CCM
MPYA TANZANIA MPYA – UHURU WA KIUCHUMI NI MAPAMBANO HAUTAKUJA KATIKA SAHANI YA
FEDHA
Hii
ndiyo changamoto waliyonayo viongozi wapya wa Afrika – J.K. Nyerere
Maono
ya Mwalimu kwa Uongozi wa Awamu ya V
Mwalimu Nyerere alipata kusema katika
kitabu cha Afrika Today and Tomorrow katika ukurasa wa 84 “…Africa is yet to
liberate itself – to attain Economic liberation – gaining control over, and
having responsibility for our economic development strategy and macro economic
policies in order to be able to provide for, at least, decent basic standard of
living for all our people. Unless this is done our political independence will
always be in danger – who controls money, they say, also controls politics.”
Tafsiri yangu ya maneno haya Mwalimu
Nyerere anasema “Afrika bado inahitaji kujikomboa – ili kufikia Uhuru wa
Kiuchumi – ili kuwa na udhibiti, na wajibu katika mikakati ya maendeleo yetu
kiuchumi na sera zetu za kiuchumi ili tuweze kuwapatia watu wetu angalau
kiwango cha msingi na chenye utu cha ustawi wa maisha yao. Kama hili
lisipofanyika uhuru wetu wa kisiasa bado utakuwa mashakani/hatarini – mwenye
kuzidhibiti fedha, wanasema, hudhibiti siasa pia.”
Mwalimu alipata kuyasema haya mwaka 1999
na bado alikuwa ameona mbali sana. Mwalimu alikuwa anatukumbusha kazi kubwa
ambayo kipindi kile mwaka 1999 ilikuwa haijakamilika na akiutizamia wakati ujao
kwamba bado kazi hiyo ilipasa kukamilishwa – Ukombozi wa Kiuchumi unaotuletea
Uhuru wa Kiuchumi kwa Taifa letu la Tanzania.
Kipindi fulani yeye mwenyewe Mwalimu alipata
kuamini hakika kwamba uhuru wa Tanzania haungalikuwa mkamilifu mpaka Bara lote
la Afrika kukombolewa. Mwalimu akasema mapambano yao ya kulikomboa bara la
Afrika yalikamilika mwaka 1994 walipofanikiwa kuufuta ukaburu Afrika Kusini.
Mwalimu Nyerere anaandika Mwaka 1999
kwamba sasa (1999) na kuliko kipindi kingine kabla, anaamini kwa nguvu kubwa
kwamba Uhuru wa kisiasa wa Bara la Afrika hautakuwa kamili isipokuwa watu wa
Afrika wachukue na kushika kwa mikono yao udhibiti wa uchumi wao badala la
kuuacha uchumi wa Afrika katika mikono ya nguvu za kigeni.
Aidha Mwalimu anabashiri na kwa lugha ya
kiingereza akisema “This is the Challenge of the new generation of leaders in
Africa” akimaanisha kwa kiswahili “Na hii ndiyo changamoto ambayo kizazi kipya
cha viongozi wa Afrika wanayo” Tafsiri ni yangu.
Mwalimu anaendelea kusema “Viongozi wa
kizazi chake waliweza kutenda kilichowezekana kipindi kile. Viongozi wapya ni
lazima wafanikiwe katika utume wao mpya ambao ni ukombozi wa kiuchumi na
kushindwa kufanikiwa katika utume huu kutamaanisha kuuachia uhuru wa nchi zao,
wa wananchi wao na kukubali hali ilivyo sasa ya utegemezi wa kiuchumi.
Mwalimu Nyerere alikiri kwamba Uongozi wa
Afrika unaweza kuwekwa katika mafungu matatu;
Mosi, Viongozi waliopambana kuhakikisha
Afrika inakuwa huru, Pili, viongozi waliohangaika na mdororo wa uchumi
uliotokana na sera mbovu na zisizotaarifiwa na uhalisia wa Afrika miaka ya 80
na 90. Wapo pia viongozi ambao walidumbukia katika ama rushwa kubwa na kuvuruga
Uongozi wa nchi mbalimbali Afrika au matukio ya Mapinduzi ya kijeshi kwa
kisingizio cha kupambana na ufisadi katika nchi hizo. Kwa bahati nzuri kizazi
hiki kinaelekea kwisha.
