Tujadiliane kwa HOJA na Sababu
Kuelekea
uchaguzi Mkuu 2015 mabadiliko ni
miongoni mwa mambo yanayochukua nafasi kubwa katika kampeni na ilani za vyama
vya siasa. Hoja nyingi zinatolewa hususani katika dhana ya mabadiliko ya mfumo
au kiongozi au yote mawili yaani mfumo na uongozi. Kwa bahati mbaya watanzania
hawaelezwi mahusiano kati ya mfumo na viongozi. Mbaya zaidi wengi wetu
tumeporwa uwezo wa kutafakari kutokana na kuzamishwa kwenye mahaba kwa wagombea
au vyama vya siasa.
Kwa
kuwa bado kuna siku zaidi ya arobaini ni vyema tukawatafakari baadhi ya
wagombea wa nafasi ya uraisi ambao ndio hasa wanachuana vikali katika kampeni
zinazoendelea. Yapo mambo kadhaa
yanayoweza kutuongoza katika kuwapima wagombea na sera zao. Moja, ni kutafakari
kama inatosha kuwa mashabiki wa matamko tu yenye kushawishi juu ya kuleta
mabadiliko kama ambavyo baadhi ya
wanasiasa wameendelea kuwalaghai wananchi kipindi hiki cha kampeni za uchanguzi
mkuu 2015.
Muhimu
sana ni kupima nia na zaidi sana uwezo
wa kiongozi husika kutafsiri madhui ya
ahadi zake katika vitendo. Hasa kwa
kuzingatia ukweli kwamba wameibuka
wanasiasa wanaotoa matumaini hewa kwa wananchi kwa kusema tu yale ambayo
wananchi wangependa kusikia. Ni jambo jema kuwajengea wananchi matumaini lakini
ni hatari pia kuwalaghai wananchi kwa mambo ambayo kiongozi husika sio tu yeye
mwenyewe hayaamini au hana uwezo wala dhamira ya dhati kutimiza. Maswali mawili
ni muhimu kuulizwa katika hili, moja ni mfumo gani unaolengwa kubadilishwa ili
kuleta mabadiliko ya kweli kwa watanzania? Je viongozi husika wanavyo vigezo,
uwezo na uzoefu katika kujenga mifumo
endelevu?
Edward Lowasa na dhana ya mabadiliko ndani
ya UKAWA
Tukianza
na kambi
ya UKAWA inayowakilishwa na Edward Lowasa, tukivipima vyama vya siasa vinavyounda
UKAWA kwa mifano na kutafuta vielelezo vya kimfumo inaonekana dhahiri kuwa aidha hakuna kabisa mifumo bali haiba (personalities) au kuna baadhi ya viashiria vya kuwepo kwa
mfumo lakini kutoka na kujengwa kwenye misingi dhaifu mifumo hii imekuwa sio
endelevu. Pengine kwa kutambua udhaifu huu UKAWA imefungua milango kupokea
baadhi ya wanasiasa ambao wamewahi
kuongoza nchi yetu katika nafasi kubwa za uongozi kama ile ya Waziri Mkuu. Hawa
ni pamoja na Edward Lowasa ambae ndio mgombe uraisi na Fredrick Sumaye .
Hata
hivyo ukiwauliza au hata ukijaribu
kutafuta na kupima jambo gani la kimfumo waliwezakulifanya katika nafasi
zao? Kinachojitokeza ni aidha viongozi
hawa hawakuwa na uelewa sahihi wa masuala ya kimfumo hivyo kushindwa kufanya
uchambuzi sahihi wa matatizo ya kimfumo na kuyapatia majawabu ya kiutendaji. Mara
nyingine walidandia miradi ya maendeleo
na kuisukuma kwa mabavu bila kuweka misingi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na
kujenga taasisi imara kutekeleza na kusimamia sekta husika mambo
hayo licha ya kuwa mazuri yaligeuka kusongwa na changamoto nyingi.
Mbaya
zaidi viongozi hawa na wengine wanaofanana nao walitumia nafasi zao
kujinufaisha wenyewe ikiwa ni pamoja na kujenga mitandao ya kukwapua fedha za
umma kwa maslahi yao binafsi na washirika wao. Kinachopaswa kuogopwa sana na
Watanzania ni ile hulka ya viongozi hawa kutaka kujilimbikizia mali kwa namna
yeyote ile. Hawa ni miongoni mwa viongozi
ambao wamediliki hata kusema kuwa wakichaguliwa kuongoza nchi hii watatengeneza
kundi la aina fulani ya matajiri ambao
wataendesha uchumi wa taifa letu.
Swali
la kujiuliza ni kama huu ni mkakati wa kimfumo na je haya ndio mabadiliko
ambayo Watanzania watarajie? Hii ni dhana hatari inayolenga kuchochea
kuongezeka kwa tabaka la maskini na matajiri. Ni muhimu kutambua kuwa matajiri
kazi yao kubwa ni kutengeneza faida kutokana na mitaji yao. Haishangazi kuona
kuwa matajiri hawa wanaotajwa na mmoja wa wagombea wa uraisi kuwa ni “marafiki”
zake wamekuwa wakifadhili harakati za mgombea huyo kuingia madarakani kwa zaidi
ya miaka kumi iliyopita. Jambo jingine la kujiuliza ni Je kwa uwekezaji huu
matajiri hawa wanatarajia kuvuna nini? Wasiwasi wangu ni kwamba chondechode
mgombea huyu asijekuwa ameweka rehani rasilimali za nchi hii na ikiwa ni pamoja
na maisha ya watanzania ili tu atimize ndoto yake ya kuwa raisi wa inchi.
Rai
yangu ni kwamba Watanzania tufungue fahamu zetu kipindi hiki cha kampeni na
kupima wagombea na hoja zao pasipo
ushabiki na ushawishi mwepesi. Naelewa vyema haja ya kufanya mabadiliko lakini
tujiulize ni mabadiliko ya aina gani tunahitaji. Haifai kabisa kumkubali
mgombea hana kabisa vigezo vya kuleta mabadiliko eti tu kwa sababu tunataka
mabadiliko. Mgombea ambae hana uwezo wala uthubutu wa kukemea ufisadi hatufai kabisa hasa kwa kuzingatia hulka za
kifisadi ambazo zimeshamiri katika jamii yetu sio tu kwenye sekta ya umma bali
hata sekta binafsi. Ni nani asiefahamu kuwa ufisadi uwe mkubwa au mdogo ni
kikwazo kikubwa katika maendeleo na ustawi ya nchi yetu.
Je
ni mara ngapi tumesikia mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA akiweka
bayana mkakati wa kupambana na ufisadi?
Ni nani asietambua kuwa ajenda ya mapambano dhidi ya ufisadi ndio iliyowafanya
wananchi wengi kuvutiwa na sera za CHADEMA hususani chini ya Uongozi wa Katibu
Mkuu wa zamani wa chama hicho Dr. Wilbroad Slaa? Tujiulize kwanini vita dhidi ya ufisadi sio tena hoja kubwa kwa
CHADEMA na UKAWA mara tu baada ya kumpitisha Edward Lowasa kupeperusha bendera
ya chama hich na umoja huo katika nafasi ya urais kwenye uchanguzi Mkuu.
Zaidi
sana tujiulize ni kwa nini Edward Lowasa anapata kigugumizi kukemea ufisadi?
Tumhoji atawezaje kutekeleza ahadi zake lukuki za mabadiliko bila kuwa na haki
na uthubutu wa kukemea ufisadi? Atahakikishaje huduma za jamii zinapatika kwa
wananchi wote, elimu burekwa wote mpaka chuo kikuu, na kuongeza tija kwenye
sekta mbalimbali za uzalishaji bila kudhibiti mianya ya ufisadi? Au anaikwepa
vita dhidi ya ufisadi kwa sababu anajua ni kupitia ufisadi pekee hasa kwa njia
ya manunuzi na mikataba feki ndio anaweza kulipa hisani kwa marafiki zake
wanaoendelea kufadhiri mradi wake wa kuingia Ikulu. Nachelea kusema kuwa kwa
Edward Lowasa uraisi ni mradi wakunenepesha mitaji ya matajiri wanaojiita
marafiki zake ambao sasa wamekaa mkao wa kula. Sioni dalili za mabadiliko
chanya yanayowezakutokana na kiongozi wa aina hii kwenye nchi yetu kwa
kuzingatia muktaza tulionao kijamii, Kisiasa na kiuchumi.
Wapo
wanaosema eti kwa sababu ajenda ya ufisadi ipo ndani ya Ilani ya CHADEMA ambayo
pia inanadiwa na UKAWA, hivyo ikitokea Edward Lowasa akashinda atalazimishwa na
ilani hiyo kukemea ufisadi. Wachambuzi hawa wanawezakuwa sahihi endapo wafanya
tathmini ya taswira ya uraisi anaoutamani Edward Lowasa na ukweli kwamba
ataapishwa kama Edward Lowasa. Hasa kwa
kuzingatia Katiba ya sasa ni dhahiri kwamba atakapoingia tu madarakani sioni
kama CHADEMA watakuwa tena na nguvu ya kumdhibiti.
Tusisahau
pia kuwa ni CHADEMA na UKAWA ndio walimbembeleza Edward Lowassa kujiunga nao na
ni dhahiri kwamba sharti ambalo aliwapatia ni kumpitisha yeye kugombea uraisi.
Kana kwamba haitoshi kampeni za mgombea uraisi kupitia CHADEMA na UKAWA
zinafadhiliwa kwa asilimia kubwa na Edward Lowassa na Marafiki zake. Maana yake
ni kwamba watakapoanza kutaka kudhibiti utekelezaji wa mradi wake wa
kunenepesha mitaji ya mafisadi waliofadhili safari yake kuingia Ikulu
atawauliza swali dogo tu mnategemea nitalipaje madeni ya kampeni za uchaguzi?
Kwa kuufahamu ukweli wa mkataba kati ya viongozi wa CHADEMA/UKAWA na Edward
Lowasa lakini pia kwa madaraka makubwa atakayokuwanayo kama raisi wakati huo
hawataweza kumdhibiti.
Wapo
wanaoweka imani kwenye uwezekano wa kubadilisha katiba ili pamoja na mambo
mengine kupunguza madaraka ya raisi. Ufahamu wangu juu ya uwezo wa watu binafsi
kufanya mabadiliko na kiwango cha mabadiliko huchangiwa sana na historia ya
muhusika na kundi/kizazi/tabaka anakotoka. Kwa mfano mara nyingi wazee ni
hawapendi madiliko hasa yale yanayokinzana na matakwa yao. Simuoni mzee Edward
Lowasa katika umri wake eti anatakakuleta mabadiliko ya kasi hasa ukizingatia
yeye ukiacha majanga ya kisiasa aliyokutana nayo yupo katika tabaka la
matajiri.
Dkt. John Pombe Magufuli na Mabadiliko ndani
ya CCM
Watanzania
wengi bila kujali itikadi na nafasi zao wamewahi ama kusikia, kukiri, au kuthibitisha kwa vitendo
kuwa Dkt. Magufuli ni kiongozi shupavu,
mwenye dira na uwezo wa kubadili mifumo
na utendaji katika sekta mbalimbali.
Hii inathibitika wazi pale watu wanapoamua kufanya tathmini sahihi ya utumishi
wa kiongozi huyu kwa kuangalia utendaji
wake na mafanikio yaliyofikiwa na sekta au taasisi ambazo Dkt Magufuli amewahi
kuzisimamia. Hapa ni vigumu kupinga
ukweli kwamba Dkt magufuli ndiye aliyeleta mabadiliko na maboresho katika sekta
ya Ujenzi hususani wa miundo mbinu ya barabara.
Maeneo
mengine ambayo Dkt Magufuli ameacha
mbegu ya maboresho ni katika
sekta ya ardhi pamoja na ile ya mifugo na uvuvi
licha ya kuzitumikia sekta hizi kwa muda mfupi kabla ya kurejea tena
kwenye sekta ya Ujenzi. Taswira ya sasa ya sekta ya ujenzi ambayo sio tu kwamba
ina mifumo bayana na thabiti licha ya changamoto kadhaa, sekta hii inasimamiwa
na taasisi madhubuti ambazo zinalenga kutafsiri dira na mikakati ya sekta
katika uhalisia na vitendo.
Akiwa
Naibu wa waziri wa ujenzi katika serikali ya awamu ya tatu, ni Dkt. Magufuli
ndie alibadilisha mfumo wa kutegemea wahisani kwa asilimia miamoja katika sekta
ya ujenzi wa barabara.Mfumo huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa
takwimu za wizara ya Ujenzi, takribani asilimia sabini (70%) ya miradi yote ya
ujenzi wa barabara inchini inajengwa kwa kutumia fedha za serikali. Ni asilimia
thelasini pekee ya miradi yote ya ujenzi inafaddiliwa na wahisani. Swali la
kujiuliza ni je nini kimefanikisha utelekezaji wa mfumo huu? Hapa ndipo
unawezakuona uwezo na uzoefu wa kiongozi katika kubadili mfumo kwa kujenga
taasisi zinazotakiwa ili kusimamia na kuendeleze mfumo. Ni Dkt. John Pombe Magufuli ndie alieanzisha
harakati za maboresho katika usimamizi, utekelezaji na uendelezaji wa sekta ya
ujenzi nchini.
Kiongozi
huyu amesimamia kuanzishwa kwa taasisi kadhaa muhimu katika sekta ya ujenzi
ambazo ni pamoja na Mfuko wa barabara (Road Funds) ambao mapato yake
yameongezeka kutoka shilingi bilioni 73.08 mwaka 2005/2006 hadi shilingi
bilioni 751.7 mwaka 2014/15. Taasisi nyingine ni pamoja na Wakalawa barabara (TANROADS)
inayosimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja. Pia zipo
taasisi kama Wakala wa Majengo Tanzania (TBA); Board ya Usajili wa Wahandisi
(ERB); Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRD na Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa
Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB). Taasisi zote hizi zinalenga kutelekeza
majukumu tofauti lakini yanayotegemeana katika ustawi wa sekta ya ujenzi. Hapa
unaweza kuona mantiki ya ujenzi wa mfumo sio hisia wala propaganda.
Mifano
hii michache ni kielelezo cha uzoefu, dhamira na upeo, na umakini wa kiongozi
katika kuchambua, kuamua na kusimamia
mambo miradi ya maendeleo. Ni mgombea Dkt. John Pombe Magufuli ndie ambae
amembanua wazi dhamira na mikakati yake kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Huyu sio
tu kwamba anasema dhahiri kwamba
atafungua mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi lakini pia
uzoefu katika wizara alozitumikia una akisi dhamira hii.
Ni
vigumu kupinga ukweli kwamba hatua ambayo nchi yetu imefika inahitaji kiongozi
ambae sio tu anapenda kusema kile ambacho watanzania wanapenda kusikia bali
kile watanzania wanachohitaji yaani Kiongozi mwenye uwezo wa kurejesha
uadilifu, uaminifu na uchapa kazi katika sekta zote.