Friday, September 11, 2015

DR. JOHN POMBE MAGUFULI NA UWEZO WAKE WA KULETA MABADILIKO CHANYA



Tujadiliane kwa HOJA na Sababu

Kuelekea uchaguzi Mkuu 2015  mabadiliko ni miongoni mwa mambo yanayochukua nafasi kubwa katika kampeni na ilani za vyama vya siasa. Hoja nyingi zinatolewa hususani katika dhana ya mabadiliko ya mfumo au kiongozi au yote mawili yaani mfumo na uongozi. Kwa bahati mbaya watanzania hawaelezwi mahusiano kati ya mfumo na viongozi. Mbaya zaidi wengi wetu tumeporwa uwezo wa kutafakari kutokana na kuzamishwa kwenye mahaba kwa wagombea au vyama vya siasa.

Kwa kuwa bado kuna siku zaidi ya arobaini ni vyema tukawatafakari baadhi ya wagombea wa nafasi ya uraisi ambao ndio hasa wanachuana vikali katika kampeni zinazoendelea.  Yapo mambo kadhaa yanayoweza kutuongoza katika kuwapima wagombea na sera zao. Moja, ni kutafakari kama inatosha kuwa mashabiki wa matamko tu yenye kushawishi juu ya kuleta mabadiliko  kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wameendelea kuwalaghai wananchi kipindi hiki cha kampeni za uchanguzi mkuu 2015.

Muhimu sana ni  kupima nia na zaidi sana uwezo wa  kiongozi husika kutafsiri madhui ya ahadi zake katika vitendo.  Hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba  wameibuka wanasiasa wanaotoa matumaini hewa kwa wananchi kwa kusema tu yale ambayo wananchi wangependa kusikia. Ni jambo jema kuwajengea wananchi matumaini lakini ni hatari pia kuwalaghai wananchi kwa mambo ambayo kiongozi husika sio tu yeye mwenyewe hayaamini au hana uwezo wala dhamira ya dhati kutimiza. Maswali mawili ni muhimu kuulizwa katika hili, moja ni mfumo gani unaolengwa kubadilishwa ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa watanzania? Je viongozi husika wanavyo vigezo, uwezo  na uzoefu katika kujenga mifumo endelevu?

Edward Lowasa na dhana ya mabadiliko ndani ya UKAWA

Tukianza  na kambi  ya UKAWA inayowakilishwa na Edward Lowasa, tukivipima vyama vya siasa vinavyounda UKAWA kwa mifano na kutafuta vielelezo vya kimfumo inaonekana  dhahiri kuwa  aidha hakuna kabisa mifumo bali haiba (personalities)  au kuna baadhi ya viashiria vya kuwepo kwa mfumo lakini kutoka na kujengwa kwenye misingi dhaifu mifumo hii imekuwa sio endelevu. Pengine kwa kutambua udhaifu huu UKAWA imefungua milango kupokea baadhi ya  wanasiasa ambao wamewahi kuongoza nchi yetu katika nafasi kubwa za uongozi kama ile ya Waziri Mkuu. Hawa ni pamoja na Edward Lowasa ambae ndio mgombe uraisi na Fredrick Sumaye .

Hata hivyo  ukiwauliza au hata ukijaribu kutafuta na kupima jambo gani la kimfumo waliwezakulifanya katika nafasi zao?  Kinachojitokeza ni aidha viongozi hawa hawakuwa na uelewa sahihi wa masuala ya kimfumo hivyo kushindwa kufanya uchambuzi sahihi wa matatizo ya kimfumo na kuyapatia majawabu ya kiutendaji. Mara nyingine  walidandia miradi ya maendeleo na kuisukuma kwa mabavu bila kuweka misingi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kujenga  taasisi imara  kutekeleza na kusimamia sekta husika mambo hayo licha ya kuwa mazuri yaligeuka kusongwa na changamoto nyingi.

Mbaya zaidi viongozi hawa na wengine wanaofanana nao walitumia nafasi zao kujinufaisha wenyewe ikiwa ni pamoja na kujenga mitandao ya kukwapua fedha za umma kwa maslahi yao binafsi na washirika wao. Kinachopaswa kuogopwa sana na Watanzania ni ile hulka ya viongozi hawa kutaka kujilimbikizia mali kwa namna yeyote ile. Hawa ni miongoni mwa viongozi  ambao wamediliki hata kusema kuwa wakichaguliwa kuongoza nchi hii watatengeneza kundi la aina  fulani ya matajiri ambao wataendesha uchumi wa taifa letu.

Swali la kujiuliza ni kama huu ni mkakati wa kimfumo na je haya ndio mabadiliko ambayo Watanzania watarajie? Hii ni dhana hatari inayolenga kuchochea kuongezeka kwa tabaka la maskini na matajiri. Ni muhimu kutambua kuwa matajiri kazi yao kubwa ni kutengeneza faida kutokana na mitaji yao. Haishangazi kuona kuwa matajiri hawa wanaotajwa na mmoja wa wagombea wa uraisi kuwa ni “marafiki” zake wamekuwa wakifadhili harakati za mgombea huyo kuingia madarakani kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita. Jambo jingine la kujiuliza ni Je kwa uwekezaji huu matajiri hawa wanatarajia kuvuna nini? Wasiwasi wangu ni kwamba chondechode mgombea huyu asijekuwa ameweka rehani rasilimali za nchi hii na ikiwa ni pamoja na maisha ya watanzania ili tu atimize ndoto yake ya kuwa raisi wa inchi.

Rai yangu ni kwamba Watanzania tufungue fahamu zetu kipindi hiki cha kampeni na kupima wagombea na hoja  zao pasipo ushabiki na ushawishi mwepesi. Naelewa vyema haja ya kufanya mabadiliko lakini tujiulize ni mabadiliko ya aina gani tunahitaji. Haifai kabisa kumkubali mgombea hana kabisa vigezo vya kuleta mabadiliko eti tu kwa sababu tunataka mabadiliko. Mgombea ambae hana uwezo wala uthubutu wa kukemea ufisadi  hatufai kabisa hasa kwa kuzingatia hulka za kifisadi ambazo zimeshamiri katika jamii yetu sio tu kwenye sekta ya umma bali hata sekta binafsi. Ni nani asiefahamu kuwa ufisadi uwe mkubwa au mdogo ni kikwazo kikubwa katika maendeleo na ustawi ya nchi yetu.

Je ni mara ngapi tumesikia mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA akiweka bayana  mkakati wa kupambana na ufisadi? Ni nani asietambua kuwa ajenda ya mapambano dhidi ya ufisadi ndio iliyowafanya wananchi wengi kuvutiwa na sera za CHADEMA hususani chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho Dr. Wilbroad Slaa?  Tujiulize kwanini vita  dhidi ya ufisadi sio tena hoja kubwa kwa CHADEMA na UKAWA mara tu baada ya kumpitisha Edward Lowasa kupeperusha bendera ya chama hich na umoja huo katika nafasi ya urais kwenye uchanguzi Mkuu.

Zaidi sana tujiulize ni kwa nini Edward Lowasa anapata kigugumizi kukemea ufisadi? Tumhoji atawezaje kutekeleza ahadi zake lukuki za mabadiliko bila kuwa na haki na uthubutu wa kukemea ufisadi? Atahakikishaje huduma za jamii zinapatika kwa wananchi wote, elimu burekwa wote mpaka chuo kikuu, na kuongeza tija kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji bila kudhibiti mianya ya ufisadi? Au anaikwepa vita dhidi ya ufisadi kwa sababu anajua ni kupitia ufisadi pekee hasa kwa njia ya manunuzi na mikataba feki ndio anaweza kulipa hisani kwa marafiki zake wanaoendelea kufadhiri mradi wake wa kuingia Ikulu. Nachelea kusema kuwa kwa Edward Lowasa uraisi ni mradi wakunenepesha mitaji ya matajiri wanaojiita marafiki zake ambao sasa wamekaa mkao wa kula. Sioni dalili za mabadiliko chanya yanayowezakutokana na kiongozi wa aina hii kwenye nchi yetu kwa kuzingatia muktaza tulionao kijamii, Kisiasa na kiuchumi.

Wapo wanaosema eti kwa sababu ajenda ya ufisadi ipo ndani ya Ilani ya CHADEMA ambayo pia inanadiwa na UKAWA, hivyo ikitokea Edward Lowasa akashinda atalazimishwa na ilani hiyo kukemea ufisadi. Wachambuzi hawa wanawezakuwa sahihi endapo wafanya tathmini ya taswira ya uraisi anaoutamani Edward Lowasa na ukweli kwamba ataapishwa kama Edward Lowasa.  Hasa kwa kuzingatia Katiba ya sasa ni dhahiri kwamba atakapoingia tu madarakani sioni kama CHADEMA watakuwa tena na nguvu ya kumdhibiti.

Tusisahau pia kuwa ni CHADEMA na UKAWA ndio walimbembeleza Edward Lowassa kujiunga nao na ni dhahiri kwamba sharti ambalo aliwapatia ni kumpitisha yeye kugombea uraisi. Kana kwamba haitoshi kampeni za mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA zinafadhiliwa kwa asilimia kubwa na Edward Lowassa na Marafiki zake. Maana yake ni kwamba watakapoanza kutaka kudhibiti utekelezaji wa mradi wake wa kunenepesha mitaji ya mafisadi waliofadhili safari yake kuingia Ikulu atawauliza swali dogo tu mnategemea nitalipaje madeni ya kampeni za uchaguzi? Kwa kuufahamu ukweli wa mkataba kati ya viongozi wa CHADEMA/UKAWA na Edward Lowasa lakini pia kwa madaraka makubwa atakayokuwanayo kama raisi wakati huo hawataweza kumdhibiti. 

Wapo wanaoweka imani kwenye uwezekano wa kubadilisha katiba ili pamoja na mambo mengine kupunguza madaraka ya raisi. Ufahamu wangu juu ya uwezo wa watu binafsi kufanya mabadiliko na kiwango   cha mabadiliko huchangiwa sana na historia ya muhusika na kundi/kizazi/tabaka anakotoka. Kwa mfano mara nyingi wazee ni hawapendi madiliko hasa yale yanayokinzana na matakwa yao. Simuoni mzee Edward Lowasa katika umri wake eti anatakakuleta mabadiliko ya kasi hasa ukizingatia yeye ukiacha majanga ya kisiasa aliyokutana nayo yupo katika tabaka la matajiri.

Dkt. John Pombe Magufuli na Mabadiliko ndani ya CCM

Watanzania wengi bila kujali itikadi na nafasi zao wamewahi ama  kusikia, kukiri, au kuthibitisha kwa vitendo kuwa  Dkt. Magufuli ni kiongozi shupavu, mwenye dira na uwezo wa kubadili mifumo  na utendaji  katika sekta mbalimbali. Hii inathibitika wazi pale watu wanapoamua kufanya tathmini sahihi ya utumishi wa kiongozi huyu kwa kuangalia  utendaji wake na mafanikio yaliyofikiwa na sekta au taasisi ambazo Dkt Magufuli amewahi kuzisimamia.  Hapa ni vigumu kupinga ukweli kwamba Dkt magufuli ndiye aliyeleta mabadiliko na maboresho katika sekta ya Ujenzi hususani wa miundo mbinu ya barabara.

Maeneo mengine ambayo Dkt Magufuli ameacha  mbegu ya maboresho ni  katika sekta ya ardhi pamoja na ile ya mifugo na uvuvi  licha ya kuzitumikia sekta hizi kwa muda mfupi kabla ya kurejea tena kwenye sekta ya Ujenzi. Taswira ya sasa ya sekta ya ujenzi ambayo sio tu kwamba ina mifumo bayana na thabiti licha ya changamoto kadhaa, sekta hii inasimamiwa na taasisi madhubuti ambazo zinalenga kutafsiri dira na mikakati ya sekta katika uhalisia na vitendo.

Akiwa Naibu wa waziri wa ujenzi katika serikali ya awamu ya tatu, ni Dkt. Magufuli ndie alibadilisha mfumo wa kutegemea wahisani kwa asilimia miamoja katika sekta ya ujenzi wa barabara.Mfumo huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Ujenzi, takribani asilimia sabini (70%) ya miradi yote ya ujenzi wa barabara inchini inajengwa kwa kutumia fedha za serikali. Ni asilimia thelasini pekee ya miradi yote ya ujenzi inafaddiliwa na wahisani. Swali la kujiuliza ni je nini kimefanikisha utelekezaji wa mfumo huu? Hapa ndipo unawezakuona uwezo na uzoefu wa kiongozi katika kubadili mfumo kwa kujenga taasisi zinazotakiwa ili kusimamia na kuendeleze mfumo.  Ni Dkt. John Pombe Magufuli ndie alieanzisha harakati za maboresho katika usimamizi, utekelezaji na uendelezaji wa sekta ya ujenzi nchini.

Kiongozi huyu amesimamia kuanzishwa kwa taasisi kadhaa muhimu katika sekta ya ujenzi ambazo ni pamoja na Mfuko wa barabara (Road Funds) ambao mapato yake yameongezeka kutoka shilingi bilioni 73.08 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 751.7 mwaka 2014/15. Taasisi nyingine ni pamoja na Wakalawa barabara (TANROADS) inayosimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja. Pia zipo taasisi kama Wakala wa Majengo Tanzania (TBA); Board ya Usajili wa Wahandisi (ERB); Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRD na Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB). Taasisi zote hizi zinalenga kutelekeza majukumu tofauti lakini yanayotegemeana katika ustawi wa sekta ya ujenzi. Hapa unaweza kuona mantiki ya ujenzi wa mfumo sio hisia wala propaganda.

Mifano hii michache ni kielelezo cha uzoefu, dhamira na upeo, na umakini wa kiongozi katika  kuchambua, kuamua na kusimamia mambo miradi ya maendeleo. Ni mgombea Dkt. John Pombe Magufuli ndie ambae amembanua wazi dhamira na mikakati yake kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Huyu sio tu kwamba anasema dhahiri kwamba  atafungua mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi lakini pia uzoefu katika wizara alozitumikia una akisi dhamira hii.


Ni vigumu kupinga ukweli kwamba hatua ambayo nchi yetu imefika inahitaji kiongozi ambae sio tu anapenda kusema kile ambacho watanzania wanapenda kusikia bali kile watanzania wanachohitaji yaani Kiongozi mwenye uwezo wa kurejesha uadilifu, uaminifu na uchapa kazi katika sekta zote.

5 comments:

  1. So Pole Pole the reason for all these attacks to Lowasa/UKAWA is to promote your candidate? It therefore goes without saying no one can afford to be 100% Neutral. Is it not high time you promote the candidate of your choice and stop malice against opponents?? May God Bless YOU.

    ReplyDelete
  2. Ndg Polepole, wewe unampigia debe Magufuri na kuyasema mabaya ya Lowasa na kwamba hawezi kuleta Mabadiliko ya kweli ndani ya UKAWA, mimi kwa ntampigia Lowasa kura yangu bila kuangalia ataleta nn ila ni dhamira yangu kwamba ili kuleta nidham katika utendaji ni kuondoa dhana ya kubweteka kwa viongozi kwa mamlaka kukaa muda mrefu na kuzani hii nchi ni ya ccm tuu, nitamchagua Lowasa na chadema ili kuonyesha kwamba Tanzania si ya ccm tuu. No matter ataleta nn.
    Hatuchagui malaika hapa, kama ni ubovu wote wana matatizo yao, tunabadilisha mfumo.

    ReplyDelete
  3. Kingine unam attack Lowasa personally kwamba ni fisadi na kikubwa ni kuhusu Richmond, kwa tunaofuatilia mambo tunajua kwamba toka jambo hili liibuliwe kulikuwa na sintofahamu nyingi kuhusu Richmond. Na ufisadi huo ulikuwa na mnyororo mrefu ndo maana hajapelekwa mahakamani mpaka Leo.
    Mbona Leo tunawaona wote waliotajwa kwenye list of shame wapo na hawaguswi na wewe pia kama mchambuzi huwagusi kabisa. Nitamchagua Lowasa

    ReplyDelete
  4. Ndg Polepole, wewe unampigia debe Magufuri na kuyasema mabaya ya Lowasa na kwamba hawezi kuleta Mabadiliko ya kweli ndani ya UKAWA, mimi kwa ntampigia Lowasa kura yangu bila kuangalia ataleta nn ila ni dhamira yangu kwamba ili kuleta nidham katika utendaji ni kuondoa dhana ya kubweteka kwa viongozi kwa mamlaka kukaa muda mrefu na kuzani hii nchi ni ya ccm tuu, nitamchagua Lowasa na chadema ili kuonyesha kwamba Tanzania si ya ccm tuu. No matter ataleta nn.
    Hatuchagui malaika hapa, kama ni ubovu wote wana matatizo yao, tunabadilisha mfumo.

    ReplyDelete
  5. Ndg Polepole, wewe unampigia debe Magufuri na kuyasema mabaya ya Lowasa na kwamba hawezi kuleta Mabadiliko ya kweli ndani ya UKAWA, mimi kwa ntampigia Lowasa kura yangu bila kuangalia ataleta nn ila ni dhamira yangu kwamba ili kuleta nidham katika utendaji ni kuondoa dhana ya kubweteka kwa viongozi kwa mamlaka kukaa muda mrefu na kuzani hii nchi ni ya ccm tuu, nitamchagua Lowasa na chadema ili kuonyesha kwamba Tanzania si ya ccm tuu. No matter ataleta nn.
    Hatuchagui malaika hapa, kama ni ubovu wote wana matatizo yao, tunabadilisha mfumo.

    ReplyDelete