Thursday, October 1, 2015

“HASIRA HASARA”: KUPIGA KURA KWA HASIRA NI UJUHA NA SI HEKIMA, TUPIGE KURA TUKILITIZAMA TAIFA


Utamaduni wa kukosa uhimilivu umetoka wapi?

Bado nimepigwa na butwaa kwa namna ambavyo baadhi ya watanzania wenzangu wanakosa ustahimilivu katika kipindi tunapoelekea uchaguzi mkuu. Nimegundua kwamba unapotoa hoja ambayo wengine hawaiungi mkono basi kumekuwa na ugumu katika kustahimiliana. Nashangazwa zaidi pia pale ambapo hata wale ambao ni wana mageuzi au wafuasi wa vyama vyenye mawazo mbadala, hawa wamekuwa wakali kweli pale mtu anapotoa hoja ambazo hazifanani na mitizamo yao.

Nimeanza kuona dalili ya Taifa kuanza kupoteza utamaduni wa ustahimilivu, utamaduni wa kuheshimiana, utamaduni wa kujadiliana kwa hoja na sababu na utamaduni wa mijadala inayojengwa katika dhana ya nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu. Kwa wale ambao ni wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii utagundua kwa sasa kuna mgombea ukimjadili ni tatizo, au ukimjadili mmoja bila kumgusa mwingine ni tatizo kubwa.

Jamii yetu imegeuka kuwa kama genge litishalo na kuamulia watu wazungumze nini, kwa nani na wakati gani. Ni katika kipindi hiki na ajabu kabisa baadhi ya wananchi wamekuwa wakilazimisha wananchi wengine na hasa wale wanaopenda kuweka mawazo yao hadharani kwamba ni lazima wawe katikati. Hivi kuwa katikati unapotoa hoja maana yake nini? Mtoa hoja mmoja ambaye pia ni kiongozi wa dini aliwahi kuniasa kuwa ninapojenga hoja niwe katikati au “neutral” na pasina kuainisha nani mbaya na nani mzuri. Nikamwuliza, je katika kazi ya kuhubiri dini, kuna siku amewahi kumtendea haki shetani anapohubiri na kwa maana ya kusema shetani naye ni mzuri kwasababu watu wengi pia wananufaika naye? Au wakati wote yeye huhubiri na kumtukuza Mungu wa Mbinguni pekee kwa yeye ndiye mwema na mtenda mema yote na wema wote huyoka kwako na Shetani au Ibilisi ni mwizi, muuaji na mharibifu na kwake hakuna wema bali ubaya wote.

Je kama mimi ni muumini wa kusimamia kweli na uadilifu, dhambi iko wapi iwapo nitasema katika wagombea Urais mtizamo wangu ni kwamba mgombea fulani kwa vigezo vya kibinadamu yuko vizuri na mgombea fulani kwa vigezo vya kibinadamu namwona sio mwadilifu na ana uchu wa madaraka na anadhani yeye aliandikiwa Urais na Mungu.

Ninaendelea kuuliza hasira iko wapi kama nitatumia uhuru wangu kumjadili mgombea mmoja ambaye kwa ushahidi nafahamu hana sifa ya uadilifu na ananasibishwa na ufisadi kwa zaidi ya miongo miwili?

Labda nieleze kwa sehemu, mimi ni mwana CCM na wakati wa Mchakato wa Katiba nakumbuka watu wote waliotukwamisha na walikuwa katika makundi mawili, kundi la kwanza lilikuwa watu na hasa mtu aliyekuwa hapendi maoni ya wananchi na katika namna yalikuwa yatumike kuandika Katiba Mpya. Mtu huyu anajulikana wazi kwamba alijipambanua kama mgombea pekee na mwenye hatimiliki ya Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mtu huyu mimi na wenzangu tulikuwa na kikao naye cha zaidi ya saa mbili nikimfafanulia Rasimu ya Warioba na faida zake, akakataa katakata. Mtu huyu tuliamua kwenda kumwona baada ya kuambiwa na wapambe wake kwamba Rasimu ya Warioba asingeruhusu ipite na kwamba kaweka mguu chini hivyo labda tukajaribu kumfafanulia, tulifanya hivyo, nilikuwepo na alikataa mbele ya macho yangu na akatupa mapendekezo ambayo ndio hatimaye yalikuwa katika Katiba Inayopendekezwa mwishoni.

