Mhe. Rais na Makamu wa Rais wakipata picha ya pamoja na wajumbe wapya wa Tume ya Maadili |
Kudhoofisha maadili ya uongozi ni sawasawa
na madaraka pasina udhibiti
Maadili na uwajibikaji wa viongozi wa Umma
Tanzania, kama ilivyo nchi nyingine za
Kiafrika, ina changomto za kiuwajibikaji na wananchi wametoa mawazo yao wakati
wa mchakato kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya. Wananchi walizungumzia
changamoto za uwajibikaji kwa viongozi wa umma na wakatoa sababu na mantiki ya
kuunda mfumo thabiti wa uwajibikaji.
Uwajibikaji ni dhana pana, inahusu utaratibu
endelevu wa udhibiti na uwekaji wa mipaka katika matumizi ya madaraka.
Vilevile, ina maana ya kuwepo utaratibu wa kuwalazimisha wenye madaraka kufanya
wanayotakiwa kuyafanya na kuacha kufanya wasiyotakiwa kuyafanya na ya kujibu
maswali au hoja zinazohusiana na matumizi ya madaraka aliyopewa. Kwa mantiki
hii, uwajibikaji unamaanisha pia kipengele cha adhabu kwa wale wanaotumia
madaraka ya umma vibaya. Kwa hiyo, dhana ya uwajibikaji inahusu masuala yafuatayo:
kwanza, uwepo wa mfumo wa udhibiti wa madaraka; pili, uwepo wa utaratibu wa
kuwalazimisha wale walio na madaraka kutekeleza wajibu wao na kuwazuia kukiuka
wajibu wao; na tatu, kuwepo utaratibu wa kuwaadhibu wenye madaraka pale
wanapokosea.
Kwa upande mwingine, maadili maana yake ni
kanuni au misingi inayoelekeza ni kitu gani kibaya au kisichofaa au kizuri au
kinachofaa. Misingi hii inaweza kujengwa katika utamaduni wa jamii husika.
Vilevile, misingi hiyo inaweza kuandikwa na kwa kanuni ya maadili. Kwa maneno
mengine na hasa kwa hali ilivyo katika nchi yetu sasa na hata kwa vizazi
vijavyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka masharti mahususi ya maadili ya viongozi
katika Katiba kama sehemu ya kujenga utamaduni wa kikatiba wa kuendelea
kudhibiti matumizi ya madaraka.
Kuna aina nyingi za uandishi wa Katiba, moja
ni ile ambayo kitaalamu huitwa “instrumentalist approach” Katiba hizi huwa
hazijipambanui sana, kwa asili yake huwa zinaweka misingi na kujenga taasisi,
huwa fupi na maeneo mengi huja kufanyiwa kazi na sheria zitakazotungwa na
Bunge. Aina ya pili ni ile inayoitwa “Programmatic approach” ambayo huwezesha
uandishi wa Katiba za mfano wa Katiba ya uhuru wa Taifa la Ireland. Ni Katiba
ambayo huweka bayana ndoto, malengo makuu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za
serikali na sera za kitaifa ambazo kwa ujumla wake katika Katiba hutanabaisha
dira ya nchi.
Katiba ambazo ni programmatic huweka ndani
yake pia masharti mahususi juu ya misingi ya Taifa, misingi juu ya maadili ya
Taifa, misingi ya maadili ya viongozi sambamba na utaratibu wa uwajibikaji kwa
viongozi wa umma. Moja ya changamoto kubwa katika taifa lolote lile ni namna
gani Taifa linaweza kuwa na mfumo wa kikatiba ambao unawazuia viongozi wa
Serikali kuyatumia madaraka ya umma vibaya.
Mwanafalsafa wa Uskochi David Hume katika
Karne ya 18, alipata kunena haya, “tunapotengeneza mfumo wa Serikali katika
Katiba na kuweka udhibiti na urari wa madaraka ni vizuri kuzingatia kuwa kila
mtu siyo mwaminifu na kwamba binadamu yeyote katika matendo yake mengi huwa
hana malengo mengine isipokuwa kutafuta manufaa binafsi. Hume anaendelea kusema
ni lazima kuweka utaratibu wa kuyadhibiti madaraka hayo ili mtu huyo aweze
kutoa ushirikiano wake katika masuala ya umma. Anaonya kuwa tusipofanya hivyo
tutajisifu kuwa tuna katiba lakini kumbe hatuna usalama wa mali na uhuru wetu
isipokuwa tu kwa matakwa ya watawala au viongozi wetu, na jambo linapotolewa
kwa utashi wa viongozi na hasa katika mambo ya msingi kama hatutakuwa na
usalama kabisa. Kwa ujumla, mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa madaraka wanayopewa
viongozi ni lazima yadhibitiwe kikatiba; haifai kumwamini mtu kwa sababu ni
vizuri kila mtu achukuliwe siyo mwaminifu au kwa kimombo anasema “every man
ought to be supposed a knave”.
Maadili katika Rasimu ya Warioba ukilinganisha na Katiba Inayopendekezwa
Rasimu ya Katiba Toleo la Pili ilijaribu kwa
mara ya kwanza baada ya marekebisho makubwa yaliyofanyika mwaka 1984 kwa Katiba
ya Mwaka 1977 yaliyoigeuza kwa sehemu Katiba ya Mwaka 1977 kuwa “programmatic”.
Licha ya marekebisho hayo bado Katiba ya mwaka 1977 haikuwa imejipambanua
ipasavyo ili kuendana na mahitaji ya wakati, yaliyohitaji misingi ya maadili na
uwajibikaji pamoja na uanzishwaji wa taasisi huru za kusimamia maadili na
uwajibikaji wa viongozi wa umma.
Wengi wenu mtakuwa mlishuhudia kile
kilichokuja kuwa maarufa miongoni wa mitandao ya kijamii kama sinema ya Baraza
la Maadili. Iliitwa sinema kwasababu watuhumiwa waliopata kuhojiwa katika
baraza letu la Maadili chini ya Jaji Msumi hawakuonekana kuitetemekea Mamlaka
ile ambayo ndio ina dhamana ya kuwawajibisha viongozi wanaokwenda kinyume na
maadili ya uongozi. Hata pale waandishi walipomhoji mwenyekiti wa Baraza juu ya
hatima ya viongozi wale, aliishia kusema wakimaliza kazi watapeleka taarifa kwa
mamlaka za juu. Swali ambalo wananchi wamekuwa wakijiuliza ni vipi pale ambapo
wanaohojiwa ni viongozi na watumishi kutoka mamlaka ya juu? Je utekelezwaji wa
mapendekezo ya Baraza utazingatiwaje katika mazingira hayo?, haya si maneno
yangu ninayasikia huku na huko.
Tunaposema kwamba Katiba Inayopendekezwa
imetupilia mbali masharti mahususi kuhusu maadili ya uongozi, hebu tutizame
mfano huu;- Ibara ya 15 ya Warioba ilisema “Kiongozi wa umma wakati
anapotekeleza shughuli zakiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni
mali ya Jamhuriya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitiakwa
Katibu Mkuu wa Wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikaliinayohusika,
akiainisha: (a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa
zawadi; na
(d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo”.
Kifungu cha pili cha Ibara hii kinasema “Neno “zawadi” kama lilivyotumika
katika Ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani atakachopewa
Kiongoziwa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma. (3) Bunge litatunga
sheria itakayosimamia, pamoja na
mambomengine, thamani, kiwango, aina na
uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
Katiba Inayopendekezwa imeiboresha Ibara hii
na kuandika Ibara ya 29(2)(a) ambayo kwa jumla inasema “Kwa madhumuni ya Katiba
hii, Bunge litatunga sheria itakayoweka, pamoja na mambo mengine: (a) tafsiri
ya neno zawadi, aina, thamani, kiwango na uhifadhi wa zawadi ambayo kiongozi
anapokea wakati akitekeleza
majukumu yake.
Nikitazama kwa kina maboresho hayo utagundua
masharti ambayo wananchi walikuwa wanayapendekeza kuwa yawepo katika Katiba kama
masharti mahususi, Katiba Inayopendekezwa imeyatupilia mbali na kuacha ombwe
hilo kufanyiwa kazi na Sheria zitakazotungwa na Bunge. Ikumbukwe hata wabunge
ni viongozi na masharti haya kikatiba yangewawajibisha hata wao na kama
yasingefutwa basi wangelazimika kutunga sheria ambazo misingi yake imo katika
Katiba tofauti na mtindo wa uandishi wa Katiba Inayopendekezwa ambao unawapa
viongozi nguvu za kutumia utashi wao kutunga masharti ya kuwawajibisha na
kuwadhibiti viongozi wao wenyewe. Kwa maneno mengine misingi ya kuwadhibiti
viongozi wetu na namna wanatumia madaraka yao inapaswa iwekwe kwenye Katiba na
wananchi na si viongozi waje kujitungia masharti ya kuwadhibiti wao wenyewe,
hawatatenda.
Warioba alisema katiba Ibara ya 16 kwamba
“Kiongozi wa umma - (a) hatafungua au kumiliki akaunti ya benki
nje ya Jamhuriya Muungano isipokuwa tu kwa
namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na (b) hataomba au kupokea mkopo au
faida yoyote kwa namnaau mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya
utumishi wa umma”.
Ukiitizama Katiba Inayopendekezwa namna
ambavyo imeiboresha Ibara hii katika Ibara ya 29(2) inasomeka kama ifuatavyo
“Kwa madhumuni ya Katiba hii, Bunge litatunga sheria itakayoweka, pamoja na
mambo mengine: (b) masharti ya kufungua akaunti za nje kwa kiongozi wa umma.
Hivi kweli ukisoma Ibara za 15 na 16 za
Rasimu ya Warioba, je uboreshwaje wake ni kama ulivyowekwa katika Ibara ya
29(2) ya Katiba Inayopendekezwa? Tafakarini kwa kina kabla ya kusema Katiba
Inayopendekezwa ni Bora Afrika.
Warioba alisema katiba Ibara ya 21(3) kwamba
“Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosaya: kimaadili; (b) udhalilishaji
wa mtu au wa kijinsia; au (c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa
kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu washeria za nchi au taratibu
nyingine zinazowahusu viongozi waumma.
Katiba Inayopendekezwa imeyafuta kabisa
masharti haya, kwa msingi huu tusishangae kiongozi anayetuhumiwa kwa masuala
tajwa hapo juu akaendelea kutoa huduma kwa wananchi ilhali tukijua mzizi wa
tatizo uko kwa kiongozi au mtumishi huyo wa umma.
Katiba Inayopendekezwa inapokuja katika
suala la Maadili kwakweli haijawatendea haki watanzania, hasa katika kipindi
hiki ambapo taifa letu limepitia katika kufichuka kwa tuhuma na kashfa za
ufisadi mkubwa katika taasisi zetu za serikali tena karibu katika ngazi zote.
Labda kabla ya kuwaacha niwape mfano wa
mwisho, Ukiangalia Tume ya Maadili na uwajibikaji utagundua kwa sababu ambazo
hazieleweki masharti mengi na muhimu yaliyokuwa sehemu ya majukumu ya Tume ya
Maadili kwa Rasimu ya Warioba yamefutiliwa mbali katika Katiba Inayopendekezwa.
Rejea masharti ya ibara ya 203(2)(b), (e) hadi (o) ya Rasimu ya Tume, juu ya
majukumu ya Tume ya maadali yauongozi.Ukisoma kifungu cha 231 cha Katiba
Inayopendekezwa masharti hayo yamefutwa.
Hakika Katiba Inayopendekezwa itaturudi
nyuma kabisa katika uandishi bora wa Katiba Barani Afrika, lakini fursa ya
kuirekebisha kabla haijawa rasmi mpya iko pale pale ukirejea kifungu cha 35(3)
na (4) cha Sheria ya Kura ya Maoni.
Karibu kutoa Maoni
Karibu kutoa Maoni
Hongera Kijana
ReplyDelete