Thursday, February 26, 2015

KWA UNYENYEKEVU MKUBWA NAWASIHI VIONGOZI WANGU TUAHIRISHE KURA YA MAONI

KWA UNYENYEKEVU MKUBWA NAWASIHI VIONGOZI WANGU TUAHIRISHE KURA YA MAONI. KWA MAZINGIRA HAYA TUTAKUWA NA BORA KURA YA MAONI NA SI KURA YA MAONI BORA

Ndugu zangu watanzania naomba mlitazame hili kwa fikra chanya, na ninaomba msitukane wala msighadhibike, bali mshauriane, mjadiliane na kisha kwa pamoja na kama mnalipenda Taifa lenu kikweli kweli na si hapa mtandaoni, basi kila mmoja wenu amtafute Mbunge Wake na akamjulishe haya.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kupokea maombi ya asasi zitakazopenda kutoa elimu ya uraia kwa Katiba Inayopendekezwa na siku ya mwisho ilipekekwa mpaka tarehe 23 Februari yaani siku tatu zilizopita. Nina uhakika asasi nyingi zilizochelewa kuomba kwenye tarehe ya awali yaani Februari 10, ziliweza kufanya hivyo hadi tarehe 23.

Ni vema mkafahamu kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Kura ya Maoni Tume inaweza kuzialika asasi za kiraia kutoa elimu kwa muda wa siku 60 kabla ya siku ya kupiga kura ya maoni yaani Aprili 30. Siku hizo sitini zitaanza tarehe 1 Machi, yaani siku tatu kutoka leo tarehe 26 Februari. Mpaka leo sijaona watu wa Asasi za Kiraia ambao wamekubaliwa kutoa elimu hiyo ili waanze kati mara moja ifikapo tarehe 1 Machi kama Sheria ya Kura ya Maoni inavyoelekeza.

Kitendo chochote cha kuchelewesha Asasi za Kiraia kutoa elimu hii baada ya tarehe 1 Machi ni kitendo cha kuvunja Sheria na kuwakosea haki watanzania ambao wana haki ya kikatiba kupata elimu hii ili wawezi kufanya maamuzi sahihi ifikapo tarehe 30 Aprili 2015.

Ikumbukwe pia kwamba katika Tangazo la Tume ya Uchaguzi waliweka bayana kwamba, Tume haitagharimia asasi yoyote itakayokuwa imekubaliwa kutoa elimu ya uraia kwa Katiba Inayopendekezwa. Hii inamaanisha kwamba kila asasi ambayo itakubaliwa inapaswa kutafuta fedha za kugharimia zoezi la kutoa elimu, tayari serikali imeshasema kupitia Tume kwamba kwao hakuna fedha. Mbadala uliobaki ni kwa asasi za kiraia kutafuta fedha kutoka kwa wahisani yaani wafadhili mbalimbali wengi wakiwa wale wa kidesturi kwa maana ya Balozi mbalimbali pamoja na mashirika yanayotoa ruzuku ya kimataifa na ya hapa nyumbani.

Ni vema mkafahamu kwamba ili taasisi itoe fedha kwa asasi mpya inapaswa kwanza mambo kadhaa yazingatiwe ikiwemo taasisi itoayo fedha kujiridhisha kwamba asasi inayoomba fedha ina uwezo wa kusimamia kwa uadilifu na kwa malengo husika fedha itakayotolewa. Taasisi itoayo fedha pia hupenda kujiridhisha kama taasisi inayoomba imepata kukubalika na mamlaka ya nchi kufanya kazi hiyo na kwa maana hii ya sasa, hakuna mfadhili ambaye atatoa fedha bila kupata nakala ya kibali kutoka kwa Tume ya Uchaguzi kwenda kwa asasi ya kiraia husika. Muda muafaka kwa mfadhili kutoa fedha mpya kwa asasi ya kiraia ambayo ana uhusiano nao huwa si chini ya wiki mbili ukijumlisha uidhinishwaji wa ruzuku, kusaini makubaliano pamoja mchakato wa kibenki. Kama ni uhusiano huo ni mpya kwa wengine ni miezi mitatu hadi mwaka mmoja, na kama kuna mazingira maalum basi si chini ya mwezi mmoja na hapo ni kama asasi ya kiraia iko vema katika uadilifu wa kimfumo, kiuongozi na taswira yake.

Sasa tujadili, leo tarehe 26 Februari, ni Asasi gani ya Kiraia iliyopo nje ya Dar es Salaam ambayo itaweza kupata fedha za kuendesha elimu ya uraia kwa Katiba Inayopendekezwa kabla ya tarehe 1 Machi? yaani ndani ya siku hizi 3? Ili ianze kazi hiyo tarehe 1 Machi.

Asasi za Kiraia hazitaweza kabisa kutoa elimu kwa muda uliopangwa na kwa ufanisi katika mazingira haya. Ninayasema haya nikiwa na uhakika wa namna mazingira magumu katika kupanga (planning) yanaweza kuathiri ubora wa elimu ya umma ya uraia juu ya Katiba Inayopendekezwa.

Ni vema ikafahamika muda wa Kampeni kwa Kura ya Maoni bado ni siku 30 kabla ya tarehe 30 Aprili. Itakuwa kitendo cha ajabu kabisa kama elimu ya Katiba Inayopendekezwa tutaitoa kwa kulipua lipua halafu tukawalazimisha wananchi kusema ndio au hapana. Hawa ndio wenye nchi na raia wa Taifa letu.

Tafsiri yangu kwa changamoto hizi za muda, uwezeshwaji wa kifedha na maadalizi ya kutosha kutoa elimu kwa weledi, ufanisi na kuwafikia watu wengi zaidi, ni kwamba hatuwezi kuwatendea haki watanzania. Wananchi wa Tanzania ndio msingi wa Mamlaka yote ya Nchi yetu na Raia ndio cheo cha msingi katika taifa letu, vyeo vinginevyo ni chini ya hapo. Kama Raia wa Tanzania ni msingi wa Mamlaka yote, sisi kama viongozi kwa nafasi yoyote katika umma wa Taifa letu tunapaswa kuheshimu haki zao za msingi ikiwamo kuwapa elimu ya kutosha juu ya Katiba Inayopendekezwa ambayo ndio inapendekezwa kuwa Sheria Mama, Msingi wa Sheria na Katiba ya Taifa letu.

Kukimbizana huku kunatoka wapi? kwa faida ya nani? na hasara ya nani? Wahenga wamepata kusema haraka haraka haina baraka.

Kwa kila msomaji wa maelezo haya nakusihi nenda kajadiliane na Mbunge wako na umueleze uhalisia huu, anza kuwa na endelea kuwa raia makini wa Taifa lako. Kuipenda Nchi yako na kuwajibika kwa Nchi yako na kuona tunaenenda sawasawa kama Taifa ni Ibada tosha ya Mwenyezi Mungu.

Wajulishe wengine Ujumbe huu. Sambaza Uzalendo, huu ndio upendo kwa Taifa lako