Kuahirishwa
kwa Kura ya Maoni
Wiki iliyopita nilieleza furaha yangu baada
ya serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuahirisha Kura ya Maoni
iliyokuwa ifanyike tarehe 30 Aprili, kitendo cha serikali ni cha kiungwana
licha ya kwamba kimekuja kwa kuchelewa sana. Serikali kwa ukubwa wake na
taasisi zake lukuki ambazo nyingine zimepewa hata dhamana ya kutumia
intelijensia kuyaelewa mambo na kutoa ushauri stahiki kwa viongozi wetu,
hatukutarajia tupige kelele kwa miezi mitano kusema Kura ya Maoni haiwezekani
mwaka 2015, na hasahasa mwezi wane. Sote tulijua bado hatukuwa na vifaa (BVR)
vya kuwaandikisha watu, sote tulijua tunatumia mfumo mpya kuwaandikisha watu na
hivyo kutarajia sintofahamu kadhaa wa kadhaa, sote tulijua sheria ya Kura ya
Maoni ilikuwa imeweka utaratibu na masharti ya kuzingatiwa kabla ya kwenda
kwenye zoezi la Kura ya Maoni, na sote tunajua masharti hayo na utaratibu kwa
kiasi kikubwa haukuwahi kufuatwa.
Zaidi ya yote, kila mtu anajua kwamba mpaka
mwezi wa pili kwenda wa tatu na hata leo bado tunaendelea kugawa Katiba
Inayopendekezwa kwa umma wa watanzania. Na sote tunafahamu kwa serikali yetu
imechapa nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa ambayo ni wastani wa
Katiba Inayopendekezwa moja inapaswa kusomwa na watu kati ya 12 hadi 13. Katiba
Inayopendekezwa moja kusomwa na watu 12 au 13, tafsiri yake ni kwamba, wewe
ambaye hujapata kuiona Katiba Inayopendekezwa kuna wenzake 11 au 12 ambao
wakimaliza kusoma ndipo na wewe itafika zamu yako, kuwa mvumilivu maana sasa
una muda wa kutosha.
Ilikuwa bayana pia kwamba tusingeweza kwenda
kwenye Kura ya Maoni tukiwa tumegawika kabisa, kisiasa na kiimani. Kura ya
Maoni ingeendeleza mpasuko ambayo kuuziba ingetugharimu zaidi kama Taifa. Na
kama ambavyo utakuwa umefuatilia, dini zote mbili zina madai na kwa msingi huo,
zote hazijaridhika na zote zilishajipanga kupiga kura ya Hapana. Kwa maneno
mengine tarehe 30 Aprili angekuwa ni mtu basi angeshakuwa mhanga wa mpasuko wa
kijamii na kwa maana hiyo tokeo lolote la Aprili 30 lingekuwa limepasua Taifa
kuliko kutujenga.
Nyote mmeshuhudia kwamba kuelekea Kura ya
Maoni Aprili 30 ambayo sasa imeahirishwa tulikuwa tayari na mpasuko mkubwa wa
kisiasa, vyama vikubwa vilikuwa vimesusia kushiriki katika zoezi la Kura ya
Maoni. Kuna baadhi ya watu walichukulia mzaha kwamba hata wakisusia kama vyama
itakuwa kazi bure iwapo watu watajitokeza na kushiriki katika Kura ya Maoni.
Baadhi ya watu hawa walienda mbali zaidi na kuhamasisha kwamba watu wapuuze
msimamo wa vyama kususia na badala yake wakashiriki Kura ya Maoni. Mimi kwa
mfano chama changu hakikususia, na nilikuwa nimejiandaa kwenda kupiga kura ya
Hapana na vivyo hivyo nikajaribu kulisemea hili kwamba kuna tofauti kubwa kati
ya msimamo wa chama kama taasisi na haki ya mwananchi kushiriki katika shughuli
za umma ikiwemo kupiga kura ya maoni.
Watu huenda kupiga kura kama raia wa
Tanzania, na hushiriki zoezi la kupiga kura kama haki yao ya kimsingi na
haijalishi watu hawa ni wanachama wa chama cha siasa au la. Chama cha Siasa
kama taasisi inayotambuliwa kisheria (rejea Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya
258), kina uongozi, kina utaratibu wa kufanya uamuzi kupitia vikao na
kadharika,chama kinaweza kutoa msimamo, kufanya uamuzi na uamuzi huo
usiingiliwe na uhuru wa raia mmoja mmoja kutumia haki zake katika Jamhuri yetu.
Kwahiyo vyama vikisema tunasusia Kura ya Maoni hilo ni tatizo na wa kulitatua
sio wananchi bali ni vyama kukaa na kutatua matatizo yaliyopo miongoni mwao.
Makubaliano
ya Rais na TCD
Juzi juzi hapa nikapata kusikia jamaa yangu
mmoja ambaye alisemalo mara nyingi huwa ama huwa lina wakilisha msimamo, huyu
jamaa ni kama mpishi, mpishi akikwambia leo hakuna nyama ni maharagwe usimbishie
maana yeye anakaa jikoni kila wakati, anajua. Katika mazungumzo anaonesha kana
kwamba hakuna kitu kama Makubaliano ya Rais na Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD). Watu kama hawa huwa sio wa kupuuzwa hata kidogo, lakini kubwa ni kwamba
yeye namshukulia kama mwakilisha fikra, na mimi nawaeleza ninyi wanachama wa
TCD. Napenda kuwaeleza kwamba Tanzania na watanzania waliona mwanga kupitia
ninyi, waliwaamini na kuwaheshimu, nawasihi enendeni kwa moyo huyo.
Naomba niwakumbushe, siku Mhe. Cheyo anasoma
Makubaliano ya Rais na TCD, kushoto kwake aliketi Mhe. Dovutwa na kushoto kwa
Mhe. Dovutwa aliketi Mhe. Philip Mangula. Kwa ishara hii ya umoja na mshikamano
wa TCD, tusaidie watanzania kuvuka kipindi hiki chenye changamoto nyingi. Ninyi
(viongozi na wanachama wa TCD) mnajua fika, na ninajua mnajua na mko katika
nafasi ya kujua ukweli wa mambo kwamba hatuwezi tena kuwa na Kura ya Maoni
mwaka huu. Kinyume na fikra hiyo ni kujaribu kulazimisha mambo halafu mwishowe
tuharibu kila kitu, na ninauhakika miongoni mwenu kuna wazee wenye hekima na
wenye hofu ya Mungu, mnajua fika kwa joto la kisiasa lilipo sasa hivi kuelekea
uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, kimsingi haiwezekani tena kuchomeka
Katiba Inayopendekezwa ili ipigiwe Kura ya Maoni.
Juzi waziri mmoja wa zamani akaandika katika
mitandao ya kijamii, kulikoni katika chama cha Mapinduzi, mbona kimya mpaka
sasa kuhusu kinyang’anyiro cha watangaza nia ya Urais kupitia CCM ilhali kila
kitu kinapaswa kuwa kimekamilika ifikapo mwezi Mei. Swali la makusudi kutoka kwa
mwanasiasa huyu maarufu, ni ishara inayotuonesha uzito wa hali ilivyo kisiasa
nchini, huku kwenye CCM peke yake kuna hali ngumu, kuna joto mithiri ya
tanuruni, bado kwenye vyama vinavyoboresha mawazo (wengine wanaita vyama vya
upinzani) vinyang’anyiro bado. Katika ngazi za ubunge, wabunge wa sasa pamoja
na watangaza nia za ubunge wote akili zinawapaa kujaribu kuwapa maneno matamu
matamu ya lala salama au maneno matamu ya kufunga uchumba kwa miaka mingine
mitano au mwanzo mpya wa miaka mitano.