Tatu, ni awamu mpya ya viongozi
inayoibuka, hii ni awamu ambayo tutashuhudia kuongezeka kwa viongozi waadilifu
na wazalendo wanaochukua Uongozi wa nchi za Afrika. Awamu hii ndio ambayo
inakuja kusafisha masalia ya Uongozi usiowajibika na chembechembe za uzembe.
Awamu hii itatoa Uongozi bora ambao utaweza kusema HAPANA kwa wale ambao
wanacheza na mambo yetu ya ndani katika nchi zetu.
Aidha Mwalimu Nyerere anaendelea kusema
viongozi hawa wa awamu mpya wanajua matakwa ya wananchi wao, ni aina mpya ya
viongozi wanaotoa aina mpya ya Uongozi. Viongozi hawa wamenia kukamilisha
mapambano ya ukombozi – ukombozi wa kiuchumi.
Wajibu Mkuu Mwalimu Nyerere anaeleza wa
Maendeleo ya Afrika unabaki kwa waafrika wenyewe. Msaada wowote utakuwa ni
nyongeza tu katika jitihada za waafrika wenyewe. Na kama kutakuwa na uhusiano
wowote basi lazima mahusiano haya yajengwe katika namna ambayo yatanufaisha
waafrika kwa haki na sio katika misingi ya unyonyaji. Mwalimu anamaliza kwa
kusema “shime sote tuungane mikono kuiokoa Afrika dhidi ya unyonyaji wowote
baadaye”.
Baada ya rejea na nukuu hizi za Mwalimu
napenda kujadili CCM MPYA TANZANIA MPYA na ukweli kwamba uhuru wa kiuchumi ni
mapambano na asilani hautakuja katika sahani ya fedha. Tafakuri yangu nimeigawa
katika vipindi tatu, Mosi, Tulikotoka ni mbali, Pili, Tuliko sasa na Tatu,
Tunakokwenda.
Tulikotoka
ni mbali
Serikali za Awamu ya Kwanza na ya Pili
zimepambana sana kuleta maendeleo ya Taifa la Tanzania, kwanza ya ujenzi wa
Taifa Moja Imara na madhubuti linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tanganyika na Zanzibar kwa pamoja tumezirithi kutoka kwa wakoloni lakini
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ujenzi wake tumeufanya wenyewe. Mwaka 1964 ni
mwaka muhimu katika ujenzi wa Taifa na kisha baada ya hapo tunalo zoezi
endelevu la kujenga Taifa hili.
Ujenzi wa Taifa la Tanzania haukuwahi
kuwa rahisi na umepitia changamoto na mitihani mingi sana. Natafakari katika
pande la ardhi ambalo kuna watu wenye lugha na makabila tofauti tofauti zaidi
ya 120, na kila kabila likiwa na utamaduni wake, desturi zake na Uongozi wake
(Machifu).
Hili Mwalimu Nyerere alianza na viongozi
waliofuatia baada yake wakaendelea nalo na leo tunajivuna Tanzania ndio nchi
pekee katika Afrika ambayo watu wake wana lugha moja ya Taifa ambayo sio ya
kabila mojawapo.
Mitihani ilianza mwaka 1964, wakati wa
uamuzi wa kihistoria wa kuunganisha nchi mbili zilizokuwa huru kwa maana ya
Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja mpya na huru ilopewa jina “Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania”. Wahisani wetu wakubwa wa maendeleo kipindi hicho
Ujerumani Magharibi hawakupendezwa na uamuzi huu na wakatishia kuvunja uhusiano
nasi.
Kabla hatujatishika tukajitathimini kama
Taifa, heshima yetu na umuhimu wa tunu yetu ya UMOJA. Kwa kauli moja tukavunja
uhusiano na Ujerumani Magharibi na kurudisha msaada wa fedha ambao tayari
ulikuwa umetolewa kwetu. Funzo hapa ni haijalishi tunapitia wakati gani lakini
wakati wote tunapaswa kulinda heshima na umoja wa Taifa letu.
Mtihani wa pili ulikuwa mwaka 1965, hii
ilikuwa baada ya kikundi cha watu wachache kujitangazia uhuru kule Zimbabwe ya
leo (Unilateral Declaration of Independence). Tanzania iliamini katika uhuru wa
kweli na wa wengi nchini humo. Tukawaeleza waingereza kwamba tabia ile ni mbaya
na haikubaliki na kwa kuwa Uingereza ndiye dada mkubwa katika familia ya
Jumuiya ya Madola tukamtaka achukue hatua dhidi ya utawala wa wachache
uliojitangazia uhuru chini ya bwana Smith.
Waingereza walisua sua na hata baada ya
nchi za Afrika kulaani vikali kitendo kile bado hawakuchukua hatua kali na
stahiki. Kati ya Nchi za Afrika huru ni Tanzania na Ghana tu ndio zilizovunja
mahusiano na Uingereza, kitendo hiki kililenga kupeleka ujumbe kwamba
hatuukubali unyonyaji wa aina yoyote iwe Tanzania au nje ya Tanzania na hasa
kwa mataifa rafiki kipindi kile.
Mwaka 1970-75 tukapata ukame mkubwa
katika nchi yetu, wakati hali hiyo ikiendelea tukatoka na mikakati ya kupambana
na hali hiyo kwa kuanzisha skimu kadhaa za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji
wa chakula nchini. Haikuwa kazi rahisi, ilitaka Chama, Serikali na Umma wa
Wananchi kuwa na uelewa wa pamoja wa hali iliyokuwa inatukabili na kusimama
imara pamoja ili kukabiliana nayo.
Tukavuka salama, na mwaka 1977 tukaandika
historia nyingine kubwa ya kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka mmoja baadaye tukaingia katika Vita
dhidi ya Nduli Iddi Amin, vita ya Kagera. Vita hii ilitupa heshima kubwa maana
tuliipigana wenyewe na licha ya kwamba Nduli alisaidiwa na mataifa mengine
lakini Wananchi wa Tanzania na Jeshi letu la Wananchi (JWTZ) tukamfurushia
mbali hadi nje ya mipaka yetu. Vita ya Kagera licha ya heshima kubwa ilituacha
katika wakati mgumu sana kiuchumi maana tulitumia karibia hifadhi yetu yote ya
fedha za kigeni ambayo hutumika kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje.
Kuna kipindi tulifika tukabaki na akiba
isiyozidi wiki mbili ya Mafuta ya Magari, ulikuwa wakati mgumu sana. Huwa
nafananisha Uongozi wa Nchi kama Uongozi wa familia inayojitahidi sana
kujikwamua kihali na kiuchumi licha ya changamoto mbalimbali. Baba au Mama
anaweza kurudi nyumbani na chakula hakuna na ilhali watoto hujua baba au mama
lazima awe na uwezo wa kuleta chakula nyumbani. Nadhani Mama na Baba wote
wataungana na mimi kwamba hakuna wakati mgumu ambapo watoto wanakutegemea
uwawezeshe na hauko katika uwezo wa kuwezesha lakini unapambana uwawezeshe
maana hawawezi amini kwamba baba au mama hawezi kuwezesha mahitaji yao.
Miaka ya Themanini (80) ikawa na
Changamoto zaidi na ukiongeza na masharti gandamizi ya Taasisi za Kifedha za
Kidunia zijulikanazo kwa kiingereza kama “Britton Woods Institutions”.
Wakatulazimisha Serikali isifanye tena uzalishaji na iachane na umiliki wa
mashirika ya umma, wakalazimisha tushushe thamani ya fedha yetu (shilingi ya
Tanzania) na wakatueleza ili tupate misaada kutoka kwao kwanza ni lazima
turidhie masharti haya niliyoyataja kwa uchache na tukubali kutekeleza programu
za kurekebisha uchumi wetu (Structural Adjustment Programmes – SAPs).
