Kumekuwa na kuchanganya mambo katika majadiliano yetu katika kila kona juu ya suala la shirikisho ambalo limetajwa katika ibara ya kwanza ya Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Warioba na suala la muundo wa serikali tatu katika Jamhuri ya Muungano lililomo katika Sura ya Sita ya Rasimu ya Warioba. Imefikia hatua sasa wapo wanaodhani ukizungumzia shirikisho maana yake ni serikali tatu na ukizungumzia serikali mbili umekataa shirikisho. Mtizamo huo sio sahihi kama nitakavyoeleza baadaye.
Pili inaelekea kuwa wapo watu ambao wana mzio (allergy) na neno
“Shirikisho” na hivyo kulichukia na kulipa maana hasi ambayo siyo sahihi. Kwa
watu hao kwao neno shirikisho wamelipa maana ya kubuni ya kifo cha Muungano.
Mtizamo huo sio sahihi na ni mtizamo
potofu kabisa. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa kufa kwa Miungano duniani na
dhana ya shirikisho. Kwani ipo Miungano ya Serikali moja ambayo ilikufa katika
kipindi kifupi sana kama ule wa Misri na Syria na ipo Miungano ya shirikisho
ambayo inadumu mpaka leo kama vile Ethiopia, Nigeria, Jamhuri ya Shirikisho la
Ujerumani, Marekani na India.
Tatu kuna dhana potofu kuwa shirikisho na muungano wa serikali tatu
unaopendekezwa katika Rasimu ya Warioba utahamasisha utaifa wa Tanganyika.
Dhana hiyo pia ni potofu kwani zipo nchi zenye muungano wa serikali moja kwa
sababu ya kulazimisha kufuta utambulisho wa upande mmoja wa Muungano huo leo
baada ya zaidi ya miaka hamsini ya Muungano wao upande ule ambao ulizikwa
utambulisho wake unadai sasa utaifa wake. Nchi hiyo ni Jamhuri ya Cameroon
ambayo ni muungano wa serikali moja wa
iliyokuwa “French Cameroon” na “British Cameroon” zilizoungana mwaka 1961. Hali
hiyo imechambuliwa vizuri sana na
Verkijika G. Fanso katika makala yake “Anglophone and Francophone Nationalism in Cameroon” [The Round
Table (1991) 350, 281 – 296] na pia katika makala ya Piet Konings na Francis G.
Nyamnjoh “The Anglophone Problem in Cameroon” [The Journal of Modern African
Studies, 35, (1997), 207 – 229]
Nilianza kwa kusema kuwa suala la shirikisho na suala serikali tatu
hayahusiani ingawa yanaingiliana. Mjadala wa aina ya Muungano wa Tanzania
umekuwa na ubishani mkubwa kwa miaka mingi. Je Muungano huu ni serikali moja
yaani “Unitary State” au ni wa shirikisho yaani “Federation”?.Wapo wanazuoni
maarufu wa sheria hapa Tanzania na wanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao
wamechambua Muungano huu wa sasa wa serikali mbili na kuhitimisha kuwa ni wa
mfumo wa Shirikisho. Hii ina maana hata sasa tuna shirikisho la serikali mbili.
Kwa hali hiyo basi Rasimu ya Warioba ilipendekeza tutoke kwenye shirikisho la
serikali mbili la sasa na kwenda katika shirikisho la serikali tatu.
Miongoni wa wanazuoni hao ni Profesa P.B. Srivastava ambaye alifundisha
sheria za Katiba (Constitutions and Legal Systems of East Africa) na Sheria za
Utawala (Administrative Law) katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam katika miaka ya 1980 ndiye aliyechambua kwa kina muungano wa Tanzania na
kuhitimisha kuwa ni wa aina ya shirikisho katika Mhadhara wake wa Kiprofesa
(Professorial Inaugral Lecture) wake alioutoa Machi 1982 iitwayo “The Constitution of the United Republic of
Tanzania 1977:Some Salient Features – Some Riddles”.
Miaka minane baadaye, yaani mwaka 1990,
msomi mwingine Profesa Issa Gulamhussein Shivji, ambaye kwa miaka yote
kabla ya hapo alikuwa akijihusisha na Sheria za Kazi (Labour Law) alitoa
Mhadhara wa Kiprofesa (Professorial Lecture)
wake uitwao “The Legal
Foundation of the Union in Tanzania’s
Union and Zanzibar Constitutions” naye alihitimisha kuwa Muungano wa sasa
wa Tanzania ni wa mfumo wa shirikisho kama nitavyofafanua baadaye.
