Friday, September 11, 2015

DR. JOHN POMBE MAGUFULI NA UWEZO WAKE WA KULETA MABADILIKO CHANYA



Tujadiliane kwa HOJA na Sababu

Kuelekea uchaguzi Mkuu 2015  mabadiliko ni miongoni mwa mambo yanayochukua nafasi kubwa katika kampeni na ilani za vyama vya siasa. Hoja nyingi zinatolewa hususani katika dhana ya mabadiliko ya mfumo au kiongozi au yote mawili yaani mfumo na uongozi. Kwa bahati mbaya watanzania hawaelezwi mahusiano kati ya mfumo na viongozi. Mbaya zaidi wengi wetu tumeporwa uwezo wa kutafakari kutokana na kuzamishwa kwenye mahaba kwa wagombea au vyama vya siasa.

Kwa kuwa bado kuna siku zaidi ya arobaini ni vyema tukawatafakari baadhi ya wagombea wa nafasi ya uraisi ambao ndio hasa wanachuana vikali katika kampeni zinazoendelea.  Yapo mambo kadhaa yanayoweza kutuongoza katika kuwapima wagombea na sera zao. Moja, ni kutafakari kama inatosha kuwa mashabiki wa matamko tu yenye kushawishi juu ya kuleta mabadiliko  kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wameendelea kuwalaghai wananchi kipindi hiki cha kampeni za uchanguzi mkuu 2015.

Muhimu sana ni  kupima nia na zaidi sana uwezo wa  kiongozi husika kutafsiri madhui ya ahadi zake katika vitendo.  Hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba  wameibuka wanasiasa wanaotoa matumaini hewa kwa wananchi kwa kusema tu yale ambayo wananchi wangependa kusikia. Ni jambo jema kuwajengea wananchi matumaini lakini ni hatari pia kuwalaghai wananchi kwa mambo ambayo kiongozi husika sio tu yeye mwenyewe hayaamini au hana uwezo wala dhamira ya dhati kutimiza. Maswali mawili ni muhimu kuulizwa katika hili, moja ni mfumo gani unaolengwa kubadilishwa ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa watanzania? Je viongozi husika wanavyo vigezo, uwezo  na uzoefu katika kujenga mifumo endelevu?

Edward Lowasa na dhana ya mabadiliko ndani ya UKAWA

Tukianza  na kambi  ya UKAWA inayowakilishwa na Edward Lowasa, tukivipima vyama vya siasa vinavyounda UKAWA kwa mifano na kutafuta vielelezo vya kimfumo inaonekana  dhahiri kuwa  aidha hakuna kabisa mifumo bali haiba (personalities)  au kuna baadhi ya viashiria vya kuwepo kwa mfumo lakini kutoka na kujengwa kwenye misingi dhaifu mifumo hii imekuwa sio endelevu. Pengine kwa kutambua udhaifu huu UKAWA imefungua milango kupokea baadhi ya  wanasiasa ambao wamewahi kuongoza nchi yetu katika nafasi kubwa za uongozi kama ile ya Waziri Mkuu. Hawa ni pamoja na Edward Lowasa ambae ndio mgombe uraisi na Fredrick Sumaye .

Hata hivyo  ukiwauliza au hata ukijaribu kutafuta na kupima jambo gani la kimfumo waliwezakulifanya katika nafasi zao?  Kinachojitokeza ni aidha viongozi hawa hawakuwa na uelewa sahihi wa masuala ya kimfumo hivyo kushindwa kufanya uchambuzi sahihi wa matatizo ya kimfumo na kuyapatia majawabu ya kiutendaji. Mara nyingine  walidandia miradi ya maendeleo na kuisukuma kwa mabavu bila kuweka misingi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kujenga  taasisi imara  kutekeleza na kusimamia sekta husika mambo hayo licha ya kuwa mazuri yaligeuka kusongwa na changamoto nyingi.

Mbaya zaidi viongozi hawa na wengine wanaofanana nao walitumia nafasi zao kujinufaisha wenyewe ikiwa ni pamoja na kujenga mitandao ya kukwapua fedha za umma kwa maslahi yao binafsi na washirika wao. Kinachopaswa kuogopwa sana na Watanzania ni ile hulka ya viongozi hawa kutaka kujilimbikizia mali kwa namna yeyote ile. Hawa ni miongoni mwa viongozi  ambao wamediliki hata kusema kuwa wakichaguliwa kuongoza nchi hii watatengeneza kundi la aina  fulani ya matajiri ambao wataendesha uchumi wa taifa letu.

Swali la kujiuliza ni kama huu ni mkakati wa kimfumo na je haya ndio mabadiliko ambayo Watanzania watarajie? Hii ni dhana hatari inayolenga kuchochea kuongezeka kwa tabaka la maskini na matajiri. Ni muhimu kutambua kuwa matajiri kazi yao kubwa ni kutengeneza faida kutokana na mitaji yao. Haishangazi kuona kuwa matajiri hawa wanaotajwa na mmoja wa wagombea wa uraisi kuwa ni “marafiki” zake wamekuwa wakifadhili harakati za mgombea huyo kuingia madarakani kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita. Jambo jingine la kujiuliza ni Je kwa uwekezaji huu matajiri hawa wanatarajia kuvuna nini? Wasiwasi wangu ni kwamba chondechode mgombea huyu asijekuwa ameweka rehani rasilimali za nchi hii na ikiwa ni pamoja na maisha ya watanzania ili tu atimize ndoto yake ya kuwa raisi wa inchi.

Rai yangu ni kwamba Watanzania tufungue fahamu zetu kipindi hiki cha kampeni na kupima wagombea na hoja  zao pasipo ushabiki na ushawishi mwepesi. Naelewa vyema haja ya kufanya mabadiliko lakini tujiulize ni mabadiliko ya aina gani tunahitaji. Haifai kabisa kumkubali mgombea hana kabisa vigezo vya kuleta mabadiliko eti tu kwa sababu tunataka mabadiliko. Mgombea ambae hana uwezo wala uthubutu wa kukemea ufisadi  hatufai kabisa hasa kwa kuzingatia hulka za kifisadi ambazo zimeshamiri katika jamii yetu sio tu kwenye sekta ya umma bali hata sekta binafsi. Ni nani asiefahamu kuwa ufisadi uwe mkubwa au mdogo ni kikwazo kikubwa katika maendeleo na ustawi ya nchi yetu.

Je ni mara ngapi tumesikia mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA akiweka bayana  mkakati wa kupambana na ufisadi? Ni nani asietambua kuwa ajenda ya mapambano dhidi ya ufisadi ndio iliyowafanya wananchi wengi kuvutiwa na sera za CHADEMA hususani chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho Dr. Wilbroad Slaa?  Tujiulize kwanini vita  dhidi ya ufisadi sio tena hoja kubwa kwa CHADEMA na UKAWA mara tu baada ya kumpitisha Edward Lowasa kupeperusha bendera ya chama hich na umoja huo katika nafasi ya urais kwenye uchanguzi Mkuu.

Zaidi sana tujiulize ni kwa nini Edward Lowasa anapata kigugumizi kukemea ufisadi? Tumhoji atawezaje kutekeleza ahadi zake lukuki za mabadiliko bila kuwa na haki na uthubutu wa kukemea ufisadi? Atahakikishaje huduma za jamii zinapatika kwa wananchi wote, elimu burekwa wote mpaka chuo kikuu, na kuongeza tija kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji bila kudhibiti mianya ya ufisadi? Au anaikwepa vita dhidi ya ufisadi kwa sababu anajua ni kupitia ufisadi pekee hasa kwa njia ya manunuzi na mikataba feki ndio anaweza kulipa hisani kwa marafiki zake wanaoendelea kufadhiri mradi wake wa kuingia Ikulu. Nachelea kusema kuwa kwa Edward Lowasa uraisi ni mradi wakunenepesha mitaji ya matajiri wanaojiita marafiki zake ambao sasa wamekaa mkao wa kula. Sioni dalili za mabadiliko chanya yanayowezakutokana na kiongozi wa aina hii kwenye nchi yetu kwa kuzingatia muktaza tulionao kijamii, Kisiasa na kiuchumi.

Wapo wanaosema eti kwa sababu ajenda ya ufisadi ipo ndani ya Ilani ya CHADEMA ambayo pia inanadiwa na UKAWA, hivyo ikitokea Edward Lowasa akashinda atalazimishwa na ilani hiyo kukemea ufisadi. Wachambuzi hawa wanawezakuwa sahihi endapo wafanya tathmini ya taswira ya uraisi anaoutamani Edward Lowasa na ukweli kwamba ataapishwa kama Edward Lowasa.  Hasa kwa kuzingatia Katiba ya sasa ni dhahiri kwamba atakapoingia tu madarakani sioni kama CHADEMA watakuwa tena na nguvu ya kumdhibiti.

Tusisahau pia kuwa ni CHADEMA na UKAWA ndio walimbembeleza Edward Lowassa kujiunga nao na ni dhahiri kwamba sharti ambalo aliwapatia ni kumpitisha yeye kugombea uraisi. Kana kwamba haitoshi kampeni za mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA zinafadhiliwa kwa asilimia kubwa na Edward Lowassa na Marafiki zake. Maana yake ni kwamba watakapoanza kutaka kudhibiti utekelezaji wa mradi wake wa kunenepesha mitaji ya mafisadi waliofadhili safari yake kuingia Ikulu atawauliza swali dogo tu mnategemea nitalipaje madeni ya kampeni za uchaguzi? Kwa kuufahamu ukweli wa mkataba kati ya viongozi wa CHADEMA/UKAWA na Edward Lowasa lakini pia kwa madaraka makubwa atakayokuwanayo kama raisi wakati huo hawataweza kumdhibiti. 

Wapo wanaoweka imani kwenye uwezekano wa kubadilisha katiba ili pamoja na mambo mengine kupunguza madaraka ya raisi. Ufahamu wangu juu ya uwezo wa watu binafsi kufanya mabadiliko na kiwango   cha mabadiliko huchangiwa sana na historia ya muhusika na kundi/kizazi/tabaka anakotoka. Kwa mfano mara nyingi wazee ni hawapendi madiliko hasa yale yanayokinzana na matakwa yao. Simuoni mzee Edward Lowasa katika umri wake eti anatakakuleta mabadiliko ya kasi hasa ukizingatia yeye ukiacha majanga ya kisiasa aliyokutana nayo yupo katika tabaka la matajiri.

Dkt. John Pombe Magufuli na Mabadiliko ndani ya CCM

Watanzania wengi bila kujali itikadi na nafasi zao wamewahi ama  kusikia, kukiri, au kuthibitisha kwa vitendo kuwa  Dkt. Magufuli ni kiongozi shupavu, mwenye dira na uwezo wa kubadili mifumo  na utendaji  katika sekta mbalimbali. Hii inathibitika wazi pale watu wanapoamua kufanya tathmini sahihi ya utumishi wa kiongozi huyu kwa kuangalia  utendaji wake na mafanikio yaliyofikiwa na sekta au taasisi ambazo Dkt Magufuli amewahi kuzisimamia.  Hapa ni vigumu kupinga ukweli kwamba Dkt magufuli ndiye aliyeleta mabadiliko na maboresho katika sekta ya Ujenzi hususani wa miundo mbinu ya barabara.

Maeneo mengine ambayo Dkt Magufuli ameacha  mbegu ya maboresho ni  katika sekta ya ardhi pamoja na ile ya mifugo na uvuvi  licha ya kuzitumikia sekta hizi kwa muda mfupi kabla ya kurejea tena kwenye sekta ya Ujenzi. Taswira ya sasa ya sekta ya ujenzi ambayo sio tu kwamba ina mifumo bayana na thabiti licha ya changamoto kadhaa, sekta hii inasimamiwa na taasisi madhubuti ambazo zinalenga kutafsiri dira na mikakati ya sekta katika uhalisia na vitendo.

Akiwa Naibu wa waziri wa ujenzi katika serikali ya awamu ya tatu, ni Dkt. Magufuli ndie alibadilisha mfumo wa kutegemea wahisani kwa asilimia miamoja katika sekta ya ujenzi wa barabara.Mfumo huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Ujenzi, takribani asilimia sabini (70%) ya miradi yote ya ujenzi wa barabara inchini inajengwa kwa kutumia fedha za serikali. Ni asilimia thelasini pekee ya miradi yote ya ujenzi inafaddiliwa na wahisani. Swali la kujiuliza ni je nini kimefanikisha utelekezaji wa mfumo huu? Hapa ndipo unawezakuona uwezo na uzoefu wa kiongozi katika kubadili mfumo kwa kujenga taasisi zinazotakiwa ili kusimamia na kuendeleze mfumo.  Ni Dkt. John Pombe Magufuli ndie alieanzisha harakati za maboresho katika usimamizi, utekelezaji na uendelezaji wa sekta ya ujenzi nchini.

Kiongozi huyu amesimamia kuanzishwa kwa taasisi kadhaa muhimu katika sekta ya ujenzi ambazo ni pamoja na Mfuko wa barabara (Road Funds) ambao mapato yake yameongezeka kutoka shilingi bilioni 73.08 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 751.7 mwaka 2014/15. Taasisi nyingine ni pamoja na Wakalawa barabara (TANROADS) inayosimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja. Pia zipo taasisi kama Wakala wa Majengo Tanzania (TBA); Board ya Usajili wa Wahandisi (ERB); Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRD na Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB). Taasisi zote hizi zinalenga kutelekeza majukumu tofauti lakini yanayotegemeana katika ustawi wa sekta ya ujenzi. Hapa unaweza kuona mantiki ya ujenzi wa mfumo sio hisia wala propaganda.

Mifano hii michache ni kielelezo cha uzoefu, dhamira na upeo, na umakini wa kiongozi katika  kuchambua, kuamua na kusimamia mambo miradi ya maendeleo. Ni mgombea Dkt. John Pombe Magufuli ndie ambae amembanua wazi dhamira na mikakati yake kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Huyu sio tu kwamba anasema dhahiri kwamba  atafungua mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi lakini pia uzoefu katika wizara alozitumikia una akisi dhamira hii.


Ni vigumu kupinga ukweli kwamba hatua ambayo nchi yetu imefika inahitaji kiongozi ambae sio tu anapenda kusema kile ambacho watanzania wanapenda kusikia bali kile watanzania wanachohitaji yaani Kiongozi mwenye uwezo wa kurejesha uadilifu, uaminifu na uchapa kazi katika sekta zote.

NI SAWA TUNATAKA MABADILIKO: JE NI YA MAGUFULI AU LOWASSA??


Tutafakari kwa Hoja na Sababu

Wagombea Urais wa CCM, Dr. John Magufuli na mwenzake wa CHADEMA Ndg Edward Lowassa wanakubaliana jambo moja kubwa: Haja ya kuwa na mabadiliko katika nchi yetu. Wagombea wote wameahidi kila mmoja kuwa iwapo atashinda ataleta mabadiliko. Tulinganishe sasa na kupima aina ya mabadiliko ambayo yanaweza kutokea iwapo mmojawapo atachaguliwa kuwa Rais wa nchi yetu.

Kulingana na historia ya utendaji wake katika wizara alizokabidhiwa na ahadi anazotoa mgombea wa CCM, Dr. John  Magufuli, chini ya Urais wake inaonekana  utawala wa sheria na nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma itatamalaki.  Magufuli anajulikana zaidi kwa Watanzania kuwa ni mtu anayesimamia sheria hata pale zinapogusa maslahi ya wakubwa zake. Watanzania watakumbuka jinsi Magufuli alivyoweza kurudisha magari yaliyokuwa yameporwa kinyemela  na vigogo wa serikali enzi za utawala wa Benjamin Mkapa.

Kwa upande wa  Ndg. Edward Lowasa, iwapo  atachaguliwa kuwa Rais, kuna uwezekano mkubwa kukawa na utawala unaotegemea hisia za Rais na ‘marafiki’ zake  badala ya utawala wa sheria. Utendaji wake wa nyuma unaonyesha wazi kuwa Lowassa kama kiongozi ni mtu anayeamini matashi yake binafsi bila kuzingatia utawala wa sheria. Watanzania watakumbuka kuwa March 2006, akiwa waziri mkuu, Lowassa alimfukuza kazi mhandisi wa Manispaa ya Temeke bila kumpa nafasi ya kujitetea na tena mbele ya waandishi wa habari na kundi la wananchi waliokuwepo katika tukio la kuporomoka jengo la Chang’ombe Village.  

Hivi karibuni, wakati anazindua kampeni zake, Lowassa alitoa ahadi kuwa ikiwa atashinda atamuchia huru Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya aliyefungwa maisha jela kwa kwa kosa la  kubaka na kulawiti watoto katika hukumu iliyotolewa na mahakama ya hakimu mkazi kisutu mwaka 2004. Kesi hiyo ilipelekwa katika mahakama ya rufaa mwaka 2010 na Mahakama ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya chini. Tena, mwaka 2013, jopo la majaji wa mahakama ya rufaa watatu likijumuisha Jaji Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Msati walifanya mapitio ya mahakama hiyo na kuwaona wafungwa hao kuwa wana hatia.

Ikumbukwe kuwa sheria za Tanzania zinamyima Rais mamlaka ya kusamehe watu waliofungwa kwa makosa ya kubaka na kulawiti. Kwa kutamka kuwa atawachia wazi wafungwa hao,bila ya kusema chochote juu ya wale watoto waliolawitiwa na kubakwa na haja ya kufuata utawala wa sheria nchini ni dhahiri kuwa katika utawala wa  Lowassa utawala wa sheria utawekwa kando na matashi ya watawala ndio yatakuwa yanaongoza nchi. Hili linadhibitishwa na ahadi nyingine  ya  Lowassa  kuwa  akiwa Rais, watuhumiwa wa kesi za ugaidi waliokamatwa huko Zanzibar wataachiwa huru kwa amri ya Rais. Ikumbukwe kuwa kwa sasa dunia iko kwenye vita dhidi ya ugaidi na ugaidi ni hatari kubwa na thahiri kwa maisha ya  wananchi na mali zao.

Wagombea wote wameahidi kupambana na ufisadi na rushwa iwapo watachaguliwa kushika nafasi ya Urais. Magufuli ameahidi wazi kuwa ataleta  mabadiliko katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia masuala hayo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa rushwa itaweza kudhibitiwa katika utawala wake ukizingatia kuwa katika harakati zake zote hakuungwa mkono na genge la mafisadi kama ilivyozoeleka kwa siasa za CCM tangu mwaka 2005 ilipotekwa na genge la wanamtandao.

Hali hii itamfanya aweze kutawala bila kuwa na  deni la kulipa fadhila kwa mtu yeyote. Uzoefu wa siku za karibuni unaonyesha kuwa rushwa na ufisadi mkubwa unasababishwa na kujaza ‘marafiki’ katika nafasi muhimu za maamuzi. Kujaza marafiki hasa waliokufadhili kwenye harakati za uchaguzi kunafanya mifumo ya uwajibkaji katika nchi iwe na ganzi ya kufanya kazi dhidi ya marafiki hao.

Kwa upande wake Lowassa hajaeleza atafanya nini bayana katika kupambana na rushwa zaidi ya kusema atashughulikia rushwa. Kama ambavyo ilibainishwa na waziri mkuu mstaafu na mpambe wa Lowassa katika harakati za Urais, Fredrick Sumaye,  katika viwanja vya jangwani, Lowassa ndiye mwasisi wa ‘mtandao’ uliomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005. Kundi hili lilimjumisha pia Rostam Azizi na Laurence Masha ambao leo hii ndio pia ndio wanaongoza mikakati ya Lowassa. Rushwa katika mikataba ya aina mbalimbali na hata ukwapuaji wa fedha za umma kupitia maskandali mbalimbali kama EPA, Richmond  na Dowans ulifanyika kama njia ya kulipa deni la fadhila wakati wa uchaguzi. Kama tulivyogusia hapo juu, ni vigumu kuchukua hatua dhidi ya marafiki na maswahiba.

Baada ya CCM kujikomboa kutoka katika makucha ya wanamtandao kwa kuwaondoa wagombea wa kundi hili akiwemo Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea Urais kupitia chama hicho, kundi hilo limeweza ‘kuiteka nyara’ CHADEMA na kupitia kwake vyama vikuu vya upinzani kupitia UKAWA. Lowassa amesema waziwazi kuwa fedha anazogawa kwa wananchi mbalimbali zinatokana na ‘marafiki’ zake. Kwa hiyo, kama atachaguliwa, utawala wa Lowassa utaendeleza utawala wa wanamtandao, na watanzania watarajie kushamiri kwa ufisadi nchini kwa sababu tulizoeleza hapo juu.

Watanzania watakumbuka kuwa kile kinachoonekana kuwa ni ushabiki wa kupindukia kwa Lowassa hauna tofauti na ushbiki uliokuwepo mwaka 2005  kwa Kikwete. Hii inatokana na ukweli kuwa kundi linaloratibu na kuongoza kampeni za Lowassa ni lilile lililofanya kazi hiyo mwaka 2005. Tayari, kuna taarifa zinazosema kuwa wanamtandao wameshagawana nafasi muhimu za uongozi na mikataba katika maeneo manono kama bandari, madini na vitalu vya gesi na mafuta iwapo watafanikiwa kuiteka dola kupitia uchaguzi.

Magufuli ameahidi kuwa ataleta mabadiliko katika utendaji wa watumishi wa umma kwa kuweka mifumo imara ya uwajibikaji. Watu walio karibu na Magufuli wanasema kuwa Magufuli ameahidi kuwa akiwa Rais atawekeana mikataba ya utendaji kazi (Perfomance contracts) na mawaziri wake ambapo kila waziri ataingia kama yeye binafsi na akishindwa kufikia malengo atawajibishwa kwa kuondolewa madarakani. Magufuli ameahidi pia kuwa mafisadi watakaotiwa hatiani watafilisiwa mali zao. 

Kwa upande wake Lowassa amesema kuwa akiingia madarakani atabadilisha mfumo wote wa nchi. Hii ina maana kuwa Lowassa akiwa Rais, taasisi za utawala kama vile Polisi, Jeshi, Utumishi wa Umma na vyombo vingine vitafumuliwa na kuundwa upya na kuwekwa watu wapya. Muhimu hapa ni kukubaliana  kuwa siyo rahisi kwa jambo hilo kufanyika kwa kuwa kama ilivyo duniani kote yeyote atakaye shinda atalazimika kufanya kazi na vyombo hivyo. Mabadiliko yeyote ya utendaji wa vyombo hivyo vitategemea na hulka, tabia na haiba ya Rais. Hakika duniani kote mabadiliko katika nchi huletwa kwa vyombo hivyo kufanya kazi zao ipasavyo kutokana na uongozi na usimamizi dhabiti wa mkuu wa nchi.

Hitimisho


 Haya ni baadhi ya mabadiliko yanaweza kutokea iwapo mmoja wa wagombea wetu watachaguliwa katika nafasi ya Urais. Mabadiliko haya yanaonyesha wazi kuwa uchaguzi ni muhimu sana kwa mustakabali wetu kama mtu mmoja mmoja na kama Taifa. Kwa sababu hiyo, ushabiki na uungwaji mkono wa wagombea lazima uzingatie faida na hasara zake kwa nchi na kwetu binafsi. Ni wakati wa kuwahoji na kuwatathimini wagombea wetu ili siku ya upigaji kura tisije tukafanya kosa litakalotuathiri sisi na vizazi vyetu.  Tathmini hiyo ni muhimu kwa kujua kuwa utendaji kazi wa Rais huakisi na kuathiri utendaji kazi wa serikali na taasisi zote zilizo chini yake. Yaani Rais akiwa fisadi serikali na vyombo vyote chini yake vitakuwa vya kifisadi. La, Rais akiwa mwadilifu na mchapakazi na serikali yake itakuwa vivyo hivyo. 

Saturday, August 29, 2015

CCM, UKAWA NA KUNG’OA MFUMO WA KIFISADI NCHINI



Wananchi wengi tunakubalina kuwa adui mkubwa wa Tanzania kwa sasa ni  ufisadi ambao ndio umekuwa chanzo kikubwa cha utajirisho wa  watu wachache  na huku ukistawisha umaskini kwa wananchi walio wengi. Baadhi ya wananchi wamekuwa na mawazo kuwa hatuwezi kupambana na ufisadi bila ya kwanza kuiondoa CCM madarakani kwani kwa maoni yao CCM ndio mfumo wenyewe wa kifisadi.  Lengo langu leo ni kutaka tutafakari usahihi wa dhana hii katika uhalisia wake ili itusaidie kuchukua hatua sahihi katika kuung’oa mfumo wa kifisadi nchini.

Kwanza, kuna haja ya kutambua ukweli kuwa rushwa na ufisadi ndiyo adui mkubwa wa maendeleo ya kweli ya nchi yetu. Ukweli huu uligundulika mapema kabisa  baada ya nchi yetu kupata uhuru pale ambapo sehemu ya tabaka la watu walioshika nafasi za uongozi baada ya uhuru kutaka kutumia nafasi zao kwa ajili ya kujitajirisha wao binafsi kwa gharama ya wananchi wenzao. Tabaka hili lililokuwa linajulikana enzi hizo kama wabenzi, ikimaanisha wamiliki wa magari ya Mercedez Benz ambayo ndio ilikuwa alama ya kuwa tajiri, liliona kuwa kushika nafasi ya uongozi katika dola ni kupata fursa ya kijitajirisha. 

Hali  hiyo ingeruhusiwa kuendelea ingewakatisha tamaa wananchi na kujenga ufa baina yao na uongozi wa nchi. Pia hali hiyo ilionekana kusaliti matumaini ya wananchi katika kupigania na kupata uhuru. Hakika hali hiyo ingeruhusiwa kuendelea  ingefanya uhuru usiwe na maana kwa wananchi. Kwa bahati nzuri uongozi wa TANU chini ya Baba wa Taifa uliligundua tatizo hilo na kuchukua hatua za kukabiliana nazo.

Ili kupambana na ufisadi uliokuwa umeanza kujengeka, mwaka 1966 , Mwalimu Nyerere baada ya kupokea changamoto kutoka kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam waliokuwa wanaandamana, wakilalamika pamoja na mambo mengine kuwa viongozi walikuwa wanatumia nafasi zao kujinufaisha alipunguza mishahara ya  viongozi kwa kuanzia na kupunguza mshahara wake kwa asilimia ishirini. Mwaka 1967, TANU ilitangaza sera ya Ujamaa na Kujitengemea iliyokuwa inalengo la kujenga jamii yenye usawa na haki na kukomesha unyonyaji na ukupe kati ya mtu na mtu.

Miiko ya uongozi iliwekwa  ili kuhakikisha kuwa viongozi wanatumia madaraka yao kulingana na dhamana waliyokabidhiwa na si kwa faida  zao binafsi. Miiko hiyo ilidumu mpaka mwaka 1992 tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi.  Baadhi ya Miiko hii bado ni sehemu ya katiba ya CCM. Ibara ya 18 ya Katiba ya CCM inazuia  kiongozi:- “(1) Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa upendeleo, au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo. (2) Kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa, kushiriki katika mambo yoyote ya magendo au mambo mengine yaliyo kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo.” 

KUTEKWA CCM NA UFISADI

Kwa hiyo, CCM kwa asili yake na mfumo wake imeundwa kupambana na ufisadi na si kukumbatia ufisadi, hata hivyo tunajua kuwa  kwa miaka ya karibuni ufisadi umemea na kukuwa kwa kiwango kikubwa nchini. Hali hii imesababishwa kwa kiwango kikubwa na kufanikiwa kwa kundi la watu wachache lakini lenye ukwasi mkubwa lijulikanalo kama ‘mtandao’  kufanikiwa ‘kuiteka nyara’ CCM kwa kufadhili wagombea kwenye nafasi za ubunge na Uraisi.  Walioshika madaraka katika nyadhifa za uongozi walitumia nafasi hizo kulipa fadhila kwa wafadhili wao kwa njia ya mikataba minono lakini yenye athari kubwa kwa maisha ya wananchi. Ni katika kipindi hichi ndio tumeshuhudia maskandali  ya kifisadi kama vile mkataba wa Richmond, Meremeta, ukwapuaji wa fedha za EPA, n.k. Hali hii ilitokea ili ngenge la mtandao liweze kufidia gharama walizotumia kufadhili kampeni za mawakala wao kuingia madarakani. Hali hii iliimarika zaidi baada ya  uchaguzi wa 2005.

Katika uchaguzi wa mwaka huu na kama ilivyokuwa katika chaguzi za kuanzia mwaka 1995, ili kuendelea kunufaika na rasilimali za nchi kundi la mtandao, limejizatiti kwa kutumia nguvu ya hela kuingiza mawakala wao katika nafasi ya Urais. 

Hata hivyo, mara hii CCM ilifanikiwa kuzishinda  jitihada za kundi hili ‘kuiteka’na kuhakikisha kuwa mgombea wa kundi hili  katika nafasi ya Urais hateuliwi kugombea Urais kupitia chama hicho.  Jitihada hizo ndio zilisababisha mgombea wa sasa wa Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dr. John Magufuli kuteuliwa. Sifa kubwa iliyombeba Magufuli ni kutokuwa ngenge la watu wenye fedha wanaomfadhili.  Kwa uteuzi wa Magufuli, CCM inaonyesha kuwa imejizatiti kurudi kwenye asili yake ya chama kinacho simamia maadili na miiko ya viongozi.

KUTEKWA NYARA KWA UKAWA

Baada ya kundi la mtandao kung’olewa CCM na ili liendelee kunyonya  na kufisadi rasilimali za nchi,  lilifanya jitihada kubwa kwa kutumia nguvu ya pesa kuviteka vyama vya upinzani vyenye nguvu nchini kupitia umoja wao wa UKAWA. Kwa kuelewa kuwa kundi hili linataka madaraka si kwa sababu nyingine ila kuendelea ‘kuifaidi’ Tanzania lakini kwa gharama  ya maisha ya Mtanzania wa leo na vizazi vijavyo, waasisi wa UKAWA ambao walitoa maisha yao  kuunda na kuujenga UKAWA  kama njia ya kuimarisha upinzani nchini, Dr Wilbroad Slaa na Prof. Haruna Lipumba wameamua kukaa pembeni ili kuepuka kushiriki kuingiza madarakani mfumo wa kifisadi ambao walitumia muda na maisha yao kupambana nao.

Hakika historia itawakumbuka viongozi hawa  kwa misimamo yao imara ya kupinga mfumo wa  ufisadi kokote hata kama wanufaika wa mfumo  huo watakuwa wao. Maana nafasi zao ziliwahakikishia kufaidi matunda ya mfumo huo kwa sasa na ikitokea kundi hilo likashinda uchaguzi.

KUNG’OA MFUMO WA KIFISADI

Tumeona kuwa chanzo kikubwa cha kuvurugika kwa mfumo wa maadili nchini ni ngenge la mtandao ambalo kwa kutumia nguvu ya pesa limeweza kuingiza mawakala wao kwenye nafasi za uongozi kupitia CCM. Bahati nzuri CCM wameweza kupambana na kundi hilo kwa kuzuia jitihada zake za kuendelea kuiteka nyara. Tumeona kuwa, baada ya kushindwa kundi hilo sasa limeuteka upinzani nchini kupitia UKAWA kwa kutumia nguvu ya fedha. Wananchi wameshuhudia kundi hili likigawa hela kwa makundi mbalimbali ya wananchi katika kujihakikishia wanapata uungwaji mkono ili  mgombea wao aweze kushinda Urais.


Kundi hili haliamini katika sera au itikadi yeyote ndio maana liliposhindwa CCM limehamia UKAWA  ambapo kila chama kina ilani,sera na itikadi tofauti. Hali haliwasumbui kwa maana shida yao kama wanavyosema wenyewe siyo sera bali kushika madaraka ili waendelee kuifisadi nchi.  Kwa kuhitimisha kama tunataka kung’oa ufisadi nchini, inabidi tuhakikishe kuwa kundi hili la haliingii tena kushika madaraka ya nchi. 

Sunday, July 26, 2015

TUJIKUMBUSHE: KATIBA BORA AFRIKA NI ILE ITOKANAYO NA MAONI YA WANANCHI




Nianze kwa kuzurula

Unajua furaha ya ujana ni kuweza kufanya makosa, kueleweka, kusamehewa, na kupuuzwa kwa kigezo kwamba ni ujana unasumbua au unajua damu bado inachemka na sababu kadhaa wa kadhaa zinazofanana nazo. Sidhani kama vijana wenzangu wameling’amua hili, kwamba ni wakati wa ujana mtu huruhusiwa kwa kiasi fulani kukosea kama sehemu ya kujifunza. Ni kipindi hiki kijana anaweza akasema mambo mazito na yakachukuliwa kawaida kwa kile kile kigezo kwamba ujana huo, akikua ataacha. Namshukuru Mungu kwamba nimo kwenye rika la kujifunza na hasa na niseme kwa kiingereza “interest” yangu imekuwa kujifunza kuhusu nchi yetu, ikoje, inaongozwaje, changamoto zake, magumu ambayo viongozi wetu au kama wanavyojulikana wakubwa, wanayokabiliana nayo siku hadi siku katika uongozi na utumishi.

Nimeanza hivyo makusudi kwasababu naanza kuona kama katika Makala hii nitaongea mambo ambayo niombe samahani mapema na nitashukuru kama nitachukuliwa kama ni ujana tu unanisumbua na ni damu inachemka. Siku moja Mama Mwatum Jasmine Malale Mjumbe wa Tume ya Katiba aliniambia kitu ambacho mpaka leo huwa nikipata wasaa nawasimulia na vijana wenzangu. Alisema kuna tofauti kati ya kuwa na akili au uwezo wa kufanya mambo labda kwa haraka, kwa ustadi na kwa umahiri upande mmoja na kuwa na hekma au hekima, uwezo wa kuyatizama masuala kwa undani, kwa pande zote na hasa hasa ukizingatia uzoefu unaojengwa na wakati. Akaniambia unaweza kuwa na akili na ukakosa faida ya uzoefu unaokuja kwa wingi wa wakati. Mtu mwenye akili ni mwepesi kuhadaika lakini mtu asiye na werevu wa akili ya darasani au hii akili ya kileo ya kukurupuka ni vigumu sana na nikitumia lugha ya vijana “kuuingia mkenge” kwasababu ameshaona “mikenge mingi” katika maisha yake na hivyo kuikwepa si bahati ni hekma (hapa msisitizo ni wangu).

Sasa nauanza ujana, juzi juzi hapa nalipata kusikia kwamba Katiba Inayopendekezwa ni bora kuliko Katiba zote Afrika, nikasema hilo nalo neno na sikupenda linipite pasina kusema neno. Unaposema Katiba Bora unamaanisha nini? Na je umepima kwa vigezo vipi? Au tunarudi kule kule kwenye simulizi pasina ushahidi? Najua baadhi yetu sisi vijana wa leo tungepata fursa ya kupata kile kifaa cha kurudisha wakati nyuma labda miaka 30, huenda tungewapuuza wananchi katika mambo mengi sana. Kwa namna ambavyo naona baadhi yetu kipindi hicho tungeamua mambo sisi wenyewe, watu tungesema hawa wanapaswa kutengenezewa vitu na kupelekewa na wala hawana haja ya kuulizwa maana tungeamini kabisa wao (wananchi) ni wa kutawaliwa tu.

Yaani nawaona baadhi yetu tukitembea huku na huko tukijua sisi ndio tujuao kuliko wananchi na kwamba hata inapokuja masuala makubwa yawahusuyo wao wananchi basi, tutaambiana kama wakati mwingine ni lazima watu watuelewe, uongozi sio jambo dogo. Naona kama tumekaa kwenye viti katika mduara mdogo kwenye bustani nzuri na tunafurahi kwa vinywaji na tukipata mchapalo taratiibu na tukisema unajua kamaradi, uongozi hapa sio kama kilimo cha nyanya, uongozi sio kama ufundi gereji, uongozi ni kazi, na michapalo hiyo inakuwa ndio wigo wa kutuweka mbali na watu wetu. Hapo ni Miaka ya 80 tukiwa tumerudisha wakati kwa kutumia kile kifaa maalum “time machine”.

Lakini muda unafika na tunarudi tena katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa dijitali, karibu kila mtu anajua kitokeacho duniani katika viganja vya mikono yake. Ulimwengu ambao tofauti na ule wa miaka ya 80, siku hizi ukisema uongo watu wanabaki na sauti yako au video yako ukisema uongo, ukiwa holela hata mambo ya kusitiriwa yanawekwa bayana Astakafilulah ni sheedah! Naona ulimwengu wa leo watu hasa vijana hawapokei tu eti tu kwasababu amesema mkubwa, hapa, wanapenda kuhoji kwanza, wanapenda waelezwe misingi kabla ya kuunga mkono hoja, na kadhalika.

Katiba Bora ikoje?

Katiba huwa ndio sheria mama, huwa ndio msingi mkuu wa sheria katika nchi au taasisi. Katiba kwa kawaida na kidesturi hutungwa na wenye kuitumia, bado haijawa mifano mizuri kwa baadhi ya katiba kutungwa na watu wachache na zikawa nzuri na kutumiwa na watu wengi kwa muda mrefu. Katiba Bora siku hizi ni ile ambayo imeandikwa kwa kuzingatia uwakilishi mpana, na tukumbuke dhana ya uwakilishi mpana si nyepesi, na tunaposema uwakilishi mpana tunakwenda mbali zaidi kusema ni kwa kiasi gani kila mtu anayeshiriki, mchango wake unaheshimiwa na sio ule mchezo wa hadaa wa wengi wape wachache wasikilizwe, la hasha.

Ushiriki huanzia kwenye sheria inayo ongoza mchakato, kisha katika ushiriki wa watu, wanapotoa maoni na hapa nyumbani walipokaa kwenye mabaraza na hatimaye walipokaa kwenye Bunge Maalum. Hivi nikuulize baba, na naomba unijibu kweli na kweli tupu ile ya kutoka ndani ya moyo wako, hivi wananchi tuliwaacha huru wakati wa kutoa maoni?

Hebu ngoja nikusimulie kitu kidogo, si unajua karibu kila mtu ana kadi ya chama chake? Sasa kipindi kile kule Tume wako waliokuwa wanajulikana itikadi zao na vyama vyao na wapo wale waliokuwa wana vyama lakini kwa asili ya kazi zao, utambulisho wa vyama vyao ulibaki uhusiano wa ndani kati yao na vyama vyao. Mimi ni mmoja wapo, sasa kuna mzee wangu mmoja, alijaribu sana kunipa kadi ya chama chake, masikini hakujua na mimi ni mwanachama tayari wa chama kingine, nikamkwepa kwepa sana. Lakini leo nikiri kwa mara ya kwanza nilishikwa na uchungu mkubwa sana baada ya kuona namna vyama vilivyokuwa vikilazimisha wananchi kutotoa maoni yao na wakati mwingine wakiwatisha kabisa watoa maoni wale. Nakumbuka nilichukia vyama vya siasa, mpaka ndani ya moyo wangu, nikajiambia inakuwaje vyama kuwa magenge ya maharamia wawatishao watu ili wasiseme Tanzania yao wangependa iweje.

Kuna wakati na ujana wangu ilipasa niwe mkali kila nilipo ona vitisho vinaongezeka, kuna siku ilikuwa katika Baraza la Katiba la Wilaya mojawapo kusini mwa Tanzania, na mtoa maoni alikuwa Mkuu wa Wilaya Mstaafu, huyu alisema wazi kwamba yeye amekataa kupokea maelekezo na atatumia fursa ile kusema yake. Wakati akiongea wengine walijaribu kumzonga zonga, nimeumia sana kwa matukio yale na nimeendelea kuumia. Sasa “baba” unasema kwa mazingira yale ya Bunge Maalum na namna ambavyo vyama viliuteka mchakato bila simile, je hii ni Katiba ya Wananchi na Bora Afrika au ni yale yale ya safari yangu iliyonipeleka miaka ya 80 kipindi mimi na wenzangu tukiwapuuza wananchi. Tena nikumbushe kipindi kile niko miaka ya 80 tulikuwa tukiambiana kabisa wananchi wanapaswa kupigwa propaganda na watakaa sawa. Nauliza, hizo ndio zama za leo?

Kauli ya Mheshimiwa Rais

Mhe. Rais wakati alipokabidhiwa Katiba Inayopendekezwa alisema wakati mwingine mambo mazuri yapasa yasubiri wakati upite, haya, tujadili, unakumbuka msingi wa kwanini alisema yasubiri wakati upite? Alisema baadhi yetu tuna hofu, anhaa, sasa nauliza hivi dawa ya hofu ipo au itakuja kulingana na muda unavyokwenda?

Je Hofu ya Mapendekezo makubwa ya Tume ya Jaji Warioba, ni ya kusubiri miaka 10, 20, 30 ijayo au ni suala la kueleweshana kwa taarifa na maarifa sahihi? Najiuliza. Maana siku hizi kila mtu ameshika lake tu, ooo Rais amesema tusubiri, narudia kusema tuache kumtafsiri Rais ili kukidhi matakwa yetu.

Nimalizie kwa kusema “ee baba” Katiba Inayopendekezwa sio bora hata kidogo na kimsingi inatugawa watanzania, inalinda maslahi ya wachache na imetupilia mbali maoni ambayo wananchi walitaka yawemo.

Rai kwa wagombea Urais na Ubunge

Nendeni mkawaambie wananchi kwamba mtajitahidi kushughulikia suala la Katiba ili tuwe na uelewa wa pamoja, tujenge muafaka wa kitaifa na tufanye maridhiano inapobidi, huo ndio uongozi. Hatuwezi kamwe kuwa na kura ya maoni tukiwa tumegawika kiitikadi na kimsimamo kama vyama vya siasa, mgawanyiko huu utashuka kwa wananchi na hii sio afya kwa Taifa letu.

Sunday, July 19, 2015

UKAWA, NI AMA MPITE KATIKA TANURU NA KUTOKA KAMA DHAHABU SAFI AMA OMBENI RADHI WATANZANIA



Siasa safi na si siasa ya uadui

Kila siku huwa ninapozungumzia ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu, baadhi ya watu huwa hawanielewi ninaposema kwamba CCM imara ni lazima iambatane na upinzani makini. Na kwamba kwa mazingira yalivyo sasa pasina kuwa na upinzani makini CCM itayumba, na kuyumba huku sio lazima kuiangushe CCM leo, lakini sote tunakubali kwamba kuwa katika safari ambamo gari linayumba yumba huwa si dalili njema. Nadhani wengine wanaendelea kutonielewa, mantiki ya uwepo wa vyama vya siasa katika ulimwengu wa leo ni kuibua hoja, kujenga hoja, kuleta mawazo ya kustawisha maisha ya watu na raia wa Taifa letu.

Kama chama kimojawapo kipo madarakani na kinatekeleza mawazo yake ya kustawisha maisha ya Wananchi, kazi ya vyama ambavyo haviko madarakani ni kuibua hoja na kujenga hoja ya namna mawazo hayo ama yanafanikiwa au la na kuhakikisha chochote kinachofanyika kweli kina mguso chanya kwa Wananchi. Aidha vyama vile ambavyo havipo madarakani vina kazi kubwa pia ya ama kuboresha mawazo ya chama kilichopo madarakani au wanaweza kuja na mawazo mbadala kabisa, ilhali lengo likiendelea kuwa kustawisha maisha ya watu na raia wa Taifa letu.

Sijui niseme hivi karibuni au tangu kitambo, kumejengeka dhana mbaya kwamba mkiwa katika vyama tofauti basi ninyi ni mahasimu, ninyi ni maadui na wengine huenda mbali na kujinasib wao ni wa utawala wa nuru na wengine ni wa utawala wa giza. Mimi nakubali kabisa vyama kama Taasisi ni watu na watu hukosea na tukubaliane kwamba watu wanapokosea wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa taratibu  tulizojiwekea, Katiba na sheria zetu ikiwa ni mojawapo. Kwahiyo watu wakikosea, wawajibishwe, hata kama watu hao wanatoka chama chako, na si ustaarabu iwapo unashabikia watu kuwajibika kutoka vyama vingine wakati katika chama chako kuna matatizo.

Unapokuwa sio msafi unapoteza mamlaka ya kimaadili “moral authority” ya kukemea wengine wasio wasafi. Hata katika vitabu vya dini imeandikwa “ufalme mmoja hauwezi kuinuka juu ya ufalme uleule bali ufalme mwingine”, tafsiri yangu ya ufalme hapa yaweza kuwa watu wasio wasafi hawawezi kamwe kuwawajibisha watu wachafu na halkadharika watu safi hawana sababu ya kuwawajibisha watu walio safi, hiyo ni asili. Tunataka watu wasafi zaidi kama mtu mmoja mmoja katika mifumo yetu na mamlaka zetu za nchi ili watu hawa wasafi sio tu waende kuhakikisha mifumo na Taasisi zetu zinafanya kazi kwa uadilifu ili kutoa haki na hukumu kwa kila anayestahili bali wakajenge pia utamaduni wa watu wasafi tu kushika mamlaka. Imeandikwa katika vitabu vya dini watu wenye haki wakishika mamlaka Wananchi hufurahi na kunufaika.

Katika mazingira ya leo na nikizungumzia namna ya kuenenda katika siasa safi na uongozi bora, ni dhambi kwa mtu wa CCM kufanya hila ila kudhoofisha vyama vyenye mawazo mbadala na vivyo hivyo ni dhambi kubwa kwa vyama vyenye mawazo mbadala kutumia hila kuhujumu utekelezaji wa mawazo ya yule aliye madarakani.

Fitina na hujuma haziwezi kutujengea misingi ya demokrasia ambapo washiriki wa demokrasia wakiwemo wanasiasa na wengi wengineo, wanaheshimia, wanapendana wana aminiana na wana uelewa mmoja kuhusu nini watanzania wanataka kama nchi na Taifa. Hivi karibuni tumeona mtindo kwa kila chama kuwa na vikundi vyake vya usalama, hili si jambo la kufurahia hata kidogo, hii si dalili njema kwa ustawi wa demokrasia katika Taifa letu. Ukiona baadhi ya vyama vinapoteza imani na polisi wakati vyama vingine vinaonekana kuwa na amani na polisi, ujue kuna tatizo hapo, kama viongozi tunapaswa kujadili hilo na kulipatia ufumbuzi ili lisikue kuwa sehemu ya uvunjifu wa amani.

Mchakato wa Ukawa na sintofahamu

Nimefuatilia kwa karibu sana mchakato wa UKAWA kupata mgombea Urais pamoja na namna watajiratibu kwa nafasi za ubunge, udiwani na baada ya uchaguzi. Nikiri kwamba njia waliyoichagua UKAWA si rahisi hata kidogo, ni njia ngumu, ina Changamoto nyingi na ina makwazo mengi. Pasina hekima za hali ya juu, busara ya tofauti, pasina kuwatia moyo na kuwapa maneno ya kuwajenga ili wajiamini kwamba njia wanayoipitia ni sehemu muhimu ya “kuzaliwa upya” kidemokrasia, itakuwa vigumu kwao na kwa akili za kibinadamu kufanikiwa.

Nimeongea na mzee wangu na rafiki yangu Profesa Baregu kwamba katika hali waliyonayo akumbuke hali ngumu ilivyokuwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK). Kuna wakati lazima ukubali kupoteza ili kupata, na nilazima wadau wa UKAWA wakafahamu kwamba kupata haimaanishi kupata kila kitu. Lakini moyo wa upole na uelewa unahusika sana, mkumbuke kuna baadhi ya vyama kwa fanikio lolote la UKAWA katika hatua hii ya awali inaweza kuonekana kama jaribio la kujitoa mhanga ambalo mara nyingi matokeo yake huwa kifo. Hivyo wale wakubwa wawafikirie wadogo, sio tu kwa nafasi zinazohesabika kwa idadi ya wabunge na madiwani bali katika kujitoa kwao na kukubali kwao kuwa sifuri kwa wakati ili nyote muweze kuwa nambari inayohesabika na yenye maana “significant”.

Katika mchakato wa UKAWA sasa ni lazima mjue mkubwa anapaswa kumhakikishia mdogo kuwa kinachoendelea ni mapenzi ya dhati na mdogo alione hilo. Na kama miongoni mwa UKAWA kuna wanaolingana kimo kwa sehemu ni vema wakaa pembeni ili wengine wakasaidia kutoa uongozi, kwa kufanya hivyo imani itaongezeka. Mlipofika ni imani tu itawavusha, kazi ni kuondoa kila alama ya kuteteresha imani. Muungano huu una wakubwa na wadogo na wadogo sana, alama moja ya kujenga imani ni kuhakikisha wakubwa hawahodhi madaraka makubwa kabisa. Unajua kwanini Tume ya Katiba ilipendekeza Serikali 3 ni kwasababu ilibidi na mdogo aonekane, na mkubwa akubali hilo na kuwekwa kwenye nafasi sawa na mdogo, ni imani tu hata kama mkubwa ataendelea kuwa mkubwa na mdogo vivyo hivyo.

Kubwa kabisa, mkishindwa kuafikiana na kutoka kama washindi, mtakuwa mmewakwaza watanzania, mtakuwa mmerudisha nyuma zoezi adhimu la ujenzi endelevu wa demokrasia yetu. Mimi nitapata wakati mgumu kuwaelewa, mlishindwaje kujikana nafsi zenu ili UKAWA ndio utamalaki?

Hivi mnajua kwamba kama mngechukua msimamo mkubwa kabisa ambao nao usingekuwa na shida, ni mgumu lakini ungetuzalia taswira mpya ya demokrasia katika Taifa letu. Msimamo mkali kabisa “extreme position” ingekuwa vyama kukubali kufa na kubaki na kimoja lakini roho zote za vyama zikahamishwa katika kile chama kimoja, kisha lengo likawa kuutafuta ushindi na hatimaye kushika dola. Utaratibu wa nani atapata nini huo ni wa badaaye, kwa kiingereza ningesema “the details will be sorted later”. UKAWA bado kwa utaratibu wenu mnaweza kulifanikisha hili kuelekea uchaguzi mkuu.

Haya ni mapito, mkiwa pamoja na mkiondoa ubinafsi mtapita na ushindi utakuwa kwa watanzania, mkishindwa mtakuwa mmeimarisha zoezi la kuidhoofisha CCM na mtapoteza imani ya Wananchi. Na pindi Wananchi wakipoteza imani na upinzani, wanachama wabaya wa CCM wale ambao wanaamini CCM imara ni kubomoka kwa upinzani watashika hatamu, na hao kamwe hawanii kwa dhati kubadilisha maisha ya watanzania. Wana CCM wazuri wanapenda upinzani usio dhaifu na hawafanyi siasa za chuki na fitina ili kupata ushindi.

Ujumbe mdogo kwa Dkt. Magufuli

Hongera sana kwa ushindi ndani ya CCM uliokupa dhamana ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu. Nimesema hapo awali, rai yangu kwako, ukawe ile nguvu ya kutuunganisha katika chama. Ukumbuke kuna mawazo ya Wananchi na baadhi ya wana CCM hayakubaliki CCM, lakini mawazo hayo yanakubalika hata na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), maadamu unatafuta kura, zingatia mawazo yao.

Nimekusikia pia ukijibu hoja ya mchakato wa CCM na nafasi yako, nimekuelewa sana, Bob Marley aliwahi kuimba wimbo akisema tujikwamue kutoka utumwa wa kifikra “emancipate yourself from mental slavery...”, mimi nakuombea kwa Mungu utusaidie katika CCM kujikwamua kutoka siasa zisizofaa, kuondoa kiburi, kuondoa maslahi binafsi yayozidi sana maslahi ya umma wa watanzania. Wengi wameanza kusema oo sijui ushindi wako ni wa maridhiano, vijana wanasema wapotezee, waoneshe kwamba wewe ni wa tofauti, kwa mtindo huo nakuona ukiendelea kuandika historia yako katika ukuta wa dhahabu.

*Mwandishi ni Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi anayeamini katika misingi ya kuanzishwa kwa chama cha Mapinduzi na Ahadi za Mwanachama wa CCM.

Saturday, July 11, 2015

NILIYASEMA HAYA KWAMBA TUWE WAANGALIFU NA SASA YAMETIMIA. CCM HATUPASWI KUSHEREHEKEA USHINDI BADO KUNA KAZI KUBWA


WATANZANIA CHUNGENI NCHI YENU, HIYO NDIO MALI YENU NA URITHI WA WATOTO WENU


KUJIANDIKISHA NA KUSHIRIKI KATIKA UCHAGUZI MKUU NI HATUA YA KWANZA SASA

Nimefuatilia kwa karibu sana mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, nimejifunza mengi na ninaendelea kujifunza sana. Nimefuatilia mchakato wa ndani ya vyama vya siasa kupitisha wagombea wa nafasi ya Urais na hasa hasa mchakato wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nimetupia jicho pia, mashirikiano ya vyama vyenye mawazo mbadala chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), huko nako nimejifunza.

Nikiri kwamba katika miaka 10 iliyopita ushiriki wangu katika siasa za maendeleo umenifunza mengi, nimeona namna ambavyo siasa za asasi za kiraia zilivyo na zinavyogubikwa ila ile dhana na uhalisia wa kutafuta madaraka au “struggle for power”. Kimsingi asasi hizi za kiraia ndio hasa sauti za wananchi, maana hata shule tunasoma kwamba asasi za kiraia ndio uwanja wa wananchi kudai na kutetea haki zao dhidi ya Dola (state), sekta binafsi (Private sector) na nguvu ya soko (Market forces). Nikang’amua nako kuna siasa kweli kweli, lakini kazi lazima iende, lazima tuendelee kusimamia maslahi ya raia na wananchi wa Taifa letu.

Rai yangu kwa asasi za kiraia ni kuweka mbele maslahi ya Wananchi na kujitahidi kuweka pembeni maslahi binafsi, tukumbuke asasi za kiraia imara ndio sauti ya Wananchi kwa serikali yao dhidi ya nguvu za soko pamoja na sekta binafsi.

Baada ya kushiriki mchakato wa Katiba, huko nako nikaona siasa za kutosha, huko ndio nikajua siasa za vyama vya siasa ambazo kimsingi zinalenga kulinda maslahi yake kwanza kuliko hata yale ya Taifa. Na ninapozungumzia vyama nazungumzia vyama vyote, kwa maana ya chama kilichopo madarakani na vyama vyenye mawazo mbadala. Hapo niliona namna gani ukijaribu kugusa maslahi ya watu na vyama vyama siasa, hasa yale ambayo yamejikita katika kujenga himaya za kisiasa, kukamata nafasi za madaraka na kuzishikilia ikiwezekana wakati wowote, utapata upinzani mkubwa. Ninaposema kugusa maslahi ya watu na ya vyama vya siasa namaanisha maslahi ambayo mara nyingi hujikita katika kunufaisha wachache katika gharama ya wengi.

Kwenye sekta binafsi ndio kuna matatizo makubwa, huko lengo kuu ni kuongeza faida kwa namna yoyote. Wengi wao wanalo pia lengo la kujitahidi kukwepa kodi ili mapato ambayo wanayakusanya kutoka kwa umma wa watanzania yasiguswe kwa namna yoyote. Huu unaitwa udhalimu, uporaji wa rasilimali za watanzania na wizi ambao hautendwi katika nchi ya mbali bali hapa hapa nchini kwetu. Ukitizama vizuri utagundua hawa jamaa ndio ambao wameshikilia hata uwezo wa serikali kufanya maamuzi lakini hawa huwa hawaonekani mbele ya hadhira, mara nyingi hukaa nyuma ya pazia na mara chache hujitokeza kutoa mtisho mkuu na kutokomea nyuma ya pazia baada ya kutufanya tuweweseke sisi raia na serikali yetu.

Sekta binafsi na wadau wake ni watu wenye nguvu kweli na ukitaka kujua nguvu yao jaribu kurejea mifano michache tu kama vile siku wenye mabasi ya abiria wakigomea nauli au kiwango cha mwendo kasi, itabidi waziri afanye mazungumzo mara moja. Licha ya kwamba tuna reli ya kati na ile ya TAZARA yenye uwezo mkubwa wa kubeba shehena za mizigo lakini siku wamiliki wa malori TATOA wakigoma kusogeza tu malori yao bandarini kwa kigezo kwamba uendeshaji wa mizani katika barabara zetu una tatizo vivyo hivyo serikali itakimbia mara moja na kutatua suala lao.

Hawa watu wa sekta binafsi na Taasisi zao huwa hawana mzaha na kazi zao, kama nilivyosema ni kutengeneza faida katika gharama yoyote. Katika nchi nyingine na wala haziko mbali nasi, sekta binafsi ndio hufadhili hata vita zinazoendelea ili mkiwa mnapigana wao wanachukua rasilimali zenu.

Tunamshukuru Mungu hapa kwetu tuko sawa, lakini haimaanishi tukiwa wazembe tutaendelea kuwa sawa, na uzembe namaanisha pale Wananchi tutakapoiacha nchi yetu mikononi mwa viongozi na watumishi wa umma pekee. Ni lazima tuwe mstari wa mbele kujua kila linaloendelea kwasababu faida ya usimamizi mzuri wa siasa zetu ambazo ndio huamua mustakabali wa matumizi ya rasilimali zetu huwa kwetu sote. Aidha, usimamizi mbovu wa siasa zetu na kwa uzembe tu kushindwa kushiriki katika shughuli za kiraia kama raia hutuzalishia viongozi wabovu, wabinafsi, wabadhirifu na wenye kujipenda wenyewe na si maendeleo na ustawi wa watu wetu.

Hapa nyumbani tumeshaanza kuona viashiria, unakumbuka Wananchi mlisema mikataba ya madini lazima iwe wazi kwa kila raia anayetaka kujua yaliyomo kwenye mikataba hiyo. Rasimu ya Warioba ilisema Bunge liwe linaridhia mikataba ya rasilimali kabla haijaanza kutumika katika Jamhuri yetu. Bunge Maalum lilifuta masharti hayo muhimu yaliyokuwa na lengo la kuweka uwazi katika matumizi ya rasilimali zetu na hatimaye Katiba Inayopendekezwa haina masharti haya muhimu yaliyotolewa na Wananchi.

Unakumbuka pia kipindi baada ya Bunge Maalum, katika vikao vya Bunge la Muungano ilizuka hoja ya kudai mikataba ya gesi na mafuta iletwe, lakini serikali ikakataa. Unakumbuka Kamati ya Mahesabu ya mashirika ya umma (PAC) nayo ikaomba kupewa mikataba, ikanyimwa, hata wakaenda mbali kwa hasira kuielekeza polisi kuwakamata watendaji wakuu wa Shirika la Taifa la Uendelezaji wa Sekta ya Mafuta (TPDC). Mwisho wa siku Bunge likashindwa, na mikataba bado ni siri, na utagundua hata wale walioshabikia kufutwa kwa masharti ya Rasimu ya Warioba ya uwazi wa mikataba baadaye walianza kujirudi kwamba lazima mikataba iwe wazi, kwa kiingereza tabia hii ningeita “too good too late” kwa maana ya ukifanya mazuri mwishoni ni kazibure.

Tafsiri ya kuwa raia makini na majukumu yako kwa Taifa

Hapa nataka nianze na imani zetu, nianze na uislamu, katika uislamu kuna mstari mwembamba sana kati ya imani ya muumin na masuala ya kiraia yakiwemo yahusuyo utawala wa nchi. Katika uislam, kimsingi imani inapasa kutoa hamasa kwa namna ulimwengu wa siasa unaenenda. Tafsiri yangu ni kwamba katika mazingira ya kawaida na hasa katika nchi kama yetu ya Tanzania ambapo tuna mfumo unaotenganisha utendaji wa shughuli za dini/imani na mamlaka ya nchi, jukumu pekee nilionalo kwa watanzania waumin wa kiislam ni kuhakikisha wanafuata maagizo ya vitabu vya dini. Muumin mzuri wa dini ya kiislamu ameelekezwa kwamba imani (ya uislamu) lazima itoe hamasa ya namna mamlaka ya nchi inaenenda. Ili utoe hamasa ni lazima ushiriki katika shughuli za kiraia na za kisiasa ili matendo yako mema kama muumin tukayaone katika utendaji wa mamlaka za nchi.

Tafsiri inaendelea, hivyo kama wewe ni muumin wa dini ya kiislamu hufuatilii namna nchi yako inaongozwa kwa kigezo kwamba unawaachia viongozi pekee na huhudhurii vikao vya maendeleo katika eneo lako na hujajiandikisha na hutakwenda kusikiliza wagombea wakijinadi katika kampeni na hutapiga kura katika siku ya uchaguzi ujue unakwenda kinyume na Quran Tukufu na katika siku ya kiyama jehanum inakusubiri, yaani ule moto wa milele ni halali yako.

Kwa waumini wa dini ya kikristo, wao Biblia Takatifu imeeleza kabisa kwamba katika Warumi 13:1-7 “1 Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. 2 Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe, 3 Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu; 4 maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kutoa adhabu. Yeye ni mtumishi wa Mungu na huitekeleza ghadhabu ya Mungu kwao watendao maovu. 5 Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo. 6 Kwa sababu hiyohiyo ninyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao. 7 Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.”

Nikitafsiri maandiko hayo, ni dhahiri kwamba kwa waumini wa dini ya kikristo Mamlaka ya nchi imeletwa na Mungu, na kama mjuavyo yote yaletwayo na Mungu huwa ni maelekezo na amri. Kama Serikali, Bunge na Mahakama zimeletwa na Mungu, je sisi waumini tunapaswa kujiepusha nazo? Je kujiepusha na mambo yaliyoletwa na Mungu katika imani ya kikristo tafsiri yake ni nini? Na ninapozungumzia kujiepusha kimsingi nazungumzia kwamba mamlaka ya nchi hutolewa na Wananchi kikatiba kwa kupiga kura na kushiriki katika shughuli za umma. Kwahiyo mkristo ambaye hafuatilii namna nchi yako inaongozwa kwa kigezo kwamba unawaachia viongozi pekee na huhudhurii vikao vya maendeleo katika eneo lako eti kisa umeenda katika “fellowship” kanisani wakati wote na hujajiandikisha na hutakwenda kusikiliza wagombea wakijinadi katika kampeni na hutapiga kura katika siku ya uchaguzi ujue unakwenda kinyume na Maelekezo ya Mungu wa Mbinguni na katika siku ya hukumu utaelekezwa katika ziwa la moto wa milele, na milele ukisaga meno.