Saturday, June 20, 2015

KWA HALI ILIPOFIKA, KUMPATA MMOJA TUNAHITAJI HEKIMA ZAIDI KULIKO VIGEZO NA SIFA



Inaonekana kuna kila dalili kwamba tunaweza kufika arobaini, namaanisha idadi ya watu ambao wanatangaza nia kupitia Chama cha Mapinduzi. Idadi kubwa ikiwa ni pamoja na mawaziri ambao wako katika serikali inayomaliza muda wake, wabunge, na makada wengine wa CCM.

Waumini wa dini nyingi wanajua hata kipindi kile cha agano la kale wakati Nabii Samweli alipokwenda kwa Yese ili kutoka kwa watoto wake achague mfalme wa wayahudi. Yese aliwapitisha watoto wake wote, wale ambao katika macho ya watu walionekana wamejengeka lakini kila alipokuja huyu, Samweli alisema Mungu hakumchagua huyu pia. Naona rundo la watangaza nia kupitia Chama cha Mapinduzi na baada ya mchakato wa kichama ili mmojawao awe mrithi wa Rais Kikwete wakiakisi kwa karibu hadithi ile ya kale ya rundo la watoto wa Yese ambao Mungu alimwambia Samweli hakuona mmoja miongoni mwao.

Naizungumza hadithi hii kwasababu bado kulikuwa na fursa ya kumpata mrithi wa mfalme hata pale ambapo baada ya watoto wote wa Yese kupita, Samweli akasema hakuna mwingine? Watoto wako ni hawa tu? Ndipo Yese akakumbuka kuwa Daudi hakuwepo pale, akasema yuko mdogo wao, yuko machungani, Yese akasema mlete huyo, na Daudi alipoletwa huku akionekana mwekundu kabisa kwa maana mwenye ngozi angavu maana alitumia muda wake mwingi nyikani, hodari na mwenye ujasiri, Mungu akamwambia Sauli huyu ndiye, mpake mafuta awe mfalme wa watu wangu.

Nikiutizama mchakato wa CCM naona rundo la watangaza nia wakiakisi watoto wa Yese, lakini maadamu mpaka leo hii bado tuna siku kama 10 nina uhakika bado tuna watu ambao huenda nao wana maono ya kiuongozi kwa Taifa letu. Rai yangu ni kwamba watu hawa wajitokeze ili michakato ya vyama iwaridhie kama wagombea na huku wakiamini hata Mungu wa Mbinguni akiangalia atasema mtu huyo mnayempendekeza ndiye na atawaongoza salama na kwa uadilifu watu wangu wa Tanzania.

Tusiwatizame watangaza nia sura zao, umaarufu wao, ufuasi wao ambao wameujenga, tusitizame tunanufaika nao sasa kwa kiasi gani, kwa maneno mengine tusitizame masilahi yetu binafsi, tulitizame Taifa kwanza. Nina uhakika michakato katika vyama vya siasa inapaswa kuwa huru na inayozingatia haki ya wanachama kuomba nafasi mbalimbali za uongozi. Rai yangu tena bora watoto wa “Daudi” waendelee kujitokeza na huenda mwishoni tutampata Yule ambaye kwa hakika atakuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano.

Kuhusu Vigezo na Sifa za Mgombea

Kwa jinsi utaratibu ulivyo sasa ni kwamba majina ya watangaza nia yatapelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itayapitia na huenda wengine watakwamia hapo kisha baadaye kwenda Kamati Kuu kwa ajili ya uteuzi wa majina matano.

Haya majina matano yatapelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili yaweze kupigiwa kura na kupatikana majina matatu ambayo yatapelekwa katika Mkutano Mkuu ambao nao utapiga kura ili kumpata mgombea mmoja.

Sifa za wagombea urais katika Chama cha Mapinduzi zinafahamika ambazo watangaza nia watapimwa nazo ili mtangaza nia kwa nafasi ya Urais wa CCM aweze kuchaguliwa katika nafasi hiyo. Mbali ya kupitia taratibu za chama, watangaza nia wanapaswa pia kukidhi vigezo na sifa zifuatazo; Mosi, anapaswa kuwa na uwezo wa kuliongoza Taifa kwa kuzingatia uzoefu alionao katika uongozi wa shughuli za Serikali, umma na taasisi.

Pili, awe mwadilifu, mwenye hekima na busara, tatu, awe na elimu ya kiwango cha Chuo Kikuu au inayolingana na hiyo, nne, awe mwenye upeo na uwezo mkubwa wa kudumisha, kuimarisha na kuendeleza Muungano wetu, umoja, amani na utulivu wetu pamoja na mshikamano wa kitaifa.

Tano, awe mtu wa kuona mbali, asiyeyumbishwa, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara kuhusu masuala nyeti na muhimu ya Taifa kwa wakati unaofaa, sita, awe na upeo mkubwa usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi yetu na Dunia yote kwa jumla.

Saba, asiwe mtu mwenye hulka ya udikteka au ufashisti bali aheshimu na kuilinda Katiba ya nchi, sheria, utawala bora, kanuni na taratibu za utawala bora, nane, awe mtetezi wa wanyonge, kusimamia haki za binadamu, mzingatiaji makini wa maendeleo ya raia wote na asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu wake binafsi.

Tisa, awe mstari wa mbele kuzifahamu, kuzieleza, kuzitetea na kuzitekeleza Sera za CCM na Ilani ya CCM ya Uchaguzi, kumi, awe mpenda haki na jasiri wa kupambana na dhuluma, maovu yote nchini, kumi na moja, asitumie nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali.

Kumi na mbili; awe ni mtu anayekubalika na wananchi, kumi na tatu; awe makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa uongozi, watendaji, asiyevumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ili kuinua nidhamu ya kazi, tija na ufanisi.

Uhalisia wa hali ilivyo

Kwanza ile kusema ni watano tu, tayari ni mgogoro, kama tuna makada wanaokaribia 40 kupata watano inaweza kuwa ngumu kama tutajikita tu kwenye vigezo 13. Nikupe Mfano, kuna ile desturi ya viongozi wakuu ambao wameonesha nia kwamba lazima wawemo katika ile tano ya kwanza, lakini pia lazima tuzingatie uwakilishi wa Bara na Zanzibar, kisha ongeza watu wenye makundi makubwa na kwa bahati mbaya ambayo mpaka sasa yameshaanza kujikita kikanda yaani kimakabila. Halafu kuna hoja ya ujinsia, nina uhakika hii inachukuliwa kama hoja ya kujikosha siku hizi. Utagundua ile tano haitoshi.

Lakini hii ya watano ni desturi tu, bado kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kinaweza kuiagiza Kamati Kuu (CC) kuleta majina zaidi na si matano tu, lakini pia Mkutano Mkuu (Congress) unaweza kusema pia kipindi hiki tunataka majina zaidi ili kutoa haki kwa wagombea wengi zaidi badala ya kuwakata mapema.

Ukilitizama jambo hili vizuri utagundua hekima inahitajika zaidi na hasa hekima kwa viongozi watakaokuwa wanafanya maamuzi. Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete nadhani ndiye mtu ambaye ana mtihani mkubwa zaidi, kwasababu kipindi hiki na kwa uzoefu wa hali, hili ni pori jipya na mbinu za zamani zaweza kuwa sio muafaka katika pori hili nene. Makundi ya sasa ni mabaya zaidi kuliko ya mwaka 1995 na zaidi ya mwaka 2005, maamuzi mabaya ama yatatupeleka katika hali mbaya kuliko 2005 au yatahuisha furaha na imani ya Wananchi kwa Chama cha Mapinduzi.

Tukiwatizama watu tutajiingiza katika mtego wa kuogopana, kuoneana haya, ubinadamu ukiingia, haki itaondoka, na maamuzi hayatokuwa katika maslahi mapana ya chama na Taifa kwa ujumla. Nimeanza kusema sema kwa sauti ya chini, karibia wagombea wote hasa wakubwa wanatumia fedha, ni kweli kwamba hawawezi kutumia mawe, lakini kama tuna nia ya kuwaengua waovu waliozidi ambao sio mmoja kwa hakika lazima tutumie utaratibu safi. Kwa haya maneno tunayoyasikia mitaani ya kutumia mbinu za ujanja ujanja, ni dhahiri kwamba mbinu hizo hazitaweza kuwadhibiti wajanja ambao mpaka sasa ni wengi miongoni mwa watangaza nia.

Tuangalie watu wana matarajio gani kwa serikali ya awamu ya Tano, tutizame kero kubwa ambazo zinakera watu wetu. Kisha mtusaidie kwenye vyama vyenu sio kutuletea watu wenye sifa ya kuwa madiwani, wabunge, mawaziri, mawaziri wakuu, makamu wa Rais, wachambuzi wa sera na kadhalika na mkawafanya hao kuwa ndio mnaowapendeza wachukue nafasi ya Urais wa Nchi yetu. Msifanye makosa kudhani kila mtu anaweza kuwa Rais, msifanye makosa na hapa nizungumzie CCM kudhani kwamba maadamu chama kitambeba basi watu watamkubali, la hasha.

Kizazi cha leo kinajitambua, kinapima, kinapambanua, kinachekecha, tuleteeni mtu ambaye, tukimtizama tupate amani ya nafsi na amani kwamba maslahi yetu kama Taifa yatalindwa kwa manufaa ya Wananchi raia wa Jamhuri yetu.

Hasara ya kuleta bora mtu au mtu mwenye sura nzuri, au mwenye mbinu nzuri za wazi au za siri siri ni kwamba Wananchi wataona mmewachukulia nafuu, na adhabu yake hawataitoa kwa mgombea Urais, watawanyima wabunge, na mkumbuke wakiwanyima wabunge mtakuwa serikali boya.

Tupatieni mgombea ambaye akienda kuwanadi wagombea wenu wa udiwani na hasahasa ubunge Wananchi kwa heshima yake mtu huyo watawapeni wabunge wengi pia. Mkidharau ushauri huu, yatawapata ya serikali za mitaa, Mwenyekiti ni wa CCM na Kikao chote ni UKAWA, kama CCM mnaweza msifike huko. Na ninyi watu wa vyama vyenye mawazo mbadala mnafanya kazi nzuri, narudia tena endeleeni kujenga taasisi zenu na kujiimarisha, kwa mujibu wa Katiba ya Mwaka 1977 na inayotumika sasa, mkipata wabunge wengi, mtakuwa na uwezo wa kutoa Waziri Mkuu, mkifika hapo itakuwa ni hatua kubwa kabisa katika historia ya Taifa letu. Hii tama ya Urais ni ya kusadikika, nimeona niwaseme kidogo, pokeeni na mtafakari.

Naomba mrejee Ibara ya 51 ya Katiba inayosema “(1) Kutakuwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais kwa kufuata masharti ya ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais kwa kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge. (2) Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua Mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye Wabunge wengi zaidi Bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye Wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na Wabunge walio wengi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, naye hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za Wabunge walio wengi.


Karibu msome na tujadiliane kwa hoja na sababu.

No comments:

Post a Comment