Tutafakari kwa Hoja na Sababu
Wagombea Urais wa CCM, Dr. John Magufuli
na mwenzake wa CHADEMA Ndg Edward Lowassa wanakubaliana jambo moja kubwa: Haja
ya kuwa na mabadiliko katika nchi yetu. Wagombea wote wameahidi kila mmoja kuwa
iwapo atashinda ataleta mabadiliko. Tulinganishe sasa na kupima aina ya
mabadiliko ambayo yanaweza kutokea iwapo mmojawapo atachaguliwa kuwa Rais wa
nchi yetu.
Kulingana na historia ya utendaji wake
katika wizara alizokabidhiwa na ahadi anazotoa mgombea wa CCM, Dr. John Magufuli, chini ya Urais wake inaonekana utawala wa sheria na nidhamu ya kazi kwa
watumishi wa umma itatamalaki. Magufuli
anajulikana zaidi kwa Watanzania kuwa ni mtu anayesimamia sheria hata pale
zinapogusa maslahi ya wakubwa zake. Watanzania watakumbuka jinsi Magufuli
alivyoweza kurudisha magari yaliyokuwa yameporwa kinyemela na vigogo wa serikali enzi za utawala wa
Benjamin Mkapa.
Kwa upande wa Ndg. Edward Lowasa, iwapo atachaguliwa kuwa Rais, kuna uwezekano mkubwa
kukawa na utawala unaotegemea hisia za Rais na ‘marafiki’ zake badala ya utawala wa sheria. Utendaji wake wa
nyuma unaonyesha wazi kuwa Lowassa kama kiongozi ni mtu anayeamini matashi yake
binafsi bila kuzingatia utawala wa sheria. Watanzania watakumbuka kuwa March 2006,
akiwa waziri mkuu, Lowassa alimfukuza kazi mhandisi wa Manispaa ya Temeke bila kumpa
nafasi ya kujitetea na tena mbele ya waandishi wa habari na kundi la wananchi
waliokuwepo katika tukio la kuporomoka jengo la Chang’ombe Village.
Hivi karibuni, wakati anazindua kampeni
zake, Lowassa alitoa ahadi kuwa ikiwa atashinda atamuchia huru Nguza Viking,
maarufu kama Babu Seya aliyefungwa maisha jela kwa kwa kosa la kubaka na kulawiti watoto katika hukumu
iliyotolewa na mahakama ya hakimu mkazi kisutu mwaka 2004. Kesi hiyo ilipelekwa
katika mahakama ya rufaa mwaka 2010 na Mahakama ilikubaliana na uamuzi wa
mahakama ya chini. Tena, mwaka 2013, jopo la majaji wa mahakama ya rufaa watatu
likijumuisha Jaji Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Msati walifanya mapitio
ya mahakama hiyo na kuwaona wafungwa hao kuwa wana hatia.
Ikumbukwe kuwa sheria za Tanzania
zinamyima Rais mamlaka ya kusamehe watu waliofungwa kwa makosa ya kubaka na
kulawiti. Kwa kutamka kuwa atawachia wazi wafungwa hao,bila ya kusema chochote juu
ya wale watoto waliolawitiwa na kubakwa na haja ya kufuata utawala wa sheria
nchini ni dhahiri kuwa katika utawala wa
Lowassa utawala wa sheria utawekwa kando na matashi ya watawala ndio
yatakuwa yanaongoza nchi. Hili linadhibitishwa na ahadi nyingine ya
Lowassa kuwa akiwa Rais, watuhumiwa wa kesi za ugaidi waliokamatwa
huko Zanzibar wataachiwa huru kwa amri ya Rais. Ikumbukwe kuwa kwa sasa dunia
iko kwenye vita dhidi ya ugaidi na ugaidi ni hatari kubwa na thahiri kwa maisha
ya wananchi na mali zao.
Wagombea wote wameahidi kupambana na
ufisadi na rushwa iwapo watachaguliwa kushika nafasi ya Urais. Magufuli
ameahidi wazi kuwa ataleta mabadiliko
katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuanzisha mahakama maalum ya
kushughulikia masuala hayo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa rushwa itaweza
kudhibitiwa katika utawala wake ukizingatia kuwa katika harakati zake zote
hakuungwa mkono na genge la mafisadi kama ilivyozoeleka kwa siasa za CCM tangu
mwaka 2005 ilipotekwa na genge la wanamtandao.
Hali hii itamfanya aweze kutawala bila
kuwa na deni la kulipa fadhila kwa mtu
yeyote. Uzoefu wa siku za karibuni unaonyesha kuwa rushwa na ufisadi mkubwa unasababishwa
na kujaza ‘marafiki’ katika nafasi muhimu za maamuzi. Kujaza marafiki hasa
waliokufadhili kwenye harakati za uchaguzi kunafanya mifumo ya uwajibkaji
katika nchi iwe na ganzi ya kufanya kazi dhidi ya marafiki hao.
Kwa upande wake Lowassa hajaeleza
atafanya nini bayana katika kupambana na rushwa zaidi ya kusema atashughulikia
rushwa. Kama ambavyo ilibainishwa na waziri mkuu mstaafu na mpambe wa Lowassa
katika harakati za Urais, Fredrick Sumaye,
katika viwanja vya jangwani, Lowassa ndiye mwasisi wa ‘mtandao’
uliomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005. Kundi hili lilimjumisha pia
Rostam Azizi na Laurence Masha ambao leo hii ndio pia ndio wanaongoza mikakati
ya Lowassa. Rushwa katika mikataba ya aina mbalimbali na hata ukwapuaji wa
fedha za umma kupitia maskandali mbalimbali kama EPA, Richmond na Dowans ulifanyika kama njia ya kulipa deni
la fadhila wakati wa uchaguzi. Kama tulivyogusia hapo juu, ni vigumu kuchukua
hatua dhidi ya marafiki na maswahiba.
Baada ya CCM kujikomboa kutoka katika
makucha ya wanamtandao kwa kuwaondoa wagombea wa kundi hili akiwemo Lowassa
kwenye kinyang’anyiro cha kugombea Urais kupitia chama hicho, kundi hilo
limeweza ‘kuiteka nyara’ CHADEMA na kupitia kwake vyama vikuu vya upinzani
kupitia UKAWA. Lowassa amesema waziwazi kuwa fedha anazogawa kwa wananchi
mbalimbali zinatokana na ‘marafiki’ zake. Kwa hiyo, kama atachaguliwa, utawala
wa Lowassa utaendeleza utawala wa wanamtandao, na watanzania watarajie kushamiri
kwa ufisadi nchini kwa sababu tulizoeleza hapo juu.
Watanzania watakumbuka kuwa kile kinachoonekana
kuwa ni ushabiki wa kupindukia kwa Lowassa hauna tofauti na ushbiki uliokuwepo
mwaka 2005 kwa Kikwete. Hii inatokana na
ukweli kuwa kundi linaloratibu na kuongoza kampeni za Lowassa ni lilile
lililofanya kazi hiyo mwaka 2005. Tayari, kuna taarifa zinazosema kuwa
wanamtandao wameshagawana nafasi muhimu za uongozi na mikataba katika maeneo
manono kama bandari, madini na vitalu vya gesi na mafuta iwapo watafanikiwa
kuiteka dola kupitia uchaguzi.
Magufuli ameahidi kuwa ataleta
mabadiliko katika utendaji wa watumishi wa umma kwa kuweka mifumo imara ya
uwajibikaji. Watu walio karibu na Magufuli wanasema kuwa Magufuli ameahidi kuwa
akiwa Rais atawekeana mikataba ya utendaji kazi (Perfomance contracts) na mawaziri wake ambapo kila waziri ataingia
kama yeye binafsi na akishindwa kufikia malengo atawajibishwa kwa kuondolewa
madarakani. Magufuli ameahidi pia kuwa mafisadi watakaotiwa hatiani
watafilisiwa mali zao.
Kwa upande wake Lowassa amesema kuwa
akiingia madarakani atabadilisha mfumo wote wa nchi. Hii ina maana kuwa Lowassa
akiwa Rais, taasisi za utawala kama vile Polisi, Jeshi, Utumishi wa Umma na
vyombo vingine vitafumuliwa na kuundwa upya na kuwekwa watu wapya. Muhimu hapa
ni kukubaliana kuwa siyo rahisi kwa
jambo hilo kufanyika kwa kuwa kama ilivyo duniani kote yeyote atakaye shinda
atalazimika kufanya kazi na vyombo hivyo. Mabadiliko yeyote ya utendaji wa
vyombo hivyo vitategemea na hulka, tabia na haiba ya Rais. Hakika duniani kote
mabadiliko katika nchi huletwa kwa vyombo hivyo kufanya kazi zao ipasavyo
kutokana na uongozi na usimamizi dhabiti wa mkuu wa nchi.
Hitimisho
Haya
ni baadhi ya mabadiliko yanaweza kutokea iwapo mmoja wa wagombea wetu
watachaguliwa katika nafasi ya Urais. Mabadiliko haya yanaonyesha wazi kuwa
uchaguzi ni muhimu sana kwa mustakabali wetu kama mtu mmoja mmoja na kama
Taifa. Kwa sababu hiyo, ushabiki na uungwaji mkono wa wagombea lazima uzingatie
faida na hasara zake kwa nchi na kwetu binafsi. Ni wakati wa kuwahoji na
kuwatathimini wagombea wetu ili siku ya upigaji kura tisije tukafanya kosa
litakalotuathiri sisi na vizazi vyetu. Tathmini
hiyo ni muhimu kwa kujua kuwa utendaji kazi wa Rais huakisi na kuathiri
utendaji kazi wa serikali na taasisi zote zilizo chini yake. Yaani Rais akiwa
fisadi serikali na vyombo vyote chini yake vitakuwa vya kifisadi. La, Rais
akiwa mwadilifu na mchapakazi na serikali yake itakuwa vivyo hivyo.
asante kwa uchambuzi mzuri japo umesahau kuelezea uuzwaji wa wa nyumba za selekali ambapo magufuli anahusishwa. Binafsi nakubaliana na wote wanaotaka mabadiliko lakini pia sikubaliani na njia wanayotaka kuitumia. Mimi nimekuwa mpinzani wa Lowasa tangu alipokuwa anatafuta kuteuliwa na Chama chake CCM kwasabu naamini kama angeteuliwa na mwisho angekuwa raisi nchi ingeendelea kuendeshwa kwa kulipana fadhila kama ilivyokuwa enzi za JK. Wanamtandao walimwingiza Ikulu, baada ya hapo likaundwa baraza la mawaziri la watu 60, Lowasa akawa waziri mkuu na baada ya muda mfupi wakatuletea Richmond. Ilikuwa ni kulipana fadhila tu. Nashukuru mwaka huu Mwenyekiti wa CCM amehakikisha mtandao ulomwingiza yy mwenyewe madarakani hauendelei kuitesa nchi. Bila shaka Lowasa akiwa raisi ufisadi utashika hatamu. Nafikiria alitumia pesa kiasi gani kuhakikisha wale wajumbe waloimba wana imani na LOwasa pale NEC Dodoma. mipesa alokuwa anamwaga kwenye HARAMBEE ambayo alikuwa anadai anapata toka kwa marafiki zake. Mwisho wa siku akiingia madarakani hao marafiki zake watakuwa hawalipi kodi wala hawaguswi na yeyote. Na nadhani mbaka sasa hakuna tajiri aliyezoea ujanja ujanja anayependa Magufuli aingie ikulu. mana itakuwa shida kwake.
ReplyDeleteMwisho sina uhakika kama magufuli ataweza kupambana na watu wa rushwa kubwa kama alivoahidi mana mfumo wa mahakama zetu tunaujua. majaji wapo mifukoni mwa matajiri...na p[ia wanaweza waka M'SOKOINE
Kingine Mgufuli amesahau kabisa kuongelea vita ya madawa ya kulevya.cjui anaogopa????
0685818951