Thursday, January 4, 2018

WANA CCM SONGENI MBELE, MAKWAZO HAYANA BUDI KUJA


WANA CCM SONGENI MBELE, MAKWAZO HAYANA BUDI KUJA

CCM Madhubuti inajengwa katika Misingi ya Maadili, Nidhamu ya Chama na Uongozi wa Kiutumishi

Nimeketi na kutafakari sana juu ya mwenendo wa nchi kwa ujumla na nikatizamia baadhi ya mambo ambayo yametendeka katika ulimwengu wa siasa hapa nchini kwa Mwaka 2017, Napata funzo kubwa sana.

Nimejiuliza sana juu ya dhamira yetu kama Taifa, nikajiuliza zaidi juu ya dhamira ya sisi viongozi wa kisiasa wa vyama vyote na kutizama kama dhamira ya Taifa na dhamira ya sisi viongozi wa kisiasa zinawiana.

Kuwiana kwa dhamira hizi ni faida na tija kwa Taifa, maana sote tutakuwa tunajua kama Taifa watanzania wanataka nini? Na kisha tutahakikisha sisi kama viongozi wa kisiasa kwa dhamana zetu na katika vyama vyetu vyote (vyenye uwakilishi na visivyo na uwakilishi katika Mabaraza ya Madiwani na Bunge la Jamhuri) tunasimama kuhakikisha Maslahi ya Taifa yanasimama imara wakati wote.

Dhamira za viongozi wa kisiasa zinapokinzana na matarajio ya wananchi na mahitajio ya wakati, hapo ndipo huibuka msigano wa kimasilahi kati ya viongozi wale wanaosimamia Masilahi ya Taifa na ya muda mrefu na wale ambao wanasimamia masilahi binafsi na ya muda mfupi.

Hitajio la wakati ule na sasa na matakwa ya wananchi katika miaka 10 iliyopita kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 yalikuwa yafuatayo katika kada ya uongozi na kwa uchache nikitaja, kuimarishwa kwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi, kupambana kwa nguvu zote na ubadhirifu au matumizi mabaya ya mali za umma, nidhamu ya watumishi wa umma, maadili ya Taifa, Maadili ya watumishi na viongozi wa umma, viongozi na watumishi hawakuwa tena watumishi wa watu bali mangimeza wasioheshimu watu wala kusikiliza na kushughulika na shida zao.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya tafakuri kubwa kilitambua kwamba hakukuwa na namna nyingine yoyote ya kuendelea kupokea heshima na ridhaa ya wananchi isipokuwa kufanya Mageuzi makubwa ambayo yangeleta Mabadiliko makubwa katika utendaji, usimamizi wa Sera zake kwa Serikali, kuondoa kabisa desturi mbaya, kuongeza na kuimarisha kabisa nidhamu ya chama.

Ilifika pahala Chama kilipoteza heshima yake mbele ya kundi dogo la wanachama ambao walikuwa wana nguvu kuliko Chama chenyewe. Hali hii iliondoa sana imani ya wanachama wa msingi na umma wa watanzania, nidhamu ya Chama inapopotea linaibuka kundi dogo la wanachama masilahi ambao lengo lao ni kujinufaisha kwa mgongo wa Chama, hawa wakiachwa kumea, wanaamua na chama kinalazimika kufuata.

Kazi ya Kwanza ya uongozi wa Awamu ya Tano na vikao vyake vya Maamuzi ilikuwa ni kuvunja desturi hii ya hovyo, Chama kufuata mwanachama, na kurejesha nidhamu ya Chama kwamba mwanachama yeyote lazima afuate nini Chama kinasema na nini kinataka. Hii sio kazi rahisi, maana wapo ambao waliota mizizi na wamenufaika muda mrefu katika desturi hii ya kukitumia Chama kwa faida binafsi.

Kisha Uongozi ukaelekeza Serikali kushughulika kikamilifu na maswala ya ufisadi, rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya ofisi nikitaja machache, na kwa ushahidi leo hii hata tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba rushwa sio tena miongoni mwa kero kubwa miongoni mwa wananchi. Bado tunayo kazi ya kuimaanisha vita hii lakini kwa usaidizi wa wananchi tutashinda.

Kabla ya uchaguzi wa 2015, tulipata ukosoaji mkubwa wa namna tunasimamia haki ya Tanzania katika uvunaji wa rasilimali madini nchini. Na baada ya CCM kuaminiwa tena sote tu mashahidi kwamba kwa mara ya kwanza tumeandika historia kwamba Tanzania itapata 50 kwa 50 gawio la faida katika migodi mikubwa nchini na zoezi la uhakiki wa mikataba gandamizi linaendelea kote nchini.

Ukiacha namna ambavyo Uongozi wa awamu ya tano umejikita katika kurejesha misingi ya uadilifu, uaminifu, kuchapa kazi, unyenyekevu, Uongozi wa Kiutumishi, vita dhidi ya rushwa na kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, kuimarisha makusanyo ya serikali na kuweka nidhamu katika matumizi bado kazi kubwa imefanyika katika masuala ya maendeleo, leo na ndani ya miaka miwili tu, tumenunua ndege sita na moja ikiwa ndege kubwa kabisa na ya kisasa.

Tumeanza ujenzi wa kihistoria wa reli ya kiwango cha kimataifa ambayo gari moshi lake litasukumwa kwa injini za dizeli na Umeme. Gari moshi moja la mizigo litaweza kuvuta mizigo ambayo ingebebwa na malori makubwa mia tano, hata ndio Mapinduzi ambayo watanzania wametamani kuyaona, sasa yanatekelezwa ipasavyo na Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukizungumzia ujenzi wa demokrasia, kama yupo mtu mmoja ambaye amesema muda wote kauli ya “maendeleo hayana chama” ni Ndg. John Pombe Joseph Magufuli. Pale ambapo wewe ni mwakilishi wa wananchi tenda kazi yako ipasavyo, wahudumie watanzania pasina kuwabagua, na zaidi ya yote kipindi hiki ni cha siasa za maendeleo, siasa za masuala, siasa za kushughulika na shida za watu, huu si wakati wa kufanyiana vurumai za kisiasa kama ilivyozoeleka hapo awali.

Licha ya yote haya, bado utaona viongozi wa upinzani ambao walipaswa kutembea kifua mbele kwamba mambo mengi ambayo wananchi waliyasemea sasa yanatekelezwa kwa vitendo na kwa ushahidi, Mfano, leo hii Serikali iko Dodoma ndani ya miaka miwili baada ya tamko Rais Magufuli la kuhamia huko, na mwaka wa tatu 2018 Ndg. Magufuli, Rais wa Nchi yetu, mambo yote yakikaa sawa atahamia Dodoma mapema zaidi kuliko ilivyopangwa awali.

Viongozi wa upinzani ndio wamekuwa mstari wa mbele kutaka kumpunguza mwendokasi Ndg. Magufuli, Rais wetu. Kipindi kile ilifika pahala wakamuita Rais wa Kipindi kile ni dhaifu, leo Ndg. Magufuli mzee wa chuma cha pua, hachengeshi wala “harembi” inapokuja katika kufanya maamuzi.

Mwalimu Nyerere alipata kunukuliwa kuhusu kiongozi ambaye tunamuhitaji, na akasema “awe mtu anayechukizwa na rushwa, na ukimtizama wewe mwenyewe unayemtizama ujiambie kweli huyu anachukizwa na rushwa”. Huyu ndio Magufuli, mtu ambaye akisema sipendi rushwa, sipendi uzembe, sipendi Tanzania ipoteze haki yake katika madini anamaanisha na anatenda na ukimtizama unamwona anamaanisha.

Leo hii badala viongozi wa upinzani kuunga mkono pasina utofauti wa kiitikadi jitihada ambazo wala sio za kiitikadi bali masuala ya kitaifa yenye kubeba mustakabali wa Taifa letu, wao wamekuwa mstari wa mbele kutupinga, kutubeza na kutuvunja moyo.

Siku hizi ni kawaida mtu anayetuhumiwa kwa ufisadi au uhujumu uchumi akikamatwa ili taratibu za mashitaka na za kimahakama zifuate ni jambo la kawaida kuwaona viongozi wa upinzani wakizungumza kuwatetea au kuwaonea huruma watuhumiwa hao.

Si mara moja kiongozi wa Chama cha upinzani nchini amenukuliwa akisema Rais Magufuli amekuwa mkali sana kwahiyo anapendekeza aweke “maneno malaini na matamu”.

Hivi Majambazi na wezi wa Taifa letu wanahitaji lugha ya ukali na kumaanisha au maneno matamu na malaini? Hapo ndipo ulipofika upinzani wa Tanzania.

Kuhusu baadhi ya viongozi wa kiimani kukosoa na kutoa tuhuma pasina kuzingatia haki na wakati uo huo tuhuma na ukosoaji wao wa hadhara ukipigiwa chapuo na viongozi wa upinzani. Mimi naunga mkono viongozi wa kiimani kuikosoa Serikali, lakini nasisitiza, waikosoe kwa haki, kwa staha ya Mamlaka iliyotoka kwa Mungu na zaidi ya yote wakumbuke kuna namna ya kumkosoa Kiongozi Mkuu wa Nchi na kama la kukosoa lipo. Mimi ni mtu mdogo sana ni kondoo tu kiimani, nawakumbusha kwa unyenyekevu habari hii, hata Bwana Yesu alikubali kuzungumza kwa faragha na Nikodemu.

Itakuwa si vema na haki viongozi wetu Maaskofu tukianza kubishana nao hadharani, tu kwa kosa la wao kutokutambua utaratibu, kama kuna ujumbe wa Kiaskofu au kuna ujumbe kutoka kwa Mungu, milango iko wazi kwake mwenyewe (Rais) au kupitia sisi wasaidizi wa Mkuu wa Nchi (iwe kiserikali au kichama) tutafikisha maana sisi huketi mara mojamoja mezani pamoja naye twamjua yu mtu msikivu, mpole, mpenda mashauriano, ni mtu wa maridhiano, ni mtu mpenda haki kweli kweli, ni mtu wa sheria lakini ni mtu wa rohoni hakika. Kwa heshima kubwa nawaacha na changamoto hii.


Mwandishi ni Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Tuesday, October 10, 2017

CCM MPYA TANZANIA MPYA – UHURU WA KIUCHUMI NI MAPAMBANO HAUTAKUJA KATIKA SAHANI YA FEDHA

CCM MPYA TANZANIA MPYA – UHURU WA KIUCHUMI NI MAPAMBANO HAUTAKUJA KATIKA SAHANI YA FEDHA

Hii ndiyo changamoto waliyonayo viongozi wapya wa Afrika – J.K. Nyerere

Maono ya Mwalimu kwa Uongozi wa Awamu ya V

Mwalimu Nyerere alipata kusema katika kitabu cha Afrika Today and Tomorrow katika ukurasa wa 84 “…Africa is yet to liberate itself – to attain Economic liberation – gaining control over, and having responsibility for our economic development strategy and macro economic policies in order to be able to provide for, at least, decent basic standard of living for all our people. Unless this is done our political independence will always be in danger – who controls money, they say, also controls politics.”

