Mabadiliko
ya Katiba ya CCM 2017 yamegusa maeneo gani?
Hivi
karibuni kumekuwapo maneno ya upotoshwaji juu ya Mabadiliko ya Katiba ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika tarehe 12 Machi 2017. Napenda kufafanua kwa
uchache maeneo ambayo yamefanyiwa Mabadiliko ili kuanzia sasa ieleweke bayana
kwamba msingi wa Mabadiliko haya ni Mageuzi Makubwa ambayo yanafanywa na Chama
chetu ili kuongeza tija, ufanisi, uwajibikaji, kupunguza gharama za uendeshaji,
kupiga vita rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Mageuzi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanalenga kutizama Uongozi (Leadership),
Muundo/Mfumo (Structure/System) na Utawala (administration). Chama chetu
kimetimiza miaka 40 mwaka huu (2017) tangu kuanzishwa kwake na kipindi hiki
tumeazimia kwa kauli moja kukiimarisha, kukijenga na kukifanya madhubuti. Kazi
hii ya Mageuzi ya CCM ilianzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokaa
katika Mkutano wake wa mwenzi Desemba 2016 na baadaye kupitishwa kwa sauti moja
na Mkutano Mkuu Maalum wa Machi 2017.
Ikumbukwe
kwamba mabadiliko haya ya Katiba yangaliweza kupendekezwa na kuanza kutumika
pasina ya kuitisha Mkutano Mkuu, lakini hekima ya Uongozi wa Chama chini ya
Mwenyekiti Ndugu Magufuli na Katibu Mkuu Ndugu Kinana ikatuongoza kwamba
Mabadiliko haya ambayo yanajenga msingi wa Mageuzi ya Chama chetu lazima
yashirikishe wanachama wetu.
CCM
kama chama cha siasa ili kifanye kazi yake vizuri na yenye matokeo makubwa
chanya, ilikusudiwa lazima kihuishwe ili kiweze kwenda na wakati na kutekeleza
matakwa ya wanachama, kwa kuzingatia ukweli kuwa lengo kuu la chama chochote
cha siasa ni kushika dola.
Mabadiliko
ya Kikatiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yana lengo la kukiimarisha chama chetu
ili kuziteka hisia, mioyo na fikra za watanzania wengi, kwa nia ya kukiunga
mkono katika lengo lake la kushika dola na kuleta maendeleo endelevu kwa
watanzania.
Katiba
ya CCM imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara tangu ilipotungwa mwaka
1977, kwa madhumuni ya kuiboresha ili iendane na wakati uliopo. Kwasababu hiyo,
yamekuwepo matoleo 12 ya Katiba hii hadi mwaka 2012. Katiba ambayo imepitishwa
na Mkutano Mkuu Maalum tarehe 12 Machi 2017 jijini Dodoma, inakuwa toleo la 14.
Mabadiliko
haya yanalenga kurekebisha Muundo, Mfumo, Uongozi, Utendaji na mengineyo.
Kabla sijaeleza kwa kina zaidi nipende kuondoa sintofahamu ambayo imejengwa na watu ambao wamekuwa wakipotosha kwa makusudi taarifa za Chama, Hakuna katika kikao chochote ambacho tulijadili kuhusu Uchaguzi wa 2020 wala hakuna popote ambapo vikao vyote vya maamuzi vilizungumzia mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwa nafasi ya Urais ifikapo 2020.
Kabla sijaeleza kwa kina zaidi nipende kuondoa sintofahamu ambayo imejengwa na watu ambao wamekuwa wakipotosha kwa makusudi taarifa za Chama, Hakuna katika kikao chochote ambacho tulijadili kuhusu Uchaguzi wa 2020 wala hakuna popote ambapo vikao vyote vya maamuzi vilizungumzia mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwa nafasi ya Urais ifikapo 2020.
Mambo
muhimu ambayo yamezingatiwa katika marekebisho haya ni yafuatayo; -
MFUMO WA CHAMA
Mfumo
wa Chama, una sura ya serikali na utawala na kuwa na ngazi nyingi ya vikao vya
uamuzi. Hali hii inafanya gharama ya kukiendesha Chama kuwa kubwa, vikao
haviitishwi na maamuzi ya chama hayawafikii walengwa. Hivyo basi yafuatayo
yanazingatiwa,
Kupunguza
wingi wa vikao vya nadharia na badala yake kuwa na vikao vichache
vinavyofanyika, vyenye maamuzi yenye tija na kujenga uhai wa chama.
Kupunguza
idadi ya wajumbe au wawakilishi ili wawe wachache lakini wenye umakini na uwezo
wa kusimamia sera, itikadi, maamuzi ya chama pamoja na kuondoka urasimu na
kupunguza gharama za uendeshaji pasina kuathiri ubora wa uwakilishi.
Muundo
wa Wilaya za Chama uendane na uundo wa sasa wa wilaya za Serikali
Uzito
mkubwa umewekwa katika kuimarisha chama katika ngazi ya shina, eneo ambalo
ndilo waliko wapiga kura. Kwa kufanya hivyo, chama kitakuwa karibu na watu na
watakiona kuwa ni chama chao.
Uendeshaji
wa shughuli zote za jumuia za chama na mali zake uwe chini ya usimamizi wa
Chama cha Mapinduzi na Baraza la Wadhamini la Chama cha Mapinduzi.
VIONGOZI
Viongozi
wachache wamekuwa na tabia ya kujilimbikizia nafasi nyingi za Uongozi, utendaji
na uwakilishi katika Chama na Serikali. Hali hii hushusha ufanisi na kupunguza
tija. Nafasi nyingi kwa mtu mmoja ni kushindwa kuleta ufanisi katika vikao
husika.
Hapa
imezingatiwa kuwa; ukiacha wale wanaolazimishwa kikatiba kuwa na nafasi zaidi
ya moja kwa mujibu wa mamlaka yao, kuanzia sasa nafasi za Uongozi katika chama
zitakuwa si zaidi ya moja.
KURA YA MAONI
Mfumo
wa kura za maoni hukusudia kuimarisha demokrasia ndani ya chama na kuashiria
nafasi ya mgombea anayeonekana kukubalika zaidi. Hata hivyo, eneo hili limekuwa
na matokeo mabaya ya kukithiri kwa rushwa na kupata viongozi wasio na imani ya
kweli ya chama wanaosaka maslahi, wafanyabiashara wenye malengo binafsi na
mamluki.
Mapendekezo
ya kuimarisha udhibiti wa kura za maoni; -
Katiba
ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 61A(1-3) inaelekeza kura za maoni
za ubunge na uwakilishi zitapigwa kwenye mikutano mikuu ya jimbo na si kwa
wanachama wote matawini kama ilivyofanyika mwaka 2015.
Imependekezwa
ili kudhibiti taratibu za kura za maoni jimboni, kuepusha migawanyiko, kuziba
mianya ya rushwa na kuepusha wapiga kura mamluki, inapendekezwa kufanya
mabadiliko ya upigaji kura za maoni za ubunge na uwakilishi pamoja na kufuata
utaratibu ufuatao wa kuwajadili wanaogombea;
Wagombea
ubunge/uwakilishi watachukua fomu na kurudisha kwa Katibu wa CCM wa Wilaya
inayohusika. Fomu zote za wagombea ubunge/uwakilishi zitajadiliwa na kutolewa
mapendekezo katika ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa kabla ya kupigiwa kura za
maoni.
Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itateua majina yasiyozidi matatu ambayo
yatawasilishwa mbele ya Mkutano Mkuu wa Jimbo kwa ajili ya kupigiwa kura za
maoni. Mkutano Mkuu wa Jimbo utapiga kura za maoni kumpendekeza mwanachama
mmoja awe mgombea wa ubunge/uwakilishi katika jimbo hilo.
Mara
ya baada ya kura za maoni, mapendekezo ya uteuzi yataanzia kwenye Kamati ya
Siasa Jimbo (kwa Zanzibar), Kamati ya Siasa ya Wilaya (Tanzania Bara), Mkoa,
Kamati Maalum (Kwa Zanzibar), Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu ya Taifa
itafanya uteuzi wa mwisho.
Utaratibu
huu hautawapa fursa wagombea kutengeneza makundi na kutoa rushwa kwasababu
hakuna anayejua kama atakuwepo kwenye orodha ya wagombea. Wale wana CCM wenye
tabia ya kujiandaa na vyama zaidi ya kimoja, kwa utaratibu huu hawataweza
kujiandaa mapema kuhamia vyama vingine. Utaratibu huu pia utasaidia kuondoa
urasimu na migawanyiko isiyokuwa na sababu.
Aidha,
utaratibu huu utahakikisha anapatikana mgombea mwenye msimamo thabiti wa Chama
na ni utaratibu halisi kwa chama kuusimamia ipasavyo.