MASLAHI ZAIDI KWA ZANZIBAR NI SUTI KAMILI YA MUUNGANO KWA TANGANYIKA
Ni kweli kwamba Bunge Maalum lilitumia muda mwingi
baada ya kumaliza kanuni kujadili sura ya kwanza na sura ya sita na
kujiridhisha kumaliza suala la muundo wa muungano. Uhalisia ni mbali kabisa na
ukweli huu, ili kuujadili muundo wa muungano kama msingi ilipasa sura ya kwanza, sita na kumi na tano
kusomwa na kujadiliwa kwa pamoja (in tandem). Rai yangu kwa wajumbe wa Bunge
Maalum ni kuhakikisha wanasoma ibara na sura zinazoendana kwa pamoja ili kupata
mantinki na kutoa maboresho stahiki.
Kumekuwapo hoja kwamba ufike wakati suala la muungano
maadamu limeleta ubishani mkubwa na sintofahamu nyingi basi tuliweke kando na tujadili
masuala mengineyo katika rasimu. Hoja hii yaweza kuwa ina nia njema, lakini kwa
hakika haitaarifiwi na uhalisia. Taifa letu ni Muungano wa zilizokuwa nchi
mbili huru kabla ya mwaka 1964. Nchi hizi zilipoungana ziliundwa mamlaka tatu tofauti
kikatiba, kwa maana ya Mamlaka inayohusika na Mambo ya Muungano, Mamlaka
inayohusika na mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na Mamlaka inayohusika na
Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara. Unapo andika Katiba ya Mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano ni lazima uzingatie masuala ambayo kiasili ni ya Muungano
na huwa ni majukumu ya kidola (sovereign functions).
Hoja ninayojaribu kuijenga hapa ni kwamba kwa asili ya
Nchi yetu, suala la muungano huwezi kulikwepa unapozungumzia Katiba Mpya. Kabla
hatujafahamu suala la maji, barabara, kilimo, elimu, afya na masuala mengine ya
kimaendeleo, lazima tumalize suala la Muundo wa Muungano. Ni muundo wa Muungano
ndio utatupatia msingi wa kuenenda (framework) katika masuala ya muungano (majukumu
ya kidola) na masuala yasiyo ya muungano (yote yahusuyo ustawi na maendeleo ya
watu).
Tofauti kubwa kati ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
Bunge Maalum ni kwamba Tume ilipoanza kazi haikuwa na hoja mfukoni bali
ilipaswa kisheria kupokea maoni kutoka kwa wananchi. Bunge Maalum kisheria
linapaswa kupokea hoja kutoka Tume ya Katiba, kisha kuijadili na kuipitisha.
Tume ya Katiba ilipata fursa ya kusikiliza na kupokea maoni ya wananchi katika
hoja mbalimbali na hata ilipofika wakati wa uchambuzi na majadiliano ndani ya
Tume, wajumbe wake walijiwekea utaratibu wa kujadili masuala mengineyo na kisha
kulitizama suala la muungano. Ni wazi kwamba Bunge Maalum halina fursa hiyo,
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inalielekeza Bunge Maalum kupokea hoja kutoka kwa
wananchi kupitia Tume ya Katiba. Sheria inaendelea kulielekeza Bunge Maalum
katika kifungu cha 25(2) kwamba msingi wa majadiliano ya Bunge Maalum ni Rasimu
ambayo imewasilishwa na Tume ya Katiba.
Vyombo vya utendaji
vya Jamhuri ya Muungano
Kamati namba tatu chini ya uenyekiti wa Dkt. Francis
Michael katika Taarifa yake ukurasa wa 13 inatoa pendekezo la kuendelea kuwa na
serikali mbili na shughuli za Mamlaka ya nchi kusimamiwa na kutekelezwa na
vyombo viwili vya utendaji, vyombo viwili vya kutunga sheria na vyombo viwili
vyenye dhamana ya kutoa haki. Pendekezo hili kama lilivyo halina tofauti na
hali ilivyo katika Katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977 toleo la 2005.
Katika pendekezo hili najiuliza kama kamati
imejiridhisha na uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika muundo wa serikali mbili na
kuzingatia changamoto ambazo zimejitokeza kabla ya kupendekeza kuwepo kwa
serikali mbili. Nachelea kusema kwamba kamati imegubikwa na ile dhana ya ukinzani
wa mabadiliko kutokana na mazoea.
Kamati namba tatu inaendelea kujenga hoja katika
ukurasa wa 14 kwa kusema kwa maoni ya wajumbe walio wengi zipo
baadhi ya Changamoto katika mfumo wa Serikali mbili ila kinachohitajika ni
kuzitafutia ufumbuzi, kama kazi hiyo inavyoendelea na sio kuwa na mfumo wa
Shirikisho ambao utakuwa na matatizo makubwa zaidi kuliko tuliyonayo hivi sasa.
Hoja ya uchache wa changamoto haina ukweli na ni upotoshwaji, naomba turejee Taarifa ya utafiti kutoka Tume ya
Katiba katika suala la muungano katika ukurasa wake wa 32-34, yameainishwa
maeneo zaidi ya 40 yenye changamoto katika Muungano. Mambo haya sio mageni yako
na yanajulikana, kujiaminisha kwamba ziko changamoto chache ni ishara ya ama
kutokuelewa uhalisia (ambao uko vitabuni) au ni kuonesha dalili za kutokuwa na
dhamira ya dhati ya kuzifanyia kazi changamoto hizo.
Nieleze kwa ufupi sifa na tabia za miundo mbalimbali
pamoja na namna ya kuenenda na mambo ya muungano na yale yasiyo ya muungano.
Muundo wa serikali moja huwa na sifa
ya kushughulikia mambo yote na tabia mojawapo ni uratibu, usimamizi na ufuatiliaji
wa jumla kutoka Mamlaka Kuu (Supreme Authority). Muundo wa shirikisho huwa na
sifa ya kuwa na mambo machache ya muungano pamoja na ngazi mbili za usimamizi,
uratibu na ufuatiliaji. Ngazi ya kwanza ni serikali ya muungano au shirikisho
kwa mambo machache yenye asili ya majukumu ya kidola na ngazi ya pili ni
serikali za washirika kwa mambo yanayosalia ambao huwa na asili ya kimaendeleo
zaidi.
Bado katika Muundo wa shirikisho unaweza kuwekwa
utaratibu ambao unahakikisha kwamba serikali ya muungano inakuwa na mfumo
mahususi wa kuratibu, kusimamia na kufuatilia ustawi wa masuala ya maendeleo
hata katika ngazi za nchi washirika, mfano ni pendekezo la Rasimu ya Katiba
Mpya juu ya uwepo wa Tume ya Uhusiano na Uratibu ambayo kimsingi inakazi hiyo,
ibara ya 111(1)(b) inasema Tume ya Uhusiano na Uratibu ndio chombo maalum cha
Jamhuri ya Muungano chenye dhamana ya kusimamia, kuratibu na kuhakikisha kwamba
kuna kuwiana kwa sera na sheria za nchi washirika katika mambo yasiyo ya
muungano.
Muundo wa Mkataba huwezesha mahusiano katika maeneo
fulani yanayokubaliwa na nchi zinazoingia katika mkataba. Sifa ya Muungano wa Mkataba
huwa ni lazima uingiwe na mataifa mawili au zaidi yaliyo huru (sovereign
states). Kwa mazingira ya hapa kwetu ni kurudi nyuma ya mwaka 1964. Kwa mtizamo
wangu huko hatuko na binafsi sidhani kama tunapaswa hata kufikiri kwenda huko.
Sifa kubwa mojawapo ya muundo wa serikali mbili ni kuwapo
kwa mambo mengi ya muungano kama ilivyo kwenye Katiba ya 1977 au zaidi. Sifa
nyingine ni nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa na mamlaka na madaraka
ya usimamizi na ufuatiliaji wa ufanisi kwa masuala yasiyo ya muungano upande wa
Zanzibar sambamba na Tanganyika ili awe na uhusiano wa moja kwa moja na raia wa
Tanzania waishio Zanzibar kama ilivyo kwa wale wa Tanganyika. Jambo hili
linabishaniwa vikali na serikali zetu mbili hasa kutoka upande wa Zanzibar, huu
ndio ukarabati usiwezekana.
Mambo ya Muungano
Kamati namba tatu katika taarifa yake ukurasa wa 21
inakubaliana na pendekezo la rasimu kwamba mambo ya muungano yabaki saba,
pendekezo hili linapaswa lisomwe pamoja na pendekezo la serikali mbili katika
ukurasa wa 13 wa taarifa ya kamati. Kwa mtu yeyote anayejua masuala ya muungano
lazima aone tatizo la msingi hapa. Huwezi kutaka serikali mbili halafu
ukapunguza mambo ya muungano. Kitendo cha kupunguza mambo ya muungano
kinakuleta katika muundo wa shirikisho ambao mambo machache yanabaki kwa
serikali ya shirikisho (kama kwenye rasimu) na yanayobaki yanakuwa kwa
washirika.
Unapokuwa na mambo machache ya muungano ndani ya
muundo wa serikali mbili ambapo serikali ya muungano inashughulikia mambo ya
muungano na yasiyo ya muungano ya Tanzania Bara au Tanganyika tafsiri yake ni
kwamba; Jamhuri ya Muungano ndio itakuwa Tanganyika na Zanzibar itakuwa
imepachikwa tu katika muungano huu. Kwa maneno mengine tutakuwa tumeweka
uhusiano kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano katika masuala ya ulinzi na
usalama kwa kiasi kikubwa pekee.
Kwa mapendekezo haya ya kamati namba tatu,
hayatatuacha tena na Nchi moja tena yenye uraia mmoja bali tutakuwa tumeigeuza
Zanzibar kuwa Nchi kamili yenye mamlaka yote isipokuwa ulinzi na usalama ambalo
litakuwa jukumu ya Jamhuri ya Muungano. Tukifika hapo tutakuwa tunafanana
kabisa na uhusiano uliopo kati ya Nchi ya Italia na San Marino au uhusiano wa
Nchi ya Ufaransa na Monako. Narudia huo utakuwa Muungano dhaifu kabisa wa
serikali mbili ambao utaendeleza kero na kwa vile una mianya mingi ya udhaifu
mwishowe utavunja muungano wetu wa kihistoria.
Why are online casinos so popular? - WorkTomakeMoney
ReplyDeleteBest Online 바카라 사이트 Casinos for People หารายได้เสริม with a Gambling Problem. Online casino gambling is one of 메리트카지노 the most popular ways to find a good online casino for your needs.