Ushindi wa Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015 unabaki na utaendelea kubaki kuwa funzo kubwa tofauti na chaguzi
zilizopita. Tanzania ilirejesha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992
baada ya kuufuta miaka ya sitini mwanzoni. Mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa
baada ya serikali kuwahoji wananchi kupitia Tume ya Jaji Nyalali ambaye pamoja
na mambo mengine alihoji wananchi kama Tanzania ilikuwa tayari kuingia katika
siasa za vyama vingi.
Katika hali ambayo ilishangaza wengi miongoni mwa
wasomi na wananchi wa daraja la kati na juu, wananchi kwa zaidi ya asilimia 80
walipendekeza mfumo wa chama kimoja uendelee. Kipindi kile busara na hasa ya
viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwemo Mwalimu Nyerere walionelea ni
vema tukaingia katika mfumo wa vyama vingi. Msingi wa busara na hekima hii
ilitokana na ukweli kwamba katika maoni ya wale wananchi wengi waliopendekeza
mfumo wa vyama vingi uendelee walitoa mapendekezo makubwa ambayo iwapo
yangefanyiwa kazi ipasavyo tusingeweza kuwa tena na mfumo wa chama kimoja.
Wengi ya wana CCM kipindi kile hawakuonesha
kufurahishwa na hatua ile kwasababu tayari kulikuwa na hali ya mazoea, kwa
maneno mengine chama ndio kilikuwa kila kitu. Chama kilikuwa katika kipindi
chote hadi mwaka 1992 kimeshika hatamu au “party supremacy”, kimsingi Serikali
ilipata maelekezo kutoka katika chama na halkadharika Bunge nalo lilipata
msukumo mkubwa kutoka katika chama. Mfano mzuri wa Chama kushika hatamu ulijidhihirisha
wakati wa vuguvugu la G55 yaliyopelekea Bunge kupitisha azimio la kuundwa kwa
serikali ya Tanganyika.
Baafa ya mjadala mzito wa ndani ilikubalika kwamba
sera ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali Mbili na ni uamuzi uliopitishwa na
chama tena kwa turufu ya wanachama wenyewe. Ukiachilia mbali kwamba uamuzi ule
wa Bunge ulighubikwa na mihemko ambayo haikuwa imetaarifiwa sawasawa na
uhalisia. Baada ya vuta-nikuvute uamuzi wa chama ulitamalaki na maisha
yakaendelea.
Mwaka 1995 ndio ilikuwa Uchaguzi Mkuu wa kwanza
katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa na
changamoto na mhemko mkubwa kama huu wa miaka 20 baadaye yaani mwaka 2015.
Ikumbukwe mwaka 1995 Naibu Waziri Mkuu aliondoka CCM akahamia chama cha
upinzani kipindi hicho. Kampeni zilichagizwa na mihemko na mashamsham kama ya
mwaka huu. Kipindi hiki naona watu wanajitambua zaidi kwamba baada ya mkutano
gari ya Mhe. Lowassa iliachwa itembee yenyewe kuelekea nyumbani kwake baada ya
mkutano. Mwaka 1995 gari ya Mhe. Agostino Lyatonga Mrema haikuachwa iwashwe na
kutembea yenyewe, bali ilisukumwa mpaka nyumbani kwake.
Ikumbukwe pia mwaka 1995 mgombea wa CCM, Mzee Mkapa
hakuwa almaarufu katika CCM, na yeye ni kama alifichuliwa kutoka kwenye kona
iliyofichika ya jukwaa kubwa na pana la CCM. Kipindi kile walikuwapo magwiji
katika chama cha mapinduzi ambao kwa rafu nyingi walitamani wapewe dhamana ya
kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa kwanza katika demokrasia ya
vyama vingi. Kwa sauti moja CCM ilikataa hadaa na kwa kiasi msukumo wa Mwalimu
Nyerere.
Mwalimu Nyerere alizunguka huku na huko akimuuza
Mhe. Mkapa kwa watanzania, na nikiri kwamba heshima waliyokuwa nayo kwake
ilikuwa mtaji wa kura zilizompa Mhe. Benjamin Mkapa dhamana ya kuwa Rais wa
Jamhuri yetu. Kwa upande mwingine CCM ambayo tayari Mwalimu alikuwa
ameshaikosoa sana kipindi kirefu cha miaka ya 90 mwanzoni kwa kupungukiwa
uadilifu, lakini kwa tiketi ya ndugu Benjamin Mkapa aliyekuwa tunu ing’aayo na
iliyouzwa na Mwalimu mwenyewe chama kikaponea hapo na kuvuka na ushindi.
Mheshimiwa Mkapa alifanya vizuri sana awamu yake ya
kwanza ambayo iliwezesha ushindi wake katika awamu ya pili kwa maana ya
uchaguzi wa mwaka 2000.
Mwaka 2005, kilichoipa CCM ushindi ilikuwa kampeni
nzuri ya kisayansi na iliyochagizwa na tiketi ya ujana kama sehemu ya
mabadiliko ya kirika ndani ya Chama cha Mapinduzi lakini pia hilo likiwa ni
sehemu ya kiu ya watanzania kipindi kile. Wengi mtakubaliana name kwamba “ari
mpya, kasi mpya na nguvu mpya” yalikuwa maneno yaliyoongeza hamasa ya ushiriki
wa vijana katika kuleta mabadiliko katika CCM. Leo sio kusudio langu kujadili
namna mchakato wa kumpata mgombea wa CCM mwaka 2005 lakini kusudio langu ni
kuonesha katika kila uchaguzi namna ambavyo CCM imeweza kupenya ukiachilia
upinzani mkali kutoka vyama vyenye mawazo mbadala nchini.
Ipo ile desturi ya Chama cha Mapinduzi kwamba
akipewa mtu nafasi ya Madaraka ya Urais kwa awamu ya kwanza (miaka mitano) basi
apewe pia na awamu ya pili ili akamilishe kazi aliyopewa na kutimiza miaka 10.
Kwa sehemu imeonekana kuwa desturi ambayo mpaka mwaka 2010 wananchi wa kawaida
walionesha kukubaliana nayo. Hili linaonekana kupotea kipindi hiki na kadri
muda unavyoendelea hasa ukizingatia wapiga kura wengi kipindi hiki na mwaka
2020 watakuwa ni vijana chini ya miaka 40 ambao wengi wao wamepata elimu ya
msingi mpaka kidato cha nne.
Nikiongea na wengi ya vijana hawa utawasikia
wakisema “tunampa miaka mitano akiboroga toa tupa kule na tunaweka mwingine”.
Huenda ile busara ya kumwachia mtu amalize na kipindi cha pili inaweza
isiendelee katika chaguzi zinazofuata. Hili ni funzo kubwa la kwanza kwa CCM
kwamba ile dhana kwamba wananchi watatoa dhamana kwa awamu ya pili ili kutimiza
miaka 10, kwa kipindi hiki na chaguzi zinazofuata kama hatutafanya kazi ambazo
zitaonekana miongoni mwa watanzania basi tujiandae kisaikolojia kushindwa.
Uchaguzi wa Mwaka 2015, kama ule wa Mwaka 1995
zinashabihiana kwa ukaribu sana. Tofauti na mwaka ule ilikuwa Naibu Waziri Mkuu
Mhe. Mrema aliyehamia upinzani, mwaka 2015 ni Mawaziri Wakuu wawili, Mhe.
Lowassa na Mhe. Sumaye. Mgombea wa CCM ni kama alivyokuwa Mkapa mwaka 1995,
ameonekana si mjuvi wa siasa za ndani za chama hadi kufikia baadhi ya makada wa
CCM kumtamka hadharani kwamba hajui siasa. Ukiacha beza beza za baadhi ya wana
CCM kama ilivyokuwa kwa Mkapa, kipindi hiki aliyekuwa nuru inayong’aa na
inayouzika kwa wapiga kura wa kipindi hiki si mwingine bali ni Dkt. Magufuli.
Kipindi hiki Mwalimu hayuko lakini viongozi wote
wakubwa wastaafu na hasa wale ambao watanzania wanawaona wana akisi haiba ya
Mwalimu Nyerere, nawazungumzia Mzee Joseph Sinde Warioba, Dkt. Salim Ahmed
Salim na hata Mama Maria Nyerere wameonesha kumuunga mkono Dkt. Magufuli moja
kwa moja.
Mchezo ambao CCM ilifanya ikiwemo kuwaruhusu baadhi
ya makada wake waliokuwa wanautafuta urais wa kimungu chini ya Katiba ya mwaka
1977 wakavuruga mchakato wa Katiba Mpya ambao wananchi wenyewe walitoa maoni
yao. Kura za CCM kipindi hiki zimepunguzwa kama sehemu ya adhabu ya kupuuza
maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba. Nakiri kusema asingekuwa Dkt.
Magufuli, CCM ilikuwa haiuziki tena. Nakiri kusema hii ndio tiketi ya mwisho.
Iwapo CCM haitaamka na kuwajibika mchana na usiku hakika 2020 itatukuta nje ya
Bunge na nje ya Ikulu.
Itaendelea