Kibaya zaidi na kwasababu tulikuwa na
msimamo wa kuendelea na Mapambano ya kuukomboa Uchumi wetu dhidi ya mikakati ya
kinyonyaji ya kibeberu iliyokuwa inatambulishwa na Taasisi hizi za kifedha za kidunia,
waliamua pia kutuhujumu waziwazi.
Hujuma ya uchumi wetu ilikuwa kutoka nje
na ikiratibiwa kimkakati kabisa na ilikuwa pia kutoka ndani ikiratibiwa kwa
ustadi na vibaraka wa mabeberu, watanzania wachache waliokosa uadilifu,
uaminifu, uzalendo na mapenzi ya dhati kwa Taifa letu.
Vilikuwepo viwanda zaidi ya 400 na migodi
kadhaa, lakini viwanda na migodi inapojiendesha kila baada ya muda huhitaji
vipuri, basi kila tulipoagiza vipuri kutoka kampuni za nje walitoa visingizo
mbalimbali, mara kampuni zimeuzwa au kampuni ilishafilisika na kadhalika na
kadhalika. Hivyo baada ya muda viwanda vingi vilikosa vipuri na kulazimika
kusimama na watu kupoteza ajira. Hali kama hiyo ilitokea katika migodi kadhaa
na ikailazimu serikali kuweka mpango wa kuifunga migodi hiyo.
Hata pale tulipoamua kampuni yetu ya
kizalendo Nyumbu itengeneze vipuri hapa hapa nchini basi mataifa makubwa
yalififisha dhamira njema ya kampuni za kizalendo kwa kutoa misaada ili kampuni
za ndani zishindwe kufanya biashara, zishindwe kujiendesha na hatimaye
kuanguka.
Changamoto ziliongezeka sana kwasababu
tulisimamia haki huku tukiendelea kupinga udhalimu. Ililazimu serikali itafute
mbinu mbadala ya kujiendesha na ndipo mawazo kama ujenzi wa bwawa la kuzalisha
umeme la Stiegler’s Gorge likaja lakini uwezo wa kujenga hatukuwa nao wakati
huo.
Mwalimu alijua huenda katika pwani yetu
tunaweza kuwa na gesi au mafuta na akazungumza na nchi fulani za Magharibi ili
kuja kufanya utafiti wa uwepo wa mafuta na gesi. Wataalamu wa kimagharibi
wakaja na wakafanya utafiti na kusema hakuna dalili yoyote ya mafuta au gesi.
Mwalimu alikuwa mvumilivu na hakuwa mtu
wa kukata tamaa, na alizungumza na marafiki zetu wa India ambao walikuja hapa
na wakachoronga maeneo machache ya pwani ya Tanzania (Pwani na Lindi) na hatimaye
gesi ikapatikana, wakamwambia imepatikana na wakalipua kisima kimoja na
kikawaka moto bila kuzimika kwa miezi mitatu. Mwalimu Nyerere akawaambia
wakizibe kisima hicho na pasijulikane pahala pale mpaka watakapokuwa tayari
hapo baadaye.
Kuna kipindi tulipokuwa tukifanya
mashauriano (negotiations) katika masuala ya kiuchumi ili “mabwana wakubwa” ama
walegeze kamba au watusaidie, ilitubidi sisi kusafiri kuwafuata, mfano, kule
Ulaya katika vikao vya Paris Club, vikao hivi wanakaa matajiri wa dunia na mataifa
makubwa. Mzee Cleopa David Msuya alishiriki kule, ilikuwa lazima uwafuate Ulaya
mabwana wakubwa kule, na kuna kipindi aliwafuata na aliishia mapokezi, ubeberu
bila kugangamala una jeuri, kiburi na dharau sana.
Napenda watu wajua safari yetu imekuwa yenye
milima na mabonde lakini kitu kimoja cha kujivuna tumebaki na Taifa moja. Ni
wajibu wetu kukumbushana tulikotoka ni mbali na hasa vijana na watoto wetu.
