Thursday, October 8, 2015

TUTOKE KWENYE “PANGO LA PLATO,” TANZANIA YA VIWANDA INAWEZEKANA



Katika gazeti la RAI  Toleo Na. 1217 la Alhamisi ya Octoba 1-7, 2015, kulikuwa na makala ya Ndugu Kennedy Masiana  yenye kichwa cha habari “Dk. Magufuli Tanzania ya Viwanda haiwezekani.” Katika makala hiyo mwandishi amefanya juhudi kubwa kuonyesha kuwa juhudi zozote za kujenga viwanda kwa Tanzania ni ndoto kwa kuwa gharama za kujenga viwanda hivyo ni kubwa kwa nchi kama Tanzania kumudu. Mwandishi anasema Rais wa Tanzania hana haja ya kujishughulisha na ndoto za kujenga viwanda kwa kuwa ni jambo lisilowezekana.  

Kwa maneno yake  mwandishi anasema, “Watanzania  wa sasa wanamtaka Rais ajaye, awe ni yule atakayeshughulika na hali zao za mashambani, hospitalini, miundombinu bora ya barabara itakayowawezesha kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko.” ... “awahakikishie huduma nzuri za kijamii kama huduma ya maji safi na salama ya kunywa, elimu bora, umeme wa uhakika, lakini pia aguswe na hali yao ya umaskini wa kipato ili waweze kujikomboa kiuchumi.”

Kimantinki na kimaana maelezo ya mwandishi hapo juu yana matatizo makubwa ya aina kubwa tatu: Kwanza, maelezo haya yanaonyesha kukata tamaa na kukubali hali tuliyo nayo kuwa ndivyo ilivyo na haiwezi kubadilika. Kwa sasa serikali imekuwa ikijitahidi kufanya hayo aliyosema mwandishi.  Inaeleweka duniani kote kuwa maendeleo ya kweli yanakuja tu kwa kuwa na viwanda na kwamba sekta zingine zote zitaweza kustawi tu ikiwa tu zimefungamana na viwanda. Mfano, uzoefu wa nchi zote ambazo zimeendelea kiuchumi unaonyesha kuwa  mapinduzi ya kilimo yaliwezekana kwa kufungamana kwa sekta ya kilimo na ukuaji wa viwanda vya kuzalishaji pembejeo na kusindika mazao.

Vivyo hivyo, sekta ya huduma za elimu isiyofungamana na viwanda badala ya kuwa chanzo cha ustawi na maendeleo ya nchi inaweza kuwa chanzo cha matatizo. Kwa mfano, Tanzania sasa inazalisha wasomi wengi kila mwaka, hata hivyo kutokana na kukosekana kwa  viwanda, wasomi wetu hubaki mitaani wakiwa hawana ajira na matokeo yake baadhi yao hushawishika kujiingiza katika vitendo viovu kama vile ukahaba, ujambazi na uhalifu wa aina mbalimbali kama njia ya kujipatia kipato. Lakini tulipokuwa na viwanda katika miaka ya sabini na themanini wahitimu wetu walikuwa wanachagua kazi maana zilikuwepo za kutosha.

Hata sasa tatizo la ajira si kubwa katika nchi kama  China na Korea ambapo kuna uwekezeji wa kutosha kwenye viwanda.

Tatizo la pili la makala ni kuegemea kwenye falsafa za feki na zilizoshindwa za uchumi mamboleo. Msingi mkubwa wa falsafa hiyo ni kuwa dola haipaswi kujishughulisha na masuala ya kiuchumi kama vile viwanda. Kuingizwa kwa falsafa hii kupitia ushawishi na masharti ya wafadhili wakiongozwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF)  katika miaka ya tisini ndiyo sababu kubwa iliyosababisha viwanda tulivyokuwa navyo hapa nchini kubinafsishwa kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kutoendeshwa kwa ufanisi. Hata hivyo, baada ya kubinafsishwa viwanda vingi  kwa matumaini kuwa vingeendeshwa kwa faida na ufanisi, viwanda vingi vilikufa na kuiacha  Tanzania  bila viwanda. Hapo ndipo u-feki wa falsafa hiyo inayojinasibu kuwa sekta binafsi pekee ndiyo injini ya uchumi ilipoonekana wazi. U-feki huo ulijidhihirisha zaidi wakati wa msukosuko wa uchumi wa dunia ulioanzia Marekani mwaka 2008.

Marekani ambayo ndio kuhani mkuu wa falsafa hiyo ya kiuchumi iliamua kuachana nayo na dola kuingilia uchumi ili kuokoa makampuni makubwa yenye maslahi kwa nchi hiyo. Kwa nyongeza, hakuna nchi hata moja duniani zikiwemo zilizoendelea huko nyuma kama uingereza na ujerumani na zile zilizoendelea siku za karibuni kama China, Korea ya Kusini na Taiwani ambayo zilifanikiwa bila dola kujiingiza katika uwekezaji.  Kwa bahati mbaya, falsafa hii feki bado inafunga fikra za watu kama wale wafungwa kwenye hadithi ya pango la Plato. Katika pango hilo wafungwa walinyimwa fursa ya kuona mwanga wa jua.

