Saturday, July 11, 2015

WATANZANIA CHUNGENI NCHI YENU, HIYO NDIO MALI YENU NA URITHI WA WATOTO WENU


KUJIANDIKISHA NA KUSHIRIKI KATIKA UCHAGUZI MKUU NI HATUA YA KWANZA SASA

Nimefuatilia kwa karibu sana mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, nimejifunza mengi na ninaendelea kujifunza sana. Nimefuatilia mchakato wa ndani ya vyama vya siasa kupitisha wagombea wa nafasi ya Urais na hasa hasa mchakato wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nimetupia jicho pia, mashirikiano ya vyama vyenye mawazo mbadala chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), huko nako nimejifunza.

Nikiri kwamba katika miaka 10 iliyopita ushiriki wangu katika siasa za maendeleo umenifunza mengi, nimeona namna ambavyo siasa za asasi za kiraia zilivyo na zinavyogubikwa ila ile dhana na uhalisia wa kutafuta madaraka au “struggle for power”. Kimsingi asasi hizi za kiraia ndio hasa sauti za wananchi, maana hata shule tunasoma kwamba asasi za kiraia ndio uwanja wa wananchi kudai na kutetea haki zao dhidi ya Dola (state), sekta binafsi (Private sector) na nguvu ya soko (Market forces). Nikang’amua nako kuna siasa kweli kweli, lakini kazi lazima iende, lazima tuendelee kusimamia maslahi ya raia na wananchi wa Taifa letu.

Rai yangu kwa asasi za kiraia ni kuweka mbele maslahi ya Wananchi na kujitahidi kuweka pembeni maslahi binafsi, tukumbuke asasi za kiraia imara ndio sauti ya Wananchi kwa serikali yao dhidi ya nguvu za soko pamoja na sekta binafsi.

Baada ya kushiriki mchakato wa Katiba, huko nako nikaona siasa za kutosha, huko ndio nikajua siasa za vyama vya siasa ambazo kimsingi zinalenga kulinda maslahi yake kwanza kuliko hata yale ya Taifa. Na ninapozungumzia vyama nazungumzia vyama vyote, kwa maana ya chama kilichopo madarakani na vyama vyenye mawazo mbadala. Hapo niliona namna gani ukijaribu kugusa maslahi ya watu na vyama vyama siasa, hasa yale ambayo yamejikita katika kujenga himaya za kisiasa, kukamata nafasi za madaraka na kuzishikilia ikiwezekana wakati wowote, utapata upinzani mkubwa. Ninaposema kugusa maslahi ya watu na ya vyama vya siasa namaanisha maslahi ambayo mara nyingi hujikita katika kunufaisha wachache katika gharama ya wengi.

Kwenye sekta binafsi ndio kuna matatizo makubwa, huko lengo kuu ni kuongeza faida kwa namna yoyote. Wengi wao wanalo pia lengo la kujitahidi kukwepa kodi ili mapato ambayo wanayakusanya kutoka kwa umma wa watanzania yasiguswe kwa namna yoyote. Huu unaitwa udhalimu, uporaji wa rasilimali za watanzania na wizi ambao hautendwi katika nchi ya mbali bali hapa hapa nchini kwetu. Ukitizama vizuri utagundua hawa jamaa ndio ambao wameshikilia hata uwezo wa serikali kufanya maamuzi lakini hawa huwa hawaonekani mbele ya hadhira, mara nyingi hukaa nyuma ya pazia na mara chache hujitokeza kutoa mtisho mkuu na kutokomea nyuma ya pazia baada ya kutufanya tuweweseke sisi raia na serikali yetu.

Sekta binafsi na wadau wake ni watu wenye nguvu kweli na ukitaka kujua nguvu yao jaribu kurejea mifano michache tu kama vile siku wenye mabasi ya abiria wakigomea nauli au kiwango cha mwendo kasi, itabidi waziri afanye mazungumzo mara moja. Licha ya kwamba tuna reli ya kati na ile ya TAZARA yenye uwezo mkubwa wa kubeba shehena za mizigo lakini siku wamiliki wa malori TATOA wakigoma kusogeza tu malori yao bandarini kwa kigezo kwamba uendeshaji wa mizani katika barabara zetu una tatizo vivyo hivyo serikali itakimbia mara moja na kutatua suala lao.

Hawa watu wa sekta binafsi na Taasisi zao huwa hawana mzaha na kazi zao, kama nilivyosema ni kutengeneza faida katika gharama yoyote. Katika nchi nyingine na wala haziko mbali nasi, sekta binafsi ndio hufadhili hata vita zinazoendelea ili mkiwa mnapigana wao wanachukua rasilimali zenu.

Tunamshukuru Mungu hapa kwetu tuko sawa, lakini haimaanishi tukiwa wazembe tutaendelea kuwa sawa, na uzembe namaanisha pale Wananchi tutakapoiacha nchi yetu mikononi mwa viongozi na watumishi wa umma pekee. Ni lazima tuwe mstari wa mbele kujua kila linaloendelea kwasababu faida ya usimamizi mzuri wa siasa zetu ambazo ndio huamua mustakabali wa matumizi ya rasilimali zetu huwa kwetu sote. Aidha, usimamizi mbovu wa siasa zetu na kwa uzembe tu kushindwa kushiriki katika shughuli za kiraia kama raia hutuzalishia viongozi wabovu, wabinafsi, wabadhirifu na wenye kujipenda wenyewe na si maendeleo na ustawi wa watu wetu.

Hapa nyumbani tumeshaanza kuona viashiria, unakumbuka Wananchi mlisema mikataba ya madini lazima iwe wazi kwa kila raia anayetaka kujua yaliyomo kwenye mikataba hiyo. Rasimu ya Warioba ilisema Bunge liwe linaridhia mikataba ya rasilimali kabla haijaanza kutumika katika Jamhuri yetu. Bunge Maalum lilifuta masharti hayo muhimu yaliyokuwa na lengo la kuweka uwazi katika matumizi ya rasilimali zetu na hatimaye Katiba Inayopendekezwa haina masharti haya muhimu yaliyotolewa na Wananchi.

Unakumbuka pia kipindi baada ya Bunge Maalum, katika vikao vya Bunge la Muungano ilizuka hoja ya kudai mikataba ya gesi na mafuta iletwe, lakini serikali ikakataa. Unakumbuka Kamati ya Mahesabu ya mashirika ya umma (PAC) nayo ikaomba kupewa mikataba, ikanyimwa, hata wakaenda mbali kwa hasira kuielekeza polisi kuwakamata watendaji wakuu wa Shirika la Taifa la Uendelezaji wa Sekta ya Mafuta (TPDC). Mwisho wa siku Bunge likashindwa, na mikataba bado ni siri, na utagundua hata wale walioshabikia kufutwa kwa masharti ya Rasimu ya Warioba ya uwazi wa mikataba baadaye walianza kujirudi kwamba lazima mikataba iwe wazi, kwa kiingereza tabia hii ningeita “too good too late” kwa maana ya ukifanya mazuri mwishoni ni kazibure.

Tafsiri ya kuwa raia makini na majukumu yako kwa Taifa

Hapa nataka nianze na imani zetu, nianze na uislamu, katika uislamu kuna mstari mwembamba sana kati ya imani ya muumin na masuala ya kiraia yakiwemo yahusuyo utawala wa nchi. Katika uislam, kimsingi imani inapasa kutoa hamasa kwa namna ulimwengu wa siasa unaenenda. Tafsiri yangu ni kwamba katika mazingira ya kawaida na hasa katika nchi kama yetu ya Tanzania ambapo tuna mfumo unaotenganisha utendaji wa shughuli za dini/imani na mamlaka ya nchi, jukumu pekee nilionalo kwa watanzania waumin wa kiislam ni kuhakikisha wanafuata maagizo ya vitabu vya dini. Muumin mzuri wa dini ya kiislamu ameelekezwa kwamba imani (ya uislamu) lazima itoe hamasa ya namna mamlaka ya nchi inaenenda. Ili utoe hamasa ni lazima ushiriki katika shughuli za kiraia na za kisiasa ili matendo yako mema kama muumin tukayaone katika utendaji wa mamlaka za nchi.

Tafsiri inaendelea, hivyo kama wewe ni muumin wa dini ya kiislamu hufuatilii namna nchi yako inaongozwa kwa kigezo kwamba unawaachia viongozi pekee na huhudhurii vikao vya maendeleo katika eneo lako na hujajiandikisha na hutakwenda kusikiliza wagombea wakijinadi katika kampeni na hutapiga kura katika siku ya uchaguzi ujue unakwenda kinyume na Quran Tukufu na katika siku ya kiyama jehanum inakusubiri, yaani ule moto wa milele ni halali yako.

Kwa waumini wa dini ya kikristo, wao Biblia Takatifu imeeleza kabisa kwamba katika Warumi 13:1-7 “1 Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. 2 Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe, 3 Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu; 4 maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kutoa adhabu. Yeye ni mtumishi wa Mungu na huitekeleza ghadhabu ya Mungu kwao watendao maovu. 5 Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo. 6 Kwa sababu hiyohiyo ninyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao. 7 Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.”

Nikitafsiri maandiko hayo, ni dhahiri kwamba kwa waumini wa dini ya kikristo Mamlaka ya nchi imeletwa na Mungu, na kama mjuavyo yote yaletwayo na Mungu huwa ni maelekezo na amri. Kama Serikali, Bunge na Mahakama zimeletwa na Mungu, je sisi waumini tunapaswa kujiepusha nazo? Je kujiepusha na mambo yaliyoletwa na Mungu katika imani ya kikristo tafsiri yake ni nini? Na ninapozungumzia kujiepusha kimsingi nazungumzia kwamba mamlaka ya nchi hutolewa na Wananchi kikatiba kwa kupiga kura na kushiriki katika shughuli za umma. Kwahiyo mkristo ambaye hafuatilii namna nchi yako inaongozwa kwa kigezo kwamba unawaachia viongozi pekee na huhudhurii vikao vya maendeleo katika eneo lako eti kisa umeenda katika “fellowship” kanisani wakati wote na hujajiandikisha na hutakwenda kusikiliza wagombea wakijinadi katika kampeni na hutapiga kura katika siku ya uchaguzi ujue unakwenda kinyume na Maelekezo ya Mungu wa Mbinguni na katika siku ya hukumu utaelekezwa katika ziwa la moto wa milele, na milele ukisaga meno.

No comments:

Post a Comment