Mungu ametupa
akili, busara na hekima, kisha akatupa ufahamu, fikra na uwezo wa kuunda
taasisi ili zitusaidie kuturatibu, kutuwezesha na kutusaidia. Kwa ufahamu
aliotupa Mungu, akatuwezesha kuchagua na kuteua kutoka miongoni mwetu watu wa
tofauti, watu wasiojipenda wenyewe, watu wenye uwezo mkubwa na maono, watu
wapole, wenye uhalali katika jamii wa kuonya na kukemea ili hawa wawe viongozi
wetu.
Uongozi ni
dhamana, ni jukumu zito, mtu uongozi hupewa na watu, hubarikiwa na hata
kulazimishwa, uongozi huwa hautafutwi kwa udi na uvumba. Katika dini zote na
jamii za watu katika historia viongozi walitengenezwa, hata wale waliozaliwa
katika mnyonyororo wa uongozi iliwapasa kulelewa kiuongozi. Ilimpasa mtu awaye
kiongozi, kuhakikisha kwamba anawaleta watu wake pamoja, masikini na matajiri,
wakulima na wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Kiongozi anapaswa
kuwa msingi imara wa umoja wa kitaasisi, jamii na Taifa kwa ujumla. Kiongozi
anayeanza na mpasuko na si umoja, kiongozi anayeanza na chuki na si upendo,
viongozi wanaoanza na makundi na si taasisi kwanza, tafsiri yake si njema, si
afya na ni muendelezo wa nyufa katika taasisi yoyote ile.
Chama cha Mapinduzi
(CCM) hivi karibuni kitatoa utaratibu na mchakato wa kumpata mgombea wa Urais
kupitia CCM. Tukumbuke tena, CCM ndio chama kilichopo madarakani sasa, hivyo
inapaswa kuonesha mfano, CCM inapaswa kuwa kioo, najua CCM imejikwaa wakati
mwingine kwa makusudi na wakati mwingine kwa bahati mbaya. Sifa kubwa ya
uongozi thabiti ni kuonesha uongozi pale ambapo watu ndani ya taasisi au kwa
ujumla Taasisi inapojikwaa. Kuonesha uongozi kunaweza kuwa katika namna nyingi,
mojawapo ni kwa hali yoyote kuukumbatia ukweli pasina kuathiri menejimenti ya
siasa
Uongozi ni kuonesha
kutokuvunjika moyo, kutokukata tamaa, kujikwaa sio kuanguka, na kama CCM imetetereka
bado inaweza kuamka tena na kuthibitishia umma wa watanzania kwamba misingi ya
kusimamia maadili na miiko ya viongozi bado iko imara kama ilivyo misingi ya
CCM ambayo kwayo iliasisiwa.
Labda nitolee mfano
wa mambo kadhaa ambayo kwa makusudi baadhi ya wana CCM wamesaidia kuteteresha
CCM. Mosi, namna ambayo chama ambacho ndio kimeshika mamlaka ya nchi na
serikali kimeshughulikia masuala ya ubadhirifu wa mali ya umma, kumekuwa na
tuhuma kadhaa wa kadhaa katika miaka 10 iliyopita. Tumeona uwajibikaji, lakini
CCM ingeweza kufanya vizuri zaidi ili kurudisha imani ambayo inaonekana dhahiri
kutetereka miongoni mwa wananchi. Uongozi wa CCM unapaswa kuwa mkali zaidi kwa
wale wanaokwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa CCM. Urafiki ni jambo
jema, lakini misingi ya CCM inapaswa kuwa juu ya urafiki wakati wowote.
Wengi wenu,
viongozi wa CCM mlikuwepo kipindi cha Mwalimu Nyerere na kwa hakika wengi wenu
ni mashahidi wa namna alitenda kama Kiongozi. Hivi kuna kipindi kigumu kama
miaka ya 80 mwanzoni? Kipindi kile ambacho ajira rasmi ziliporomoka kwa karibu
asilimia 80, matatizo ya njaa na kutetereka kwa uchumi wa nchi. Mwalimu alikuwa
mkali kweli kweli, lakini pia alikuwa kama baba, alikuwa msikivu na mpole, kama
Kiongozi mkuu ndio mwenye dira, ndiye anayetupa hamasa kupiga makasia katika
Bahari iliyochafuka ili tuelekee uelekeo sahihi na salama, ambaye kupitia kwake
watu walipaswa kuyaona matumaini, walipaswa kuiona Tanzania njema.