Tafsiri yangu ya maneno haya Mwalimu Nyerere anasema “Afrika bado inahitaji kujikomboa – ili kufikia Uhuru wa Kiuchumi – ili kuwa na udhibiti, na wajibu katika mikakati ya maendeleo yetu kiuchumi na sera zetu za kiuchumi ili tuweze kuwapatia watu wetu angalau kiwango cha msingi na chenye utu cha ustawi wa maisha yao. Kama hili lisipofanyika uhuru wetu wa kisiasa bado utakuwa mashakani/hatarini – mwenye kuzidhibiti fedha, wanasema, hudhibiti siasa pia.”

Mwalimu alipata kuyasema haya mwaka 1999 na bado alikuwa ameona mbali sana. Mwalimu alikuwa anatukumbusha kazi kubwa ambayo kipindi kile mwaka 1999 ilikuwa haijakamilika na akiutizamia wakati ujao kwamba bado kazi hiyo ilipasa kukamilishwa – Ukombozi wa Kiuchumi unaotuletea Uhuru wa Kiuchumi kwa Taifa letu la Tanzania.

Kipindi fulani yeye mwenyewe Mwalimu alipata kuamini hakika kwamba uhuru wa Tanzania haungalikuwa mkamilifu mpaka Bara lote la Afrika kukombolewa. Mwalimu akasema mapambano yao ya kulikomboa bara la Afrika yalikamilika mwaka 1994 walipofanikiwa kuufuta ukaburu Afrika Kusini.

Mwalimu Nyerere anaandika Mwaka 1999 kwamba sasa (1999) na kuliko kipindi kingine kabla, anaamini kwa nguvu kubwa kwamba Uhuru wa kisiasa wa Bara la Afrika hautakuwa kamili isipokuwa watu wa Afrika wachukue na kushika kwa mikono yao udhibiti wa uchumi wao badala la kuuacha uchumi wa Afrika katika mikono ya nguvu za kigeni.

Aidha Mwalimu anabashiri na kwa lugha ya kiingereza akisema “This is the Challenge of the new generation of leaders in Africa” akimaanisha kwa kiswahili “Na hii ndiyo changamoto ambayo kizazi kipya cha viongozi wa Afrika wanayo” Tafsiri ni yangu.

Mwalimu anaendelea kusema “Viongozi wa kizazi chake waliweza kutenda kilichowezekana kipindi kile. Viongozi wapya ni lazima wafanikiwe katika utume wao mpya ambao ni ukombozi wa kiuchumi na kushindwa kufanikiwa katika utume huu kutamaanisha kuuachia uhuru wa nchi zao, wa wananchi wao na kukubali hali ilivyo sasa ya utegemezi wa kiuchumi.

Mwalimu Nyerere alikiri kwamba Uongozi wa Afrika unaweza kuwekwa katika mafungu matatu;

Mosi, Viongozi waliopambana kuhakikisha Afrika inakuwa huru, Pili, viongozi waliohangaika na mdororo wa uchumi uliotokana na sera mbovu na zisizotaarifiwa na uhalisia wa Afrika miaka ya 80 na 90. Wapo pia viongozi ambao walidumbukia katika ama rushwa kubwa na kuvuruga Uongozi wa nchi mbalimbali Afrika au matukio ya Mapinduzi ya kijeshi kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi katika nchi hizo. Kwa bahati nzuri kizazi hiki kinaelekea kwisha.

Tatu, ni awamu mpya ya viongozi inayoibuka, hii ni awamu ambayo tutashuhudia kuongezeka kwa viongozi waadilifu na wazalendo wanaochukua Uongozi wa nchi za Afrika. Awamu hii ndio ambayo inakuja kusafisha masalia ya Uongozi usiowajibika na chembechembe za uzembe. Awamu hii itatoa Uongozi bora ambao utaweza kusema HAPANA kwa wale ambao wanacheza na mambo yetu ya ndani katika nchi zetu.

Aidha Mwalimu Nyerere anaendelea kusema viongozi hawa wa awamu mpya wanajua matakwa ya wananchi wao, ni aina mpya ya viongozi wanaotoa aina mpya ya Uongozi. Viongozi hawa wamenia kukamilisha mapambano ya ukombozi – ukombozi wa kiuchumi.

Wajibu Mkuu Mwalimu Nyerere anaeleza wa Maendeleo ya Afrika unabaki kwa waafrika wenyewe. Msaada wowote utakuwa ni nyongeza tu katika jitihada za waafrika wenyewe. Na kama kutakuwa na uhusiano wowote basi lazima mahusiano haya yajengwe katika namna ambayo yatanufaisha waafrika kwa haki na sio katika misingi ya unyonyaji. Mwalimu anamaliza kwa kusema “shime sote tuungane mikono kuiokoa Afrika dhidi ya unyonyaji wowote baadaye”.

Baada ya rejea na nukuu hizi za Mwalimu napenda kujadili CCM MPYA TANZANIA MPYA na ukweli kwamba uhuru wa kiuchumi ni mapambano na asilani hautakuja katika sahani ya fedha. Tafakuri yangu nimeigawa katika vipindi tatu, Mosi, Tulikotoka ni mbali, Pili, Tuliko sasa na Tatu, Tunakokwenda.

Tulikotoka ni mbali

Serikali za Awamu ya Kwanza na ya Pili zimepambana sana kuleta maendeleo ya Taifa la Tanzania, kwanza ya ujenzi wa Taifa Moja Imara na madhubuti linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanganyika na Zanzibar kwa pamoja tumezirithi kutoka kwa wakoloni lakini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ujenzi wake tumeufanya wenyewe. Mwaka 1964 ni mwaka muhimu katika ujenzi wa Taifa na kisha baada ya hapo tunalo zoezi endelevu la kujenga Taifa hili.

Ujenzi wa Taifa la Tanzania haukuwahi kuwa rahisi na umepitia changamoto na mitihani mingi sana. Natafakari katika pande la ardhi ambalo kuna watu wenye lugha na makabila tofauti tofauti zaidi ya 120, na kila kabila likiwa na utamaduni wake, desturi zake na Uongozi wake (Machifu).

