Wiki hii joto
katika Chama cha Mapinduzi litazidi kuongezeka kadri makada zaidi
wanavyopambanua nia zao za kuomba ridhaa ya chama ili washike bendera ya CCM
katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo Oktoba 25 mwaka huu.
Joto hili
halitakuwa mahali pamoja, bali kila kona ya Taifa letu, hasa hasa upande wa
Tanzania Bara, kule Kaskazini Mashariki, Arusha, Kaskazini kanda ya ziwa,
Mwanza, Nyanda za juu kusini, Mbeya na kule kusini mwa Nchi Lindi. Kwa CCM hizi
ni ishara njema kwamba kuna watu na kupitia michakato ya kidemokrasia ndani ya
chama watu wanajipambanua, lakini chama kisipokuwa makini hii inaweza kuwa
dalili isiyokuwa njema, dalili ya mvurugano, dalili ya mpasuko na kugawanyika
kwa chama.
Katika Makala hii
nataka nieleze kwa sehemu, na kwa mtizamo wangu nimuonavyo Rais wa awamu ya
tano ukizingatia nafasi ambayo Marais wa awamu nne zilizotangulia michango yao
imekuwa kwa Taifa letu. Ni muhimu kwa wagombea kujitathmini nafasi zao, dhamira
zao na mipango yao ili kukidhi mahitaji ya watanzania sasa lakini pia
watanzania wanatakiwa pia watambue kila awamu kwa bahati imekuwa na utume wake.
Watanzania pia na hasa katika hatua hii wanachama wa CCM wanatakiwa watambue
utume unaotakiwa katika awamu ya tano ili waweze kuwapima wagombea kama wana
sifa, uwezo, mamlaka, uhalali na dhamira ya kutupatia uongozi wa kutimiza utume
wa awamu ya tano.
Ili tuweze kumuona
Rais wa awamu ya tano, tuna budi kuelewa utume wa awamu nne zinazotangulia kwa
ufupi,-
Awamu ya Kwanza- JK Nyerere
Mwalimu katika nchi
yetu ndiye alikuwa na dhamana ya kukata pori na kuianzisha nchi pamoja na
sambamba na mashujaa wengine wengi raia wa Taifa letu. Mwalimu alikuwa na kazi
ya kwanza kuleta Uhuru wa Tanganyika na baadaye, yeye na Sheikh Abeid Aman
Karume kuunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ili
kuunda Nchi Mpya Mwaka 1964 ambayo sasa inajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mwalimu alikuwa na kazi ya kulijenga Taifa awali, kuwaleta watu pamoja,
huku akiheshimu makabila ya watu na mtawanyiko wa makabila katika Tanzania mpya
lakini akiupinga na kuutokomeza kwa kiasi kikubwa ukabila.
Kisha akawa na kazi
ya kuliunganisha Taifa kuwa kitu kimoja, akatusaidia kukuza utanzania na
akasimamia lugha ya Kiswahili kama lugha ya Taifa. Akahakikisha kuna amani na
Umoja na ili hayo yaendelee akajenga misingi imara na thabiti ya haki na usawa
miongoni mwa watu wetu.
Akajua amani na
Umoja utakuja kama haki itatendeka, kutakuwepo usawa wa watu na wa kimaeneo
hivyo akaanza kwa sehemu kufanya majaribio ya kujenga na kuimarisha uchumi.
Akatizama uzalishaji katika ngazi zote, katika ngazi ya Taifa akawezesha dola
kushika hatamu katika uchumi kwa maana ya uzalishaji, kutoa huduma na kukusanya
kodi. Katika ngazi za msingi akaanzisha vijiji vya ujamaa, watu wafanye kazi
kwa pamoja, wazalishe pamoja na wanufaike pamoja na matokeo mazuri ya kufanya
kazi kwa mshikamano. Akailinda nchi dhidi ya maadui wa ndani na wa nje.
Alitenda kwa sehemu yake mpaka alipomwachia kijiti Mhe. Alhaji Ali Hassan
Mwinyi.
Awamu ya Pili- Alhaji Ali Hassan Mwinyi
Mhe. Mwinyi
alichukua kijiti wakati nchi ilikuwa bado imara kwa maana ya Umoja, mshikamano,
Amani na utulivu, lakini kiuchumi nchi ilikuwa imetetereka sana. Uchumi
ulioshikiliwa na dola ulikuwa umelemewa na mahitaji wananchi na utendaji wake
haukuwa wenye ufanisi mkubwa. Tulikuwa na udhaifu wa ndani kwa maana ya
kutokuwajibika miongoni wa watendaji na Wananchi lakini pia tulikuwa na shinikizo
kubwa kutoka nje hasa mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa.
Mzee Mwinyi alikuwa
na kazi ya kufungua milango ili kila anayeweza kuzalisha basi asaidie kazi ya
serikali ya uzalishaji ili chakula na bidhaa ziwafikie watu wa Taifa letu.
Kidogo kidogo akaanza kuufanyia marekebisho mfumo wa uchumi wetu kutoka uchumi
inaoshikiliwa na dola kwenda kwenye uchumi huria ambao watu na wadau mbalimbali
ni washiriki katika kufanya shughuli za uzalishaji na kutoa huduma. Lakini pia
akawa mkali kwa wale ambao hawakuwa wawajibikaji, utakumbuka kipindi kile nyimbo
maarufu zilikuwa kama vile “usipowajibika ole wako, utakumbwa na fagio la
chuma”. Aidha akawapa hamasa Wananchi kwamba kwa hali tuliokuwa nayo kipindi
kile ilikuwa budi sote tushikamane, utakumbuka misemo kama “Wananchi sote
tujifunge mikanda”.
Ni kipindi hiki
Taifa lilianza kuona huduma za kijamii sasa zikianza kutolewa na mashirika
yasiyo ya kiserikali, huduma za ughani katika kilimo, mifugo na uzalishaji
mdogomdogo. Ni katika kipindi hiki asasi mbalimbali zilianzishwa na kusajiliwa
ili ziisaidie serikali katika kujenga Taifa.
Ikawa ni dhahiri
kwamba awamu ya pili ilikuwa ya kujenga mfumo mpya wa uchumi kwa Taifa letu na
ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa unaendana na mahitaji ya wakati na dunia. Mzee
Mwinyi akaweka misingi ya uchumi huria, tuliyumba yumba kidogo lakini ilikuwa
mwanzo. Kubwa zaidi Mzee Mwinyi akaimarisha pia misingi ya demokrasia, katika
awamu ya pia tukaondoa mfumo wa demokrasia ya chama kimoja na kwenda katika
mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Mfumo huu uliongeza uwajibikaji, ushiriki
wa mpana wa Wananchi katika uongozi wa nchi na uwazi katika shughuli za
serikali.
Mzee Mwinyi
alitenda kwa sehemu yake mpaka Mhe. Benjamin W. Mkapa alipopokea kijiti.
Awamu ya Tatu- Mhe. Benjamin W. Mkapa
Mhe. Mkapa, alikuwa
na kazi moja kubwa, kuimarisha hatua zilizopigwa na awamu ya pili hasa katika
kuendelea kuupanga na kuuimarisha uchumi wetu katika mfumo mpya tuliouchukua.
Serikali ya Awamu ya tatu chini ya uongozi wa Mzee Mkapa ilijikita katika
kuhakikisha kuna “transition” nzuri kutoka uchumi uloshikwa na dola awali
kwenda uchumi huria ambao umeshikwa na watu katika sekta binafsi. Kipindi chake
kilikuwa na kazi kubwa ya marekebisho ya kimfumo na kitaasisi, wengi wenu
mtakumbuka Tume maarufu ya “Parastatal Sector Reform Commission (PSRC)” ambayo
ilianzishwa kwa sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992 na kazi kubwa ilikuwa
kufanya ubinafsishwaji wa mashirika ya umma.
Mzee Mkapa katika
ujenzi wa uchumi huria imara alisimamia uwazi na ukweli hasa kipindi chake cha
kwanza, alipiga vita na alichukizwa na rushwa. Hata katika kampeni zake za
Urais alitoa ahadi ya kupambana na rushwa, baada ya ushindi mwaka 1996 aliunda
Tume ya Kupambana na Rushwa iliyojulikana kama “Tume ya Warioba”. Kwa hakika
kulikuwa na matatizo ya hapa na pale tena mengi tu, lakini sote tunakubaliana
kwamba Mzee Mkapa alituimarishia uchumi wetu katika mfumo wa soko huria. Uchumi
Mkubwa ulikuwa unakuwa mpaka anaondoka kwa asilimia karibu saba. Kazi aliyokuwa
ameiacha haijatimia ilikuwa ni kuutafsiri ukuaji wa uchumi mkubwa ambao ulionesha
mafanikio makubwa katika maisha ya watu wa Kawaida. Kazi hiyo ilikuwa sasa ni
ya Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete Rais wa Awamu ya Nne ambaye alipokea kijiti.
Awamu ya Nne- Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Awamu ya nne kama
ambavyo ilivyojinasib wakati wa kampeni zake wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka
2005 kwamba “Maisha bora kwa kila Mtanzania”. Ukiitafsiri kauli mbiu hii
utakubaliana nami, uongozi wa awamu ya nne ulikuwa na kazi ya kutafsiri uchumi
Mkubwa (Macro) kutokana na tija itokanayo na viwanda na uwekezaji mkubwa kwenda
uchumi wa kati (Meso) katika jamii zetu na kisekta kama vile kilimo (Kilimo
Kwanza), elimu (shule za Kata) na hata tushuke kiuchumi hadi ngazi ya mtu wa
kawaida (micro) hapa ndio tungeona uhalisia wa maisha bora, watu wenye nyumba
nzuri, ajira zenye staha, kipato chenye kukidhi mahitaji na watu
wanaokopesheka.
Awamu ya nne
imekuwa na jukumu la kuendelea kujitahidi kugawa keki ya Taifa katika mazingira
na uhalisia tofauti tofauti, kama vile ujenzi zaidi wa barabara, uwekezaji
zaidi katika elimu na kilimo. Nchi inapofika katika kiwango cha kuanza kugawa
keki ya Taifa huwa inafanya hivyo baada ya kunufaika na ukuaji mkubwa wa
kiuchumi na huwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha kwamba ugawaji wa keki
unaenda sambamba na jitihada za kuendelea kukuza na kuuimarisha uchumi mkubwa.
Awamu ya nne
imeendelea pia kushughulikia pia ujenzi wa demokrasia na kuimarisha mifumo ya
udhibiti na kuweka ukomo wa matumizi ya madaraka kwa watumishi na viongozi wa umma,
hili mpaka sasa halijakamilika. Mifano ni maboresho mbalimbali ya kitaasisi
katika serikali, kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya ambayo ungehakikisha
ugawanaji wa keki unawanufaisha wengi na sio makundi ya wajanja wachache, hili
halijakamilika.
Utagundua pia
katika awamu zote nne, kimsingi tuna kila kitu ambacho kama nchi inahitaji ili
kupiga hatua. Kwa mtizamo wangu kilichobaki ni kufanya sasa marekebisho ya
mifumo na taasisi na fikra za watu (Wananchi, watumishi na viongozi wetu) na
kuhakikisha wote waliopewa dhamana wanatenda hivyo kwa uadilifu na wakijua
wakipotoka watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na kamwe hawatakaa juu ya
sheria.
Awamu ya Tano- Nimuonavyo Rais huyu (…)
Namuona Rais wa
awamu ya akisheheni haiba ya uadilifu, mtu asiyejikweza, mwenye kukubalika na
watu, mwenye “moral authority” yaani mtu mwenye uwezo na mamlaka ya kukemea
wezi, watu wasio na uadilifu. Mtu ambaye anatambua kwamba mafanikio yote
tuliyoyapata katika awamu zote nne hayawezi kutimia pasina kuwa na mifumo ya
udhibiti “systems and controls” inayofanya kazi katika taasisi zetu kutoka
ngazi ya kitaifa mpaka mtu mmoja mmoja.
Kuna kipindi katika
historia za dini kuna kitu kiliitwa “reformation” au matengenezo, tumefika
pahala ambapo tunahitaji Kiongozi ambaye atakuja kufanya matengenezo,
marekebisho na maboresho kuanzia ikulu hadi katika jamii zetu. Baada ya kipindi
cha reformation kupita sasa nitawaona wajenzi wa barabara, wajenzi wa shule,
waboresha kilimo na huduma za afya. Kwa sasa tunataka mtu wa kuja kutunyooshea
njia, kuturudishia maadili ya Taifa, Maadili ya utumishi na Uongozi wa Umma,
kutujengea mifumo na taasisi imara na madhubuti ambazo zitahakikisha kuna
uadilifu na uwajibikaji katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Rais ajaye
nimuonavyo ni yule ambaye anajua watanzania wameshaibiwa sana, vijana wanasema
tumeshapigwa sana. Kilimo hakikui kwasababu kuna watu wananufaika na kuagiza
mchele kutoka nje. Kilimo cha sukari hakikui kwasababu kuna watu wana mirija ya
chuma katika kuagiza sukari kutoka nje. Reli ya Kati inadororora kila siku
kwasababu watu wana maslahi na biashara ya maroli. Tunataka Rais ajaye aje na
aanzie hapo kutuwekea mifumo ya kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka.
Tunataka Rais ajaye
Kiongozi akila rushwa hatasubiri akemewe atajiondoa mwenyewe haraka. Tunataka
baba, Kiongozi, mtu ambaye tukimtizama tutakuwa na amani na maisha yetu,
tunamtaka mtu ambaye sasa anaonesha kupenda heshima ya Wananchi. Tunamtaka mtu
ambaye atarudisha heshima ya cheo cha msingi ambacho ni “Raia”. Tunamtaka mtu
asiyejipeleka kwa “wazi” au kwa “kificho”, kwa “kelele” au “kimya kimya”.
Mwisho tunamtaka na
nimwonavyo Rais wa Awamu ya Tano, ni mtu mwenye uhalali, mtu anayekubalika
katika pande zote za Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mtu
ambaye kwasasa Wananchi wanajinasibisha naye, kwasababu anawajua, na wanajua anajua
mahitaji yao. Mtu ambaye amesimama nao bega kwa bega na ambaye hajaona aibu
kusimamia maslahi yao wakati wowote.
Naomba mnitegulie
kitendawili.