Wanasiasa wa CCM ambao walisema kuwa Muungano wa sasa ni shirikisho ni
Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Msimamo huo uliungwa mkono na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika hotuba iliyotolewa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Brigedia – Jenerali Ramadhan Haji Faki mwaka
1983 alipojibu hoja ya ushauri kuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Moringe
Sokoine aliposhauri Chama cha Mapinduzi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
ina mamlaka juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. [Zanzibar Government: A Reaction to Prime Minister Ndugu Sokoine’s
Advice to the Party to Restructure the Government given to the Party and
Government Leaders Tabled by the Chief Minister to the House of Representatives,
Zanzibar Printing Press, 1983, p. 5). Msimamo huo pia uliungwa mkono na
aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Wolfgang Dourado.
Msimamo huo wa Mzee Jumbe kuwa muundo wa Muungano ni shirikisho ulileta
kuchafuka kwa hali ya hewa wakati wa mjadala wa Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano na Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Pamoja na Mwasisi wa
Muungano na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutofautiana na
Mzee Jumbe, kama ilivyoelezwa katika Randama ya Rasimu ya Warioba katika
ukurasa wa tatu, nanukuu:
“Kwa mujibu wa kumbukumbu za kikao cha halmashauri ya Taifa ya Chama cha
Mapinduzi katika mkutano wa tano ambao ulikuwa maalumu uliofanyika Dodoma
Januari 24-30, 1984, Mwalimu Nyerere alitamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ukiangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa Shirikisho lakini ukiangalia
kutoka Tanzania Bara ni serikali moja. Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi
aliyesema kuwa Muungano wa Tanzania umeunda shirikisho (Federation) na sio
serikali moja (Unitary State).
Mfumo wa Shirikisho unaopendekezwa katika Rasimu ya Warioba unaendeleza
hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Nchi na ni Dola moja lenye
mamlaka kamili yenye serikali tatu, shirikisho hili linatokana na muungano wa
hiari wa Tanganyika na Zanzibar ambazo zilikuwa Jamhuri zenye mamlaka kamili
kabla ya kuungana tarehe 27 Aprili 1964”
Msimamo huo wa Mwalimu Nyerere kuwa kwa upande wa Zanzibar Jamhuri ya
Muungano ya Muungano ina sura ya shirikisho inafanana kwa kiasi fulani na
uchambuzi wa mtaalam nguli Mwingereza wa masuala ya katiba Professor S.A. de
Smith ambaye katika kitabu chake kiitwacho Constitutional and Administrative
Law, 2nd Edition, 1973, p.33 anasema kwamba:
“Tanzania is part federation, since Zanzibar has
exclusive fields of competence both in theory and in practice, but for
political reasons the term ‘federal’ does not appear in the constitution and in
as much as it implies a degree of disunity as well as diversity.”
Kwa kiswahili akimaanisha “Tanzania kwa sehemu ni shirikisho kwa sababu Zanzibar
ina mamlaka yake kamili ya ndani kinadharia na kivitendo lakini kwa sababu za
kisiasa neno shirikisho halionekani katika Katiba huku hali hii ikionesha
kiwango cha utengano pamoja na utofauti” (Tafsiri ni yangu).
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha “Uongozi wetu na
Hatima ya Tanzania” katika ukurasa wa 15, alipata kusema “Nchi mbili
zinapoungana na kuwa Nchi Moja mifumo ya kawaida mifumo ya miundo ya Katiba ni
miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na Nchi mpya
inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja.
Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa
na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu
ya mambo yaliobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale
ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana basi nchi hizo huwa huru.
Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu,
Serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali
zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”
Muundo wa Shirikisho, ambao ni tofauti na muundo wa serikali moja. Katika
muundo huu, nchi zinapoungana kunakuwa na ngazi mbili za serikali, yaani
serikali ya muungano au shirikisho na serikali za washirika. Serikali ya
Muungano inakuwa na mamlaka kwa masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya muungano,
wakati serikali za washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba kushughulikia
mambo yote yasiyo ya muungano.
Sababu nyingine ya kuendelea kupendekeza muundo wa shirikisho lenye
serikali tatu ni uhalisia kwamba Muundo wa Shirikisho utaendelea kuhifadhi
asili, taswira na hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jumuiya ya
kimataifa kwa mujibu wa Kifungu cha 2 cha Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933
unaohusu Haki na Majukumu ya Nchi (the Montevideo
Convention on Rights and Duties of States) unaosema na ninanukuu “the
federal state shall constitute a sole person in the eyes of international law”
inayomaanisha nchi yenye muundo wa shirikisho katika sheria za kimataifa ni
nchi na dola moja.