Hili Mwalimu Nyerere alianza na viongozi waliofuatia baada yake wakaendelea nalo na leo tunajivuna Tanzania ndio nchi pekee katika Afrika ambayo watu wake wana lugha moja ya Taifa ambayo sio ya kabila mojawapo.

Mitihani ilianza mwaka 1964, wakati wa uamuzi wa kihistoria wa kuunganisha nchi mbili zilizokuwa huru kwa maana ya Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja mpya na huru ilopewa jina “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Wahisani wetu wakubwa wa maendeleo kipindi hicho Ujerumani Magharibi hawakupendezwa na uamuzi huu na wakatishia kuvunja uhusiano nasi.

Kabla hatujatishika tukajitathimini kama Taifa, heshima yetu na umuhimu wa tunu yetu ya UMOJA. Kwa kauli moja tukavunja uhusiano na Ujerumani Magharibi na kurudisha msaada wa fedha ambao tayari ulikuwa umetolewa kwetu. Funzo hapa ni haijalishi tunapitia wakati gani lakini wakati wote tunapaswa kulinda heshima na umoja wa Taifa letu.

Mtihani wa pili ulikuwa mwaka 1965, hii ilikuwa baada ya kikundi cha watu wachache kujitangazia uhuru kule Zimbabwe ya leo (Unilateral Declaration of Independence). Tanzania iliamini katika uhuru wa kweli na wa wengi nchini humo. Tukawaeleza waingereza kwamba tabia ile ni mbaya na haikubaliki na kwa kuwa Uingereza ndiye dada mkubwa katika familia ya Jumuiya ya Madola tukamtaka achukue hatua dhidi ya utawala wa wachache uliojitangazia uhuru chini ya bwana Smith.

Waingereza walisua sua na hata baada ya nchi za Afrika kulaani vikali kitendo kile bado hawakuchukua hatua kali na stahiki. Kati ya Nchi za Afrika huru ni Tanzania na Ghana tu ndio zilizovunja mahusiano na Uingereza, kitendo hiki kililenga kupeleka ujumbe kwamba hatuukubali unyonyaji wa aina yoyote iwe Tanzania au nje ya Tanzania na hasa kwa mataifa rafiki kipindi kile.

Mwaka 1970-75 tukapata ukame mkubwa katika nchi yetu, wakati hali hiyo ikiendelea tukatoka na mikakati ya kupambana na hali hiyo kwa kuanzisha skimu kadhaa za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini. Haikuwa kazi rahisi, ilitaka Chama, Serikali na Umma wa Wananchi kuwa na uelewa wa pamoja wa hali iliyokuwa inatukabili na kusimama imara pamoja ili kukabiliana nayo.

Tukavuka salama, na mwaka 1977 tukaandika historia nyingine kubwa ya kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka mmoja baadaye tukaingia katika Vita dhidi ya Nduli Iddi Amin, vita ya Kagera. Vita hii ilitupa heshima kubwa maana tuliipigana wenyewe na licha ya kwamba Nduli alisaidiwa na mataifa mengine lakini Wananchi wa Tanzania na Jeshi letu la Wananchi (JWTZ) tukamfurushia mbali hadi nje ya mipaka yetu. Vita ya Kagera licha ya heshima kubwa ilituacha katika wakati mgumu sana kiuchumi maana tulitumia karibia hifadhi yetu yote ya fedha za kigeni ambayo hutumika kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje.

Kuna kipindi tulifika tukabaki na akiba isiyozidi wiki mbili ya Mafuta ya Magari, ulikuwa wakati mgumu sana. Huwa nafananisha Uongozi wa Nchi kama Uongozi wa familia inayojitahidi sana kujikwamua kihali na kiuchumi licha ya changamoto mbalimbali. Baba au Mama anaweza kurudi nyumbani na chakula hakuna na ilhali watoto hujua baba au mama lazima awe na uwezo wa kuleta chakula nyumbani. Nadhani Mama na Baba wote wataungana na mimi kwamba hakuna wakati mgumu ambapo watoto wanakutegemea uwawezeshe na hauko katika uwezo wa kuwezesha lakini unapambana uwawezeshe maana hawawezi amini kwamba baba au mama hawezi kuwezesha mahitaji yao.

Miaka ya Themanini (80) ikawa na Changamoto zaidi na ukiongeza na masharti gandamizi ya Taasisi za Kifedha za Kidunia zijulikanazo kwa kiingereza kama “Britton Woods Institutions”. Wakatulazimisha Serikali isifanye tena uzalishaji na iachane na umiliki wa mashirika ya umma, wakalazimisha tushushe thamani ya fedha yetu (shilingi ya Tanzania) na wakatueleza ili tupate misaada kutoka kwao kwanza ni lazima turidhie masharti haya niliyoyataja kwa uchache na tukubali kutekeleza programu za kurekebisha uchumi wetu (Structural Adjustment Programmes – SAPs).

Kibaya zaidi na kwasababu tulikuwa na msimamo wa kuendelea na Mapambano ya kuukomboa Uchumi wetu dhidi ya mikakati ya kinyonyaji ya kibeberu iliyokuwa inatambulishwa na Taasisi hizi za kifedha za kidunia, waliamua pia kutuhujumu waziwazi.

Hujuma ya uchumi wetu ilikuwa kutoka nje na ikiratibiwa kimkakati kabisa na ilikuwa pia kutoka ndani ikiratibiwa kwa ustadi na vibaraka wa mabeberu, watanzania wachache waliokosa uadilifu, uaminifu, uzalendo na mapenzi ya dhati kwa Taifa letu.

Vilikuwepo viwanda zaidi ya 400 na migodi kadhaa, lakini viwanda na migodi inapojiendesha kila baada ya muda huhitaji vipuri, basi kila tulipoagiza vipuri kutoka kampuni za nje walitoa visingizo mbalimbali, mara kampuni zimeuzwa au kampuni ilishafilisika na kadhalika na kadhalika. Hivyo baada ya muda viwanda vingi vilikosa vipuri na kulazimika kusimama na watu kupoteza ajira. Hali kama hiyo ilitokea katika migodi kadhaa na ikailazimu serikali kuweka mpango wa kuifunga migodi hiyo.

Hata pale tulipoamua kampuni yetu ya kizalendo Nyumbu itengeneze vipuri hapa hapa nchini basi mataifa makubwa yalififisha dhamira njema ya kampuni za kizalendo kwa kutoa misaada ili kampuni za ndani zishindwe kufanya biashara, zishindwe kujiendesha na hatimaye kuanguka.

Changamoto ziliongezeka sana kwasababu tulisimamia haki huku tukiendelea kupinga udhalimu. Ililazimu serikali itafute mbinu mbadala ya kujiendesha na ndipo mawazo kama ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Stiegler’s Gorge likaja lakini uwezo wa kujenga hatukuwa nao wakati huo.

Mwalimu alijua huenda katika pwani yetu tunaweza kuwa na gesi au mafuta na akazungumza na nchi fulani za Magharibi ili kuja kufanya utafiti wa uwepo wa mafuta na gesi. Wataalamu wa kimagharibi wakaja na wakafanya utafiti na kusema hakuna dalili yoyote ya mafuta au gesi.

Mwalimu alikuwa mvumilivu na hakuwa mtu wa kukata tamaa, na alizungumza na marafiki zetu wa India ambao walikuja hapa na wakachoronga maeneo machache ya pwani ya Tanzania (Pwani na Lindi) na hatimaye gesi ikapatikana, wakamwambia imepatikana na wakalipua kisima kimoja na kikawaka moto bila kuzimika kwa miezi mitatu. Mwalimu Nyerere akawaambia wakizibe kisima hicho na pasijulikane pahala pale mpaka watakapokuwa tayari hapo baadaye.

Kuna kipindi tulipokuwa tukifanya mashauriano (negotiations) katika masuala ya kiuchumi ili “mabwana wakubwa” ama walegeze kamba au watusaidie, ilitubidi sisi kusafiri kuwafuata, mfano, kule Ulaya katika vikao vya Paris Club, vikao hivi wanakaa matajiri wa dunia na mataifa makubwa. Mzee Cleopa David Msuya alishiriki kule, ilikuwa lazima uwafuate Ulaya mabwana wakubwa kule, na kuna kipindi aliwafuata na aliishia mapokezi, ubeberu bila kugangamala una jeuri, kiburi na dharau sana.

Napenda watu wajua safari yetu imekuwa yenye milima na mabonde lakini kitu kimoja cha kujivuna tumebaki na Taifa moja. Ni wajibu wetu kukumbushana tulikotoka ni mbali na hasa vijana na watoto wetu.

Tulipo sasa

Tanzania iko katika awamu ya Tano ya Uongozi wake tangu kuasisiwa kwake. Baada ya vipindi viwili vya awamu ya Nne, CCM iliamua kufanya Mageuzi Makubwa ambayo yanahakikisha chama hiki kinabaki kuwa Chama cha Wanachama na kinachoshughulika na shida za watu wetu.

Mageuzi ya CCM yanalenga pia kuhakikisha katika kila mawanda haki ya watanzania inapatikana. Taifa hili ni tajiri sana na linaweza kujitosheleza ndani lakini tumeshindwa kwa muda mrefu kujenga uwezo wa ndani ili kutimiza ndoto hii ya kujitegemea ama kwa unyonge au wakati mwingine kwa uzembe wa baadhi yetu.

Chama Cha Mapinduzi baada ya kujitathimini kikatafuta mtu ambaye ataweza kuishika agenda ya Mageuzi ya CCM, na ieleweke Mageuzi ya CCM yatatoa mwelekeo kwa Mageuzi ya Serikali ili sote tuweze kukidhi na kuweka jitihada kubwa ya kutosheleza mahitaji na matarajio ya msingi ya watanzania.

Mtu huyu ambaye ameaminiwa kwanza na wana CCM kisha watanzania ni Ndugu yetu John Pombe Joseph Magufuli, mtanzania kweli kweli na mwenye uchungu wa kuhujumiwa kwetu. Mtu ambaye CCM ilimleta (Ndg. Magufuli) ilipasa awe mtu ambaye hatatuonea soni, hataleta urafiki, hataona haya kutuambia hapa na pale tulikosea.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitafakari na kuamua kutuletea Ndg. Magufuli ili pia aweze kutusimamia kwa haki tena pasina kujiona mnyonge hata mbele ya wabwana wakubwa wa ndani na nje ya nchi.

Leo Afrika nzima inazizima kwamba yuko mwanaume ambaye ameweza kusema imetosha “enough is enough” sio haki na ni unyonyaji kuchukua madini yetu katika namna ambayo haki yetu inapokwa. Ndugu Magufuli ana amini sana katika sekta binafsi na hasa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda sambamba na sekta ya umma, lakini ana amini zaidi katika sekta binafsi inayojiendesha kwa kanuni za maadili ikiwemo kulipa kodi. Ana amini katika uwekezaji kutoka nje, lakini unaotambua kwamba sisi ni Taifa huru na tunayo haki ya kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zetu.

