Saturday, April 25, 2015

MIAKA 51 YA MUUNGANO: HUU NI WAKATI MUAFAKA WA KUWEPO HAKI ZA WANAWAKE KIKATIBA

Katiba Inayopendekezwa imefuta misingi ya usawa kati ya wanawake na wanaume

Hivi karibuni nilipata wasaa wa kuonana na watetezi wa haki za binadamu, watetezi hawa wanawake na wanaume kutoka asasi za kiraia walinialika kujadiliana nao juu ya mchakato wa Katiba. Katika vikao viwili tulikaa pamoja, sote tulikubaliana kila mwenye uelewa au msimamo kuhusu Katiba Inayopendekezwa apewe fursa kuusema na asizongwe. Wote tulikubaliana kwamba utofauti wa mawazo ni afya kwa hakika na hasa pale wote wenye misimamo wanapojenga hoja zao kwa sababu za msingi na zenye mashiko.

Nilijielekeza kuelewa hoja zao, hasa za wale ambao wanasema Katiba Inayopendekezwa imelinda haki za wanawake, nilisikiliza kwa dhamira ya kuelewa na kujifunza kutoka kwao. Baada ya mjadala niligundua kwamba wanawake walikuwa na hoja kadhaa ambazo kwa maelezo yao zilifanikiwa kuingia katika Katiba Inayopendekezwa, na kwa mantiki hiyo wanawajibika kuipigia chapuo Katiba Inayopendekezwa.

Kabla ya kufafanua namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imelitizama suala la haki za wanawake ni vema nikagusia kwa sehemu dhana ya Mahitaji ya Kimkakati ya jinsia au kwa kiingereza “Strategic Gender Needs”.

Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia na Katiba

Mahitaji ya kimkakati ya jinsia au “Strategic Gender Needs” ni yale ambayo wanawake na wanaume huyahitaji ili kubadilisha nafasi zao katika jamii, mahitaji haya yanajumuisha mgawanyo wa madaraka kijinsia, mamlaka na udhibiti wa rasilimali, fursa sawa kwa wanawake na wanaume, haki za kipato sawa kwa kazi sawa kati ya wanawake na wanaume, Mageuzi ya kikatiba, kisheria na kimfumo ambayo yanatambua nafasi muhimu ya wanawake pamoja na wanaume kwa usawa katika kuleta maendeleo ya jamii. Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ndio humlinda mwanamke dhidi ya utegemezi, umasikini, kunyanyaswa, unyonyaji au “exploitation” na kuwekwa nje ya mfumo wa kufanya maamuzi.

Mara zote Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia kwa maana ya “Strategic Gender Needs” ndio huwa ufunguo kwa Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au kwa kiingereza “Practical Gender Needs”. Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au “Practical Gender Needs” hujumuisha yale mambo ya kawaida na yanayoshikika ambayo mtu wa kawaida huyahitaji wakiwemo wanawake. Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia yanajumuisha mahitaji ya msingi katika maisha ya siku hadi siku kama vile upatikanaji wa maji, huduma za afya na ajira. Kupatikana kwa mahitaji ya kawaida ya jinsia kwa mwanamke huwa hayamwondoi mwanamke katika nafasi yake ya utegemezi, unyonyaji na kutokuwa maamuzi juu ya rasilimali zake mwenyewe.

Swali langu muhimu kwa wanawake wote, dada zangu, shangazi zangu na mama zangu wote wenye mapenzi mema na kuona utu wa mwanamke unaheshimiwa, haki za wanawake zinatolewa, zinatunzwa, zinahifadhiwa na kuheshimiwa, Je Katiba Inayopendekezwa na bila kuweka misimamo ya kisiasa imezingatia Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia au “Strategic Gender Needs”?

Katiba Inayopendekezwa inapaswa kupimwa ni kwa kiwango gani imetizama na kujumuisha Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo kwayo mahitaji ya kawaida ya jinsia hupatikana. Tunapoweza kuhakikisha uwepo wa mahitaji ya kimkakati katika Katiba, huu huwa msingi wa kuona utolewaji haki za wanawake.