Kama kwenye Urais na Ubunge watu hawalali
mpaka kieleweke, kwenye udiwani, vikumbo ni zaidi katika ngazi ya kata. Sasa
nikuulize unadhani Taifa liko katika akili iliyotulia ya kuipigia Kura ya Maoni
Katiba Inayopendekezwa kwa maana viongozi wetu waongoza kampeni ambao wengi ni
wanataka kuendelea kushikilia majimbo au wametingwa na kutangaza nia pamoja na
wananchi raia mmoja mmoja ambao saizi tunatathmini nani abaki na nani asirudi
na kwanini abaki na kwanini asirudi. Hivi kweli ukituongezea na Katiba
Inayopendekezwa si utatuvuruga?
Kibaya zaidi, kitendo chochote cha
kuchanganya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu itakuwa ni dhambi kubwa kuliko, tutageuza
Mchakato wa Katiba na Katiba Inayopendekezwa kuwa ajenda ya uchaguzi, hilo
litavuruga maana ya Katiba isiyopasualiwa kisiasa katika ya ndio na hapana
zinazohamasishwa kwa minajiri ya siasa zetu ambazo mara nyingi huwa hazina
maslahi ya umma mpana wa watanzania.
TCD, nawasihi tena, kutaneni na jadilini,
huyu Rais wetu ni muungwana na msikivu, mkimweleza kwa hoja hizi na zenu nzuri
zaidi atawaelewa na twaweza kuona Bunge lijalo tukijadili marekebisho ya Katiba
ya Mwaka 1977 ili tuvuke salama katika Uchaguzi Mkuu. Msipofanya hivyo,
viongozi wangu wa CCM, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI, TLP na UDP kama sehemu ya TCD,
mtapoteza imani yenu mbele ya umma wa watanzania. Nawasihi fanyeni hili kwa
maslahi ya Taifa na zaidi tumsaidie Mhe. Rais amalize na Uchaguzi kwa mara ya
kwanza usio na tashwishwi wala waa na huo utakuwa sehemu ya utumishi wake
uliotukuka kwetu na sisi kwa hakika tutamkumbuka ikiwemo pamoja na mchakato wa
Katiba ambao tutaendelea nao mwakani. Na wala msihofu, tukifanya marekebisho,
lazima tutatunga na masharti yatokanayo na masharti ya mpito na mojawapo ya
kazi za kikatiba kwa Rais ajaye na Serikali yake ni kuendelea na Mchakato wa
Katiba, sio utashi bali ni takwa la kikatiba.
Fursa ya
Mjadala
Kilichobaki sasa ni kuendelea kujadiliana
kuhusu mchakato wa Katiba, Rasimu ya Warioba, Katiba Inayopendekezwa na
tuulizane maswali na kupeana majibu. Kama ilivyo ada wikendi hii Taasisi ya
Mwalimu Nyerere imeandaa Mdahalo wa Katiba huko Mbeya, ni sehemu ya
kujadiliana. Na ninawasihi Taasisi ya Mwalimu Nyerere wasiishie hapo, waende na
mikoa mingine mingi zaidi maana elimu hii inahitajika sana.
Tunapojiandaa
kisaikolojia na Uchaguzi Mkuu
Tuipe Tume ya Taifa ya Uchaguzi ushirikiano
wa kutosha wanapoendelea na zoezi la uandikishwaji wapiga kura. Tujitokeze kwa
wingi kuandikishwa na kupata vitambulisho vya mpiga kura, bila kitambulisho cha
mpiga kura hutaweza kutumia haki yako kufanya uamuzi wa ni nani na nani wapewe
dhamana ya kukuongoza katika ngazi ya kata, jimbo na Jamhuri yetu.
Wito, kwa unyenyekevu niwasihi serikali
msiwaingilie Tume wanapotenda kazi yao, wapeni uhuru wa kutosha kama ambavyo
wanapaswa kuwa. Waacheni ili watanzania kwa muda huu uliobaki wapate huduma ya
Tume bila matatizo. Rai yangu kwa vyama vya siasa, jipangeni, pigeni siasa
safi, jengeni hoja, toeni sababu na onesheni ushahidi, watu watawaelewa tu, ila
achene kuisakama Tume ya Uchaguzi bila sababu, maana hiyo ni tabia mbaya.
No comments:
Post a Comment