Sunday, July 26, 2015

TUJIKUMBUSHE: KATIBA BORA AFRIKA NI ILE ITOKANAYO NA MAONI YA WANANCHI




Nianze kwa kuzurula

Unajua furaha ya ujana ni kuweza kufanya makosa, kueleweka, kusamehewa, na kupuuzwa kwa kigezo kwamba ni ujana unasumbua au unajua damu bado inachemka na sababu kadhaa wa kadhaa zinazofanana nazo. Sidhani kama vijana wenzangu wameling’amua hili, kwamba ni wakati wa ujana mtu huruhusiwa kwa kiasi fulani kukosea kama sehemu ya kujifunza. Ni kipindi hiki kijana anaweza akasema mambo mazito na yakachukuliwa kawaida kwa kile kile kigezo kwamba ujana huo, akikua ataacha. Namshukuru Mungu kwamba nimo kwenye rika la kujifunza na hasa na niseme kwa kiingereza “interest” yangu imekuwa kujifunza kuhusu nchi yetu, ikoje, inaongozwaje, changamoto zake, magumu ambayo viongozi wetu au kama wanavyojulikana wakubwa, wanayokabiliana nayo siku hadi siku katika uongozi na utumishi.

Nimeanza hivyo makusudi kwasababu naanza kuona kama katika Makala hii nitaongea mambo ambayo niombe samahani mapema na nitashukuru kama nitachukuliwa kama ni ujana tu unanisumbua na ni damu inachemka. Siku moja Mama Mwatum Jasmine Malale Mjumbe wa Tume ya Katiba aliniambia kitu ambacho mpaka leo huwa nikipata wasaa nawasimulia na vijana wenzangu. Alisema kuna tofauti kati ya kuwa na akili au uwezo wa kufanya mambo labda kwa haraka, kwa ustadi na kwa umahiri upande mmoja na kuwa na hekma au hekima, uwezo wa kuyatizama masuala kwa undani, kwa pande zote na hasa hasa ukizingatia uzoefu unaojengwa na wakati. Akaniambia unaweza kuwa na akili na ukakosa faida ya uzoefu unaokuja kwa wingi wa wakati. Mtu mwenye akili ni mwepesi kuhadaika lakini mtu asiye na werevu wa akili ya darasani au hii akili ya kileo ya kukurupuka ni vigumu sana na nikitumia lugha ya vijana “kuuingia mkenge” kwasababu ameshaona “mikenge mingi” katika maisha yake na hivyo kuikwepa si bahati ni hekma (hapa msisitizo ni wangu).

Sasa nauanza ujana, juzi juzi hapa nalipata kusikia kwamba Katiba Inayopendekezwa ni bora kuliko Katiba zote Afrika, nikasema hilo nalo neno na sikupenda linipite pasina kusema neno. Unaposema Katiba Bora unamaanisha nini? Na je umepima kwa vigezo vipi? Au tunarudi kule kule kwenye simulizi pasina ushahidi? Najua baadhi yetu sisi vijana wa leo tungepata fursa ya kupata kile kifaa cha kurudisha wakati nyuma labda miaka 30, huenda tungewapuuza wananchi katika mambo mengi sana. Kwa namna ambavyo naona baadhi yetu kipindi hicho tungeamua mambo sisi wenyewe, watu tungesema hawa wanapaswa kutengenezewa vitu na kupelekewa na wala hawana haja ya kuulizwa maana tungeamini kabisa wao (wananchi) ni wa kutawaliwa tu.

Yaani nawaona baadhi yetu tukitembea huku na huko tukijua sisi ndio tujuao kuliko wananchi na kwamba hata inapokuja masuala makubwa yawahusuyo wao wananchi basi, tutaambiana kama wakati mwingine ni lazima watu watuelewe, uongozi sio jambo dogo. Naona kama tumekaa kwenye viti katika mduara mdogo kwenye bustani nzuri na tunafurahi kwa vinywaji na tukipata mchapalo taratiibu na tukisema unajua kamaradi, uongozi hapa sio kama kilimo cha nyanya, uongozi sio kama ufundi gereji, uongozi ni kazi, na michapalo hiyo inakuwa ndio wigo wa kutuweka mbali na watu wetu. Hapo ni Miaka ya 80 tukiwa tumerudisha wakati kwa kutumia kile kifaa maalum “time machine”.

Lakini muda unafika na tunarudi tena katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa dijitali, karibu kila mtu anajua kitokeacho duniani katika viganja vya mikono yake. Ulimwengu ambao tofauti na ule wa miaka ya 80, siku hizi ukisema uongo watu wanabaki na sauti yako au video yako ukisema uongo, ukiwa holela hata mambo ya kusitiriwa yanawekwa bayana Astakafilulah ni sheedah! Naona ulimwengu wa leo watu hasa vijana hawapokei tu eti tu kwasababu amesema mkubwa, hapa, wanapenda kuhoji kwanza, wanapenda waelezwe misingi kabla ya kuunga mkono hoja, na kadhalika.

Katiba Bora ikoje?