Kama Katiba Inayopendekezwa imejaribu kuweka Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia pasina kuweka misingi kwa mahitaji ya kimkakati ni kazi bure kwasababu haki za wanawake zitabakia kuwa kiini macho. Kama haki za wanawake hazikubainishwa ipasavyo katika Katiba Inayopendekezwa bado mwanamke wa Tanzania ataendelea kuwa tegemezi, fukara na ushiriki wake kwenye nyanja za utoaji maamuzi zitabakia kutegemea utashi na fadhila kutoka kwa viongozi wa juu.

Tuitazame Katiba Inayopendekezwa kwa jicho la Rasimu ya Warioba

Rasimu ya Warioba Katiba Ibara ya 47(1)(b) ilisema “Kila mwanamke ana haki ya kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili”. Rasimu ililenga kujenga msingi wa kumpa mwanamke udhibiti wa rasilimali zake na kumlinda na ukatili ambao huja kama sehemu ya kumpora rasilimali alizo nazo. Mfano mzuri ni mwanamke wa kijijini na mkulima, anayelima kwa jembe la mkono na kupata mazao yake, je ni mara ngapi mwanamke huyu huwa na mamlaka juu ya wakati gani mazao yatauzwa, na yatauzwa kwa bei gani na pesa ikipatikana je mwanamke huyu huipangia matumizi yake mwenyewe?

Ukienda kwenye Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 masharti ya 47(1)(b) kutoka katika Rasimu yamefutwa, huwa najiuliza msingi wa kufuta masharti yale ya Rasimu ni upi?.

Ukiendelea kusoma Ibara ya 47(2) ya Rasimu ya Warioba inasema “Mamlaka za nchi zitaweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara hiiikiwa ni pamoja na kukuza utu, heshima, usalama na fursa za wanawakewakiwemo wajane”. Ibara hii ilikuwa ina lengo la kutoa maelekezo kwa mamlaka za nchi kutekeleza masharti yaliyoainishwa katika Ibara hii. Ieleweke pia masuala ya maendeleo ikiwemo suala la jinsia kwa asili ya Nchi yetu sio jambo la Muungano.

Kwa uelewa huu ndio maana Rasimu ya Warioba iliona Katiba itoe maelekezo kwa Mamlaka za Nchi ambazo ziko tatu ambazo ni (i) Mamlaka ya Mambo ya Muungano ambayo chombo cha utendaji ni Serikali ya Muungano, (ii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na (iii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara au Tanganyika. Warioba alijua kwamba kuna masuala ya Haki za Wanawake ambayo kila Mamlaka ingeweza kuyashughulikia kwa sehemu, nafasi na mamlaka yake. Huu ulikuwa msingi mkubwa wa kuhakikisha tunalinda Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo yangepelekea kutolewa kwa haki za wanawake raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanapatikana Tanzania Bara na Zanzibar.

Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 imeyafuta na hivyo haina masharti ya Rasimu yaliyomo katika Ibara ya 47(2) ambayo ukiacha kutoa maelekezo ya utendaji lakini pia kitaalamu ni masharti wezeshi au kwa kiingereza huitwa “enabling provision”. Najiuliza dhambi ya masharti yale ambayo baada ya kuwasikiliza Wananchi na hasa wanawake na zaidi wanawake wajane walio ona ingefaa yawepo kikatiba.

Ili ujue Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanawake wanakubwa sehemu ya wanufaikaji wa Katiba Mpya na Bora na inayotokana na maoni ya Wananchi. Ukisoma Ibara ya 54 inaeleza kuhusu usimamizi wa haki za binadamu na ukiendelea na kusoma Ibara ya 54(1)(a) inaeleza “Katika kutafsiri masharti ya Sura hii ya Haki za Binadamu, Mahakama au chombo kingine chochote cha kufanyauamuzi kitazingatia mambo yafuatayo:- haki ya usawa, utu na uhuru wa mtu binafsi”. Kwa kiingereza haki ya usawa ndio huitwa “equality principle”, kwamba tunapozitoa haki, lazima tuangalie je wanawake wapo? Je wanaume wapo?

Na neno “Utu” ni kuhusu masikini na matajiri wa Taifa letu, tunapogawana keki ya Taifa je nani waanze kula, matajiri au masikini? Rasimu ya Warioba ilipendekeza katika Katiba misingi hii ya kuzingatiwa, Katiba Inayopendekezwa imeifuta yote katika Ibara ya 65, na ukiisoma Ibara hii utagundua haina masharti ya 54(1)(a). Najiuliza dhambi ya masharti haya ilikuwa nini? Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia hayawezi kuwapo kama msingi huu umefutwa.

Rasimu ya Warioba katika Ibara yake ya 113 ilieleza bayana kwamba uwakilishi katika chombo cha kutunga sheria kwa maana ya Bunge uwe nusu wanawake na nusu wanaume. Warioba alitizama mbali kwamba kwa namna ambavyo jamii yetu imejengwa katika mfumo dume ufike wakati wa kubadili fikra na kuwa na chombo cha kutunga sheria ambacho kinazingatia uwakilishi unaojengwa katika kuheshimu misingi ya usawa wa kijinsia.

Warioba alijua kwamba wakulima wengi nchini ni wanawake, alijua pia kwamba wahanga na wanufaikaji wa mfumo wa afya nchini ni wanawake na kwa mantiki hiyo watu ambao wako kwenye sehemu na nafasi nzuri ya kuwasilisha mawazo ya watanzania ni wanawake sambamba na wanaume. Na sisi kama watu ambao Rais alitupa dhamana ya kufanya kazi na Mzee Warioba tulijiridhisha kwamba hata katika Bunge wanaolala wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea ni wanaume na sio wanawake.

Warioba ni kama alibashiri kwamba iwapo tungekuwa na Bunge ambalo lingekuwa na uwakilishi uliosawa kati ya wanawake na wanaume ndani ya muda mfupi watanzania wangetambua wanawake wana uwezo tena hata zaidi ya wanaume na ingewajengea imani kwamba hata uongozi wa nchi ungeweza kuaminiwa kwa mwanamke.

Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 129 imefuta masharti yaliyokuwemo katika Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 113(3) yaliyosema “Katika kila Jimbo la Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamme”. Huu ulikuwa msingi wa kuhakikisha kuna usawa wa jinsi na jinsia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Sijaelewa msingi wa kufutwa kwa msingi huu ambao ungepelekea kuzingatiwa kwa asilimia 100 kwa Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo yangewakomboa mamilioni ya wanawake ambao wanakumbana na unyanyasaji uliojengwa fikra za wengi katika Taifa letu.

Ukisoma Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 193(3)(b) ilizungumzia majukumu ya Tume Huru ya Uchaguzi kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuna uwakilishi unaozingatia jinsi. Tafsiri ya Ibara hii ni kwamba kama Tume Huru ya Uchaguzi ikija katika Jimbo na hakuna mgombea mwanamke basi ujue uchaguzi hakuna na vivyo hivyo kinyume chake. Ukiisoma Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 220(3) utagundua ni kipengele cha “uwakilishi unaozingatia jinsi” ndicho pekee kilichofutwa. Nawauliza nyote dhambi ilikuwa nini hata kufuta jukumu hili la Tume Huru ya Uchaguzi?


Ni miaka 51 ya Muungano, unadhani bado wanawake wanatakiwa kupewa nafasi za uongozi kwa mbinu za miaka ya 70, kwa maana ya viti maalum na kwa kusubiri utashi na fadhila za viongozi wakubwa? Je wanawake hawastahili haki sawa na wanaume? Nimeandika nikiwa kama mwanaume anayethamini nafasi muhimu ya wanawake katika ujenzi wa Taifa letu na anaye amini kwamba Taifa hili haliwezi kupiga hatua kama tutaendelea kuwahadaa wanawake, wapenzi wetu, dada zetu, shangazi zetu, mama zetu na bibi zetu. Niwatakie Miaka 51 ya kusherehekea Muungano wetu. Muungano wa Haki na Heshima Udumu Milele.!

No comments:

Post a Comment