Saturday, June 27, 2015

WAO WAKIITIZAMA IKULU, SISI TULITIZAME TAIFA HUKU TUKIWEKA UCHAMA PEMBENI



Dhana ya kulitizama Taifa

Kwa hali ilivyo sasa ninaona jotoridi ikizidi kupanda katika vyama vya siasa hasa ukizingatia michakato ya ndani ya vyama ya kuteua watakaopewa dhamana ya kugombea nafasi za udiwani, ubunge na Urais. Kwa kiasi kikubwa kabisa, naona Wananchi wakigubikwa na mjadala wa nani ni nani na huenda nani atapata nini. Mjadala huu licha ya kwamba ni mzuri sana hasa katika jamii ya kiraia lakini huenda usiwe na tija sasa kwa raia, ushauri wangu kwa raia wenzangu ni kuanza kutizama hali halisi ya nchi yetu, tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi?

Tukijua tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi, itakuwa rahisi sana kujua haiba na wajihi wa mtu ambaye tunamtaka kwa nafasi ya udiwani, ubunge na Urais na hatutajikita katika kujadili watu na kujifunga na ushabiki wa kambi moja dhidi ya nyingine au chama kimoja dhidi ya kingine.

Ifike pahala mjadala wetu kuelekea uchaguzi ili uwe na tija tuutizame kwa msingi kwamba, licha ya kwamba nchi yetu ina changamoto nyingi lakini tuna matarajio fulani kama raia, tuna ndoto za nchi na Taifa tunalolitaka. Tukitizama amani katika Taifa letu, amani ya mtu mmoja mmoja, amani katika jamii zetu, usalama wetu, tukilitizama hili tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Tukiutizama Umoja wa Taifa letu, tumekuwa tukijinasib na kauli kama Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, je tukiutizama kwa jicho la karibu Umoja wa Taifa letu ukoje? Umoja kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, lakini hata Zanzibar, tutizame Umoja kati ya Unguja na Pemba, tuangalie Umoja katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayomaliza muda wake hivi karibuni.

Huku Bara tutizame Umoja kati ya dini mbalimbali lakini pia tutizame Umoja wetu kisiasa, tuna Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Vyama vya Siasa, niwaulize tija ya kuwa na Taasisi hizi muhimu katika kujenga mustakabali wa siasa zetu sasa na baadaye iko wapi? Juzi tu hapa mchakato wa Katiba umekwamishwa kwa makusudi na sikuona Umoja wa kisiasa wa vyama vyote au wanasiasa wote wenye mapenzi mema waliosimamia kweli ili kuokoa mchakato huu wa kihistoria.

Nimeangazia Amani na Umoja wa Taifa, nikijua misingi ya uwepo wake ni Haki na Usawa, je haki za watu na raia wa taifa letu zinalindwa, zinatunzwa, zinahifadhiwa na kutolewa kikamilifu? Bila unafiki na kwa jibu lolote lile unaloona jema, je, haki hizi zinapatikana kwa usawa? Usawa kati ya wasio nacho na walio nacho, usawa kati ya masikini na matajiri, usawa kati ya wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara wadogo-wadogo. Usawa kati ya maeneo ya mijini na maeneo ya pembezoni.

Tunaweza tukajadili usawa wa haki lakini pia usawa wa fursa, hivi ni nani katika Taifa letu ambao wananufaika na mikopo ya mabenki, hivi ni nani katika Taifa letu ambao wananufaika kwa haraka na fursa za ajira. Utasema labda tuangalie tu miongoni mwa vijana upatikanaji wa fursa za ajira ukoje, lakini juzi hapa natizama taarifa ya Habari nasikia katika jiji la Mwanza kuna ongezeko kubwa la wazee wasio na ajira, hii tafsiri yake nini? Tunatoka wapi, tuko wapi na tunataka kuelekea wapi? Tukijikita katika mjadala huuu na kulitizama Taifa hatutakuwa na muda wa kuzongwa na mbwembwe za watangaza nia ambao nia yao na nikiwasikiliza wengi ni kufika ikulu wakati sisi tunataka tufike kule katika nchi ya ahadi ambayo Wananchi, watu na raia wa Taifa letu wanastahili kuwepo.