Katika mfumo huu, kwa kawaida mamlaka ya mwisho au mamlaka kamili
(sovereignty) yanabaki katika serikali ya shirikisho. Kama nilivyosema,
utambulisho wa nchi katika mahusiano ya kimataifa na vyombo vya ulinzi na
usalama hubaki katika serikali ya shirikisho. Sifa nyingine ya shirikisho ni
kuwa mwananchi anatawaliwa na serikali mbili ilihali katika muundo wa muungano
wa serikali moja mwananchi anatawaliwa na serikali moja pekee. Muungano wa
Tangannyika na Zanzibar siku zote umekuwa na sura mbili. Kwa wananchi wa
Zanzibar wamekuwa katika shirikisho tangu mwaka 1964 kwa sababu wanatawaliwa na
serikali mbili (serikali ya muungano na serikali ya Zanzibar). Kwa upande wa
Tanzania Bara kuna sura ya muungano zaidi kwa sababu kuna serikali moja kwa
maana serikali ya Tanzania Bara au Tanganyika haipo.
Sababu nyingine ya kupendekeza muundo wa shirikisho ni kukuza demokrasia
kwa maana ya kutoa mamlaka zaidi kwa nchi washirika kujiamulia mambo yao
wenyewe. Hii inatekeleza madai ya miaka mingi ya Zanzibar kuwa na Shirikisho la
Serikali Tatu tangu wakati wa Mzee Aboud Jumbe Mwinyi na baada ya hapo ambalo
liliungwa mkono na watu wengi akiwemo Profesa Issa Gulamhussein Shivji. Hoja
hiyo ya Prof. Issa Shivji kuunga mkono madai ya Zanzibar ya kuanzishwa kwa
mfumo wa shirikisho lenye serikali tatu limo katika kitabu chake kiitwacho
“Pan-Africanism or Pragmatism?: Lessons of the Tanganyika – Zanzibar Union
(2008 ukurasa 250 anaposisitiza kuwa;
“A demand for a three government federation, greater
autonomy for Zanzibar, reduction in union matters, from Zanzibar was a demand
for the right to self-determination, a democratic demand” [ yaani, madai ya
shirkisho la serikali tatu na kupunguzwa kwa mambo ya muungano yanayotolewa na
Zanzibar ni madai ya haki ya kujiamulia mambo yao na ni haki ya kidemokrasia
Uk. I.G. Shivji, Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika- Zanzibar
Union,2008, P. 250]
Pia, Chini ya mfumo wa Muungano wa Shirikisho, ugawaji wa madaraka huwekwa
kwenye Katiba kiasi kwamba katika hali ya kawaida serikali ya muungano haiwezi
kuingilia na kunyang’anya madaraka ya serikali za washirika bila ya kufuata
utaratibu uliyowekwa kwenye Katiba. Nchi ambazo zimeimarika katika mfumo huo ni
pamoja na Marekani, Kanada, India, Brazil, Ujerumani, Uswisi, Australia,
Nigeria na Ethiopia. Mfumo wa Shirikisho unawezesha nchi washiriki kuwa na
nguvu kubwa ya kushughulikia maslahi ya pamoja huku kila moja ikiwa na mamlaka
ya kushughulika masuala yasiyo ya pamoja. Mfumo huu unawapa washirika wa
Muungano fursa ya kuhifadhi utambulisho wao wa kihistoria.
Sababu nyingine muhimu ya kupendekeza muungano wa shirikisho la serikali
tatu ni kuweka bayana mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano zilizobainishwa
na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano
ya Mwaka 1977 katika Ibara ya 4, 34, 64 na 102. Mamlaka hizo ni Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya
Tanzania Bara. Hoja hii inatiliwa nguvu
na Msomi Maarufu wa Masuala ya Katiba Professor Srivastava, kwamba:
“The United Republic envisages a
triangular system with Tanzania Mainland and Zanzibar forming two corners of
the base and the United Republic constituting the vortex. Accordingly, there
are three jurisdictional areas territory-wise and subject-wise for the
operation of governmental powers, both legislative and executive, which
necessitate existence of three governments, namely, Government of United
Republic, Government of Tanzania Mainland and Government of Zanzibar corresponding
to three jurisdictions.”
[Tafsiri
yangu: Jamhuri ya Muungano ni mfumo wa serikali tatu, Tanzania Bara na Zanzibar
zikiwa ni nguzo za pembeni na Jamhuri ya Muungano ikiwa ni kilele chake: Hivyo,
kuna mamlaka tatu kieneo na kimatumizi ya madaraka ya kiserikali, kibunge
ambayo yanalazimu kuwe na serikali tatu: yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano,
Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar] { B. P. Srivastava, 'The Constitution of the United
Republic of Tanzania 1977 - Some Salient Features, Some Riddles' Eastern Africa Law Review 11-14
(1978-81}, 73-127, at pp.79-80.}
No comments:
Post a Comment