Ndugu Magufuli ana amini kwa hakika uwekezaji kutoka nje unapaswa kujengwa katika misingi ya haki na usawa na kwamba kila upande una wajibu Tanzania na wawekezaji, Tanzania iweke mazingira ya uwekezaji hasa wa viwanda na wawekezaji watende sawa sawa na kanuni za kidunia za maadili ikiwemo kutokuiba kwa ujanja ujanja, kutokwepa kodi, kutosafirisha pesa kwenda nje “capital flight” wakati zinawezwa kutunzwa hapa na kadharika.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemleta ndugu Magufuli wakati muafaka wakati tunamhitaji zaidi mtu kama yeye. Ukisoma Maelezo na Nukuu za Mwalimu Nyerere katika maelezo yangu ya awali juu ya Maono ya Mwalimu Nyerere utaungana nami kusema ile aina ya Uongozi mpya katika bara la Afrika, Tanzania tumekuwa kinara wa kwanza na wengine watafuata ili bara la Afrika lirejeshe heshima yake ya uhalisia na asili.

Wiki ijayo nitaeleza kuhusu tunakokwenda na kwanini Ndugu Magufuli ni zawadi na tumtumie katika kipindi hiki cha mpito na cha kunyooshana nidhamu ili maisha yetu katika miaka mikuu 75 “The Great 75 Years” iwe rahisi na yenye mafanikio makubwa hii ni kati ya Mwaka 2025 na Mwaka 2100. Huu ni wakati wa siasa za Maendeleo na sio siasa za Madaraka.

Makala hii imeandikwa na Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi


Sunday, September 17, 2017

HATUTARUDI NYUMA KATIKA JITIHADA ZETU ZA KUPINGA UDHALIMU NCHINI


HATUTARUDI NYUMA KATIKA JITIHADA ZETU ZA KUPINGA UDHALIMU NCHINI

Uhuru wetu wa kisiasa ni kazi bure pasina kuumiliki na kuudhibiti uhuru wetu wa kiuchumi

Mageuzi Makubwa ya Chama na Serikali

Tunapitia kipindi cha tofauti katika historia ya Taifa letu, kipindi ambacho naweza kukiita kipindi cha mpito, hiki ni kipindi ambacho tunatoka katika hali moja na tunapaswa kwenda kwenye hali nyingine ambayo ni bora zaidi.

Kipindi hiki cha mpito kinaongozwa na kauli mbiu ya CCM Mpya Tanzania Mpya. Ni kipindi ambacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kujitizama kitofauti, kimeamua kujitafakari na kujihoji, maswali yafuatayo na kwa ufupi, tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejitizama mwenendo wake, matendo yake, itikadi yake, siasa yake, dhamira yake, malengo yake na Imani yake. Kisha Chama kikaenda mbele kikatizama viongozi wake, nidhamu yao kwa Chama, tabia zao, mienendo yao, matendo yao, na kuoanisha hayo yote na ahadi tisa za mwanachama wa CCM.

Chama kikachukua muda zaidi kuangalia sauti za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo mara zote zimeendelea kuelekeza nini mwelekeo sahihi wa CCM chama ambacho si tu ni Chama kilichopo madarakani lakini ni Chama kikubwa Tanzania na Afrika.

Tafakuri hii ndefu ya CCM ndiyo iliyopelekea kuandikwa kwa waraka wa Chama uliopewa jina la “Umuhimu wa kufanya Mageuzi ndani ya Chama”.

Katika waraka huu wa Mageuzi inafafanuliwa kwamba kabla ya awamu ya tano, suala la rushwa (ufisadi) limekuwa ni mzigo mkubwa ambao Chama chetu kimebebeshwa. Pamoja na juhudi kubwa ambazo serikali ya awamu ya nne ilifanya katika kupambana na rushwa ikiwa pamoja na kutunga sheria mpya wakati huo, kuiunda na kuiimarisha taasisi yetu ya kupambana na rushwa na kutunga sheria ya kudhibiti Matumizi ya Fedha za Uchaguzi wananchi bado waliona Chama chetu kilikumbatia wala rushwa.

Chama baada ya tafakuri jadidi na shirikishi kikaamua kwa kauli na sauti moja kufanya Mageuzi makubwa yatakayokitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mwonekano huu hasi mbele ya umma wa wanachama na wananchi na kuwa Chama ambacho kinamaanisha kwa maneno na matendo chuki yake dhidi ya rushwa na wala rushwa.

Mageuzi Makubwa yanalengwa katika Chama chenyewe (CCM) na katika Serikali.

Mwelekeo ni kukifanyia Chama Mageuzi makubwa katika mawanda ya Kiuongozi, Kimuundo na Kiutendaji. Mageuzi haya katika mawanda haya matatu yataongeza tija, ufanisi, uwajibikaji, faida, itapunguza gharama za uendeshaji wa Chama na huduma za wanachama zitaboreka zaidi.

Mageuzi haya katika Chama msingi wake ni kukirejesha Chama chetu kwa Wanachama na kuimarisha msingi wa kuwa chama kinachoshughulika na shida za watu.

Mojawapo ya sababu za hamasa ya Mageuzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tunaipata kutoka kwa Mwalimu Nyerere katika kitabu cha Binadamu na Maendeleo katika ukurasa wake wa 18 na 19, Mwalimu anasema “ Kazi ya Chama Cha Siasa kilicho imara ni kuwa kama daraja la kuwaunganisha watu na serikali waliyoichagua, na kuiunganisha serikali na watu inayotaka kuwahudumia...”