Kiongozi anayeweza kusimamia Amani na Umoja unaojengwa katika misingi ya Haki na Usawa, ni yule mwenye uthubutu, ni yule asiyeona haya kusimama na watanzania, mwenye hekima, mpole, baba wa wote, ishara ya Umoja wetu, jamii inamuamini na sisi tunajua kwa hakika anajua matatizo yetu na tukimuona tunajua ana dhamira ya kweli kutufikisha katika Tanzania tunayoitaka, kwanza kwa kuijengea misingi imara na pili kutuleta kama Taifa pamoja.

Elimu ya kuhamasisha uandikishaji

Nina uhakika kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura amejiandikisha, ama yuko anajiandikisha au ameshajiandaa tayari kuandikishwa pindi Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakapofika katika eneo lake. Na kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine, kwa makusudi au kwa bahati mbaya wameikosa haki yao ya kikatiba ya kuandikishwa kwenye daftari la wapiga kura, naomba mjitokeze mara moja sasa ili Tume ya Uchaguzi itimize ile ahadi yake kwamba hakuna raia mwenye sifa ya kuandikishwa atakayeachwa kuandikishwa.

Nitoe rai kwa Wananchi wenzangu hasa wale wenye sifa ya kuandikishwa na hawajaandikishwa bado wajitokeze, ili sote tusaidie kuikumbusha Tume ili iwaandikishe wakati muda ungalipo.

Kuhusu uandikishwaji wa wanafunzi walioko shuleni na vyuoni, nimefuatilia hoja za wanafunzi na hoja za Tume ya Uchaguzi, wanafunzi wana hofu juu ya watakapojiandikisha na uhalisia wa watakapopigia kura ifikapo Oktoba 25, hapa kuna hoja. Kama zoezi linavyoendelea kutoka mwanzoni mwa mwaka huu ni hakika kuna wanafunzi wengi watakuwa wameandikishwa wakiwa mashuleni na vyuoni kwao na wakati wa kupiga kura ama watakuwa shuleni na vyuoni au watakuwa likizo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, kutakuwa na fursa ya kubadili eneo la kupigia kura, ambapo mpiga kura kule ambako anajua atakuwepo mwezi Oktoba basi atakwenda na kuboresha taarifa zake na hapo ndipo Tume itahamisha taarifa zake za ukaazi wa awali kwenda eneo jipya atakalopigia kura. Fursa hii ya kubadili taarifa za ukaazi kutoka eneo moja kwenda lingine itakuwepo kati ya tarehe 11 hadi 18 Agosti 2015. Rai yangu, wanafunzi wote zingatieni fursa hii.

Wakati nikiwasihi wanafunzi kuzingatia fursa hii, napenda nieleze pia changamoto zinazoambatana na fursa ya kubadili eneo la kupigia kura. Wanafunzi hawa mwezi wa Agosti ama watakuwa likizo au watakuwa shuleni na watakuwa wameandikishwa katika eneo tofauti na kwao au shule, na tuzingatie Oktoba 25 wanafunzi hawa watakuwa wapi kwao au shule? Kama Tume ya Uchaguzi ikijipanga vizuri mwezi Agosti na iwe zaidi ya wiki moja kama ambavyo wao wamejipangia, basi zoezi la kuboresha taarifa kwa wale watakaotaka kubadili maeneo ya upigaji kura litawezekana.

Bila kusahau kwamba inawezekana kabisa baadhi ya wanafunzi watakuwa shuleni mwezi Agosti na huenda mwezi wa Oktoba wataruhusiwa kwenda kupiga kura makwao, wanafunzi hawa watakuwa wamenyimwa haki ya kupiga kura katika maeneo yao, Tume na Wizara ya Elimu zingatieni hili mapema ili lisituletee lawama baadaye.

Kuhusu watangaza nia wa CCM

Nimeamua kuujadili mchakato wa CCM kwasababu bado ni chama Kiongozi, bado nasisitiza, kila nikipita huku na huko naona mnasemana na kunyoosheana vidole. Nawakumbusha kwamba mbinu za ujanja haziwezi kuwaondoa wajanja. Vitabu vya dini vimeandika, je ufalme mmoja waweza kusimama juu ya ufalme uleule? La hasha, bali ufalme mmoja waweza kuinuka juu ya ufalme mwingine. Najaribu kusema ubaya hauwezi kuushinda ubaya bali ni wema pekee huweza kuushinda ubaya.

