Hivi karibuni
nilipata wasaa wa kuonana na watetezi wa haki za binadamu, watetezi hawa
wanawake na wanaume kutoka asasi za kiraia walinialika kujadiliana nao juu ya
mchakato wa Katiba. Katika vikao viwili tulikaa pamoja, sote tulikubaliana kila
mwenye uelewa au msimamo kuhusu Katiba Inayopendekezwa apewe fursa kuusema na
asizongwe. Wote tulikubaliana kwamba utofauti wa mawazo ni afya kwa hakika na
hasa pale wote wenye misimamo wanapojenga hoja zao kwa sababu za msingi na
zenye mashiko.
Nilijielekeza
kuelewa hoja zao, hasa za wale ambao wanasema Katiba Inayopendekezwa imelinda
haki za wanawake, nilisikiliza kwa dhamira ya kuelewa na kujifunza kutoka kwao.
Baada ya mjadala niligundua kwamba wanawake walikuwa na hoja kadhaa ambazo kwa
maelezo yao zilifanikiwa kuingia katika Katiba Inayopendekezwa, na kwa mantiki
hiyo wanawajibika kuipigia chapuo Katiba Inayopendekezwa.
Kabla ya kufafanua
namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imelitizama suala la haki za wanawake ni
vema nikagusia kwa sehemu dhana ya Mahitaji ya Kimkakati ya jinsia au kwa
kiingereza “Strategic Gender Needs”.
Mahitaji
ya Kimkakati ya Jinsia na Katiba
Mahitaji ya
kimkakati ya jinsia au “Strategic Gender Needs” ni yale ambayo wanawake na
wanaume huyahitaji ili kubadilisha nafasi zao katika jamii, mahitaji haya
yanajumuisha mgawanyo wa madaraka kijinsia, mamlaka na udhibiti wa rasilimali,
fursa sawa kwa wanawake na wanaume, haki za kipato sawa kwa kazi sawa kati ya
wanawake na wanaume, Mageuzi ya kikatiba, kisheria na kimfumo ambayo yanatambua
nafasi muhimu ya wanawake pamoja na wanaume kwa usawa katika kuleta maendeleo
ya jamii. Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ndio humlinda mwanamke dhidi ya utegemezi,
umasikini, kunyanyaswa, unyonyaji au “exploitation” na kuwekwa nje ya mfumo wa
kufanya maamuzi.
Mara zote Mahitaji
ya Kimkakati ya Jinsia kwa maana ya “Strategic Gender Needs” ndio huwa ufunguo
kwa Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au kwa kiingereza “Practical Gender Needs”.
Mahitaji ya Kawaida ya Kijinsia au “Practical Gender Needs” hujumuisha yale
mambo ya kawaida na yanayoshikika ambayo mtu wa kawaida huyahitaji wakiwemo
wanawake. Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia yanajumuisha mahitaji ya msingi katika
maisha ya siku hadi siku kama vile upatikanaji wa maji, huduma za afya na
ajira. Kupatikana kwa mahitaji ya kawaida ya jinsia kwa mwanamke huwa hayamwondoi
mwanamke katika nafasi yake ya utegemezi, unyonyaji na kutokuwa maamuzi juu ya
rasilimali zake mwenyewe.
Swali langu muhimu
kwa wanawake wote, dada zangu, shangazi zangu na mama zangu wote wenye mapenzi
mema na kuona utu wa mwanamke unaheshimiwa, haki za wanawake zinatolewa,
zinatunzwa, zinahifadhiwa na kuheshimiwa, Je Katiba Inayopendekezwa na bila
kuweka misimamo ya kisiasa imezingatia Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia au
“Strategic Gender Needs”?
Katiba
Inayopendekezwa inapaswa kupimwa ni kwa kiwango gani imetizama na kujumuisha
Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia ambayo kwayo mahitaji ya kawaida ya jinsia
hupatikana. Tunapoweza kuhakikisha uwepo wa mahitaji ya kimkakati katika
Katiba, huu huwa msingi wa kuona utolewaji haki za wanawake.
Kama Katiba
Inayopendekezwa imejaribu kuweka Mahitaji ya Kawaida ya Jinsia pasina kuweka
misingi kwa mahitaji ya kimkakati ni kazi bure kwasababu haki za wanawake
zitabakia kuwa kiini macho. Kama haki za wanawake hazikubainishwa ipasavyo
katika Katiba Inayopendekezwa bado mwanamke wa Tanzania ataendelea kuwa
tegemezi, fukara na ushiriki wake kwenye nyanja za utoaji maamuzi zitabakia
kutegemea utashi na fadhila kutoka kwa viongozi wa juu.
Tuitazame
Katiba Inayopendekezwa kwa jicho la Rasimu ya Warioba
Rasimu ya Warioba
Katiba Ibara ya 47(1)(b) ilisema “Kila
mwanamke ana haki ya kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili”. Rasimu
ililenga kujenga msingi wa kumpa mwanamke udhibiti wa rasilimali zake na
kumlinda na ukatili ambao huja kama sehemu ya kumpora rasilimali alizo nazo.
Mfano mzuri ni mwanamke wa kijijini na mkulima, anayelima kwa jembe la mkono na
kupata mazao yake, je ni mara ngapi mwanamke huyu huwa na mamlaka juu ya wakati
gani mazao yatauzwa, na yatauzwa kwa bei gani na pesa ikipatikana je mwanamke
huyu huipangia matumizi yake mwenyewe?
Ukienda
kwenye Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 masharti ya 47(1)(b)
kutoka katika Rasimu yamefutwa, huwa najiuliza msingi wa kufuta masharti yale
ya Rasimu ni upi?.
Ukiendelea
kusoma Ibara ya 47(2) ya Rasimu ya Warioba inasema “Mamlaka za nchi zitaweka
utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti
ya Ibara hiiikiwa ni pamoja na kukuza utu, heshima, usalama na fursa za
wanawakewakiwemo wajane”. Ibara hii ilikuwa ina lengo la kutoa maelekezo kwa
mamlaka za nchi kutekeleza masharti yaliyoainishwa katika Ibara hii. Ieleweke
pia masuala ya maendeleo ikiwemo suala la jinsia kwa asili ya Nchi yetu sio
jambo la Muungano.
Kwa
uelewa huu ndio maana Rasimu ya Warioba iliona Katiba itoe maelekezo kwa
Mamlaka za Nchi ambazo ziko tatu ambazo ni (i) Mamlaka ya Mambo ya Muungano
ambayo chombo cha utendaji ni Serikali ya Muungano, (ii) Mamlaka ya Mambo
yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na (iii) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya
Tanzania Bara au Tanganyika. Warioba alijua kwamba kuna masuala ya Haki za
Wanawake ambayo kila Mamlaka ingeweza kuyashughulikia kwa sehemu, nafasi na
mamlaka yake. Huu ulikuwa msingi mkubwa wa kuhakikisha tunalinda Mahitaji ya
Kimkakati ya Jinsia ambayo yangepelekea kutolewa kwa haki za wanawake raia wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanapatikana Tanzania Bara na Zanzibar.
Katiba
Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 57 imeyafuta na hivyo haina masharti ya
Rasimu yaliyomo katika Ibara ya 47(2) ambayo ukiacha kutoa maelekezo ya
utendaji lakini pia kitaalamu ni masharti wezeshi au kwa kiingereza huitwa
“enabling provision”. Najiuliza dhambi ya masharti yale ambayo baada ya
kuwasikiliza Wananchi na hasa wanawake na zaidi wanawake wajane walio ona
ingefaa yawepo kikatiba.
Ili
ujue Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanawake
wanakubwa sehemu ya wanufaikaji wa Katiba Mpya na Bora na inayotokana na maoni
ya Wananchi. Ukisoma Ibara ya 54 inaeleza kuhusu usimamizi wa haki za binadamu
na ukiendelea na kusoma Ibara ya 54(1)(a) inaeleza “Katika kutafsiri masharti
ya Sura hii ya Haki za Binadamu, Mahakama au chombo kingine chochote cha
kufanyauamuzi kitazingatia mambo yafuatayo:- haki ya usawa, utu na uhuru wa mtu
binafsi”. Kwa kiingereza haki ya usawa ndio huitwa “equality principle”, kwamba
tunapozitoa haki, lazima tuangalie je wanawake wapo? Je wanaume wapo?
Na
neno “Utu” ni kuhusu masikini na matajiri wa Taifa letu, tunapogawana keki ya
Taifa je nani waanze kula, matajiri au masikini? Rasimu ya Warioba ilipendekeza
katika Katiba misingi hii ya kuzingatiwa, Katiba Inayopendekezwa imeifuta yote
katika Ibara ya 65, na ukiisoma Ibara hii utagundua haina masharti ya 54(1)(a).
Najiuliza dhambi ya masharti haya ilikuwa nini? Mahitaji ya Kimkakati ya Jinsia
hayawezi kuwapo kama msingi huu umefutwa.
Rasimu
ya Warioba katika Ibara yake ya 113 ilieleza bayana kwamba uwakilishi katika
chombo cha kutunga sheria kwa maana ya Bunge uwe nusu wanawake na nusu wanaume.
Warioba alitizama mbali kwamba kwa namna ambavyo jamii yetu imejengwa katika
mfumo dume ufike wakati wa kubadili fikra na kuwa na chombo cha kutunga sheria
ambacho kinazingatia uwakilishi unaojengwa katika kuheshimu misingi ya usawa wa
kijinsia.
Warioba
alijua kwamba wakulima wengi nchini ni wanawake, alijua pia kwamba wahanga na
wanufaikaji wa mfumo wa afya nchini ni wanawake na kwa mantiki hiyo watu ambao
wako kwenye sehemu na nafasi nzuri ya kuwasilisha mawazo ya watanzania ni
wanawake sambamba na wanaume. Na sisi kama watu ambao Rais alitupa dhamana ya
kufanya kazi na Mzee Warioba tulijiridhisha kwamba hata katika Bunge wanaolala
wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea ni wanaume na sio wanawake.
Warioba
ni kama alibashiri kwamba iwapo tungekuwa na Bunge ambalo lingekuwa na
uwakilishi uliosawa kati ya wanawake na wanaume ndani ya muda mfupi watanzania
wangetambua wanawake wana uwezo tena hata zaidi ya wanaume na ingewajengea
imani kwamba hata uongozi wa nchi ungeweza kuaminiwa kwa mwanamke.
Katiba
Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 129 imefuta masharti yaliyokuwemo katika
Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 113(3) yaliyosema “Katika kila Jimbo la
Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja
kwa ajili ya mwanamme”. Huu ulikuwa msingi wa kuhakikisha kuna usawa wa jinsi
na jinsia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Sijaelewa msingi wa kufutwa kwa
msingi huu ambao ungepelekea kuzingatiwa kwa asilimia 100 kwa Mahitaji ya
Kimkakati ya Jinsia ambayo yangewakomboa mamilioni ya wanawake ambao
wanakumbana na unyanyasaji uliojengwa fikra za wengi katika Taifa letu.
Ukisoma
Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 193(3)(b) ilizungumzia majukumu ya Tume Huru
ya Uchaguzi kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuna uwakilishi unaozingatia jinsi.
Tafsiri ya Ibara hii ni kwamba kama Tume Huru ya Uchaguzi ikija katika Jimbo na
hakuna mgombea mwanamke basi ujue uchaguzi hakuna na vivyo hivyo kinyume chake.
Ukiisoma Katiba Inayopendekezwa katika Ibara yake ya 220(3) utagundua ni
kipengele cha “uwakilishi unaozingatia jinsi” ndicho pekee kilichofutwa.
Nawauliza nyote dhambi ilikuwa nini hata kufuta jukumu hili la Tume Huru ya
Uchaguzi?
Ni
miaka 51 ya Muungano, unadhani bado wanawake wanatakiwa kupewa nafasi za
uongozi kwa mbinu za miaka ya 70, kwa maana ya viti maalum na kwa kusubiri
utashi na fadhila za viongozi wakubwa? Je wanawake hawastahili haki sawa na
wanaume? Nimeandika nikiwa kama mwanaume anayethamini nafasi muhimu ya wanawake
katika ujenzi wa Taifa letu na anaye amini kwamba Taifa hili haliwezi kupiga
hatua kama tutaendelea kuwahadaa wanawake, wapenzi wetu, dada zetu, shangazi
zetu, mama zetu na bibi zetu. Niwatakie Miaka 51 ya kusherehekea Muungano wetu.
Muungano wa Haki na Heshima Udumu Milele.!