Walizoea kuona vivuli vya mwanga wa jua ukipiga ukutani kupitia kwenye mlango wa pango, na kwao vivuli hivyo ndiyo ulikuwa mwanga halisi. Siku walipotolewa nje wakaonyeshwa mwanga walikataa kuwa huo siyo mwanga kwa maana kwao vile vivuli walivyozoea kuviona ndiyo mwanga wenyewe. Inabidi tufungue fikra zetu tuangalia hali halisi ya mwenendo wa kiuchumi duniani na tutaona kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana.

Tatu, mwandishi anaonekana kutokujua chanzo halisi cha matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Tanzania kwa sasa. Matatizo hayo ni pamoja na  ukosefu wa ajira, utegemezi wa misaada kwa bajeti yetu, umaskini uliotopea, kudorora kwa huduma za jamii kutokana na kukosekana kwa fedha za kuboresha miundombinu ya kugharamia ubora wa utoaji huduma. Chanzo kikubwa cha matatizo hayo ni kuwa na uchumi usiotosheleza mahitaji.

Hivyo, kama tutakubali maoni ya mwandishi kama yalivyonukuliwa kwenye aya ya kwanza, Tanzania itakuwa imekubali kuwa kwenye “vicious cycle of poverty” yaani  mduara wa umaskini. Kwa maana tutaendelea kuwa kwenye kilimo kisicho na tija, tutaendelea kukopa nje na kuongeza deni la Taifa ili tutoe huduma za jamii. Tutazalisha wasomi ambao wataishia mitaani na kuwa chanzo cha maovu katika jamii. Mwisho wa yote Tanzania si tu kuwa itaendelea kuwa nchi maskini na tegemezi.

Tanzania ya Viwanda anayoinadi Dk. Magufuli Inawezekana.

Hakika ujenzi wa viwanda ndiyo namna pekee ya kujikwamua kutoka katika matatizo yetu ya kiuchumi na kuhakikisha ustawi wa Tanzania ya leo na ya vizazi vijavyo. Bahati nzuri Dk. Magufuli ameeleza ni namna gani atatekeleza azma yake ya kuleta mapinduzi ya viwanda Tanzania ikiwa tutampa ridhaa ya kuwa Rais wetu.

Kwanza, serikali inaweza ikajenga viwanda vya aina mbalimbali nchini kwa kuweka sera nzuri zinazovutia wawekezaji watakojenga viwanda katika maeneo ya kimkakati na kipaumbele kwa nchi.  Bahati nzuri hapa Tanzania tunayo mifano hai kupitia  kujengwa kwa kiwanda cha Dangote (Dangote Industries Limited Tanzania [DIL]),  moja ya viwanda vikubwa vya kuzalisha sementi barani Afrika,  mkoani Mtwara. Kiwanda hiki kimeajiri zaidi ya Watanzania elfu kumi. Serikali pia inapata mapato ya kodi mbalimbali kutoka kwenye kiwanda hicho na kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho. Pia,  Watanzania wengi wameajiriwa na wanauza mazao yao kwa viwanda vya mwekezaji mzawa,  Azam Bakhresa Group of Companies. Dk.Magufuli ameahidi kuwa  moja ya sera zake za kiuchumi ni kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji  wa ndani na nje kuwekeza katika  sekta ya viwanda nchini. Bahati nzuri serikali imeshatenga maeneo maalum ya kiuchumi kule Bagamoyo, Mtwara na Kigoma. Atakachohitaji kufanya Dk.Magufuli ni kuongeza maeneo maalum ya viwanda na kuweka miundombinu muhimu kwa ajili kuleta ufanisi katika shughuli za viwanda katika maeneo hayo. 

Pili, Serikali inaweza kuingia ubia na wawekezaji binafsi kupitia kile kinachojulikana siku hizi kama (Public Private Partnership[PPP]) yaani, ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma. Kwa taarifa tu viwanda vikubwa katika nchi mbalimbali kama China, Korea, Ujerumani vimeundwa kwa mtindo huo.

Tatu, serikali inaweza ikajenga yenyewe viwanda hasa kwenye maeneo ya kimkakati kwa maslahi ya nchi hasa viwanda vikubwa. Hapa inabidi tuelewe kuwa siyo lazima kuwa na fedha taslimu kama mwandishi alivyoashiria. Kama ilivyo kwa wawekezaji wengine wakubwa, serikali inaweza kukopa mtaji kwa ajili ya kugharamikia uanzishwaji wa viwanda husika. Jambo la msingi ni kufanya upembuzi yakinifu na kuonyesha namna kiwanda kitavyotengeneza faida na kulipa deni. Ukopaji huu ni tofauti na ukopaji ambao tunaufanya kugharamia huduma za jamii badala ya sekta za uzalishaji. Tukiwa na viwanda vinavyofanya kazi kwa faida, Watanzania watapata ajira, tutaondoa utegemezi na kuondoa umaskini. 

Nne, kama alivyobainisha Dk.Magufuli, serikali inaweza ikaanzisha mitaji maalum yaani “venture capital” kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia inayohitajika kwa viwanda. Mitaji hii inaweza kupatikana kwa njia mbalimbali kama vile  serikali kukopa, kuingia ubia na wawekezaji, ama kutoka kwenye hazina ya nchi. Mitaji hii kwa kawaida siyo mikubwa lakini ni kichocheo kikubwa katika maendeleo ya teknolojia hasa ya mawasiliano. Ni kwa njia hii ndio viwanda vingi vimechipuka kutoka katika eneo lijulikanalo kama “Silicon Valley” huko Marekani. Hapa ndipo makampuni makubwa ya kiteknolojia kama vile Apple inayozalisha simu za Iphone ilipozaliwa.

Kwa ufupi, hakuna nchi ambayo imeweza kujikomboa katika umaskini na kujiletea maendeleo bila ya kuwa na viwanda. Tanzania haiwezi kukwepa ukweli huo ikiwa inataka kuondokana na mnyororo wa umaskini na matatizo ya kiuchumi yaliyopo.  Tanzania ya viwanda inawezekana tukiweza kuwa na uongozi wenye dira na mikakati dhabiti ya kutufikisha huko.


Na hapa Dk.Magufuli amejipambanua kuwa ana dira na uwezo wa kuleta mapinduzi ya viwanda Tanzania.  

Sunday, October 4, 2015

UCHAGUZI WA MWAKA HUU NI WAADILIFU NA WAZALENDO V/S GENGE LA WAHUNI “CARTEL” NA WASAKA MADARAKA KWA MANUFAA BINAFSI


Kwa muda mrefu kikundi cha wahuni kilijaribu na kufanikiwa kupoka madaraka ndani ya Chama cha Mapinduzi. Watu hawa walitaka kujijengea "cartel" ya kuongoza nchi, humo walikuwemo watu kadhaa na hasa wafanyabiashara akiwemo Lowassa na yeye ndiye alikuwa Msanifu wa genge hilo na hasa ili kutimiza ndoto yake ya kuwa Rais hata kwa kuununua Urais wa nchi yetu, alifanya hivyo mwaka 1995 akashindwa maana Mwalimu alikuwepo. Baada ya hapo genge hili lilijiposition kwenye maeneo yote nyeti ya nchi yetu.

Mwaka huu wana CCM tumekataa upumbavu huu wa kudhani Urais na Uongozi unaweza kununuliwa kama nyanya. Tumekataa na tumehakikisha katika ile "CARTEL" au GENGE la WAHUNI hakuna kati yao ambaye anaiona IKULU kwa tiketi ya CCM. Imewauma sana, Huyu bosi ndio kaenda UKAWA na wako waliobaki CCM, tutashughulika nao strategically, lakini kwanza ni lazima tupate Rais Mwadilifu KWANZA ambaye atatusaidia kazi ya Pili ya Kusafisha UFISADI. kazi ya Kwanza imekuwa kuwanyima Dhamana ya Urais kupitia CCM.

Hapa CCM wanapaswa kwakweli kujitoa kimasomaso. GENGE sasa limehamishia mapambano kutoka Kambi ya Upinzani. Utagundua hoja ya UFISADI ilishamiri sana na ndio maana kipindi fulani UKAWA waliunga Mkono kazi yetu ya Katiba ambayo lengo lake lilikuwa kuja kuua CARTEL au GENGE la WAHUNI, leo UKAWA hawana tena uhalali (legitimacy) ya kukemea UFISADI maana UFISADI umetamalaki kati na juu yao.

Hebu tafakari mtu kama ndugu yangu na kaka yangu Saeed Kubenea kwa kazi yooote aliyofanya miaka nenda rudi mpaka akashambuliwa, juzi alijisikiaje pale kawe aliponyooshwa mkono juu na Edward Lowassa? Dhamira yake ilimweleza nini? Na Lowassa hakusita kumpiga kijembe kwamba huyu alikuwa machachari sana kwenye Media sasa apunguze, hivi Kubenea amejiuliza Lowassa alimaanisha apunguze nini na kwa faida ya nani.?

Mimi mpaka TV mbili kubwa zimekataa nisikaribishwe kwenda kwenye vipindi kwa maelekezo ya wamiliki. Je kukataliwa kwangu ni kwa faida ya nani? Mbona kama ni siasa kila siku kwenye TV hizo wadau wa UKAWA wanajimwaga vilivyo, je mimi tatizo langu ni nini? Wengine walifurahia TCRA kutoa tamko la kukataza watu kwenda kwenye vipindi vya moja kwa moja, na wengi walisema mitandaoni wamenikomesha mimi, hivi mimi nikikomeshwa ni kwa faida ya nani?

TCRA walilazimisha kwamba ili uruhusiwe kushiriki kwenye vipindi vya moja kwa moja ni lazima uwe mwakilishi wa vyama vya siasa. Mimi nikasema kwa hakika ningemwambia ndugu Kinana Katibu Mkuu wa CCM angenipa barua ili niendelee kushiriki. Lakini nikasema hivi wanaoruhusiwa kushiriki ni wanasiasa peke yake? Je uchaguzi ni haki uhodhiwe na wanasiasa pekee? Nikaendelea kujiuliza hivi uchaguzi mkuu wanaotakiwa kujadiliana zaidi ni Wananchi wanaochagua ili kutoa dhamana au wale wanaoomba kuchaguliwa ili kupewa dhamana? Nikasema mbona Katiba inasema kuna Uhuru wa kuweka mawazo hadharani je mawazo hayo yako limited wamakati wa uchaguzi?

Nikafunga safari kwenda TCRA nikawauliza maswali hayo na namshukuru Mungu aliwapa busara kubwa na baadaye walitoa tamko kubatilisha katazo lao la awali. Lakini nikajiuliza zaidi kwanini hata wale wadau wa asasi za kiraia hawakuoneshwa kukasirishwa na kitendo kile cha TCRA? Nikasema hata watu wote wakisimama mimi nitaendelea kudai haki na kweli katika nchi yangu.

Leo siwezi kwenda kwenye TV mbili kubwa na wamiliki wameweka msimamo, kwanini? Wale wanaofurahia mimi kukataliwa je wanapata faida gani.? Mbona mimi nikionana na vijana na wadogo zangu ambao wako katika vyama vya upinzani nawapa moyo na kuwaambia watende sawasawa na dhamira zao njema na kwamba walitizame Taifa kwanza? Najiuliza je Tatizo langu ni nini? Au sijitambui? Au niko naïve?

Nitasema kweli Daima na fitina kwangu mwiko na nitatumia elimu yangu kwa manufaa ya Wananchi wa Taifa langu. Kwanini leo baadhi ya watu wamenigeuka, watu ambao walifurahia nilipowaambia pale Ubungo plaza na pale Mlimani city kwamba maslahi binafsi yanahatarisha mustakabali wa Taifa letu. Nilikwenda mbali na kuwataja watu hao na watanzania baadhi na wengi wakanifurahi sana. Mbona leo naendelea kuwasema watu wale wale na baadhi ya watanzania wananiona nimegeuka? Kwanini waliniamini kipindi kile na wakijua mimi ni CCM na nilikuwa nawasema CCM na leo Mimi nikiwa bado CCM nawasema watu ambao wanataka kutununua ili waendeleze GENGE la KIHUNI mbona watu wanaema mimi ni kigeugeu? Naendelea kutafakari.

Siku moja nilikaa na viongozi wawili wa CCM, mmoja akasema nadhani mchakato wa Katiba ni lazima kabla ya kura ya maoni tujenge muafaka na kufanya maridhiano ili kila sauti ya Mtanzania isikilizwe. Kiongozi mwenzake mdogo kidogo kwa cheo akabisha sana na akasema ni lazima twende kwenye kura ya maoni kwasababu tendo la Katiba kwa lilipofika ni kama maji yanayomwaga kutoka katika bilauli kwamba ni lazima yafike chini.

Nikamtazama na kumkazia macho na nikamweleza wacha na mimi nizungumze kama mwana CCM. Nikawaomba niwaeleze historia ndogo ya namna nipo nilipo. Nikasema nianzie kwenye Katiba, nikawaambia unajua mimi nilikuja Tume ya Katiba nikiwa simfahamu mtu yeyote isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano? Nikawaeleza mimi sikumfahamu Mzee Warioba, Jaji Ramadhani, Mzee Butiku, Dkt. Salimu wala Profesa Kabudi na wengineo, sikumfahamu hata mmoja. Nilikuwa namfahamu Rais Kikwete tu. Alipotupa kazi na akatuagiza tuwasikilize watanzania na watakachosema ndicho ambacho tukiandike, tulifanya hivyo kwa unyenyekevu mkubwa kwa watanzania.

Hata pale ambapo Rais alionekana kutoka na msimamo tofauti na wetu nilibaki kuwaambia watanzania kwamba Tanzania njema itajengwa na watanzania wenyewe. Hatukuishia pale tuliokuwa wajumbe wa Tume ya Katiba tulifanya utafiti kwa kuzungumza na wadau mbalimbali, wabunge, viongozi wastaafu, watu mashuhuri ili kuelewa tatizo lilikuwa wapi.

Utafiti huu wa chini chini ulinipa fursa ya kuonana na wabunge wengi wa CCM na wa upinzani na wote walikiri kwamba “Bwana Mkubwa amekataa” na tulipozidi kuhoji hoji tulikuja kukutana na wapambe wake kwanza ambao walisema “tatizo lenu mmedhoofisha Urais na kwamba Kikwete anataka kuondoka ameweka masharti na kanuni ngumu za uongozi hilo haliwezekani” wakaendelea kusema “yeye (Kikwete) aende na sisi tubaki na madaraka yale yale au zaidi na tuwe na mamlaka kama aliyonayo sasa katika nchi”.

Wapambe hawa tulizungumza nao kwa maana ya kuwapa elimu ya Rasimu ya Katiba na wakawa wanatuuliza “kwahiyo ninyi (Tume ya Katiba) mnashauri ‘Mkubwa’ achukue Urais wa Tanzania au Urais wa Tanganyika?” Tukasema achukue ya Muungano, wakasema “je itahusisha madini, gesi na ardhi”? Tukasema hapana, wakaendelea kuuliza “je akichukua ya Tanganyika atakuwa na uwezo wa kusafiri nje ya nchi kama Rais Kikwete na kupigiwa mizinga 21”? Tukasema hapana, mmoja wao akasema “anhaaa hapo ndio mnapokosea, sisi tunataka zote za Tanganyika na Muungano ziwe pamoja”, kwa kusema hivyo walikuwa wanamaanisha serikali mbili.

Hatukuchoka tukafanya utaratibu na tukaenda kumuona “Bwana Mkubwa” yaani Edward Lowassa, tulikutania ofisini kwake mikocheni. Ili kuweka uwazi katika mkutano ule tulijumuisha pia wawakilishi watatu wa Asasi za Kiraia na Makamishna Wawili, mimi nikiwa mmojawapo, tulikuwa na kikao ambacho hakikupungua saa mbili.

Ni katika kikao kile nilithibitisha kwamba aliyebuni mkakati wa kuikataa Rasimu ya Warioba kwa CCM alikuwa Edward Lowassa tena akaonesha kufurahishwa na Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa Chama kuzomewa na hatimaye Rasimu aliyoipeleka katika Chama kukataliwa. Nilijuliza sana mimi kama Kiongozi kijana, tafsiri yake ni nini? Huyu ni mwana CCM na anafurahia Mwenyekiti wake kudhihakiwa na kutupiwa Rasimu yake katika kikao. Leo najiuliza kama alikuwa na dhamira ya kuikubali rasimu ya Warioba kwanini alikaa kimya wakati Mwenyekiti wake akidhihakiwa?

Nikawaeleza iliyokuwa Tume ya Katiba iliwahi kumwita hata mzee Kingunge aje tujadiliane kuhusu Rasimu ya Warioba na alipokuja aliwatukana wajumbe wa Tume pamoja wageni wengine waalikwa akiwemo Profesa Sherrif kutoka Zanzibar, nilipoona anamwunga mkono Lowassa sasa namwelewa na ndio maana katika mkutano wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere nilidiriki kusema Mungu akinipa umri mrefu na kufikia uzee namwomba Mungu nisiwe kama wao.

Nikamwambia yule Kiongozi mdogo, unadhani ni kazi rahisi mimi kama kijana mdogo kusimama kidete kutetea maoni ya Wananchi? Nilijua aliyekuwa na maslahi katika kutupilia maoni ya Wananchi hakuwa Kikwete bali Edward Lowassa ambaye amekuwa akiutafuta Urais wa kifalme. Kuthibitisha hilo nilimtamka kwa jina mara kadhaa Ndugu Edward Lowassa kwamba hafai kuwa Rais wa Tanzania.

Na kwangu mimi nilikuwa najiuliza hata kupitia CCM ambako mimi ni mwanachama, iweje mtu ambaye anakosa kuheshimu watanzania wanapotoa maoni yao ya Katiba akawa ni mtu ambaye atasimama ili wampe dhamana ya kuwa Rais wao. Mimi nilimkataa tangu CCM na nilipoona CCM kama vile wanachelewa, mimi (Polepole), Mzee Butiku na Mzee Warioba tulifanya mdahalo na tukaweka msimamo kama Lowassa atapewa tiketi ya kugombea Urais kupitia CCM basi sisi watatu tusingejitoa bali tungepiga kampeni ya kusema CCM isichaguliwe.

Nikaendelea kumwambia hili la Katiba Mbaya wake namjua na alijaribu kuhonga watu, ni lazima tujenge muafaka wa kitaifa kwanza. Namshukuru Mungu Kiongozi Yule ni muelewa akasema muafaka ni kitu muhimu, hilo linawezekana na ni kwa maslahi ya watanzania wote sema tu kipindi kile kiligubikwa na ushindani wa kisiasa, ila sasa ni muhimu tukaja pamoja kama Taifa. (Mwisho wa kunukuu kikao change na viongozi wa CCM)

Uhalisia huu ndio umefanya Mzee Joseph Sinde Warioba kupiga kampeni ya Chama cha Mapinduzi. Ila kitu kimoja napenda kuwaeleza kuna maadui ndani ya CCM na nje ya CCM na hasa hasa wale ambao wako chini ya “cartel” au lile GENGE la WAHUNI ambalo linafanya kila jitihada ili Mgombea wa CCM asiye na makundi na asiye na msalie mtume na wezi, wabadhirifu na mafisadi. Maadui hawa wako radhi Mwana Mtandao mwenzao (aliyeondoka CCM na kwenda UKAWA) apewe dhamana ya Urais wa nchi yetu ili waendelee kutunyonya kwa maslahi yao.

Ikumbukwe UKAWA huu sio UKAWA ule ambao mimi na Mzee Butiku na Mzee Warioba tulifanya nao kazi pamoja, si hawa. Hawa UKAWA wa sasa ni watu wenye uchu wa ajabu wa madaraka na kwamba wako tayari kumtumia mtu mwenye nasaba zote na ufisadi ili awafikishe ikulu.

Kama ni masikini na nikaambiwa mwabudu shetani ili niwe tajiri, nitakataa na kutunza utu wangu kama ambavyo Bwana Yesu alikataa kumwabudia shetani kwa sababu hizohizo.

Hivi sielewi hawa wanachama wa Chadema ambao wamekubali kumeza matapishi yao wenyewe, wanapataje amani mioyoni mwao wanapojua mgombea Urais wao ndio Yule mtu waliyesema ni fisadi kwa zaidi ya miaka 8. John Mnyika alisema anao ushahidi wa UFISADI wa Lowassa, Mbowe alisema anashangaa vibaka wanachomwa moto na Lowassa ameachwa anadunda mtaani, Mchungaji Msingwa aliyesema anayemkubali Lowassa akapimwe akili na Godbless Lemay eye amekuwa kimya kidogo ila naye amesema ni halali kumtupia jiwe fisadi lowassa. Hawa leo wanapataje uthubutu wa kusimama katika jukwaa moja na Lowassa na tena wakainuliwa mikono akiwanadi.

Mimi nilijiapiza wale waliokataa maoni ya Wananchi sitaki urafiki nao hata leo, na Lowassa ni mfano mmoja. Na niko tayari kuendelea kuunga mkono mabadiliko chanya yaliyofanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuuvunja na kuwanyima Urais kupitia CCM. Hii ndio CCM ya kweli, CCM ya wakulima na wafanyakazi, CCM inayochukia rushwa katika uongozi na sasa tumeanza na Urais na baada ya Urais tutawashukuia wabaya wote waliosalia. CCM ambayo haishurutishwi na matajiri wanaotaka kututengenezea viongozi ikiwemo nafasi ya Urais.


ITAENDELEA

Thursday, October 1, 2015

“HASIRA HASARA”: KUPIGA KURA KWA HASIRA NI UJUHA NA SI HEKIMA, TUPIGE KURA TUKILITIZAMA TAIFA


Utamaduni wa kukosa uhimilivu umetoka wapi?

Bado nimepigwa na butwaa kwa namna ambavyo baadhi ya watanzania wenzangu wanakosa ustahimilivu katika kipindi tunapoelekea uchaguzi mkuu. Nimegundua kwamba unapotoa hoja ambayo wengine hawaiungi mkono basi kumekuwa na ugumu katika kustahimiliana. Nashangazwa zaidi pia pale ambapo hata wale ambao ni wana mageuzi au wafuasi wa vyama vyenye mawazo mbadala, hawa wamekuwa wakali kweli pale mtu anapotoa hoja ambazo hazifanani na mitizamo yao.

Nimeanza kuona dalili ya Taifa kuanza kupoteza utamaduni wa ustahimilivu, utamaduni wa kuheshimiana, utamaduni wa kujadiliana kwa hoja na sababu na utamaduni wa mijadala inayojengwa katika dhana ya nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu. Kwa wale ambao ni wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii utagundua kwa sasa kuna mgombea ukimjadili ni tatizo, au ukimjadili mmoja bila kumgusa mwingine ni tatizo kubwa.

Jamii yetu imegeuka kuwa kama genge litishalo na kuamulia watu wazungumze nini, kwa nani na wakati gani. Ni katika kipindi hiki na ajabu kabisa baadhi ya wananchi wamekuwa wakilazimisha wananchi wengine na hasa wale wanaopenda kuweka mawazo yao hadharani kwamba ni lazima wawe katikati. Hivi kuwa katikati unapotoa hoja maana yake nini? Mtoa hoja mmoja ambaye pia ni kiongozi wa dini aliwahi kuniasa kuwa ninapojenga hoja niwe katikati au “neutral” na pasina kuainisha nani mbaya na nani mzuri. Nikamwuliza, je katika kazi ya kuhubiri dini, kuna siku amewahi kumtendea haki shetani anapohubiri na kwa maana ya kusema shetani naye ni mzuri kwasababu watu wengi pia wananufaika naye? Au wakati wote yeye huhubiri na kumtukuza Mungu wa Mbinguni pekee kwa yeye ndiye mwema na mtenda mema yote na wema wote huyoka kwako na Shetani au Ibilisi ni mwizi, muuaji na mharibifu na kwake hakuna wema bali ubaya wote.

Je kama mimi ni muumini wa kusimamia kweli na uadilifu, dhambi iko wapi iwapo nitasema katika wagombea Urais mtizamo wangu ni kwamba mgombea fulani kwa vigezo vya kibinadamu yuko vizuri na mgombea fulani kwa vigezo vya kibinadamu namwona sio mwadilifu na ana uchu wa madaraka na anadhani yeye aliandikiwa Urais na Mungu.

Ninaendelea kuuliza hasira iko wapi kama nitatumia uhuru wangu kumjadili mgombea mmoja ambaye kwa ushahidi nafahamu hana sifa ya uadilifu na ananasibishwa na ufisadi kwa zaidi ya miongo miwili?

Labda nieleze kwa sehemu, mimi ni mwana CCM na wakati wa Mchakato wa Katiba nakumbuka watu wote waliotukwamisha na walikuwa katika makundi mawili, kundi la kwanza lilikuwa watu na hasa mtu aliyekuwa hapendi maoni ya wananchi na katika namna yalikuwa yatumike kuandika Katiba Mpya. Mtu huyu anajulikana wazi kwamba alijipambanua kama mgombea pekee na mwenye hatimiliki ya Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mtu huyu mimi na wenzangu tulikuwa na kikao naye cha zaidi ya saa mbili nikimfafanulia Rasimu ya Warioba na faida zake, akakataa katakata. Mtu huyu tuliamua kwenda kumwona baada ya kuambiwa na wapambe wake kwamba Rasimu ya Warioba asingeruhusu ipite na kwamba kaweka mguu chini hivyo labda tukajaribu kumfafanulia, tulifanya hivyo, nilikuwepo na alikataa mbele ya macho yangu na akatupa mapendekezo ambayo ndio hatimaye yalikuwa katika Katiba Inayopendekezwa mwishoni.

Binafsi sikukubaliana naye pale na baada ya pale na nikajiapiza kuendelea kudai maoni ya wananchi nikitumia mbinu zote halali. Itakumbukwa nilipopata mwaliko katika vipindi vya Televisheni nilipata kusema mtu huyu kama “tatizo kubwa la kitaifa” na wenzake wengine hawapaswi kupewa dhamana ya kugombea Urais kupitia CCM. Watu wengi waliniunga mkono wakiwemo wafuasi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), nakumbuka mdahalo wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na baada ya kuona kwamba mtu huyu alikuwa kana kwamba anakwenda kufanikiwa kuwahadaa watoa maamuzi wa CCM nikasema pamoja na Mzee Butiku na Mzee Warioba kwamba kama mtu huyu na wenzake watapewa dhamana ya kugombea kupitia CCM basi sisi tusingeondoka CCM ila tungesema CCM isichaguliwe.

Na labda niwarudishe nyuma kidogo, kipindi chote cha mchakato wa Katiba sote tulimjua mtu aliyekuwa anatukwamisha, kwa hakika tulimjua kwa jina na sote tuliamini yeye na watu wa aina yake hawapaswi kupewa uongozi ndani au nje ya CCM. UKAWA walijua hili na tulikuwa pamoja. Hata pale tuliposema CCM ikimpa nafasi tungezunguka nchi nzima kusema CCM isichaguliwe, UKAWA walituelewa sana. Ninapata msongo wa mawazo baada ya CCM kusikia kilio cha wananchi, UKAWA na wana CCM wenye mapenzi mema na CCM na hatimaye kumnyima dhamana ya kugombea kupitia CCM na baadaye kwenda UKAWA, iweje tena UKAWA wale wale tulihangaika nao pamoja wageuke kauli na kusema yuleyule ni jemadari? Nashindwa kumuelewa Mhe. Mbatia, huyu namtaja kwa jina ili anisaidie kujua hivi kwa ukigeugeu huu mkubwa, je wanastahili kupewa dhamana na watanzania kama UKAWA?

Leo watu wale wale walioniunga mkono kusema watu wenye nasaba na ufisadi hawapaswi kupewa nafasi za madaraka na hasa nafasi ya madaraka ya Urais wa Jamhuri yetu, ndio hao wananisema kwamba niache kumsema mtu yuleyule ambaye alitusumbua sote, mimi nikiwemo na hata viongozi wa UKAWA zaidi na wanajua tangu alipokuwa CCM.

Watu wengine wataniambia kwamba hiyo ndio siasa, na mimi kwa unyenyekevu mkubwa nasema siamini katika siasa chafu, siasa inayokumbatia wezi, siasa inayopinda ukweli, siasa inayoendeshwa kwa fedha na hata Hayati Mwalimu Nyerere alituasa kwamba ili nchi hii iendelee inahitaji siasa safi na uongozi bora na akatuasa zaidi kwamba Rushwa ni adui wa haki na Utajiri unaotumika kununua watu ili kupata madaraka ni kama na ukoma. Nimekataa kuwa sehemu ya watu hao, ninaendelea na kiapo change kwamba mtu huyu hastahili kupewa dhamana yoyote katika nchi yetu hata kama nitabaki peke yangu ila najua iko siku nikiwa nimetangulia mbele ya haki ukweli utakuja kujulikana na roho yangu itapoa hukohuko mbele ya haki.


Tusisukumwe na Hasira

Mara zote maamuzi wanayofanywa kwa msukumo wa hasira huwa aidha na tija kidogo sana ama huleta hasara kwa watu binafsi na jamii kwa ujumla. Wahenga walikwishasema “Hasira Hasara”. Ni muhimu sana kutafakari busara hizi za wahenga kipindi hiki ambacho Watanzania tunajiandaa kufanya maamuzi ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kutafakari ni nani hasa anaefaa kupewa dhamana ya kuiongoza Tanzania kwa manufaa ya Watanzania.

Kwa bahati mbaya sana katika kipindi hiki kueleke Uchanguzi Mkuu wa Oktoba 2015, kumeibuka wimbi la siasa na propaganda zinazopandikiza chuki na kuchochea  hasira miongoni mwa Watanzania. Watu hawa kwa kuelewa vyema athari za chuki na hasira hawapendi kutoa fursa kwa Watanzania kutathimini kwa kina matatizo na mafanikio yetu.

Kutokana uchu wa madaraka na nia ya kutimiza ndoto zao za kushika dola, wanaochochea hasira na chuki, wanaminya nafasi ya wapiga kura kupima uwezo na dhamira ya wagombea katika kutatua matatizo ya kimaendeleo na kuendeleza ama kupanua wigo wa mafanikio na ustawi wa Watanzania. Ni muhimu pia kutambua bayana kuwa katika kinyanga’nyiro cha kutaka kutaka madaraka wanasiasa wengi kama sio wote huweka nguvu nyingi katika ushawishi unaolenga kujenga matumaini kwa wananchi ili mradi tu wapate kura. Ni wajibu wa Watanzania kuhoji na kupima uhalisia wa yale tunayoahidiwa na wagombea kwa kutafakari pasipo chuki wala hasira zinazopandikizwa na wanasiasa.   

Ni vyema tukumbuke kwamba katika hali ya hasira na chuki kuna hatari ya  kutosikiliza na kuhoji kwa makini wagombea wote wa uraisi, ubunge na udiwani ili kupima uwezo, weledi, uadilifu na uzoefu wao katika kutekeleza yale wanayoahidi katika sera  na vyama vyao. Maswali ya kujiuliza ni pamoja na Je kuna tija gani kumchagua mgombea fulani? Je mgombea husika anao uwezo, weledi na uzoefu katika kutekeleza yale anayoahidi? Je mgombea ni mwadilifu na anaweza kudiriki kukemea ufisadi? Je mgombea anaamini katika mfumo wa uzalishaji mali unaotoa fursa sawa kwa watanzania wote? Je mgombea na chama chake wanamipango na nia thabiti ya kuondoa kero mbalimbali za wananchi?

Kwa maslahi mapana ya nchi yetu kamwe tusikubali kutumiwa kukamilisha ndoto za watu wachache. Tuwaulize maswali sahihi ili kama hawana majibu sahihi tuwakatae kwa mujibu wa tathimini yetu juu ya sera na hoja zao. Tunafahamu wazi kuwa wagombea wengi wanaahidi mabadiliko ni jambo jema lakini tuwaulize uhalisia na uhakika wa ahadi zao.

Lakini pia wagombea na vyama vyao watueleze bayana tutanufaikaje na nini athari za muda mfupi na mrefu zinazoambatana na mabadiliko hayo. Mwisho ni vyema tutambue   kuwa hatuwezi kupata viongozi wenye nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa kupiga kura za hasira na chuki zinazochochewa na watu wachache wanaotaka kutimiza malengo yao binafsi. Kila tunapowasikiliza wagombea na vyama wakinadi sera zao tuanze sasa kujenga utamaduni wa tuzitafakari na kuzipima hoja zao ili kufanya maamuzi ya busara kupitia sanduku la kura ifikapo tarehe 25 Oktoba 2015.