Mnakumbuka vikao
vya Karimjee vya kuokoa uchumi wa Taifa letu miaka ya 80 katikati, nafasi ya
Mzee Kawawa ya menejimenti ya siasa au “political management” katika vikao pale
hali ilipochafuka. Hali ilipokuwa tete, na hasira ziko juu, Mzee Kawawa kwa
busara na hekima zake alijua namna ya kutukwamua na hali ikapoa, kisha Mwalimu
akaahirisha kikao mpaka siku inayofuata, hiyo ndio ilikuwa CCM.
Leo hii nidhamu ya
baadhi ya wana CCM na viongozi imeshuka, nasikia hata kuzomeana kumo katika
vikao. Kuheshimia miongoni mwa viongozi ndio msingi mkubwa wa kujengeana imani
na kuaminiana. Viongozi wasioaminiana, hawaheshimiani, viongozi wasioheshimiana
hawapendani, na viongozi wasiopendana hawazungumzi kwa uwazi na ukweli. Tunapofika
hapo, taasisi ya chama iko mashakani, uongozi wa nchi kutoka katika chama
unawekwa rehani.
Zamani ilikuwa
tunasema zidumu fikra za Mwenyekiti, usemi huu haukuwa wa bahati mbaya, ni
kwamba Kiongozi alilitizama Taifa na akatuhamasisha kupiga juhudi kuelekea kule
wananchi wetu wanapaswa kuwa, nikizungumza kwa nahau, kule kwenye nchi ya
maziwa na asali. Leo hii fikra za Mwenyekiti si jambo tena, inaweza isiwe kama
kipindi kile cha zamani, lakini sidhani kama Mwenyekiti anapewa heshima yake
kama Kiongozi. Kuhusu ubadhirifu wa mali za umma, akaja na falsafa ya “kujivua
gamba”, hii imeshindwa kabisa na kubaki kuwa mzaha, wana CCM hawakusimama bega
kwa bega na Mwenyekiti wao. Kushindwa kwa falsafa hii kukapelekea pia kushindwa
kutoa msukumo uliostahili wa kushughulikia ubadhirifu katika serikali na vyombo
vyake.
Pili, ni Mchakato
wa Katiba, huu umekuwa ni dhihaka kwa watanzania. Mwenyekiti wa CCM ambaye pia
ndiye Mkuu wa Nchi alianzisha mchakato wa kuandikwa Katiba mpya kwa maslahi ya
Taifa la Tanzania na Wananchi wake. Nini kilitokea katika kusimamia fikra yake
hii adhimu na adimu kwa Taifa letu? Mzaha kabisa. Wako waliomhoji, ninaposema
kumhoji simaanishi katika namna ya heshima ya kutaka taarifa au maelezo kutoka
kwa Kiongozi wako, bali katika namna ya kiburi, dharau na ujuvi usio na tija
kwa CCM na kwa Taifa.
Kilichotokea ni
Mwenyekiti kukosa kuungwa mkono katika CCM katika jambo ambalo lililokuwa na
maslahi kwa Taifa. Naikumbuka dhamira yake, nayakumbuka maono yake, nayasoma
maandiko yake, nasikiliza hotuba zake, kwa hakika kilichokuja kuwa Katiba
Inayopendekezwa hakiakisi dhamira ile ya awali. Hapa CCM lazima mjirekebishe,
na iwe sasa na si baadaye, na mfanye upesi maana mkichelewa chelewa mtakuta
mtoto si wenu. Ile tabia ya ninyi kulalama kila kona ya nchi huku mkiwasema
watendaji wa serikali muiache, ninyi hampaswi kulalama, mnapowalaumu kwanini
hili na lile halijatokea na wao wanawashangaa ninyi ambao mko wengi bungeni na
mmeshika madaraka ya serikali, mnapaswa kutoa uongozi.