Tulipo
sasa
Tanzania iko katika awamu ya Tano ya
Uongozi wake tangu kuasisiwa kwake. Baada ya vipindi viwili vya awamu ya Nne,
CCM iliamua kufanya Mageuzi Makubwa ambayo yanahakikisha chama hiki kinabaki
kuwa Chama cha Wanachama na kinachoshughulika na shida za watu wetu.
Mageuzi ya CCM yanalenga pia kuhakikisha
katika kila mawanda haki ya watanzania inapatikana. Taifa hili ni tajiri sana
na linaweza kujitosheleza ndani lakini tumeshindwa kwa muda mrefu kujenga uwezo
wa ndani ili kutimiza ndoto hii ya kujitegemea ama kwa unyonge au wakati mwingine
kwa uzembe wa baadhi yetu.
Chama Cha Mapinduzi baada ya
kujitathimini kikatafuta mtu ambaye ataweza kuishika agenda ya Mageuzi ya CCM,
na ieleweke Mageuzi ya CCM yatatoa mwelekeo kwa Mageuzi ya Serikali ili sote
tuweze kukidhi na kuweka jitihada kubwa ya kutosheleza mahitaji na matarajio ya
msingi ya watanzania.
Mtu huyu ambaye ameaminiwa kwanza na wana
CCM kisha watanzania ni Ndugu yetu John Pombe Joseph Magufuli, mtanzania kweli
kweli na mwenye uchungu wa kuhujumiwa kwetu. Mtu ambaye CCM ilimleta (Ndg.
Magufuli) ilipasa awe mtu ambaye hatatuonea soni, hataleta urafiki, hataona
haya kutuambia hapa na pale tulikosea.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitafakari na
kuamua kutuletea Ndg. Magufuli ili pia aweze kutusimamia kwa haki tena pasina
kujiona mnyonge hata mbele ya wabwana wakubwa wa ndani na nje ya nchi.
Leo Afrika nzima inazizima kwamba yuko
mwanaume ambaye ameweza kusema imetosha “enough is enough” sio haki na ni unyonyaji
kuchukua madini yetu katika namna ambayo haki yetu inapokwa. Ndugu Magufuli ana
amini sana katika sekta binafsi na hasa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda
sambamba na sekta ya umma, lakini ana amini zaidi katika sekta binafsi
inayojiendesha kwa kanuni za maadili ikiwemo kulipa kodi. Ana amini katika
uwekezaji kutoka nje, lakini unaotambua kwamba sisi ni Taifa huru na tunayo
haki ya kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zetu.
Ndugu Magufuli ana amini kwa hakika
uwekezaji kutoka nje unapaswa kujengwa katika misingi ya haki na usawa na
kwamba kila upande una wajibu Tanzania na wawekezaji, Tanzania iweke mazingira
ya uwekezaji hasa wa viwanda na wawekezaji watende sawa sawa na kanuni za
kidunia za maadili ikiwemo kutokuiba kwa ujanja ujanja, kutokwepa kodi,
kutosafirisha pesa kwenda nje “capital flight” wakati zinawezwa kutunzwa hapa
na kadharika.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemleta ndugu
Magufuli wakati muafaka wakati tunamhitaji zaidi mtu kama yeye. Ukisoma Maelezo
na Nukuu za Mwalimu Nyerere katika maelezo yangu ya awali juu ya Maono ya
Mwalimu Nyerere utaungana nami kusema ile aina ya Uongozi mpya katika bara la
Afrika, Tanzania tumekuwa kinara wa kwanza na wengine watafuata ili bara la
Afrika lirejeshe heshima yake ya uhalisia na asili.
Wiki ijayo nitaeleza kuhusu tunakokwenda
na kwanini Ndugu Magufuli ni zawadi na tumtumie katika kipindi hiki cha mpito
na cha kunyooshana nidhamu ili maisha yetu katika miaka mikuu 75 “The Great 75
Years” iwe rahisi na yenye mafanikio makubwa hii ni kati ya Mwaka 2025 na Mwaka
2100. Huu ni wakati wa siasa za Maendeleo na sio siasa za Madaraka.
Makala
hii imeandikwa na Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi