Kuonesha kila mtu
anaweza kutangaza nia ya Urais kwa watu wazima ni kumkosea heshima aliyeko
madarakani
Wiki ijayo nitaendelea
kujadili hasa kwenye runinga, redioni na kwenye hadhara mbalimbali juu ya mchakato
wa ndani ya Chama cha Mapinduzi wa kumpata mtu atakayepewa dhamana na chama ya
kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Ninaendelea
kusisitiza kwamba, CCM inapasa kuonesha mfano kwa vyama vingine, CCM inatakiwa
kutoka katika mchakato wake wa ndani kwa ushindi. Ninaposema ushindi
ninamaanisha, mbele ya macho ya watu na kwa wingi wa wale ambao ninaonana nao.
CCM haijajijengea taswira nzuri mbele ya watu na hasa vijana wadogo na kwa
maneno mengine hii ni fursa adimu na adhimu ya kuuthibitishia umma wa
watanzania kwamba imani yao kwa CCM haijawekwa rehani.
Lakini kabla
sijaainisha mambo machache ambayo wana CCM wanatakiwa kujipima kwayo ninabudi
ya kueleza pia kwamba, licha ya chama kutoa uhuru mpana kwa watu kutangana nia
ya uombea Urais, lakini pia jambo hilo linaleta taswira yenye ukakasi kidogo.
Inawezekana tuna wana CCM wengi wenye uwezo mkubwa wa hata kupewa utawala wa
nchi lakini inabidi kujichunguza na kutafakari ndani ya chama je kuwa na
wagombea karibia 20 ni sifa yenye tija au ni sifa za kijinga mbele ya macho ya
watu?
Kila kona watu
wanasema hata huyu, hata yule? Inaonekana kana kwamba ni mchezo wa gombania
goli, maadamu unaweza kubutua mpira mbele basi karibu uwanjani, la hasha. Najua
CCM inajua fika na kwa uzoefu kwamba Urais ndio taasisi kubwa kabisa katika
Taifa letu. Taasisi ya Urais na kiongozi wake ambaye ni Rais mwenyewe, ni
nafasi na wadhifa nyeti kabisa. Taasisi ya Urais na nafasi ya Urais si pahala
pa kukimbilia kana kwamba ni mchezo wa “chandimu” au “gombania goli”.
Nimepata kusema hapo
awali uongozi wa nchi na hasa uongozi wa juu kabisa wa nchi yetu ni kama cheo
cha kiongozi wa dini, ni kama kuhani ni kama nabii, nafasi hiyo ni takatifu.
Kwa wale wenye imani ni vema mkajua kwamba hata Mungu anapolitazama Taifa letu
ili kulibariki na kutufungulia neema, huzipitisha Baraka na neema hizo kwa yule
Kiongozi wetu mmoja ambaye ndiye taswira ya Umoja wetu, huyo ndiye Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkichagua mtu ambaye kwa sifa za kibinadamu na
kwa muonekano wa haraka haraka wa kibinadamu ni mzuri, Taifa letu litakosa
Baraka za Mungu kwa miaka mitano inayokuja.
Nafasi kama hii ya
Urais kwa asili yake mtu hutafutwa, huombwa na hata kulazimishwa na wale ambao
huwa wameonekana kutoka miongoni mwetu kuenea katika nafasi hiyo aghalabu
hukubali kwa kuumia moyo kwasababu wanajua jukumu lilopo mbele yao ni gumu,
zito na lenye changamoto nyingi.
Na hapa niwaase
viongozi wa dini kwamba wao ndio mabalozi wa Mungu hapa duniani, wawe makini
sana hasa kipindi hiki kwasababu iwapo watamwakilisha Mungu sehemu ambazo Mungu
asingependa kuwakilishwa itakuwa ni kujichumia dhambi kubwa.
Unajua katika utendaji
wa majukumu ya nchi balozi ndiye mwakilishi wa nchi na mwakilishi wa Rais, sasa
nikupe mfano, mwaka 1977 tulikuwa na mgogoro na Nduli Idi Amini Kiongozi wa
Uganda wakati huo, sasa kama ingetokea balozi wetu kila kukicha yuko kwa Idi
Amini anakula na kunywa naye kama marafiki tena kwa utashi wake mwenyewe wala
sio kwa maelekezo ya kimkakati kutoka makao makuu kwa maana ya hapa nyumbani.
Je balozi kama huyu tungemtendea vipi? Katika kipindi kile cha vita, huyu
angekuwa mhaini moja kwa moja na adhabu yake ni kifo. Sasa na ninyi viongozi wa
dini ambao mnamwakilisha Mungu katika maeneo ambayo mnajua kabisa asingependa
kuwepo, mjue, na ninawaambia leo kwamba mbele za Mungu adhabu zenu zitakuwa
zile zimstahilizo anayemuasi Mungu, kibinadamu huwa tunaita mhaini. Kuweni
macho!
Na niwaase pia wana
CCM watakao kuwa na dhamana ya kupitisha mgombea wao kwamba, msianze kuhukumu
watu kwa muonekano wao, msije nanyi mkahukumiwa, hatumpimi mtu kwa habari za
kusikia, la hasha, maana najua wako katika watangaza nia ambao wamefanikiwa
kuficha ubaya wao, lakini hawana tofauti na wale muwaonao wabaya sasa,
watendeeni haki na Mungu atawaheshimu.
Baada ya kusema
maneno ya utangulizi sasa naomba kwa sehemu nieleze baadhi ya matarajio ya
Tanzania na watanzania kwa Rais wa Awamu ya Tano. Matarajio haya yamejikita
katika namna ambavyo Rais wa awamu ya Tano ataweza kwa uwezo na ufanisi mkubwa
kushughulika na masuala ambayo kwa muda mrefu sasa yametuvuruga kama Taifa na
yametuacha katika sintofahamu juu ya mustakabali wetu kama Taifa sasa na
baadaye.
Kusimamia
Utawala Katiba na Sheria
Rais wa awamu ya
Tano anapaswa kujua kwamba kwa muda mrefu tumekwenda kinyume na Katiba au kwa
lugha kali tumekuwa tukivunja Katiba muda mrefu hata tukazoea tabia hiyo na
kuifanya mazoea, tabia na utamaduni. Rais wa awamu ya Tano anapaswa kuwa mtu
mwenye uhalali wa jamii “social legitimacy” na ambaye kwa uhalali huu atakuwa
na mamlaka ya uadilifu yaani “moral authority” ya kuondoa kabisa mazoea, tabia
na utamaduni wa kuvunja Katiba na kuenenda kinyume cha sheria za nchi.
CCM wakitupatia mtu
ambaye hana uhalali wa jamii yaani “social legitimacy” na ambaye hana mamlaka
ya uadilifu yaani “moral authority” kwa uwazi tumwonavyo sasa na kwa kificho
tusivyomjua sasa, mtu huyo kamwe hatoweza kusimamia utawala wa Katiba na
Sheria, mtu huyo ataendeleza mazoea yale yale yasiyofaa. Mtu huyo ataendelea
kulinda maslahi ya wale wanufaikao na mazoea, tabia na utamaduni wa kuvunja
sheria za nchi, mtu huyo hatakuwa Rais wa watanzania na vivyo hivyo watanzania
wasitegemee miujiza kutoka kwake.
Suala
la Muungano wetu
Matarajio ya
watanzania kwa Rais wa awamu ya Tano ni pamoja na kushughulikia na kumaliza
kabisa Changamoto za msingi zinazokabili Muungano wetu. Kila mtu anajua kwa
tuna manung’uniko kutoka kila upande wa Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na
Tanzania Visiwani. Tunataka mtu ambaye ana uhalali, ana mamlaka na anaheshimika
na viongozi wastaafu na walioko madarakani kwamba anaweza kuwaitisha na
kuwaambia “watanzania wanatatizwa na Changamoto za Muungano wetu na kwa pamoja
tunakwenda kuziondoa”. Awe mtu ambaye viongozi wa upinzani na viongozi wa CCM
wakimtizama wanasema mtu huyu ninamheshimu na nina imani naye kwamba anaweza
kufanya kazi hii.
Naomba niwaume sikio
kidogo, tunataka mtu ambaye ataimarisha heshima na nidhamu ya madaraka ya Rais,
leo hii wengi wa viongozi wetu hawaheshimiani, hawapendani, hawazungumzi na
ukiongea na huyu anamlaumu yule, ukiongea na yule anajifanya kama halioni
tatizo vile, na hawakai kwa ujumla wao wakazungumza na kuondoa tofauti zao. Hii
inakwenda kwa viongozi wa wastaafu na walioko madarakani, kila mtu anamwonea
kinyongo mwenzake. Tunamtaka mtu ambaye ana uhalali wa kuwaita wote na
wakaitikia wito. Leo hii tuna nchi mbili na serikali mbili, hili ni baa maana
hata ukisoma ibara ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema tofauti.
Muungano umejeruhiwa
zaidi miaka mitano iliyopita na hatujaweza kuponya majeraha yake hata kidogo
isipokuwa kutoa dawa za kupunguza maumivu, dawa za kupunguza maumivu ndio
kushughulika na zinazoitwa “kero za Muungano”. Sasa ufike wakati tumpate mtu
ambaye tunaamini ataweza kutoa dawa ya kuponya na kumaliza ugonjwa kabisa ili
Muungano wetu uwe na afya ya kudumu miaka 100 ijayo.
Ujenzi
wa Amani, Umoja na utulivu (stability) wa kisiasa
Tunamtaka Rais
ambaye anajua kwamba amani na Umoja wa Taifa letu msingi wake ni haki na usawa
kwa watu na Wananchi wetu. Anapaswa kujua amani ni tokeo la ujenzi endelevu wa
amani pamoja jitihada endelevu za kulileta Taifa kuwa kitu kimoja licha ya
mtawanyiko mkubwa wa makabila na dini za watu na Wananchi wetu. Matarajio ya
watanzania kwa Rais wa awamu ya Tano, ni kuona haki za watu na binadamu raia wa
nchi yetu zinaheshimiwa, zinatolewa kwa wakati, zinalindwa na kuhifadhiwa.
Aidha Rais huyu
ajaye anategemewa kutoa hamasa na kuwa mfano wa kulinda na kuzitoa haki hizi
ili watu na raia wa Taifa letu waweze kunufaika na kufurahia matokeo kuheshimu
haki za binadamu. Ili haki itolewe ni lazima usawa uzingatiwe kwa gharama
yoyote ile. Haki bila usawa ni kazi bure, Amani bila usawa ni kazi bure kabisa.
Rais ajaye anatakiwa kujua tumecheza cheza na haki za raia wetu na kwamba
hatujafanya kazi nzuri ya kuzitoa haki hizi kwa usawa kwa watu wetu katika
maeneo yote ya nchi na kati ya masikini na matajiri.
Ukicheza na haki za
binadamu na watu, kisha ukaondoa usawa kwa kupendelea wachache, jua tunakaribia
ukingoni, muda si mrefu, watu na raia wetu watakwenda kuchukua haki zao kwa
mikono yao, kwa vigezo vya maeneo ya kijiografia, dini, masikini dhidi ya
matajiri na kadharika. Tukifika huko, amani yetu tutakuwa tumeiweka rehani na
Umoja wetu mashakani. Leo hii viashiria vyote kwa amani yetu inatetereka viko
bayana, tunamtaka mtu ambaye akisimama tu imani zetu za nafsi juu ya Taifa letu
zinaanza kukua mara moja, mtu huyo akisimama hata imani ya uchumi inaanza
kuimarika na utashangaa kabla ya kuanza kutenda kiuchumi thamani ya shilingi ya
Tanzania itaimarika.
Nafasi
ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama
Tendeni haki,
shaurini viongozi wetu, msijiingize kwenye siasa na kamwe msishiriki kufanya
uamuzi wa kisiasa, kazi yenu ni ushauri na ni ushauri tu. Kama mpo wenye tabia
mbaya na isiyo na heshima ya kutisha viongozi wetu ninawaasa acheni mara moja.
Rais wa nchi hupatikana kwa ridhaa ya Wananchi na si vinginevyo, katika
utumishi uliotukuka wa vyombo vya ulinzi na usalama, mnajua ni dhambi na ni
kinyume na weledi wenu kujaribu kutengeneza Rais kwa namna na hali yoyote ile.
Najua dhamira njema
hutenda haki, na ninyi mmeapa hata kwa kufa ili nchi hii iishi, msiruhusu
wachache na wabaya na wenye dhamira mbaya miongoni mwenu kuvuruga zoezi
takatifu la kupata Kiongozi wa nchi hii. Wale ambao mtasimamia maadili ya kazi
yenu, histoa itasimama kueleza utumishi wenu uliotukuka na wale ambao tama
imewazonga, ni suala la muda tu na aibu kuu itawazonga na hatutawadhihaki bali
tutahuzunika kwamba tulifanya uamuzi mbaya kuwa nanyi katika vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama.
Maswali
kwa watangaza nia wiki hii
Walikuwa wapi
kusimamia waziwazi maslahi ya Wananchi katika mchakato wa Katiba?
No comments:
Post a Comment