Kinyang’anyiro
cha Urais-Tanzania iko njia panda
Wengi mtakubaliana
name kwamba kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais kupitia Chama cha
Mapinduzi kimekwenda kwenye kiwango kingine kabi
Wengi wamekuwa na
maswali ya kiuchokozi hapa na pale kwamba unadhani wimbi hili kubwa la wagombea
tafsiri yake ni nini? Nimejitahidi mara zote kusema kuna tafsiri zaidi ya moja,
mosi ni uhalisia kwamba wana CCM wako huru kuweka mawazo yao hadharani, pili,
demokrasia iko pana katika chama kwamba yeyote ambaye anaona anaenea katika
nafasi basi anayo fursa ya kujitokeza na kutangaza nia na hatimaye kuomba
kukubalika na chama.
Tatu, ni kwamba
huenda watu hawajui maana hali ya tafsiri ya urais kama taasisi na Rais kama
kiongozi Mkuu wa nchi na majukumu yake, huenda watu wanauona urais kwa maana ya
kusafiri kila pahala, kufungua miradi, kutoa hotuba, kutoa maelekezo, kupita
kwenye msafara wakati wengine tunasubiri foleni, kutuma watu wakafanye kazi
kana kwamba watu hawajui wanalopaswa kutenda.
Wengine wanadhani
pia ukiwa Rais kazi ya kuwashughulikia wauza dawa za kulevya, kushughulikia
wala rushwa na ufisadi ndio hasa itakuwa kazi yao, hawa nawaona wakitembea na pingu,
bakora za mibungo na magereza yanayotembea ili kila watakaye mbaini basi
watamfunga papo hapo, wapo watangaza nia ambao nikienda kwenye vichwa vya kwa
kutafakari nawaona wakiwaza hivi.
Nne, ni kwamba
huenda kuna watu wahuni pia, watu wasio na mapenzi mema na taifa hili, watu
ambao wamegeuza nafasi ya urais bidhaa ya mnadani. Hawa wako pale kuhakikisha
wanakuwa Rais, haijalishi sote tunajua Urais mtu hupewa kama dhamana na
wananchi, lakini wapo ambao tayari wameshajiona marais, hii ni kuwakosea wapiga
kura, na zaidi kukikosea heshima Chama cha Mapinduzi. Hawa watu wa namna hii
wao hawajali demokrasia kwa maana ya utawala wa watu kwa watu na watu wenyewe
yaani kiingereza “democracy”, watu hawa ni genge la wajanja wachache ambao
wanataka kushika madaraka ya nchi, maslahi yao ya msingi ni wao wenyewe
kiingereza mtindo huu tunaita “mobocracy”.
Kisiasa- Tanzania iko Njiapanda
Wengi wanahoji
dira ya Taifa hili ni ipi? Taifa halina dira, ninaposema hivi wengi mtasema
kwamba mbona tunayo ile inaitwa “vision 2025”, ni kweli lakini ile ni dira ya
Tanzania Bara pekee, na Tanzania Bara si Taifa, utaniambia pia “vision 2020”
nakubali lakini hiyo inahusu Zanzibar pekee, sasa na mimi nitakuuliza je iko vision
moja ambayo inazungumzia Taifa la Tanzania?
Kwanza nikitizama
vision 2020 na 2025 utagundua bado hazina sifa ya kuwa Dira. Dira ni waraka
ambao, Taifa kwa mwafaka limesema huko ndiko tunakotaka kwenda. Ukisoma vizuri
hizi nyaraka mbili kila moja iko huru, nikimaanisha Ukisoma vision 2025
inazungumza kana kwamba Tanzania Bara ndio Jamhuri na Muungano na vivyo hivyo
ukisoma vision 2020 unaona Zanzibar inajizungumza yenyewe kana kwamba ni huru.
Kwangu mimi kitendo cha nchi moja kuwa na dira mbili na zisizosomana ni
sawasawa kabisa na kuwa na ndege moja yenye marubani wawili wasio na uelewa wa
pamoja wa wanakwenda wapi. Juzi juzi hapa kule nchini Ujerumani kitendo cha
kuwa na marubani wawili wasio na uelewa wa pamoja ndege inapaswa kwenda wapi
kilipelekea ajali mbaya kabisa, rubani mmoja anajua tunatakiwa kuwafikisha
salama abiria wakati rubani mwingine ana mipango ya kutoa uhai wa abiria na
yeye mwenyewe kwa kuigongesha kwa makusudi ndege kwenye milima.
Mzee Warioba
alijaribu kututengenezea dira katika Rasimu ya Katiba Toleo la Pili, lakini
Katiba Inayopendekezwa ikasema hata serikali isipofanya chochote katika
utekelezaji wake isihojiwe kokote hata mahakamani na mtu yeyote asiwe na
mamlaka ya kuhoji juu ya utekelezwaji wa dira hiyo, sasa hapo ni dira au kiini
macho?
Taasisi za Mamlaka
ya nchi hasa Bunge ni dhaifu, unakumbuka wakati wa Bunge Maalum wengi ya
wabunge walitaka mikataba isipelekwe Bungeni, baada ya Bunge maalum wakazinduka
wakataka mikataba ya TPDC, wakanyimwa, roho ikawauma sana hata wakatenda
kinyume na mamlaka yao na kuelekeza Polisi iwakamate viongozi wa shirika la
mafuta, walitenda kwa hasira, kiko wapi leo? Kitendo kile kikawafanya watake
mikataba ipitie bungeni kupata ukubalifu, hawa ni wale wale ambao wengi wao
walifuta masharti ya rasimu ya Warioba yaliyosema mikataba ya madini iridhiwe
na bunge.
Wakati Bunge
likiwa na mtanziko wa kimamlaka, hali iko dhahiri shahiri kwamba kuna upungufu
wa utamaduni wa kidemokrasia (democratic culture), tumeacha kuwa watu wa
majadiliano (dialogue), hatujengi hoja bali tunapiga makelele na kushutumiana
wakati wote, Mwalimu Nyerere alipata kusema “argue, don’t shout”. Hatujengi
muafaka, hatufanyi maridhiano, hatuna uelewa wa pamoja katika masuala ya
msingi, hatuna uhimilivu (tolerance) lakini inaonekana tuna uhimilivu kwa mambo
kama rushwa, ufisadi, mauaji ya albino na vikongwe n.k.
Tumeanza kushuhudia roho mbaya ya utengano (negative
devisive force), ukabila, ukanda, udini, ubara na uzanzibari n.k. Umeshuhudia
hata watangaza nia tayari wameanza kujipanga kikanda hii ni hatari kwa ustawi
wa umoja wa kitaifa. Inaanza kuonekana Uongozi si dhamana tena bali mali ya
watu fulani. Utumishi wa umma unafanya kazi kwa woga. Maadili ya Taifa, binafsi
na ya viongozi ni tatizo kubwa, hata pale sekretarieti ya Maadili ya viongozi
inapowafuatilia wale wanaokiuka miiko ya uongozi utagundua nguvu zake zina
ukomo mkubwa.
Kuongezeka kwa vitendo vya Rushwa, ufisadi na
mmomonyoko wa maadili, angalia namna ambavyo watangaza nia wanatumia fedha
nyingi, swali la kujiuliza ni fedha zao binafsi? Na kama si zao waliowapa wana
maslahi gani na nafasi ambayo watangaza nia hawa wanaitafuta? Muungano wetu
bado una changamoto nyingi, Serikali 2 hazieleweki, sio tu kwenye Katiba ya
1977 bali hata kwenye Katiba Inayopendekezwa. Watu wa Tanzania Bara wanauona
Muungano kama mzigo na watu wa Tanzania Zanzibar wanauona Muungano kama Kero.
Kuvurugwa kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ni huzuni nyingine inayoongeza
njia panda ya kisiasa
Kiuchumi- Tanzania Njiapanda
Umma wa watanzania hauna mali za pamoja,
tulibinafsisha kila kitu na mashirika ya umma yaliyosalia ni hohehahe, mfano ni
shirika la ndege la Taifa “Air Tanzania”, shirika la reli (TRL) ni shida
nyingine kubwa licha ya kwamba tuna ubia na watu wengine. Tuna shirika la
nyumba (NHC), hili linakimbia kwa kasi baada ya maboresho makubwa ya
kiutendaji, lakini nawapa indhari kwamba uchumi wa Marekani ulianguka kwa
uwekezaji usiotabirika katika makazi na nyumba, tuwe macho.
Sekta binafsi ni dhaifu, sekta binafsi imeingia katika
huduma na si uzalishaji, tizama kampuni ambazo zinaonekana vinara ni makampuni
ya simu. Haya hayazalishi, haya yanatoa huduma na yanachukua pesa za watanzania
masikini zaidi kuliko hata faida ambayo tunanufaika nayo moja kwa moja kama
wananchi masikini na wasio na ajira.
Angalia ongezeko kubwa la mabenki, unadhani
wanufaikaji ni wakulima na wafanyabiashara ndogondogo ambao kwa kiasi kikubwa
wanaangukia katika sifa za watu wasio kopesheka, Tuamke, benki ni nzuri lakini
lazima tuwe na uchumi ambao unabeba watu wake.
Hakuna viwanda vya kutosha vya uzalishaji
kunakopelekea tatizo la ajira na kupoteza fedha za kigeni (hakuna exports za
kutosha), mchele wa mbeya na kwingineko tunao lakini tunaagiza, sukari ya
kutoka Mtibwa, Kilombero na Kagera tunayo lakini tunaagiza, tunayo gesi lakini
bado tunaagiza mafuta mazito. Halafu dola ya kimarekani ikifika zaidi ya
shilingi 2000 tukiuliza tunaambiwa huko duniani dola imeimarika zaidi, kweli?
Sekta binafsi iliyo dhaifu haiwezi kusimamia
demokrasia na kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwepo. Na hapa niwaseme
kidogo Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwamba wameona Bunge Maalum
lilivyoendeshwa na namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imedhoofisha maadili ya
viongozi na kuvuruga Dira ya Taifa kwa kuiwekea vikwazo, lakini kwani umesikia
wakikemea au wakishauri kitaalamu madhara ya kubomoa misingi ya maadili na
uwajibikaji katika Katiba? Nawapa changamoto, na wao wajitafakari.
Mkazo haujawekwa katika uchumi wa kujitegemea
unaozingatia ukuaji wa kilimo kinachotoa malighafi kwa ajili ya viwanda ambavyo vinachakata
malighafi kuwa bidhaa zilizochakatwa au bidhaa kamili ambazo ziko tayari kurudi
na kutumika katia sekta nyinginezo ikiwemo kilimo
Kukosekana kwa uchumi imara unaojitegemea kunazalisha
watu masikini wengi zaidi katika Taifa letu. Tuna walipakodi wachache na tuna
walaji wengi katika Taifa lakini pia mianya ya wanaokula zaidi yaw engine
kinyume cha sheria ni wengi zaidi na kusababisha chakula wanachokusanya
wachache wetu ama kinaliwa na wachache wetu kinyume na sheria na matokeo yake hakitoshelezi
mahitaji yetu kama Taifa. Tunalo pia Tatizo la kuwa na vyanzo mbadala mbali na
hivi vya sasa vya mapato ya Taifa na Serikali, na bado tunalo tatizo la
Makampuni ya madini kutokutoa kodi ya mapato kutoka faida zao.
Wengi wanasema wanatoa kodi lakini ni kodi wanazokatwa
wafanyakazi wao na sio kodi inayokatwa kutokana na shughuli za ushalishaji wa
makampuni. Kwenye gesi ni eneo linguine ambalo ukiachia kwamba limegubikwa na
sintofahamu juu ya namna mikataba yake imefungwa hasa katika ngazi ya utafutwaji
wa gesi ni kizungumkuti kingine kinachotuweka kwenye njiapanda kama Taifa.
Rais tunayemtaka
Awamu ya Tano
Tunataka Rais ambaye anajua tuko njia panda, ana ana
uwezo na mamlaka ya kukemea kwasababu na yeye ni mwadilifu “moral authority”.
Tunataka kiongozi ambaye anakubalika na jamii na jamii inamwona kama sehemu ya
majibu ya changamoto zao. Hatutaki watu wajitembeze kwetu, tunajua tunataka
Rais ambaye atasimamia masilahi yetu.
Leo karibu kila mtia nia, nasikia huyu kapata pesa
kule, huyu kapata pale, huyu hela za wizi, huyu kapokea hela chafu, huyu
kachukua za watu wabaya na kadharika. Watanzania tuache ushabiki, tusimame na
tuwe wamoja katika hili. Rais wetu akiletwa na watu maana yake si wetu ni wao.
Tafakari
Great Job kaka keep it up
ReplyDeleteKijana upo vinzuri, naomba nipate namba yako ili ukipata mda tukuombe kundi letu la CHADEMA vs CCM lijifunze jambo toka kwako
ReplyDelete0786146700 Karibu
ReplyDelete