguzi ikachukua nafasi yake. Wanasiasa wasio makini wakaishia kuhamishia malumbano mitandaoni badala ya kuitafuta suluhu ya kisiasa na pale siasa iliposhindikana basi wangeitafuta suluhu katika mahakama za Zanzibar. Mezani wakashindwa, mahakamani hawakwenda. Tume ikachukua uongozi, uchaguzi ukaitishwa Wananchi wakapiga kura na sasa huko Zanzibar kuna serikali na baraza la wawakilishi. Hata mimi sifurahii sana njia waliyoichukua Zanzibar lakini ilibidi siasa za madaraka zisite ili tuanze kufanya siasa za maendeleo. Je wamarekani walitaka muujiza gani utokee huko.?

Kuhusu Sheria ya Mitandao, hata mimi siipendi, si twende mahakamani, bunge litaanza vikao muda si mrefu je wabunge si wapeleke hoja ya kuifanyia marekebisho sheria hii. Sasa Marekani (MCC) inapoweka shinikizo kwa suala la Sheria ambayo ni jambo la ndani na linaloweza kujadilika, sijaelewa. Mbona sie hatujapiga kelele Yule jamaa yao Trump alipotutusi waafrika na kusema sisi stahili yetu ni kuwekwa tena chini ya ukoloni (hapa nimechomekea tu).

INDHARI

Ni aibu kwa viongozi wa kisiasa kufurahia jambo hili, ni ishara ya ukuwadi wa kisiasa na ambao uko tayari kukumbatia mahusiano yanayotweza Uhuru wetu. It is now high time kufanya siasa safi za maendeleo (politics of development) na sio kujikita katika katika siasa za madaraka (Politics of Power).


Mwandishi, Ndg. Humphrey Polepole amenufaika na uelewa wa watu wenye uzoefu wa mahusiano ya Tanzania na nchi za Nje. Aidha, ni mnufaikaji (alumni) wa programu ya uongozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.