Hapa nikisaini kiapo
Hapa nikitoa neno kwa umma wa wana Musoma na watendaji wa Halmashauri
SALAMU ZANGU KUTOKA WILAYA YA
MUSOMA
Ndugu zangu wapendwa na watanzania,
nawasalimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa kibali.
Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini, kunipa heshima na dhamana ya kuwa
Msaidizi wake katika nafasi ya madaraka ya utumishi na uongozi kama Mkuu wa
Wilaya ya Musoma.
Wilaya ya Musoma ina maeneo mawili
ya kimamlaka kwa maana ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Musoma na yenye
zaidi ya wakazi 360,000. Dhamana hii niliyopewa na Mhe. Rais, inanilazimu
kuhakikisha ustawi wa watanzania waishio Wilaya ya Musoma unaimarika, dhamana
hii inakwenda sambamba na kuhakikisha Serikali (Kuu, Manispaa na Halmashauri)
tunaenenda katika namna ambayo inakuza na kuongeza tija kwa maisha ya wananchi
tuliopewa dhamana ya kuwahudumia na kuwaongoza.
Nimeupokea Uteuzi wa Mhe. Rais kwa
furaha na heshima kubwa, Nimewaahidi wakazi wa Musoma kuifanya Musoma MFANO wa
Kuigwa katika kila nyanja, ni lazima tushirikiane, tushauriane, tusaidiane na
kuelekezana katika namna ambayo ni ya UWAZI na inazingatia misingi ya UKWELI, HAKI,
UMOJA, UWAJIBIKAJI na UADILIFU.
Kwa kipindi cha mwezi hivi
nitapotea ili kujifunza na kuielewa Musoma, kuwafahamu na kuwajua watumishi
wenzangu katika Wilaya ya Musoma.
Hapo awali nalipata heshima na
fursa ya kuaminiwa dhamana ya uongozi katika ngazi ya Kitaifa kama Kamishna wa
Tume ya Katiba. Kazi ya Ukamishna wa Tume ya Katiba, ilinipa fursa ya kuiona
Tanzania, kuielewa Tanzania, kuijua misingi ya kuanzishwa nchi yetu. Kazi ya
Katiba ilinipa fursa ya kutembelea Nchi nzima na kuzijua kero, changamoto,
shida, manung'uniko, lakini pia nilijua fursa adhimu mbalimbali zilizopo katika
nchi yetu. Nalipata bahati ya kukaa Mkoa wa Mara kwa miezi miwili ikiwemo
Wilaya ya Musoma. Kazi ya Katiba ilinipa fursa ya kuiona Tanzania katika jicho
la Uongozi wa Nchi lakini pia kusikiliza matakwa, matamanio na matarajio ya
wananchi wenzangu wa Tanzania. Nilipata fursa ya kufanya kazi na viongozi
waliopo madarakani katika ngazi ya Taifa na viongozi wastaafu na hakika
nimejifunza mengi na ninaendelea kujifunza mengi zaidi kutoka kwa viongozi
hawa. Wamenifunza juu ya Misingi ya Taifa, Katiba, Sera, Sheria, Kanuni,
Miongozo, Utamaduni na desturi za Serikali na Mamlaka za Nchi.
Mheshimiwa Rais ameniamini na
kuniongeza fursa ya kuifahamu Nchi yangu kwa kukaa na wananchi wetu kila siku
kama mtu mwenye nafasi ya madaraka (dhamana) ya kushirikiana na wananchi
kutatua changamoto zao na kuhakikisha dhamira na ndoto ya Mheshimiwa Rais
ambayo ameelekezwa na watanzania inatimia na kuwa hakika kweli.
Mimi nahisi kupendelewa kipekee,
Mkoa wa Mara na hasa Musoma ndio Muasisi wa Taifa hili alizaliwa na kukulia,
lakini pia wazee wangu wa nguvu ninaowapenda kupitiliza (hawa ni kama
nimpendavyo Mzee Polepole) wamezaliwa katika Mkoa huu, Mzee wa Nguvu Mhe.
Joseph S. Warioba, Mzee wa Nguvu Joseph W. Butiku na Balozi Marwa. Hili
linanipa mguso wa kipekee sana kujituma na kuuishi utume wa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere wa kujitoa maisha yake kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Kwa
hili Nakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipendelea
Kama kazi ya Tume ilikuwa Darasani,
Hapa niko Maabara, kufanya majaribio na utekelezaji wa elimu niliyoipata shule
na kutoka kwa malezi na maongozi ya viongozi ambao nimepitia mikononi mwao.
Mpaka sasa nimetambua hakika hakuna
kazi nyingine kwa wakati huu ambayo itaniweka karibu na wananchi na kuwaelewa
kama nafasi ambayo Mheshimiwa Rais amenipa dhamana ya kumsaidia.
Kwa msaada wa Mungu hakuna kero
ambayo hatutaitatua, hakuna changamoto ambayo hatutafanyia kazi na hakuna kero
ambayo hatutaishughulikia.
Nitaendelea kutumia fursa hii
kuendelea kujenga uwezo wa vijana wenzangu katika uongozi maana sasa tumepata
"kisa mafunzo"
Kipekee nimshukuru sana Mkuu wa
Mkoa wa Mara Mheshimiwa Magesa Mulongo, ananipa ushirikiano, maongozi,
maelekezo, ushauri na amenipa uhuru wa kutenda na kujiamini au kimombo "to
exercise leadership". Yeye ana upeo Mkubwa na Uzoefu, na hakika uwepo wake
Mkoa wa Mara unatosha kutupa hamasa ya kumsaidia kufikia Mara ambayo ni Mkoa wa
Mfano kwa Tanzania.
Niwashukuru Wakuu wa Wilaya
wenzangu wa wilaya zote za Mkoa wa Mara, upendo mlionionesha mpaka leo hakika
umenifanya nisiikose (nisi-imiss) Dar es Salaam, ninyi ndio ndugu zangu
kiutumishi na kiuongozi, nitashirikiana nanyi, nitajifunza kwenu na nitawaomba
ushauri kila mara.
Kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na
Wilaya ya Musoma, nina maelekezo ya kuwahudumia kwa kauli mbiu na falsafa ya
HAPAKAZITU!!
Mungu awabariki
Mimi Rafiki yenu Mpendwa