Binafsi sikukubaliana naye pale na baada ya pale na nikajiapiza kuendelea kudai maoni ya wananchi nikitumia mbinu zote halali. Itakumbukwa nilipopata mwaliko katika vipindi vya Televisheni nilipata kusema mtu huyu kama “tatizo kubwa la kitaifa” na wenzake wengine hawapaswi kupewa dhamana ya kugombea Urais kupitia CCM. Watu wengi waliniunga mkono wakiwemo wafuasi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), nakumbuka mdahalo wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na baada ya kuona kwamba mtu huyu alikuwa kana kwamba anakwenda kufanikiwa kuwahadaa watoa maamuzi wa CCM nikasema pamoja na Mzee Butiku na Mzee Warioba kwamba kama mtu huyu na wenzake watapewa dhamana ya kugombea kupitia CCM basi sisi tusingeondoka CCM ila tungesema CCM isichaguliwe.

Na labda niwarudishe nyuma kidogo, kipindi chote cha mchakato wa Katiba sote tulimjua mtu aliyekuwa anatukwamisha, kwa hakika tulimjua kwa jina na sote tuliamini yeye na watu wa aina yake hawapaswi kupewa uongozi ndani au nje ya CCM. UKAWA walijua hili na tulikuwa pamoja. Hata pale tuliposema CCM ikimpa nafasi tungezunguka nchi nzima kusema CCM isichaguliwe, UKAWA walituelewa sana. Ninapata msongo wa mawazo baada ya CCM kusikia kilio cha wananchi, UKAWA na wana CCM wenye mapenzi mema na CCM na hatimaye kumnyima dhamana ya kugombea kupitia CCM na baadaye kwenda UKAWA, iweje tena UKAWA wale wale tulihangaika nao pamoja wageuke kauli na kusema yuleyule ni jemadari? Nashindwa kumuelewa Mhe. Mbatia, huyu namtaja kwa jina ili anisaidie kujua hivi kwa ukigeugeu huu mkubwa, je wanastahili kupewa dhamana na watanzania kama UKAWA?

Leo watu wale wale walioniunga mkono kusema watu wenye nasaba na ufisadi hawapaswi kupewa nafasi za madaraka na hasa nafasi ya madaraka ya Urais wa Jamhuri yetu, ndio hao wananisema kwamba niache kumsema mtu yuleyule ambaye alitusumbua sote, mimi nikiwemo na hata viongozi wa UKAWA zaidi na wanajua tangu alipokuwa CCM.

Watu wengine wataniambia kwamba hiyo ndio siasa, na mimi kwa unyenyekevu mkubwa nasema siamini katika siasa chafu, siasa inayokumbatia wezi, siasa inayopinda ukweli, siasa inayoendeshwa kwa fedha na hata Hayati Mwalimu Nyerere alituasa kwamba ili nchi hii iendelee inahitaji siasa safi na uongozi bora na akatuasa zaidi kwamba Rushwa ni adui wa haki na Utajiri unaotumika kununua watu ili kupata madaraka ni kama na ukoma. Nimekataa kuwa sehemu ya watu hao, ninaendelea na kiapo change kwamba mtu huyu hastahili kupewa dhamana yoyote katika nchi yetu hata kama nitabaki peke yangu ila najua iko siku nikiwa nimetangulia mbele ya haki ukweli utakuja kujulikana na roho yangu itapoa hukohuko mbele ya haki.


Tusisukumwe na Hasira

Mara zote maamuzi wanayofanywa kwa msukumo wa hasira huwa aidha na tija kidogo sana ama huleta hasara kwa watu binafsi na jamii kwa ujumla. Wahenga walikwishasema “Hasira Hasara”. Ni muhimu sana kutafakari busara hizi za wahenga kipindi hiki ambacho Watanzania tunajiandaa kufanya maamuzi ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kutafakari ni nani hasa anaefaa kupewa dhamana ya kuiongoza Tanzania kwa manufaa ya Watanzania.

Kwa bahati mbaya sana katika kipindi hiki kueleke Uchanguzi Mkuu wa Oktoba 2015, kumeibuka wimbi la siasa na propaganda zinazopandikiza chuki na kuchochea  hasira miongoni mwa Watanzania. Watu hawa kwa kuelewa vyema athari za chuki na hasira hawapendi kutoa fursa kwa Watanzania kutathimini kwa kina matatizo na mafanikio yetu.

Kutokana uchu wa madaraka na nia ya kutimiza ndoto zao za kushika dola, wanaochochea hasira na chuki, wanaminya nafasi ya wapiga kura kupima uwezo na dhamira ya wagombea katika kutatua matatizo ya kimaendeleo na kuendeleza ama kupanua wigo wa mafanikio na ustawi wa Watanzania. Ni muhimu pia kutambua bayana kuwa katika kinyanga’nyiro cha kutaka kutaka madaraka wanasiasa wengi kama sio wote huweka nguvu nyingi katika ushawishi unaolenga kujenga matumaini kwa wananchi ili mradi tu wapate kura. Ni wajibu wa Watanzania kuhoji na kupima uhalisia wa yale tunayoahidiwa na wagombea kwa kutafakari pasipo chuki wala hasira zinazopandikizwa na wanasiasa.   

Ni vyema tukumbuke kwamba katika hali ya hasira na chuki kuna hatari ya  kutosikiliza na kuhoji kwa makini wagombea wote wa uraisi, ubunge na udiwani ili kupima uwezo, weledi, uadilifu na uzoefu wao katika kutekeleza yale wanayoahidi katika sera  na vyama vyao. Maswali ya kujiuliza ni pamoja na Je kuna tija gani kumchagua mgombea fulani? Je mgombea husika anao uwezo, weledi na uzoefu katika kutekeleza yale anayoahidi? Je mgombea ni mwadilifu na anaweza kudiriki kukemea ufisadi? Je mgombea anaamini katika mfumo wa uzalishaji mali unaotoa fursa sawa kwa watanzania wote? Je mgombea na chama chake wanamipango na nia thabiti ya kuondoa kero mbalimbali za wananchi?

Kwa maslahi mapana ya nchi yetu kamwe tusikubali kutumiwa kukamilisha ndoto za watu wachache. Tuwaulize maswali sahihi ili kama hawana majibu sahihi tuwakatae kwa mujibu wa tathimini yetu juu ya sera na hoja zao. Tunafahamu wazi kuwa wagombea wengi wanaahidi mabadiliko ni jambo jema lakini tuwaulize uhalisia na uhakika wa ahadi zao.

Lakini pia wagombea na vyama vyao watueleze bayana tutanufaikaje na nini athari za muda mfupi na mrefu zinazoambatana na mabadiliko hayo. Mwisho ni vyema tutambue   kuwa hatuwezi kupata viongozi wenye nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa kupiga kura za hasira na chuki zinazochochewa na watu wachache wanaotaka kutimiza malengo yao binafsi. Kila tunapowasikiliza wagombea na vyama wakinadi sera zao tuanze sasa kujenga utamaduni wa tuzitafakari na kuzipima hoja zao ili kufanya maamuzi ya busara kupitia sanduku la kura ifikapo tarehe 25 Oktoba 2015.

2 comments:

  1. Asante kwa articles unazoandika brother. Zinafungua macho na kutupa mwongozo tukielekea October 25. Keep up the good work.

    ReplyDelete
  2. Penda taifa lako bomoa kundi la mtandao

    ReplyDelete