Nianze na nukuu hizi mbili
kuntu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere- Mwenyezi Mungu amrehemu.
“Democracy is not a bottle of Coca-Cola which you can import. Democracy
should develop according to that particular country”. June 1991 in Rio De
Janeiro, Brazil
"Demokrasia
sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza. Demokrasia lazima ikue na
kuendelezwa kulingana na nchi husika". Juni 1991 Rio De Janeiro, Brazil
(Tafsiri ni yangu)
“No nation has the right to make decisions for another nation; no people
for another people”. From ‘A Peaceful New Year’ speech, Tanzania, January 1968
"Hakuna Taifa
lina haki ya kufanya maamuzi juu ya Taifa lingine; wala watu juu ya watu
wengine ". Hotuba ya Amani ya Mwaka Mpya, Tanzania, Januari 1968 (Tafsiri
ni yangu)
Hili la Marekani
na uamuzi wa MCC ni jambo la mpito na haliwezi kuua mahusiano yetu na Marekani.
Tanzania na Marekani zinashirikiana kwa mambo mengi na MCC ni sehemu tu tena ni
eneo jipya la ushirikiano. Uamuzi huu ni jaribio kwa uhuru wa Taifa letu. Hakuna
namna nyingine ila kushinda hili kama tulivyoshinda mengine huko nyuma. Kwa
wale ambao wameuona umri watakumbuka namna tulivunja uhusiano na Ujerumani
Magharibi 1964 pale walipotaka kuwa na kauli hasi dhidi ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Tulivunja uhusiano
na Ujerumani Magharibi baada ya kutaka kuingilia Uhuru wa Mataifa Mawili huru
yaliyoamua kuungana na kuunda Nchi Mpya ambayo leo tunajivunia, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. 1965 Tulivunja uhusiano na Uingereza kufuatia na kitendo
cha wazungu wachache kujitangazia Uhuru (Unilateral Declaration of
Independence) kule Rhodesia na uingereza kukaa kimya na kushindwa kuchukua
hatua stahiki.
Tulivunja Uhusiano
na Uingereza kuieleza Dunia kwamba Uhuru wa nchi za Afrika ni kipaumbele muhimu
kwa Tanzania. Jambo tunalopaswa kufahamu
ni kuwa MCC 2 toka mwanzo imekuwa ni mtihani
dhidi ya uhuru wetu. Napenda ieleweke kwamba kipindi hiki kilichotokea
sio kuvunjika kwa uhusiano wetu na Marekani bali taasisi ya MCC ndio imesitisha
msaada wao kwetu, lakini mahusiano yetu na marekani bado yako pale pale, na si
Marekani au Tanzania inayoweza kuugharimu uhusiano wetu.
MCC 1 ilikuwa ni
chambo cha kutuvuta na tulipewa bila masharti tena hela nyingi dola milioni 698
na ni fedha tulizopewa moja kwa moja na kupewa uhuru wa kuamua tuzitumieje. Tanzania
ilitakiwa kuainisha maeneo kisha wao wanatoa hela. Ndio maana miradi kama ile
barabara ambazo hazikuwa zikipata ufadhili kwa kuwa hazikuonekana ni za
kiuchumi na miradi ya maji ya Morogoro na kwingineko iliingizwa humu na kupata
ufadhili. MCC 2 sio hivyo. Kwenye MCC 2 walengwa wakubwa ni sekta binafsi ya
Marekani, hapa kuna mtego hapa, hapa ni biashara hapa.
Mchakato wa MCC 2
ulipoanzishwa, wafanyabiashara kwa kushirikiana na Maseneta wakaanzisha hoja
kuwa kwanini Marekani inatoa fedha kwa ufadhili katika nchi ambazo China ndio
wenye kufaidika na fedha hizo? Wakaleta hoja ya kuwa Serikali ya Marekani
ifanye jitihada ya kuweka fedha kwa kusaidia Sekta Binafsi ya Marekani kupenya
Afrika.
Ukaitishwa mkutano
wa US-Africa Summit na agenda kubwa ikawa Power Africa. Katika Power Africa,
Marekani ikalichagua eneo la Nishati (si uzalishaji viwanda) kwa kutambua kuwa
ndio eneo pekee wanaloweza kushindana na wachina. Wakasema wataelekeza fedha
huko kuisaidia Afrika kutatua tatizo la nishati ambalo ndio pembejeo ya
viwanda. Wakaweka sharti kuwa fedha hizo na miradi hiyo itatekelezwa na Sekta
Binafsi ya Marekani.
Ndio sababu wengi
wenu mtakumbuka hata Rais Obama alitangazia dhamira ile pale Ubungo kwenye
Mitambo ya Symbion Power na sio kwamba alipenda kwenda kutembea Ubungo. Kuanzia
hapo kumekuwepo na shinikizo kubwa sana na masharti magumu na yenye kuhamahama
(shifting goal post) kutaka kuibaka sekta ya nishati nchini ikiwemo mageuzi ya
TANESCO. Zikaainishwa hatua kadhaa,ambazo utekelezaji wake baadhi ni kisheria
na kisera na hivyo haziwezi kwenda kwa deadline walizotaka. Kila bodi ikikutana
wanaibua hiki na kile lakini wakisema hela watatoa. Hela hizi zikawa zimeshikiliwa
kama chambo ukisogelea zinasogea, ni sawa na ule mchoro wa Mpanda Punda aliyeshika fimbo yenye majani na akiielekeza mbele ya punda, kwamba punda
ataendelea kuyafuata majani akidhani atayafikia kumbe ndio anaupiga mwendo.
Hatimaye wakasema wanasubiri uchaguzi mkuu jambo ambalo halihusiani na madai ya
mwanzoni. Baada ya uchaguzi wakaibuka na suala la Zanzibar.
Hivyo, uamuzi wao
wa leo ni uamuzi uliotarajiwa. Pia ni uamuzi wenye madhara kwa sekta binafsi ya
Marekani pia ambayo ndio ilikuwa itekeleze miradi hiyo. Kama Taifa ni muhimu
kulinda utu na uhuru wetu. Ndio msingi wa sera yetu ya nje toka mwanzo na hata
sasa. Tumetofautiana na Marekani katika hili tutapatana katika mengine. Ndio
uhai wa maisha ya diplomasia.
Wao nao wanayo hadhira
ya wapiga kura wao wanayojaribu kuituliza huko nchini kwao kwa uamuzi huu.
Tunapaswa kuheshimu uamuzi wao kama ambavyo wanapaswa kuuheshimu wetu. Hatimaye
baadae tutapatana. Marekani inaihitaji Tanzania zaidi na Tanzania inaihitaji
Marekani. Marekani inahitaji MCC 2 zaidi hali kadhalika Tanzania inahitaji MCC
2.
Mahusiano ya
Tanzania na Marekani hayakuanza na hayataisha na MCC. MCC imeyakuta na
itayaacha.
Kama marudio ya
uchaguzi wa Zanzibar ndio kigezo, basi Marekani isingekuwa inatoa zaidi ya Dola
Bilioni 3 kila mwaka kwa Egypt iliyo chini ya utawala wa kijeshi kwa sababu ya
kuununua ugomvi wa Egypt na Israel na isingetoa kiasi cha dola bilioni 6 kwa
Israel kila mwaka kwa yale wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina.
Huu ni wakati
ambao Taifa linawaita Wazalendo wake. Wazalendo wasimame na kusema 'Nchi yangu
KWANZA, iwe Sahihi au Imekosea" na Makuwadi watashangilia na kusema
"si mnaona sasa kiko wapi?".
Huu ni wakati wa
kujifunga mikanda na kulinda heshima yetu kama Taifa letu. Tuna vyanzo vya
mapato vingi sana ambavyo hatujaanza kukusanya mapato, tuwe wabunifu na
tusibweteke na kutegemea mapato yataongezeka maradufu kwa vyanzo vile vile.
Niseme kwa
uchache, sababu walizotoa MCC, na ieleweke aliyetoa tamko ni MCC, heri
lingetoka tamko hili Wizara ya Mambo ya Nje au Ikulu ya Marekani, moja ni
Zanzibar na pili ni Sheria ya Makosa ya Mitandao (Cyber crimes Act).
Sasa hebu tujadili
kidogo, hivi kule Zanzibar tulitaka kitokee nini pale ambapo wanasiasa walikuwa
hawataki kujadiliana? Tume ile ile ya Uchaguzi ambayo bado ilikuwa na uhalali
wa kikatiba na kisheria kuuitisha, kuufuta na kuuitisha tena uchaguzi ikachukua
nafasi yake. Wanasiasa wasio makini wakaishia kuhamishia malumbano mitandaoni
badala ya kuitafuta suluhu ya kisiasa na pale siasa iliposhindikana basi wangeitafuta
suluhu katika mahakama za Zanzibar. Mezani wakashindwa, mahakamani hawakwenda.
Tume ikachukua uongozi, uchaguzi ukaitishwa Wananchi wakapiga kura na sasa huko
Zanzibar kuna serikali na baraza la wawakilishi. Hata mimi sifurahii sana njia
waliyoichukua Zanzibar lakini ilibidi siasa za madaraka zisite ili tuanze
kufanya siasa za maendeleo. Je wamarekani walitaka muujiza gani utokee huko.?
Kuhusu Sheria ya
Mitandao, hata mimi siipendi, si twende mahakamani, bunge litaanza vikao muda
si mrefu je wabunge si wapeleke hoja ya kuifanyia marekebisho sheria hii. Sasa
Marekani (MCC) inapoweka shinikizo kwa suala la Sheria ambayo ni jambo la ndani
na linaloweza kujadilika, sijaelewa. Mbona sie hatujapiga kelele Yule jamaa yao
Trump alipotutusi waafrika na kusema sisi stahili yetu ni kuwekwa tena chini ya
ukoloni (hapa nimechomekea tu).
INDHARI
Ni aibu kwa
viongozi wa kisiasa kufurahia jambo hili, ni ishara ya ukuwadi wa kisiasa na
ambao uko tayari kukumbatia mahusiano yanayotweza Uhuru wetu. It is now high
time kufanya siasa safi za maendeleo (politics of development) na sio kujikita
katika katika siasa za madaraka (Politics of Power).
Mwandishi, Ndg.
Humphrey Polepole amenufaika na uelewa wa watu wenye uzoefu wa mahusiano ya
Tanzania na nchi za Nje. Aidha, ni mnufaikaji (alumni) wa programu ya uongozi
chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.