Kitu kibaya kabisa
ni pale ambapo Kituo cha Demokrasia (TCD) kilipopiga hatua ya kuwa na
“Makubaliano na Rais” juu ya kuokoa mchakato wa Katiba na kutoka na mapendekezo
ya kutuvusha katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na CCM ikapuuza juhudi hii kubwa.
Ninyi mnajua CCM iliwakilishwa na Kiongozi wa juu kabisa, Makamu wa Mwenyekiti,
Mhe. Phillip Mangula, na yeye hajawahi kukana kuwa sehemu ya mchakato wa TCD,
haipendezi pale ambapo Makamu wa Mwenyekiti hajakana matokeo halafu Katibu wa
Itikadi na Uenezi aje aseme chama hakiko huko. Vitendo kama hivi Wananchi na
wanachama wanavitizama kwa ukaribu sana, vitendo vinavunja mioyo ya Wananchi na
wanachama.
Leo ni tarehe 24
Mei, kama CCM haitachukua uamuzi wa haraka kutoa uongozi katika Mchakato wa
Katiba na Uchaguzi Mkuu, hii haitakuwa ishara nzuri ya chama kuimarika na kukua
kiuongozi. Hebu tufuatilia kalenda hii, Tume ya Uchaguzi imesema itamaliza
kuandikisha wapiga kura Julai 16, kisha litafuata zoezi ya uhakiki wa orodha
kwa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine itakuwa imemaliza au inamalizia
zoezi la uhakiki. Ikumbukwe pia kwa desturi Bunge huvunjwa mwezi wa Julai, na
imekuwa desturi kwamba kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
huanza kwenye tarehe 20 Agosti mpaka siku ya uchaguzi ambayo huwa wiki ya
mwisho ya mwezi Oktoba.
Mpaka leo, hakuna
mswada wowote wa kurekebisha Katiba ya Mwaka 1977 ambao kuna fununu au ambao
imejulikana kwamba utapelekwa Bungeni ili kutekeleza “Makubaliano ya Rais na
TCD”. Sitaki kusema kwamba tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu bila marekebisho ya
Katiba ya Mwaka 1977 kwa maana hata si kila dalili ya mawingu huleta mvua.
Iko bayana kwamba
hatuwezi kufanya kura ya maoni mwaka huu, kwa kalenda niliyoieleza hapo juu,
Kura ya Maoni inataka siku 30 za kampeni, kati ya leo na Oktoba hakuna siku 30
za bure ambazo hazitaingilia ratiba ya uchaguzi mkuu. Katika hili lazima CCM
ioneshe uongozi, mkishindwa katika hili, mimi nitaendelea kupenda misingi ya
kuanzishwa CCM ila heshima ya viongozi wetu katika chama na chama kama taasisi
itakuwa inakaribia ukingoni. Tusifike huko.
Viongozi wetu,
wenye dhamana katika CCM nawaombea mkaongozwe na hekima ya kiMungu. Mkawatazame
viongozi wenye nia ya kushika hatamu ya Taifa letu kwa macho ya kiMungu na si
vinginevyo.
Mkifanya maamuzi
mabaya, mtaivuruga CCM, wanachama na watanzania watahuzunika sana, mtatuachia
matatizo, leo hii sura ya CCM haijatukuka katika kiwango chake, watu wetu wana
maswali zaidi kuliko majibu.
Nihitimishe kwa
kusemea siasa za makundi CCM, wala tusijaribu kujitoa ufahamu, Makundi
yalitetemesha CCM Mwaka 1995 bahati nzuri alikuwepo Mwalimu Nyerere akasaidia.
Makundi yalitikisa chama mwaka 2005 na bahati mbaya athari zake ziko hata leo. CCM
haiwezi kumudu mwendelezo wa siasa za makundi zisizo na tija, uzoefu unaonesha
CCM inadhoofika kutokana na makundi haya.
Wana CCM wanapaswa
kuchagua hivi leo kwamba watakitazama chama na kukiimarisha ama sivyo wana CCM
waamue kufuata uelekeo wa siasa za mihemko ya makundi na wale wote watumiao
mbinu mbaya za makundi ambayo mwishowe yatakivuruga Chama cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment