HATUTARUDI NYUMA KATIKA JITIHADA ZETU ZA
KUPINGA UDHALIMU NCHINI
Uhuru
wetu wa kisiasa ni kazi bure pasina kuumiliki na kuudhibiti uhuru wetu wa
kiuchumi
Mageuzi
Makubwa ya Chama na Serikali
Tunapitia kipindi cha tofauti katika
historia ya Taifa letu, kipindi ambacho naweza kukiita kipindi cha mpito, hiki
ni kipindi ambacho tunatoka katika hali moja na tunapaswa kwenda kwenye hali
nyingine ambayo ni bora zaidi.
Kipindi hiki cha mpito kinaongozwa na
kauli mbiu ya CCM Mpya Tanzania Mpya. Ni kipindi ambacho Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kimeamua kujitizama kitofauti, kimeamua kujitafakari na kujihoji, maswali
yafuatayo na kwa ufupi, tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejitizama
mwenendo wake, matendo yake, itikadi yake, siasa yake, dhamira yake, malengo
yake na Imani yake. Kisha Chama kikaenda mbele kikatizama viongozi wake,
nidhamu yao kwa Chama, tabia zao, mienendo yao, matendo yao, na kuoanisha hayo
yote na ahadi tisa za mwanachama wa CCM.
Chama kikachukua muda zaidi kuangalia
sauti za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo mara zote zimeendelea
kuelekeza nini mwelekeo sahihi wa CCM chama ambacho si tu ni Chama kilichopo
madarakani lakini ni Chama kikubwa Tanzania na Afrika.
Tafakuri hii ndefu ya CCM ndiyo
iliyopelekea kuandikwa kwa waraka wa Chama uliopewa jina la “Umuhimu wa kufanya
Mageuzi ndani ya Chama”.
Katika waraka huu wa Mageuzi
inafafanuliwa kwamba kabla ya awamu ya tano, suala la rushwa (ufisadi) limekuwa
ni mzigo mkubwa ambao Chama chetu kimebebeshwa. Pamoja na juhudi kubwa ambazo
serikali ya awamu ya nne ilifanya katika kupambana na rushwa ikiwa pamoja na
kutunga sheria mpya wakati huo, kuiunda na kuiimarisha taasisi yetu ya
kupambana na rushwa na kutunga sheria ya kudhibiti Matumizi ya Fedha za
Uchaguzi wananchi bado waliona Chama chetu kilikumbatia wala rushwa.
Chama baada ya tafakuri jadidi na
shirikishi kikaamua kwa kauli na sauti moja kufanya Mageuzi makubwa
yatakayokitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mwonekano huu hasi mbele ya umma
wa wanachama na wananchi na kuwa Chama ambacho kinamaanisha kwa maneno na
matendo chuki yake dhidi ya rushwa na wala rushwa.
Mageuzi Makubwa yanalengwa katika Chama
chenyewe (CCM) na katika Serikali.
Mwelekeo ni kukifanyia Chama Mageuzi
makubwa katika mawanda ya Kiuongozi, Kimuundo na Kiutendaji. Mageuzi haya
katika mawanda haya matatu yataongeza tija, ufanisi, uwajibikaji, faida,
itapunguza gharama za uendeshaji wa Chama na huduma za wanachama zitaboreka
zaidi.
Mageuzi haya katika Chama msingi wake ni
kukirejesha Chama chetu kwa Wanachama na kuimarisha msingi wa kuwa chama
kinachoshughulika na shida za watu.
Mojawapo ya sababu za hamasa ya Mageuzi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tunaipata kutoka kwa Mwalimu Nyerere katika kitabu
cha Binadamu na Maendeleo katika ukurasa wake wa 18 na 19, Mwalimu anasema “
Kazi ya Chama Cha Siasa kilicho imara ni kuwa kama daraja la kuwaunganisha watu
na serikali waliyoichagua, na kuiunganisha serikali na watu inayotaka
kuwahudumia...”
Mwalimu Nyerere anaendelea kusema katika
kitabu hiki “…Ni wajibu wa Chama kuwasaidia watu kuelewa serikali yao inafanya
nini na kwa nini; ni wajibu wake kusaidia watu kushirikiana na serikali yao kwa
juhudi ya pamoja ili kuundosha umasikini ambao umetulemea. Na ni wajibu wa
Chama pia kuhakikisha kwamba serikali inaendelea kuyajua sana maoni, shida na
matakwa ya watu…”
Aidha Mwalimu Nyerere anatukumbusha
katika kitabu hiki “…Ni wajibu wake (CCM) kuwasemea watu. Pia ni wajibu wake
kuwaelimisha watu na kuwasaidia kuona shughuli za serikali zina maana gani
kuhusu usalama wao wenyewe wa siku zijazo na fursa zao wenyewe za siku zijazo”
Tangu Uongozi wa Awamu ya Tano uingie
madarakani mwaka 2015 kupitia tiketi ya CCM chini ya Ndugu yetu John Pombe
Joseph Magufuli Mageuzi Makubwa yanaendelea kufanyika katika Serikali na
taasisi zake katika maeneo ya utolewaji wa huduma, nidhamu ya ukusanyaji wa
mapato na matumizi ya fedha za serikali, kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya
rushwa hasa ufisadi na uhujumu uchumi, kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya,
kukabiliana na kudhibiti mtawanyiko haramu wa silaha za moto, kuwakabili na
kuwachukulia hatua kali wakwepa kodi, walanguzi, watakatisha fedha na
kushughulika na wote wale ambao kwa matendo yao uchumi wa nchi na ustawi wa
watu wake unawekwa rehani.
Mageuzi haya makubwa hayaji katika sahani
ya fedha mezani, ni kazi ngumu, napenda nikiri ina upinzani mkubwa, iko bayana
kwamba kwa watu wasio wema na wasio na mapenzi mema na maendeleo ya nchi
hawafurahishwi na Mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na katika Serikali.
Tafsiri
ya Mageuzi ya CCM
Baada ya tafakuri kubwa na kusikiliza
sauti za wananchi, CCM imenia na inatenda kwa uhalisia kukirejesha Chama kwa
wanachama. Kuna wakati Chama kilionekana ni pango la maharamia, kila mkwepa
kodi alikuwa na uhusiano na CCM, hili lilichafua sana taswira ya CCM. Taswira
hii mbaya imechafua heshima ya Chama chetu na kukifanya kinuke, lakini idadi ya
kutosha ya wachafuzi wa Chama chetu wamekuwamo ndani ya CCM yenyewe. Baadhi ya
wachafuzi hawa wa taswira na heshima ya Chama chetu ni viongozi katika Chama
chetu katika ngazi mbalimbali.
Kwa msingi huu, Mageuzi Makubwa katika Chama
yanatizama eneo la Uongozi; Chama kinataka aina ya viongozi ambao watanzania
wanawataka. Viongozi wachapa kazi, waaminifu, waadilifu, wanyenyekevu,
wanaochukizwa na rushwa, wanaochukizwa na ubadhirifu wa mali za Chama na Mali
za Serikali, viongozi wasio wabinafsi bali wanaowaweka wanachama kwanza,
viongozi wapole lakini wakali kwa mambo ya hovyo, viongozi wanaoziishi imani za
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Viongozi wanaoziishi ahadi za mwana CCM, viongozi
wasioukamia Uongozi, hawa ni viongozi ambao watakubalika si kwa fedha bali kwa
mienendo yao mema na maono yao ya kiuongozi kwa Chama chetu katika ngazi husika
na kwa umma wa watanzania hata wale ambao sio wana CCM.
Ukiwa na aina hii ya viongozi CCM
inaamini chama chetu kitakuwa imara na madhubuti zaidi na kitasimamia haki za
wanachama na wananchi kwa ujumla. Tukiwa na viongozi wa aina ambayo nimeieleza
kwa uchache hapo juu, hawa ndio wataisimamia serikali kutoka ngazi za msingi
katika Serikali za Mitaa na Vijiji, Serikali za ngazi ya Kata, Serikali katika
ngazi ya Wilaya na Halmashauri mpaka katika Mikoa, Miji na Majiji ya Nchi yetu.
Viongozi wa aina hii, hawahongeki,
hawapokei wala kutoa rushwa, ni wakali sana kwa wote wanaofanya ubadhirifu wa
mali za Chama na Mali za Umma. Viongozi hawa ambao Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kinaendelea kuwapata katika uchaguzi wake wa ndani mwaka huu wa 2017 wanapenda
HAKI na wanaheshimu wanachama wa CCM na wananchi wa Tanzania.
Kama nilivyotangulia kusema viongozi wa
aina hii huzongwa sana, hufanyiwa fitina na hufanyiwa kila aina ya hila. Chama
kimejipanga ipasavyo kuhakikisha ya kwamba haki itasimamiwa ipasavyo, na
majizi, na wote ambao wamekuwa wakijinufaisha na mali za Chama kwa faida yao
kinyume na Ahadi ya Mwana CCM hawatopewa nafasi ya kuwa viongozi katika Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongozwa kwa
Katiba, Kanuni mbalimbali, desturi njema na dhamira na utashi mwema wa viongozi
wetu, chini ya Uenyekiti wa Komredi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Msingi
wa kutokurudi nyuma
Kipindi hiki tunapofanya Mageuzi haya
Makubwa napenda ifahamike wako baadhi yetu ambao watashindwa kwenda na
mwendokasi wa Mageuzi haya makubwa.
Baadhi ya wanaoshindwa kwenda na
mwendokasi wa Mageuzi Makubwa ya CCM ni wale ambao walizoea kuishi kwa mazoea,
kula visivyo vyao, kudhulumu haki za wananchi hasa wanyonge, walizoea
kujimilikisha mali za CCM na kuzifuja watakavyo, walizoea kuwa miungu watu na
kuwadharau wanachama.
Katika historia ya Chama chetu watu hawa
wamekuwapo katika awamu zote, na ni mapambano kuwaondoa, wanachama wanawajua,
dhamira njema ya CCM Mpya inawajua, na hakika Uongozi wa CCM na Vikao vya Chama
vitahakikisha watu hawa wenye inda hawapati Uongozi katika Chama chetu.
Watu waovu wana mitandao yao ya uovu,
tuwakatae, na Chama chetu kimekuwa na desturi nzuri ya kuwakataa, kipindi hiki
tutawakataa tena na kwa sauti kuu. Mitandao imedhoofisha sana Chama chetu,
mitandao ya watu wabinafsi na wanaotaka kukitumia Chama chetu kama kitega
uchumi, mitandao ya kidhalimu haina nafasi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati mwingine hata watu ambao wamepata
kuhudumu katika nyadhifa za Uongozi wanahusika kuhujumu Chama na nchi yetu,
wanatengeneza mitandao na kushirikia na madhalimu, tunawajua, hata utu una
kikomo, hatutawaruhusu kuvuruga Chama chetu.
Shime wanachama msikubali hata kidogo
madhalimu wa kisiasa wakajaribu tena kuteka Chama chetu, walishindwa,
wameshindwa na wataendelea kushindwa. Rai yangu hapa, watu wabaya huwa
hawagombani, maslahi yao ya kidhalimu ni ya kudumu, wanaweza kuonekana hawako
pamoja lakini wanaunganishwa na maslahi yao ya kudumu ya kidhalimu. Hata kwenye
Chama chetu walikuwepo, wameondoka, wamebaki, kazi yetu ni kuwadhibiti
ipasavyo, wameanza kuzungumza, tuwe macho kulinda misingi ya Chama chetu.
Kila mwana CCM asimame kidete, akisemee
Chama, aisemee Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni wajibu wetu kuujuza
umma wa wananchi nini Serikali inafanya na kwa nini.
Tunaupinga udhalimu katika Chama chetu na
tunaupinga udhalimu katika Serikali, sio kazi rahisi lakini tutashinda
kwasababu dhamira yetu ni njema na inasimamia maslahi mapana ya Taifa la
Tanzania na watu wake.
Hata mabwana wakubwa wa dunia tumewaonesha
kwa vitendo kwamba tunamaanisha tunaposema tumechoka kuonewa, tumechoka kuibiwa
kwa makusudi au kwa kuhadaiwa. Nchi yetu ni ya kipekee sana na Mungu
ametubariki na kila aina ya utajiri wa asili na watu wenye mshikamano.
Kijiografia nchi yetu iko katika eneo la
kimkakati katika uso wa dunia. Katika bara la Afrika ni nchi mbili tu ndio
zinatengeneza nyonga ya bara la Afrika nazo ni Tanzania na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo. Hizi ndizo nchi pekee ambazo zinalikata bara la Afrika
katikati na nchi ambazo zina mipaka ya bahari kuu zinazozunguka bara la Afrika
kwa maana ya Bahari ya Hindi upande wa Mashariki inayopakana na Tanzania na
Bahari ya Atlantiki upande wa Magharibi inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo.
Ukizungumzia nguvu za siasa za kidunia
(geo-political forces) Majabali (Mataifa makubwa) ya kidunia na hasa
yanayoongozwa na mrengo wa siasa za kiliberali na yenye uchumi uliononeshwa na
matunda za udhalimu wa kibepari, utagundua wanatamani sana nchi hizi mbili
zisitawalike.
Majabali haya yanatamani nchi hizi
zisitawalike ili wapate nafasi ya kudhibiti eneo hili la kimkakati. Lakini zaidi
ya yote ifahamike kwamba katika eneo hili ndiko hazina ya rasilimali madini ya
dunia iliko, kwa uchache na kwa kutaja, hapa yako madini yenye thamani ambayo
hata duniani hakuna, ndio maana hata Tanzanite ikapewa jina hilo. Ili Majabali
wawe na uhuru wa kuchukua hapa watakacho lazima hapa pasiwe na mwenyewe,
watapandikiza chuki kwa makundi, watajaribu kutuvuruga kwa tofauti za kiimani
na watajaribu pia kupitia vyama vya siasa.
Majabali ya dunia yamefanikiwa kuiangusha
Congo ama niseme yamefanikiwa kuifanya Congo isitawalike na wamepafanya pawe
pahala ambapo wanaingia na kutoka na chochote bila kuulizwa maswali wala
kulazimika kutoa majibu.
Mwenyekiti wa CCM Ndg. Magufuli na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amebadilisha utamaduni mbaya na desturi
zisizofaa. Amewakatia mirija madhalimu wakubwa na wadogo walioko ndani ya nchi
na walioko nje ya nchi. Imewauma sana sana, na wale walioko ndani wanatafuta
kila njia ya kumhujumu asifanikiwe, uzuri wanajulikana, ni wanaume wavaao
baibui, baadhi yao ni watoto wa masikini na wamenufaika kwa fedha za masikini
ila wamechagua maisha ya kufuru na ufedhuli, kwao vikao hukutania Dubai.
Tunawajua.
Wako wachache katika Chama chetu cha
Mapinduzi (CCM), wana CCM na vikao vyake tusaidieni kuwakataa, na pale
wanapotumia hila kujipenyeza wafichueni. Hakuna Chama makini kama CCM, ndio
Chama ambacho kwa imani yake kina amini katika Ujamaa na kujitegemea, ndio
Chama pekee ambacho kinaamini binadamu wote ni sawa na ndio Chama pekee ambacho
kwa imani kinaamini utu wa binadamu unastahili kuheshimiwa. Kule nje hakuna
vyama, kuna vikundi maslahi, ni kama bidhaa sokoni, akifika mwenye bei
anachukua bidhaa, na ninyi ushahidi mmeuona Mwaka 2015.
Nakomea hapa, wiki ijayo nitazungumza
namna ambavyo ndoto ya kujenga uchumi imara na madhubuti ambayo Mwalimu Nyerere
alikuwa nayo na hakuishi kuiona imeanza kudhihirika katika awamu ya Tano.
Ombi langu kwenu, hivi ni vita vya mwili
na roho, ni vita ya haki dhidi ya udhalimu, vita ya mwili tunaimudu na
tutaishinda hakika, tusaidieni Maombi maana vita ya roho yapaswa ipiganwe na
wengi wema na waishio maisha ya kujikana nafsi na wenye hofu ya Mungu.
Makala
hii imeandikwa na Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi