Wananchi wengi tunakubalina kuwa adui
mkubwa wa Tanzania kwa sasa ni ufisadi
ambao ndio umekuwa chanzo kikubwa cha utajirisho wa watu wachache
na huku ukistawisha umaskini kwa wananchi walio wengi. Baadhi ya
wananchi wamekuwa na mawazo kuwa hatuwezi kupambana na ufisadi bila ya kwanza
kuiondoa CCM madarakani kwani kwa maoni yao CCM ndio mfumo wenyewe wa kifisadi.
Lengo langu leo ni kutaka tutafakari
usahihi wa dhana hii katika uhalisia wake ili itusaidie kuchukua hatua sahihi
katika kuung’oa mfumo wa kifisadi nchini.
Kwanza, kuna haja ya kutambua ukweli
kuwa rushwa na ufisadi ndiyo adui mkubwa wa maendeleo ya kweli ya nchi yetu.
Ukweli huu uligundulika mapema kabisa
baada ya nchi yetu kupata uhuru pale ambapo sehemu ya tabaka la watu
walioshika nafasi za uongozi baada ya uhuru kutaka kutumia nafasi zao kwa ajili
ya kujitajirisha wao binafsi kwa gharama ya wananchi wenzao. Tabaka hili
lililokuwa linajulikana enzi hizo kama wabenzi,
ikimaanisha wamiliki wa magari ya Mercedez Benz ambayo ndio ilikuwa alama
ya kuwa tajiri, liliona kuwa kushika nafasi ya uongozi katika dola ni kupata
fursa ya kijitajirisha.
Hali hiyo ingeruhusiwa kuendelea ingewakatisha tamaa
wananchi na kujenga ufa baina yao na uongozi wa nchi. Pia hali hiyo ilionekana
kusaliti matumaini ya wananchi katika kupigania na kupata uhuru. Hakika hali
hiyo ingeruhusiwa kuendelea ingefanya
uhuru usiwe na maana kwa wananchi. Kwa bahati nzuri uongozi wa TANU chini ya
Baba wa Taifa uliligundua tatizo hilo na kuchukua hatua za kukabiliana nazo.
Ili kupambana na ufisadi uliokuwa
umeanza kujengeka, mwaka 1966 , Mwalimu Nyerere baada ya kupokea changamoto
kutoka kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam waliokuwa wanaandamana, wakilalamika
pamoja na mambo mengine kuwa viongozi walikuwa wanatumia nafasi zao
kujinufaisha alipunguza mishahara ya
viongozi kwa kuanzia na kupunguza mshahara wake kwa asilimia ishirini.
Mwaka 1967, TANU ilitangaza sera ya Ujamaa na Kujitengemea iliyokuwa inalengo
la kujenga jamii yenye usawa na haki na kukomesha unyonyaji na ukupe kati ya
mtu na mtu.
Miiko ya uongozi iliwekwa ili kuhakikisha kuwa viongozi wanatumia
madaraka yao kulingana na dhamana waliyokabidhiwa na si kwa faida zao binafsi. Miiko hiyo ilidumu mpaka mwaka
1992 tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Baadhi ya Miiko hii bado ni sehemu ya katiba
ya CCM. Ibara ya 18 ya Katiba ya CCM inazuia
kiongozi:- “(1) Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake
binafsi au kwa upendeleo, au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo
lililokusudiwa madaraka hayo. (2) Kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea
rushwa, kushiriki katika mambo yoyote ya magendo au mambo mengine yaliyo
kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo.”
KUTEKWA
CCM NA UFISADI
Kwa hiyo, CCM kwa asili yake na mfumo
wake imeundwa kupambana na ufisadi na si kukumbatia ufisadi, hata hivyo tunajua
kuwa kwa miaka ya karibuni ufisadi
umemea na kukuwa kwa kiwango kikubwa nchini. Hali hii imesababishwa kwa kiwango
kikubwa na kufanikiwa kwa kundi la watu wachache lakini lenye ukwasi mkubwa
lijulikanalo kama ‘mtandao’ kufanikiwa
‘kuiteka nyara’ CCM kwa kufadhili wagombea kwenye nafasi za ubunge na Uraisi. Walioshika madaraka katika nyadhifa za uongozi
walitumia nafasi hizo kulipa fadhila kwa wafadhili wao kwa njia ya mikataba
minono lakini yenye athari kubwa kwa maisha ya wananchi. Ni katika kipindi
hichi ndio tumeshuhudia maskandali ya
kifisadi kama vile mkataba wa Richmond, Meremeta, ukwapuaji wa fedha za EPA,
n.k. Hali hii ilitokea ili ngenge la mtandao liweze kufidia gharama walizotumia
kufadhili kampeni za mawakala wao kuingia madarakani. Hali hii iliimarika zaidi
baada ya uchaguzi wa 2005.
Katika uchaguzi wa mwaka huu na kama
ilivyokuwa katika chaguzi za kuanzia mwaka 1995, ili kuendelea kunufaika na
rasilimali za nchi kundi la mtandao, limejizatiti kwa kutumia nguvu ya hela
kuingiza mawakala wao katika nafasi ya Urais.
Hata hivyo, mara hii CCM ilifanikiwa
kuzishinda jitihada za kundi hili ‘kuiteka’na
kuhakikisha kuwa mgombea wa kundi hili katika
nafasi ya Urais hateuliwi kugombea Urais kupitia chama hicho. Jitihada hizo ndio zilisababisha mgombea wa
sasa wa Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dr. John Magufuli kuteuliwa. Sifa kubwa
iliyombeba Magufuli ni kutokuwa ngenge la watu wenye fedha wanaomfadhili. Kwa uteuzi wa Magufuli, CCM inaonyesha kuwa
imejizatiti kurudi kwenye asili yake ya chama kinacho simamia maadili na miiko
ya viongozi.
KUTEKWA
NYARA KWA UKAWA
Baada ya kundi la mtandao kung’olewa CCM
na ili liendelee kunyonya na kufisadi
rasilimali za nchi, lilifanya jitihada
kubwa kwa kutumia nguvu ya pesa kuviteka vyama vya upinzani vyenye nguvu nchini
kupitia umoja wao wa UKAWA. Kwa kuelewa kuwa kundi hili linataka madaraka si
kwa sababu nyingine ila kuendelea ‘kuifaidi’ Tanzania lakini kwa gharama ya maisha ya Mtanzania wa leo na vizazi
vijavyo, waasisi wa UKAWA ambao walitoa maisha yao kuunda na kuujenga UKAWA kama njia ya kuimarisha upinzani nchini, Dr Wilbroad
Slaa na Prof. Haruna Lipumba wameamua kukaa pembeni ili kuepuka kushiriki
kuingiza madarakani mfumo wa kifisadi ambao walitumia muda na maisha yao
kupambana nao.
Hakika historia itawakumbuka viongozi
hawa kwa misimamo yao imara ya kupinga
mfumo wa ufisadi kokote hata kama
wanufaika wa mfumo huo watakuwa wao.
Maana nafasi zao ziliwahakikishia kufaidi matunda ya mfumo huo kwa sasa na
ikitokea kundi hilo likashinda uchaguzi.
KUNG’OA
MFUMO WA KIFISADI
Tumeona kuwa chanzo kikubwa cha
kuvurugika kwa mfumo wa maadili nchini ni ngenge la mtandao ambalo kwa kutumia
nguvu ya pesa limeweza kuingiza mawakala wao kwenye nafasi za uongozi kupitia
CCM. Bahati nzuri CCM wameweza kupambana na kundi hilo kwa kuzuia jitihada zake
za kuendelea kuiteka nyara. Tumeona kuwa, baada ya kushindwa kundi hilo sasa
limeuteka upinzani nchini kupitia UKAWA kwa kutumia nguvu ya fedha. Wananchi
wameshuhudia kundi hili likigawa hela kwa makundi mbalimbali ya wananchi katika
kujihakikishia wanapata uungwaji mkono ili
mgombea wao aweze kushinda Urais.
Kundi hili haliamini katika sera au
itikadi yeyote ndio maana liliposhindwa CCM limehamia UKAWA ambapo kila chama kina ilani,sera na itikadi
tofauti. Hali haliwasumbui kwa maana shida yao kama wanavyosema wenyewe siyo
sera bali kushika madaraka ili waendelee kuifisadi nchi. Kwa kuhitimisha kama tunataka kung’oa ufisadi
nchini, inabidi tuhakikishe kuwa kundi hili la haliingii tena kushika madaraka
ya nchi.