Mwalimu Nyerere anaendelea kusema katika kitabu hiki “…Ni wajibu wa Chama kuwasaidia watu kuelewa serikali yao inafanya nini na kwa nini; ni wajibu wake kusaidia watu kushirikiana na serikali yao kwa juhudi ya pamoja ili kuundosha umasikini ambao umetulemea. Na ni wajibu wa Chama pia kuhakikisha kwamba serikali inaendelea kuyajua sana maoni, shida na matakwa ya watu…”

Aidha Mwalimu Nyerere anatukumbusha katika kitabu hiki “…Ni wajibu wake (CCM) kuwasemea watu. Pia ni wajibu wake kuwaelimisha watu na kuwasaidia kuona shughuli za serikali zina maana gani kuhusu usalama wao wenyewe wa siku zijazo na fursa zao wenyewe za siku zijazo”

Tangu Uongozi wa Awamu ya Tano uingie madarakani mwaka 2015 kupitia tiketi ya CCM chini ya Ndugu yetu John Pombe Joseph Magufuli Mageuzi Makubwa yanaendelea kufanyika katika Serikali na taasisi zake katika maeneo ya utolewaji wa huduma, nidhamu ya ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za serikali, kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya rushwa hasa ufisadi na uhujumu uchumi, kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, kukabiliana na kudhibiti mtawanyiko haramu wa silaha za moto, kuwakabili na kuwachukulia hatua kali wakwepa kodi, walanguzi, watakatisha fedha na kushughulika na wote wale ambao kwa matendo yao uchumi wa nchi na ustawi wa watu wake unawekwa rehani.

Mageuzi haya makubwa hayaji katika sahani ya fedha mezani, ni kazi ngumu, napenda nikiri ina upinzani mkubwa, iko bayana kwamba kwa watu wasio wema na wasio na mapenzi mema na maendeleo ya nchi hawafurahishwi na Mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na katika Serikali.




Tafsiri ya Mageuzi ya CCM

Baada ya tafakuri kubwa na kusikiliza sauti za wananchi, CCM imenia na inatenda kwa uhalisia kukirejesha Chama kwa wanachama. Kuna wakati Chama kilionekana ni pango la maharamia, kila mkwepa kodi alikuwa na uhusiano na CCM, hili lilichafua sana taswira ya CCM. Taswira hii mbaya imechafua heshima ya Chama chetu na kukifanya kinuke, lakini idadi ya kutosha ya wachafuzi wa Chama chetu wamekuwamo ndani ya CCM yenyewe. Baadhi ya wachafuzi hawa wa taswira na heshima ya Chama chetu ni viongozi katika Chama chetu katika ngazi mbalimbali.

Kwa msingi huu, Mageuzi Makubwa katika Chama yanatizama eneo la Uongozi; Chama kinataka aina ya viongozi ambao watanzania wanawataka. Viongozi wachapa kazi, waaminifu, waadilifu, wanyenyekevu, wanaochukizwa na rushwa, wanaochukizwa na ubadhirifu wa mali za Chama na Mali za Serikali, viongozi wasio wabinafsi bali wanaowaweka wanachama kwanza, viongozi wapole lakini wakali kwa mambo ya hovyo, viongozi wanaoziishi imani za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Viongozi wanaoziishi ahadi za mwana CCM, viongozi wasioukamia Uongozi, hawa ni viongozi ambao watakubalika si kwa fedha bali kwa mienendo yao mema na maono yao ya kiuongozi kwa Chama chetu katika ngazi husika na kwa umma wa watanzania hata wale ambao sio wana CCM.

Ukiwa na aina hii ya viongozi CCM inaamini chama chetu kitakuwa imara na madhubuti zaidi na kitasimamia haki za wanachama na wananchi kwa ujumla. Tukiwa na viongozi wa aina ambayo nimeieleza kwa uchache hapo juu, hawa ndio wataisimamia serikali kutoka ngazi za msingi katika Serikali za Mitaa na Vijiji, Serikali za ngazi ya Kata, Serikali katika ngazi ya Wilaya na Halmashauri mpaka katika Mikoa, Miji na Majiji ya Nchi yetu.

Viongozi wa aina hii, hawahongeki, hawapokei wala kutoa rushwa, ni wakali sana kwa wote wanaofanya ubadhirifu wa mali za Chama na Mali za Umma. Viongozi hawa ambao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuwapata katika uchaguzi wake wa ndani mwaka huu wa 2017 wanapenda HAKI na wanaheshimu wanachama wa CCM na wananchi wa Tanzania.

Kama nilivyotangulia kusema viongozi wa aina hii huzongwa sana, hufanyiwa fitina na hufanyiwa kila aina ya hila. Chama kimejipanga ipasavyo kuhakikisha ya kwamba haki itasimamiwa ipasavyo, na majizi, na wote ambao wamekuwa wakijinufaisha na mali za Chama kwa faida yao kinyume na Ahadi ya Mwana CCM hawatopewa nafasi ya kuwa viongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongozwa kwa Katiba, Kanuni mbalimbali, desturi njema na dhamira na utashi mwema wa viongozi wetu, chini ya Uenyekiti wa Komredi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.


Msingi wa kutokurudi nyuma

Kipindi hiki tunapofanya Mageuzi haya Makubwa napenda ifahamike wako baadhi yetu ambao watashindwa kwenda na mwendokasi wa Mageuzi haya makubwa.

Baadhi ya wanaoshindwa kwenda na mwendokasi wa Mageuzi Makubwa ya CCM ni wale ambao walizoea kuishi kwa mazoea, kula visivyo vyao, kudhulumu haki za wananchi hasa wanyonge, walizoea kujimilikisha mali za CCM na kuzifuja watakavyo, walizoea kuwa miungu watu na kuwadharau wanachama.

Katika historia ya Chama chetu watu hawa wamekuwapo katika awamu zote, na ni mapambano kuwaondoa, wanachama wanawajua, dhamira njema ya CCM Mpya inawajua, na hakika Uongozi wa CCM na Vikao vya Chama vitahakikisha watu hawa wenye inda hawapati Uongozi katika Chama chetu.

Watu waovu wana mitandao yao ya uovu, tuwakatae, na Chama chetu kimekuwa na desturi nzuri ya kuwakataa, kipindi hiki tutawakataa tena na kwa sauti kuu. Mitandao imedhoofisha sana Chama chetu, mitandao ya watu wabinafsi na wanaotaka kukitumia Chama chetu kama kitega uchumi, mitandao ya kidhalimu haina nafasi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati mwingine hata watu ambao wamepata kuhudumu katika nyadhifa za Uongozi wanahusika kuhujumu Chama na nchi yetu, wanatengeneza mitandao na kushirikia na madhalimu, tunawajua, hata utu una kikomo, hatutawaruhusu kuvuruga Chama chetu.

Shime wanachama msikubali hata kidogo madhalimu wa kisiasa wakajaribu tena kuteka Chama chetu, walishindwa, wameshindwa na wataendelea kushindwa. Rai yangu hapa, watu wabaya huwa hawagombani, maslahi yao ya kidhalimu ni ya kudumu, wanaweza kuonekana hawako pamoja lakini wanaunganishwa na maslahi yao ya kudumu ya kidhalimu. Hata kwenye Chama chetu walikuwepo, wameondoka, wamebaki, kazi yetu ni kuwadhibiti ipasavyo, wameanza kuzungumza, tuwe macho kulinda misingi ya Chama chetu.

Kila mwana CCM asimame kidete, akisemee Chama, aisemee Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni wajibu wetu kuujuza umma wa wananchi nini Serikali inafanya na kwa nini.

Tunaupinga udhalimu katika Chama chetu na tunaupinga udhalimu katika Serikali, sio kazi rahisi lakini tutashinda kwasababu dhamira yetu ni njema na inasimamia maslahi mapana ya Taifa la Tanzania na watu wake.

Hata mabwana wakubwa wa dunia tumewaonesha kwa vitendo kwamba tunamaanisha tunaposema tumechoka kuonewa, tumechoka kuibiwa kwa makusudi au kwa kuhadaiwa. Nchi yetu ni ya kipekee sana na Mungu ametubariki na kila aina ya utajiri wa asili na watu wenye mshikamano.

Kijiografia nchi yetu iko katika eneo la kimkakati katika uso wa dunia. Katika bara la Afrika ni nchi mbili tu ndio zinatengeneza nyonga ya bara la Afrika nazo ni Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hizi ndizo nchi pekee ambazo zinalikata bara la Afrika katikati na nchi ambazo zina mipaka ya bahari kuu zinazozunguka bara la Afrika kwa maana ya Bahari ya Hindi upande wa Mashariki inayopakana na Tanzania na Bahari ya Atlantiki upande wa Magharibi inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ukizungumzia nguvu za siasa za kidunia (geo-political forces) Majabali (Mataifa makubwa) ya kidunia na hasa yanayoongozwa na mrengo wa siasa za kiliberali na yenye uchumi uliononeshwa na matunda za udhalimu wa kibepari, utagundua wanatamani sana nchi hizi mbili zisitawalike.

Majabali haya yanatamani nchi hizi zisitawalike ili wapate nafasi ya kudhibiti eneo hili la kimkakati. Lakini zaidi ya yote ifahamike kwamba katika eneo hili ndiko hazina ya rasilimali madini ya dunia iliko, kwa uchache na kwa kutaja, hapa yako madini yenye thamani ambayo hata duniani hakuna, ndio maana hata Tanzanite ikapewa jina hilo. Ili Majabali wawe na uhuru wa kuchukua hapa watakacho lazima hapa pasiwe na mwenyewe, watapandikiza chuki kwa makundi, watajaribu kutuvuruga kwa tofauti za kiimani na watajaribu pia kupitia vyama vya siasa.

Majabali ya dunia yamefanikiwa kuiangusha Congo ama niseme yamefanikiwa kuifanya Congo isitawalike na wamepafanya pawe pahala ambapo wanaingia na kutoka na chochote bila kuulizwa maswali wala kulazimika kutoa majibu.

Mwenyekiti wa CCM Ndg. Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amebadilisha utamaduni mbaya na desturi zisizofaa. Amewakatia mirija madhalimu wakubwa na wadogo walioko ndani ya nchi na walioko nje ya nchi. Imewauma sana sana, na wale walioko ndani wanatafuta kila njia ya kumhujumu asifanikiwe, uzuri wanajulikana, ni wanaume wavaao baibui, baadhi yao ni watoto wa masikini na wamenufaika kwa fedha za masikini ila wamechagua maisha ya kufuru na ufedhuli, kwao vikao hukutania Dubai. Tunawajua.

Wako wachache katika Chama chetu cha Mapinduzi (CCM), wana CCM na vikao vyake tusaidieni kuwakataa, na pale wanapotumia hila kujipenyeza wafichueni. Hakuna Chama makini kama CCM, ndio Chama ambacho kwa imani yake kina amini katika Ujamaa na kujitegemea, ndio Chama pekee ambacho kinaamini binadamu wote ni sawa na ndio Chama pekee ambacho kwa imani kinaamini utu wa binadamu unastahili kuheshimiwa. Kule nje hakuna vyama, kuna vikundi maslahi, ni kama bidhaa sokoni, akifika mwenye bei anachukua bidhaa, na ninyi ushahidi mmeuona Mwaka 2015.

Nakomea hapa, wiki ijayo nitazungumza namna ambavyo ndoto ya kujenga uchumi imara na madhubuti ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa nayo na hakuishi kuiona imeanza kudhihirika katika awamu ya Tano.

Ombi langu kwenu, hivi ni vita vya mwili na roho, ni vita ya haki dhidi ya udhalimu, vita ya mwili tunaimudu na tutaishinda hakika, tusaidieni Maombi maana vita ya roho yapaswa ipiganwe na wengi wema na waishio maisha ya kujikana nafsi na wenye hofu ya Mungu.

Makala hii imeandikwa na Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi