Nianze
kwa kuzurula
Unajua furaha ya
ujana ni kuweza kufanya makosa, kueleweka, kusamehewa, na kupuuzwa kwa kigezo
kwamba ni ujana unasumbua au unajua damu bado inachemka na sababu kadhaa wa
kadhaa zinazofanana nazo. Sidhani kama vijana wenzangu wameling’amua hili,
kwamba ni wakati wa ujana mtu huruhusiwa kwa kiasi fulani kukosea kama sehemu
ya kujifunza. Ni kipindi hiki kijana anaweza akasema mambo mazito na
yakachukuliwa kawaida kwa kile kile kigezo kwamba ujana huo, akikua ataacha.
Namshukuru Mungu kwamba nimo kwenye rika la kujifunza na hasa na niseme kwa
kiingereza “interest” yangu imekuwa kujifunza kuhusu nchi yetu, ikoje,
inaongozwaje, changamoto zake, magumu ambayo viongozi wetu au kama
wanavyojulikana wakubwa, wanayokabiliana nayo siku hadi siku katika uongozi na
utumishi.
Nimeanza hivyo
makusudi kwasababu naanza kuona kama katika Makala hii nitaongea mambo ambayo
niombe samahani mapema na nitashukuru kama nitachukuliwa kama ni ujana tu
unanisumbua na ni damu inachemka. Siku moja Mama Mwatum Jasmine Malale Mjumbe
wa Tume ya Katiba aliniambia kitu ambacho mpaka leo huwa nikipata wasaa
nawasimulia na vijana wenzangu. Alisema kuna tofauti kati ya kuwa na akili au
uwezo wa kufanya mambo labda kwa haraka, kwa ustadi na kwa umahiri upande mmoja
na kuwa na hekma au hekima, uwezo wa kuyatizama masuala kwa undani, kwa pande
zote na hasa hasa ukizingatia uzoefu unaojengwa na wakati. Akaniambia unaweza
kuwa na akili na ukakosa faida ya uzoefu unaokuja kwa wingi wa wakati. Mtu
mwenye akili ni mwepesi kuhadaika lakini mtu asiye na werevu wa akili ya
darasani au hii akili ya kileo ya kukurupuka ni vigumu sana na nikitumia lugha
ya vijana “kuuingia mkenge” kwasababu ameshaona “mikenge mingi” katika maisha
yake na hivyo kuikwepa si bahati ni hekma (hapa msisitizo ni wangu).
Sasa nauanza ujana,
juzi juzi hapa nalipata kusikia kwamba Katiba Inayopendekezwa ni bora kuliko
Katiba zote Afrika, nikasema hilo nalo neno na sikupenda linipite pasina kusema
neno. Unaposema Katiba Bora unamaanisha nini? Na je umepima kwa vigezo vipi? Au
tunarudi kule kule kwenye simulizi pasina ushahidi? Najua baadhi yetu sisi
vijana wa leo tungepata fursa ya kupata kile kifaa cha kurudisha wakati nyuma
labda miaka 30, huenda tungewapuuza wananchi katika mambo mengi sana. Kwa namna
ambavyo naona baadhi yetu kipindi hicho tungeamua mambo sisi wenyewe, watu
tungesema hawa wanapaswa kutengenezewa vitu na kupelekewa na wala hawana haja
ya kuulizwa maana tungeamini kabisa wao (wananchi) ni wa kutawaliwa tu.
Yaani nawaona baadhi
yetu tukitembea huku na huko tukijua sisi ndio tujuao kuliko wananchi na kwamba
hata inapokuja masuala makubwa yawahusuyo wao wananchi basi, tutaambiana kama
wakati mwingine ni lazima watu watuelewe, uongozi sio jambo dogo. Naona kama
tumekaa kwenye viti katika mduara mdogo kwenye bustani nzuri na tunafurahi kwa
vinywaji na tukipata mchapalo taratiibu na tukisema unajua kamaradi, uongozi
hapa sio kama kilimo cha nyanya, uongozi sio kama ufundi gereji, uongozi ni
kazi, na michapalo hiyo inakuwa ndio wigo wa kutuweka mbali na watu wetu. Hapo
ni Miaka ya 80 tukiwa tumerudisha wakati kwa kutumia kile kifaa maalum “time
machine”.
Lakini muda unafika
na tunarudi tena katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa dijitali, karibu kila
mtu anajua kitokeacho duniani katika viganja vya mikono yake. Ulimwengu ambao
tofauti na ule wa miaka ya 80, siku hizi ukisema uongo watu wanabaki na sauti
yako au video yako ukisema uongo, ukiwa holela hata mambo ya kusitiriwa
yanawekwa bayana Astakafilulah ni sheedah! Naona ulimwengu wa leo watu hasa
vijana hawapokei tu eti tu kwasababu amesema mkubwa, hapa, wanapenda kuhoji
kwanza, wanapenda waelezwe misingi kabla ya kuunga mkono hoja, na kadhalika.
Katiba
Bora ikoje?
Katiba huwa ndio sheria
mama, huwa ndio msingi mkuu wa sheria katika nchi au taasisi. Katiba kwa
kawaida na kidesturi hutungwa na wenye kuitumia, bado haijawa mifano mizuri kwa
baadhi ya katiba kutungwa na watu wachache na zikawa nzuri na kutumiwa na watu
wengi kwa muda mrefu. Katiba Bora siku hizi ni ile ambayo imeandikwa kwa
kuzingatia uwakilishi mpana, na tukumbuke dhana ya uwakilishi mpana si nyepesi,
na tunaposema uwakilishi mpana tunakwenda mbali zaidi kusema ni kwa kiasi gani
kila mtu anayeshiriki, mchango wake unaheshimiwa na sio ule mchezo wa hadaa wa
wengi wape wachache wasikilizwe, la hasha.
Ushiriki huanzia
kwenye sheria inayo ongoza mchakato, kisha katika ushiriki wa watu, wanapotoa
maoni na hapa nyumbani walipokaa kwenye mabaraza na hatimaye walipokaa kwenye
Bunge Maalum. Hivi nikuulize baba, na naomba unijibu kweli na kweli tupu ile ya
kutoka ndani ya moyo wako, hivi wananchi tuliwaacha huru wakati wa kutoa maoni?
Hebu ngoja
nikusimulie kitu kidogo, si unajua karibu kila mtu ana kadi ya chama chake?
Sasa kipindi kile kule Tume wako waliokuwa wanajulikana itikadi zao na vyama
vyao na wapo wale waliokuwa wana vyama lakini kwa asili ya kazi zao,
utambulisho wa vyama vyao ulibaki uhusiano wa ndani kati yao na vyama vyao.
Mimi ni mmoja wapo, sasa kuna mzee wangu mmoja, alijaribu sana kunipa kadi ya
chama chake, masikini hakujua na mimi ni mwanachama tayari wa chama kingine,
nikamkwepa kwepa sana. Lakini leo nikiri kwa mara ya kwanza nilishikwa na
uchungu mkubwa sana baada ya kuona namna vyama vilivyokuwa vikilazimisha
wananchi kutotoa maoni yao na wakati mwingine wakiwatisha kabisa watoa maoni
wale. Nakumbuka nilichukia vyama vya siasa, mpaka ndani ya moyo wangu,
nikajiambia inakuwaje vyama kuwa magenge ya maharamia wawatishao watu ili
wasiseme Tanzania yao wangependa iweje.
Kuna wakati na ujana
wangu ilipasa niwe mkali kila nilipo ona vitisho vinaongezeka, kuna siku
ilikuwa katika Baraza la Katiba la Wilaya mojawapo kusini mwa Tanzania, na mtoa
maoni alikuwa Mkuu wa Wilaya Mstaafu, huyu alisema wazi kwamba yeye amekataa
kupokea maelekezo na atatumia fursa ile kusema yake. Wakati akiongea wengine
walijaribu kumzonga zonga, nimeumia sana kwa matukio yale na nimeendelea
kuumia. Sasa “baba” unasema kwa mazingira yale ya Bunge Maalum na namna ambavyo
vyama viliuteka mchakato bila simile, je hii ni Katiba ya Wananchi na Bora
Afrika au ni yale yale ya safari yangu iliyonipeleka miaka ya 80 kipindi mimi
na wenzangu tukiwapuuza wananchi. Tena nikumbushe kipindi kile niko miaka ya 80
tulikuwa tukiambiana kabisa wananchi wanapaswa kupigwa propaganda na watakaa
sawa. Nauliza, hizo ndio zama za leo?
Kauli
ya Mheshimiwa Rais
Mhe. Rais wakati
alipokabidhiwa Katiba Inayopendekezwa alisema wakati mwingine mambo mazuri
yapasa yasubiri wakati upite, haya, tujadili, unakumbuka msingi wa kwanini
alisema yasubiri wakati upite? Alisema baadhi yetu tuna hofu, anhaa, sasa
nauliza hivi dawa ya hofu ipo au itakuja kulingana na muda unavyokwenda?
Je Hofu ya
Mapendekezo makubwa ya Tume ya Jaji Warioba, ni ya kusubiri miaka 10, 20, 30
ijayo au ni suala la kueleweshana kwa taarifa na maarifa sahihi? Najiuliza.
Maana siku hizi kila mtu ameshika lake tu, ooo Rais amesema tusubiri, narudia
kusema tuache kumtafsiri Rais ili kukidhi matakwa yetu.
Nimalizie kwa kusema
“ee baba” Katiba Inayopendekezwa sio bora hata kidogo na kimsingi inatugawa
watanzania, inalinda maslahi ya wachache na imetupilia mbali maoni ambayo
wananchi walitaka yawemo.
Rai
kwa wagombea Urais na Ubunge
Nendeni mkawaambie
wananchi kwamba mtajitahidi kushughulikia suala la Katiba ili tuwe na uelewa wa
pamoja, tujenge muafaka wa kitaifa na tufanye maridhiano inapobidi, huo ndio
uongozi. Hatuwezi kamwe kuwa na kura ya maoni tukiwa tumegawika kiitikadi na
kimsimamo kama vyama vya siasa, mgawanyiko huu utashuka kwa wananchi na hii sio
afya kwa Taifa letu.