Thursday, October 8, 2015

TUTOKE KWENYE “PANGO LA PLATO,” TANZANIA YA VIWANDA INAWEZEKANA



Katika gazeti la RAI  Toleo Na. 1217 la Alhamisi ya Octoba 1-7, 2015, kulikuwa na makala ya Ndugu Kennedy Masiana  yenye kichwa cha habari “Dk. Magufuli Tanzania ya Viwanda haiwezekani.” Katika makala hiyo mwandishi amefanya juhudi kubwa kuonyesha kuwa juhudi zozote za kujenga viwanda kwa Tanzania ni ndoto kwa kuwa gharama za kujenga viwanda hivyo ni kubwa kwa nchi kama Tanzania kumudu. Mwandishi anasema Rais wa Tanzania hana haja ya kujishughulisha na ndoto za kujenga viwanda kwa kuwa ni jambo lisilowezekana.  

Kwa maneno yake  mwandishi anasema, “Watanzania  wa sasa wanamtaka Rais ajaye, awe ni yule atakayeshughulika na hali zao za mashambani, hospitalini, miundombinu bora ya barabara itakayowawezesha kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko.” ... “awahakikishie huduma nzuri za kijamii kama huduma ya maji safi na salama ya kunywa, elimu bora, umeme wa uhakika, lakini pia aguswe na hali yao ya umaskini wa kipato ili waweze kujikomboa kiuchumi.”

Kimantinki na kimaana maelezo ya mwandishi hapo juu yana matatizo makubwa ya aina kubwa tatu: Kwanza, maelezo haya yanaonyesha kukata tamaa na kukubali hali tuliyo nayo kuwa ndivyo ilivyo na haiwezi kubadilika. Kwa sasa serikali imekuwa ikijitahidi kufanya hayo aliyosema mwandishi.  Inaeleweka duniani kote kuwa maendeleo ya kweli yanakuja tu kwa kuwa na viwanda na kwamba sekta zingine zote zitaweza kustawi tu ikiwa tu zimefungamana na viwanda. Mfano, uzoefu wa nchi zote ambazo zimeendelea kiuchumi unaonyesha kuwa  mapinduzi ya kilimo yaliwezekana kwa kufungamana kwa sekta ya kilimo na ukuaji wa viwanda vya kuzalishaji pembejeo na kusindika mazao.

Vivyo hivyo, sekta ya huduma za elimu isiyofungamana na viwanda badala ya kuwa chanzo cha ustawi na maendeleo ya nchi inaweza kuwa chanzo cha matatizo. Kwa mfano, Tanzania sasa inazalisha wasomi wengi kila mwaka, hata hivyo kutokana na kukosekana kwa  viwanda, wasomi wetu hubaki mitaani wakiwa hawana ajira na matokeo yake baadhi yao hushawishika kujiingiza katika vitendo viovu kama vile ukahaba, ujambazi na uhalifu wa aina mbalimbali kama njia ya kujipatia kipato. Lakini tulipokuwa na viwanda katika miaka ya sabini na themanini wahitimu wetu walikuwa wanachagua kazi maana zilikuwepo za kutosha.

Hata sasa tatizo la ajira si kubwa katika nchi kama  China na Korea ambapo kuna uwekezeji wa kutosha kwenye viwanda.

Tatizo la pili la makala ni kuegemea kwenye falsafa za feki na zilizoshindwa za uchumi mamboleo. Msingi mkubwa wa falsafa hiyo ni kuwa dola haipaswi kujishughulisha na masuala ya kiuchumi kama vile viwanda. Kuingizwa kwa falsafa hii kupitia ushawishi na masharti ya wafadhili wakiongozwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF)  katika miaka ya tisini ndiyo sababu kubwa iliyosababisha viwanda tulivyokuwa navyo hapa nchini kubinafsishwa kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kutoendeshwa kwa ufanisi. Hata hivyo, baada ya kubinafsishwa viwanda vingi  kwa matumaini kuwa vingeendeshwa kwa faida na ufanisi, viwanda vingi vilikufa na kuiacha  Tanzania  bila viwanda. Hapo ndipo u-feki wa falsafa hiyo inayojinasibu kuwa sekta binafsi pekee ndiyo injini ya uchumi ilipoonekana wazi. U-feki huo ulijidhihirisha zaidi wakati wa msukosuko wa uchumi wa dunia ulioanzia Marekani mwaka 2008.