Natizama siasa zinavyoendelea nasema, siasa na mikakati ya hila kamwe haiwezi kuwa suluhisho la kuondokana na ubaya kuelekea uteuzi, uchaguzi mkuu na hata serikali itakapopatikana. Wagombea wabaya na ambao wamejivisha ngozi ya kondoo ni wabaya zaidi kuliko wagombea ambao tayari mnaonekana kuwajua kama sio kuwafahamu kwamba wao ni mbwamwitu. Mtaingia katika dhambi kubwa itakayokigharimu Chama cha Mapinduzi kama kwa hekima ya kiMungu mtashindwa kupambanua nani ni mbwamwitu aliyejivisha ngozi ya kondoo na mkaacha kumhukumu anavyostahili na kukimbilia kumhukumu mbwamwitu mnayemjua, hamtakuwa mmetenda haki na kitendo hicho kitawatafuna.

Rai yangu kwa wazee wa CCM, baadhi yenu mnanihuzunisha sana, mimi ni kijana mdogo tu, napenda kujifunza kwenu, lakini matendo ya baadhi yenu yananifanya nijiambie kama Mungu akinipa uhai, aslani sitapenda kuenenda katika njia yenu, mnanichanganya kwa hakika. Hekima yenu iko wapi? Inamaana hamuoni, inamaana na ninyi mmeingia katika mkumbo wa kutokuona na kujitoa ufahamu, je furaha yenu ni kuona nchi ina sintofahamu, nchi iko njiapanda na Chama cha Mapinduzi halkadharika?

Mwalimu Nyerere hakusubiri kualikwa kutoa maoni yake, pale ilipobidi alitoa maoni yake hadharani na Taifa likaponywa. Ninyi nasikia mnasema chinichini eti hamjaalikwa, eti hamshirikishwi, kweli? Ama mnasubiri ratiba au mnasubiri vikao, kweli? Hivi kusema kama mzee ni kusubiri vikao pekee? Au niseme mababa na mababu zangu na ninyi mmeingia katika ule ugonjwa wa Taifa, ule ugonjwa wa kuogopana. Ugonjwa mbaya kabisa, ninyi mnajua wengi wetu na kwa ubinadamu wetu usiofaa hata Mungu hatumwogopi, je leo hii, binadamu wenzetu ni zaidi sana kuliko Mungu? Najua wengine mko madarakani, wengine mmestaafu, lakini mimi mtoto na mjukuu wenu nawaambia kwa hakika msipochukua hatua sasa na hatua ya hekima, mtakuwa na hoja ya kujibu hapa duniani lakini pia mbele ya haki.

Utete wa suala la Zanzibar

Hili la Zanzibar nimelifuatilia kwa ukaribu, ninavyoona ni kama mnalichukulia kama kitu cha mzaha. Naona hatujifunzi kutokana na makosa, naona tunapenda sana utimilifu wa methali kama ile ya asiyesikia la mkuu, huvunjika guu. Eti viongozi wangu, hasa wale mlioko madarakani kwa hamuoni ya Zanzibar na namna ambavyo viashiria vya kuteteresha amani vinavyojidhihirisha? Je mnachukua hatua gani? Je mnataka kutatua tatizo lililoko Zanzibar kwa mbinu za hila au kwa muafaka na kuheshimiana na kulinda maslahi ya watanzania wakaazi wa Zanzibar?


Naona kila mtu yuko kimya, ni kana kwamba kila kitu kiko kawaida, sawa, na najua huwa ni kawaida yenu hasa ndugu zangu wa damu kutoka Zanzibar kujitoa ufahamu kwamba kila kitu kiko sawa. Au na ninyi mnataka mpate utimilifu wa methali za wahenga hasa ile ya mficha maradhi kifo humuumbua? Sasa ukishakufa hata ukiumbuka haitokuwa na mantiki lakini shida ni kwa wale ambao mnatuachia matatizo. Rai yangu tena kwa wazee wa Bara na wa Zanzibar, tizameni matatizo ya Zanzibar na kwa muafaka yatatueni. Na mkumbuke Mgombea Urais wa Muungano, ukomavu, hekima, busara na uelewa wake wa hali tete ya Zanzibar utatusaidia kuishi na matokeo ya baada ya Oktoba katika pande zote za Muungano na kuwa kiungo muhimu cha kuuimarisha Muungano wetu.

2 comments: