Siasa safi na si siasa ya uadui
Kila siku huwa ninapozungumzia ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu,
baadhi ya watu huwa hawanielewi ninaposema kwamba CCM imara ni lazima iambatane
na upinzani makini. Na kwamba kwa mazingira yalivyo sasa pasina kuwa na
upinzani makini CCM itayumba, na kuyumba huku sio lazima kuiangushe CCM leo,
lakini sote tunakubali kwamba kuwa katika safari ambamo gari linayumba yumba
huwa si dalili njema. Nadhani wengine wanaendelea kutonielewa, mantiki ya uwepo
wa vyama vya siasa katika ulimwengu wa leo ni kuibua hoja, kujenga hoja, kuleta
mawazo ya kustawisha maisha ya watu na raia wa Taifa letu.
Kama chama kimojawapo kipo madarakani na kinatekeleza mawazo yake ya
kustawisha maisha ya Wananchi, kazi ya vyama ambavyo haviko madarakani ni
kuibua hoja na kujenga hoja ya namna mawazo hayo ama yanafanikiwa au la na
kuhakikisha chochote kinachofanyika kweli kina mguso chanya kwa Wananchi. Aidha
vyama vile ambavyo havipo madarakani vina kazi kubwa pia ya ama kuboresha
mawazo ya chama kilichopo madarakani au wanaweza kuja na mawazo mbadala kabisa,
ilhali lengo likiendelea kuwa kustawisha maisha ya watu na raia wa Taifa letu.
Sijui niseme hivi karibuni au tangu kitambo, kumejengeka dhana mbaya
kwamba mkiwa katika vyama tofauti basi ninyi ni mahasimu, ninyi ni maadui na
wengine huenda mbali na kujinasib wao ni wa utawala wa nuru na wengine ni wa
utawala wa giza. Mimi nakubali kabisa vyama kama Taasisi ni watu na watu
hukosea na tukubaliane kwamba watu wanapokosea wanapaswa kuwajibika kwa mujibu
wa taratibu tulizojiwekea, Katiba na
sheria zetu ikiwa ni mojawapo. Kwahiyo watu wakikosea, wawajibishwe, hata kama
watu hao wanatoka chama chako, na si ustaarabu iwapo unashabikia watu
kuwajibika kutoka vyama vingine wakati katika chama chako kuna matatizo.
Unapokuwa sio msafi unapoteza mamlaka ya kimaadili “moral authority” ya
kukemea wengine wasio wasafi. Hata katika vitabu vya dini imeandikwa “ufalme
mmoja hauwezi kuinuka juu ya ufalme uleule bali ufalme mwingine”, tafsiri yangu
ya ufalme hapa yaweza kuwa watu wasio wasafi hawawezi kamwe kuwawajibisha watu
wachafu na halkadharika watu safi hawana sababu ya kuwawajibisha watu walio
safi, hiyo ni asili. Tunataka watu wasafi zaidi kama mtu mmoja mmoja katika
mifumo yetu na mamlaka zetu za nchi ili watu hawa wasafi sio tu waende
kuhakikisha mifumo na Taasisi zetu zinafanya kazi kwa uadilifu ili kutoa haki
na hukumu kwa kila anayestahili bali wakajenge pia utamaduni wa watu wasafi tu
kushika mamlaka. Imeandikwa katika vitabu vya dini watu wenye haki wakishika
mamlaka Wananchi hufurahi na kunufaika.
Katika mazingira ya leo na nikizungumzia namna ya kuenenda katika siasa
safi na uongozi bora, ni dhambi kwa mtu wa CCM kufanya hila ila kudhoofisha
vyama vyenye mawazo mbadala na vivyo hivyo ni dhambi kubwa kwa vyama vyenye
mawazo mbadala kutumia hila kuhujumu utekelezaji wa mawazo ya yule aliye
madarakani.
Fitina na hujuma haziwezi kutujengea misingi ya demokrasia ambapo
washiriki wa demokrasia wakiwemo wanasiasa na wengi wengineo, wanaheshimia,
wanapendana wana aminiana na wana uelewa mmoja kuhusu nini watanzania wanataka
kama nchi na Taifa. Hivi karibuni tumeona mtindo kwa kila chama kuwa na vikundi
vyake vya usalama, hili si jambo la kufurahia hata kidogo, hii si dalili njema
kwa ustawi wa demokrasia katika Taifa letu. Ukiona baadhi ya vyama vinapoteza
imani na polisi wakati vyama vingine vinaonekana kuwa na amani na polisi, ujue
kuna tatizo hapo, kama viongozi tunapaswa kujadili hilo na kulipatia ufumbuzi
ili lisikue kuwa sehemu ya uvunjifu wa amani.
Mchakato wa Ukawa na sintofahamu
Nimefuatilia kwa karibu sana mchakato wa UKAWA kupata mgombea Urais
pamoja na namna watajiratibu kwa nafasi za ubunge, udiwani na baada ya uchaguzi.
Nikiri kwamba njia waliyoichagua UKAWA si rahisi hata kidogo, ni njia ngumu,
ina Changamoto nyingi na ina makwazo mengi. Pasina hekima za hali ya juu,
busara ya tofauti, pasina kuwatia moyo na kuwapa maneno ya kuwajenga ili
wajiamini kwamba njia wanayoipitia ni sehemu muhimu ya “kuzaliwa upya”
kidemokrasia, itakuwa vigumu kwao na kwa akili za kibinadamu kufanikiwa.
Nimeongea na mzee wangu na rafiki yangu Profesa Baregu kwamba katika
hali waliyonayo akumbuke hali ngumu ilivyokuwa katika Tume ya Mabadiliko ya
Katiba (TMK). Kuna wakati lazima ukubali kupoteza ili kupata, na nilazima wadau
wa UKAWA wakafahamu kwamba kupata haimaanishi kupata kila kitu. Lakini moyo wa
upole na uelewa unahusika sana, mkumbuke kuna baadhi ya vyama kwa fanikio
lolote la UKAWA katika hatua hii ya awali inaweza kuonekana kama jaribio la kujitoa
mhanga ambalo mara nyingi matokeo yake huwa kifo. Hivyo wale wakubwa
wawafikirie wadogo, sio tu kwa nafasi zinazohesabika kwa idadi ya wabunge na
madiwani bali katika kujitoa kwao na kukubali kwao kuwa sifuri kwa wakati ili
nyote muweze kuwa nambari inayohesabika na yenye maana “significant”.
Katika mchakato wa UKAWA sasa ni lazima mjue mkubwa anapaswa
kumhakikishia mdogo kuwa kinachoendelea ni mapenzi ya dhati na mdogo alione
hilo. Na kama miongoni mwa UKAWA kuna wanaolingana kimo kwa sehemu ni vema
wakaa pembeni ili wengine wakasaidia kutoa uongozi, kwa kufanya hivyo imani
itaongezeka. Mlipofika ni imani tu itawavusha, kazi ni kuondoa kila alama ya
kuteteresha imani. Muungano huu una wakubwa na wadogo na wadogo sana, alama
moja ya kujenga imani ni kuhakikisha wakubwa hawahodhi madaraka makubwa kabisa.
Unajua kwanini Tume ya Katiba ilipendekeza Serikali 3 ni kwasababu ilibidi na
mdogo aonekane, na mkubwa akubali hilo na kuwekwa kwenye nafasi sawa na mdogo,
ni imani tu hata kama mkubwa ataendelea kuwa mkubwa na mdogo vivyo hivyo.
Kubwa kabisa, mkishindwa kuafikiana na kutoka kama washindi, mtakuwa
mmewakwaza watanzania, mtakuwa mmerudisha nyuma zoezi adhimu la ujenzi endelevu
wa demokrasia yetu. Mimi nitapata wakati mgumu kuwaelewa, mlishindwaje kujikana
nafsi zenu ili UKAWA ndio utamalaki?
Hivi mnajua kwamba kama mngechukua msimamo mkubwa kabisa ambao nao
usingekuwa na shida, ni mgumu lakini ungetuzalia taswira mpya ya demokrasia katika
Taifa letu. Msimamo mkali kabisa “extreme position” ingekuwa vyama kukubali
kufa na kubaki na kimoja lakini roho zote za vyama zikahamishwa katika kile
chama kimoja, kisha lengo likawa kuutafuta ushindi na hatimaye kushika dola.
Utaratibu wa nani atapata nini huo ni wa badaaye, kwa kiingereza ningesema “the
details will be sorted later”. UKAWA bado kwa utaratibu wenu mnaweza
kulifanikisha hili kuelekea uchaguzi mkuu.
Haya ni mapito, mkiwa pamoja na mkiondoa ubinafsi mtapita na ushindi
utakuwa kwa watanzania, mkishindwa mtakuwa mmeimarisha zoezi la kuidhoofisha
CCM na mtapoteza imani ya Wananchi. Na pindi Wananchi wakipoteza imani na
upinzani, wanachama wabaya wa CCM wale ambao wanaamini CCM imara ni kubomoka
kwa upinzani watashika hatamu, na hao kamwe hawanii kwa dhati kubadilisha
maisha ya watanzania. Wana CCM wazuri wanapenda upinzani usio dhaifu na
hawafanyi siasa za chuki na fitina ili kupata ushindi.
Ujumbe mdogo kwa Dkt. Magufuli
Hongera sana kwa ushindi ndani ya CCM uliokupa dhamana ya kupeperusha
bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu. Nimesema hapo awali, rai yangu kwako,
ukawe ile nguvu ya kutuunganisha katika chama. Ukumbuke kuna mawazo ya Wananchi
na baadhi ya wana CCM hayakubaliki CCM, lakini mawazo hayo yanakubalika hata na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), maadamu unatafuta kura, zingatia mawazo
yao.
Nimekusikia pia ukijibu hoja ya mchakato wa CCM na nafasi yako,
nimekuelewa sana, Bob Marley aliwahi kuimba wimbo akisema tujikwamue kutoka
utumwa wa kifikra “emancipate yourself from mental slavery...”, mimi nakuombea
kwa Mungu utusaidie katika CCM kujikwamua kutoka siasa zisizofaa, kuondoa
kiburi, kuondoa maslahi binafsi yayozidi sana maslahi ya umma wa watanzania.
Wengi wameanza kusema oo sijui ushindi wako ni wa maridhiano, vijana wanasema
wapotezee, waoneshe kwamba wewe ni wa tofauti, kwa mtindo huo nakuona
ukiendelea kuandika historia yako katika ukuta wa dhahabu.
*Mwandishi ni Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi anayeamini katika
misingi ya kuanzishwa kwa chama cha Mapinduzi na Ahadi za Mwanachama wa CCM.
No comments:
Post a Comment