Marekani ambayo ndio kuhani mkuu wa falsafa hiyo ya kiuchumi iliamua kuachana nayo na dola kuingilia uchumi ili kuokoa makampuni makubwa yenye maslahi kwa nchi hiyo. Kwa nyongeza, hakuna nchi hata moja duniani zikiwemo zilizoendelea huko nyuma kama uingereza na ujerumani na zile zilizoendelea siku za karibuni kama China, Korea ya Kusini na Taiwani ambayo zilifanikiwa bila dola kujiingiza katika uwekezaji.  Kwa bahati mbaya, falsafa hii feki bado inafunga fikra za watu kama wale wafungwa kwenye hadithi ya pango la Plato. Katika pango hilo wafungwa walinyimwa fursa ya kuona mwanga wa jua.

Walizoea kuona vivuli vya mwanga wa jua ukipiga ukutani kupitia kwenye mlango wa pango, na kwao vivuli hivyo ndiyo ulikuwa mwanga halisi. Siku walipotolewa nje wakaonyeshwa mwanga walikataa kuwa huo siyo mwanga kwa maana kwao vile vivuli walivyozoea kuviona ndiyo mwanga wenyewe. Inabidi tufungue fikra zetu tuangalia hali halisi ya mwenendo wa kiuchumi duniani na tutaona kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana.

Tatu, mwandishi anaonekana kutokujua chanzo halisi cha matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Tanzania kwa sasa. Matatizo hayo ni pamoja na  ukosefu wa ajira, utegemezi wa misaada kwa bajeti yetu, umaskini uliotopea, kudorora kwa huduma za jamii kutokana na kukosekana kwa fedha za kuboresha miundombinu ya kugharamia ubora wa utoaji huduma. Chanzo kikubwa cha matatizo hayo ni kuwa na uchumi usiotosheleza mahitaji.

Hivyo, kama tutakubali maoni ya mwandishi kama yalivyonukuliwa kwenye aya ya kwanza, Tanzania itakuwa imekubali kuwa kwenye “vicious cycle of poverty” yaani  mduara wa umaskini. Kwa maana tutaendelea kuwa kwenye kilimo kisicho na tija, tutaendelea kukopa nje na kuongeza deni la Taifa ili tutoe huduma za jamii. Tutazalisha wasomi ambao wataishia mitaani na kuwa chanzo cha maovu katika jamii. Mwisho wa yote Tanzania si tu kuwa itaendelea kuwa nchi maskini na tegemezi.

Tanzania ya Viwanda anayoinadi Dk. Magufuli Inawezekana.

Hakika ujenzi wa viwanda ndiyo namna pekee ya kujikwamua kutoka katika matatizo yetu ya kiuchumi na kuhakikisha ustawi wa Tanzania ya leo na ya vizazi vijavyo. Bahati nzuri Dk. Magufuli ameeleza ni namna gani atatekeleza azma yake ya kuleta mapinduzi ya viwanda Tanzania ikiwa tutampa ridhaa ya kuwa Rais wetu.

Kwanza, serikali inaweza ikajenga viwanda vya aina mbalimbali nchini kwa kuweka sera nzuri zinazovutia wawekezaji watakojenga viwanda katika maeneo ya kimkakati na kipaumbele kwa nchi.  Bahati nzuri hapa Tanzania tunayo mifano hai kupitia  kujengwa kwa kiwanda cha Dangote (Dangote Industries Limited Tanzania [DIL]),  moja ya viwanda vikubwa vya kuzalisha sementi barani Afrika,  mkoani Mtwara. Kiwanda hiki kimeajiri zaidi ya Watanzania elfu kumi. Serikali pia inapata mapato ya kodi mbalimbali kutoka kwenye kiwanda hicho na kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho. Pia,  Watanzania wengi wameajiriwa na wanauza mazao yao kwa viwanda vya mwekezaji mzawa,  Azam Bakhresa Group of Companies. Dk.Magufuli ameahidi kuwa  moja ya sera zake za kiuchumi ni kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji  wa ndani na nje kuwekeza katika  sekta ya viwanda nchini. Bahati nzuri serikali imeshatenga maeneo maalum ya kiuchumi kule Bagamoyo, Mtwara na Kigoma. Atakachohitaji kufanya Dk.Magufuli ni kuongeza maeneo maalum ya viwanda na kuweka miundombinu muhimu kwa ajili kuleta ufanisi katika shughuli za viwanda katika maeneo hayo. 

Pili, Serikali inaweza kuingia ubia na wawekezaji binafsi kupitia kile kinachojulikana siku hizi kama (Public Private Partnership[PPP]) yaani, ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma. Kwa taarifa tu viwanda vikubwa katika nchi mbalimbali kama China, Korea, Ujerumani vimeundwa kwa mtindo huo.

Tatu, serikali inaweza ikajenga yenyewe viwanda hasa kwenye maeneo ya kimkakati kwa maslahi ya nchi hasa viwanda vikubwa. Hapa inabidi tuelewe kuwa siyo lazima kuwa na fedha taslimu kama mwandishi alivyoashiria. Kama ilivyo kwa wawekezaji wengine wakubwa, serikali inaweza kukopa mtaji kwa ajili ya kugharamikia uanzishwaji wa viwanda husika. Jambo la msingi ni kufanya upembuzi yakinifu na kuonyesha namna kiwanda kitavyotengeneza faida na kulipa deni. Ukopaji huu ni tofauti na ukopaji ambao tunaufanya kugharamia huduma za jamii badala ya sekta za uzalishaji. Tukiwa na viwanda vinavyofanya kazi kwa faida, Watanzania watapata ajira, tutaondoa utegemezi na kuondoa umaskini. 

Nne, kama alivyobainisha Dk.Magufuli, serikali inaweza ikaanzisha mitaji maalum yaani “venture capital” kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia inayohitajika kwa viwanda. Mitaji hii inaweza kupatikana kwa njia mbalimbali kama vile  serikali kukopa, kuingia ubia na wawekezaji, ama kutoka kwenye hazina ya nchi. Mitaji hii kwa kawaida siyo mikubwa lakini ni kichocheo kikubwa katika maendeleo ya teknolojia hasa ya mawasiliano. Ni kwa njia hii ndio viwanda vingi vimechipuka kutoka katika eneo lijulikanalo kama “Silicon Valley” huko Marekani. Hapa ndipo makampuni makubwa ya kiteknolojia kama vile Apple inayozalisha simu za Iphone ilipozaliwa.

Kwa ufupi, hakuna nchi ambayo imeweza kujikomboa katika umaskini na kujiletea maendeleo bila ya kuwa na viwanda. Tanzania haiwezi kukwepa ukweli huo ikiwa inataka kuondokana na mnyororo wa umaskini na matatizo ya kiuchumi yaliyopo.  Tanzania ya viwanda inawezekana tukiweza kuwa na uongozi wenye dira na mikakati dhabiti ya kutufikisha huko.


Na hapa Dk.Magufuli amejipambanua kuwa ana dira na uwezo wa kuleta mapinduzi ya viwanda Tanzania.  

4 comments:

  1. Always a pleasure reading your articles. INSIGHTFUL. Keep up the good. Ingawa swali langu ni kwamba je kwa nchi kama Tanzania inayohitaji maendeleo kupitia uzalishaji wa kilimo na baadae viwanda vya processing inakuwaje kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinachozalishwa huko kinatumika katika kulipa administrators (civil servants) kuliko kuiirudisha fedha hiyo kuendelea kuwekeza kule kwenye uzalishaji ili kuongeza ufanisi katika huo uzalishaji na hatimaye kukuza pato la taiga, Je, Dk amejiandaaje kuleta balance katika hili?

    ReplyDelete
  2. Upo vizuri kiongozi Magufuli ndoo rais

    ReplyDelete
  3. Upo vizuri kiongozi Magufuli ndoo rais

    ReplyDelete
  4. Mungu aendelee kukulinda baba mkomboz, mzalendo, ndugu Dr magufuli

    ReplyDelete