Katiba huwa ndio sheria mama, huwa ndio msingi mkuu wa sheria katika nchi au taasisi. Katiba kwa kawaida na kidesturi hutungwa na wenye kuitumia, bado haijawa mifano mizuri kwa baadhi ya katiba kutungwa na watu wachache na zikawa nzuri na kutumiwa na watu wengi kwa muda mrefu. Katiba Bora siku hizi ni ile ambayo imeandikwa kwa kuzingatia uwakilishi mpana, na tukumbuke dhana ya uwakilishi mpana si nyepesi, na tunaposema uwakilishi mpana tunakwenda mbali zaidi kusema ni kwa kiasi gani kila mtu anayeshiriki, mchango wake unaheshimiwa na sio ule mchezo wa hadaa wa wengi wape wachache wasikilizwe, la hasha.

Ushiriki huanzia kwenye sheria inayo ongoza mchakato, kisha katika ushiriki wa watu, wanapotoa maoni na hapa nyumbani walipokaa kwenye mabaraza na hatimaye walipokaa kwenye Bunge Maalum. Hivi nikuulize baba, na naomba unijibu kweli na kweli tupu ile ya kutoka ndani ya moyo wako, hivi wananchi tuliwaacha huru wakati wa kutoa maoni?

Hebu ngoja nikusimulie kitu kidogo, si unajua karibu kila mtu ana kadi ya chama chake? Sasa kipindi kile kule Tume wako waliokuwa wanajulikana itikadi zao na vyama vyao na wapo wale waliokuwa wana vyama lakini kwa asili ya kazi zao, utambulisho wa vyama vyao ulibaki uhusiano wa ndani kati yao na vyama vyao. Mimi ni mmoja wapo, sasa kuna mzee wangu mmoja, alijaribu sana kunipa kadi ya chama chake, masikini hakujua na mimi ni mwanachama tayari wa chama kingine, nikamkwepa kwepa sana. Lakini leo nikiri kwa mara ya kwanza nilishikwa na uchungu mkubwa sana baada ya kuona namna vyama vilivyokuwa vikilazimisha wananchi kutotoa maoni yao na wakati mwingine wakiwatisha kabisa watoa maoni wale. Nakumbuka nilichukia vyama vya siasa, mpaka ndani ya moyo wangu, nikajiambia inakuwaje vyama kuwa magenge ya maharamia wawatishao watu ili wasiseme Tanzania yao wangependa iweje.

Kuna wakati na ujana wangu ilipasa niwe mkali kila nilipo ona vitisho vinaongezeka, kuna siku ilikuwa katika Baraza la Katiba la Wilaya mojawapo kusini mwa Tanzania, na mtoa maoni alikuwa Mkuu wa Wilaya Mstaafu, huyu alisema wazi kwamba yeye amekataa kupokea maelekezo na atatumia fursa ile kusema yake. Wakati akiongea wengine walijaribu kumzonga zonga, nimeumia sana kwa matukio yale na nimeendelea kuumia. Sasa “baba” unasema kwa mazingira yale ya Bunge Maalum na namna ambavyo vyama viliuteka mchakato bila simile, je hii ni Katiba ya Wananchi na Bora Afrika au ni yale yale ya safari yangu iliyonipeleka miaka ya 80 kipindi mimi na wenzangu tukiwapuuza wananchi. Tena nikumbushe kipindi kile niko miaka ya 80 tulikuwa tukiambiana kabisa wananchi wanapaswa kupigwa propaganda na watakaa sawa. Nauliza, hizo ndio zama za leo?

Kauli ya Mheshimiwa Rais

Mhe. Rais wakati alipokabidhiwa Katiba Inayopendekezwa alisema wakati mwingine mambo mazuri yapasa yasubiri wakati upite, haya, tujadili, unakumbuka msingi wa kwanini alisema yasubiri wakati upite? Alisema baadhi yetu tuna hofu, anhaa, sasa nauliza hivi dawa ya hofu ipo au itakuja kulingana na muda unavyokwenda?

Je Hofu ya Mapendekezo makubwa ya Tume ya Jaji Warioba, ni ya kusubiri miaka 10, 20, 30 ijayo au ni suala la kueleweshana kwa taarifa na maarifa sahihi? Najiuliza. Maana siku hizi kila mtu ameshika lake tu, ooo Rais amesema tusubiri, narudia kusema tuache kumtafsiri Rais ili kukidhi matakwa yetu.

Nimalizie kwa kusema “ee baba” Katiba Inayopendekezwa sio bora hata kidogo na kimsingi inatugawa watanzania, inalinda maslahi ya wachache na imetupilia mbali maoni ambayo wananchi walitaka yawemo.

Rai kwa wagombea Urais na Ubunge

Nendeni mkawaambie wananchi kwamba mtajitahidi kushughulikia suala la Katiba ili tuwe na uelewa wa pamoja, tujenge muafaka wa kitaifa na tufanye maridhiano inapobidi, huo ndio uongozi. Hatuwezi kamwe kuwa na kura ya maoni tukiwa tumegawika kiitikadi na kimsimamo kama vyama vya siasa, mgawanyiko huu utashuka kwa wananchi na hii sio afya kwa Taifa letu.

8 comments: