Tuesday, October 10, 2017

CCM MPYA TANZANIA MPYA – UHURU WA KIUCHUMI NI MAPAMBANO HAUTAKUJA KATIKA SAHANI YA FEDHA

CCM MPYA TANZANIA MPYA – UHURU WA KIUCHUMI NI MAPAMBANO HAUTAKUJA KATIKA SAHANI YA FEDHA

Hii ndiyo changamoto waliyonayo viongozi wapya wa Afrika – J.K. Nyerere

Maono ya Mwalimu kwa Uongozi wa Awamu ya V

Mwalimu Nyerere alipata kusema katika kitabu cha Afrika Today and Tomorrow katika ukurasa wa 84 “…Africa is yet to liberate itself – to attain Economic liberation – gaining control over, and having responsibility for our economic development strategy and macro economic policies in order to be able to provide for, at least, decent basic standard of living for all our people. Unless this is done our political independence will always be in danger – who controls money, they say, also controls politics.”

Tafsiri yangu ya maneno haya Mwalimu Nyerere anasema “Afrika bado inahitaji kujikomboa – ili kufikia Uhuru wa Kiuchumi – ili kuwa na udhibiti, na wajibu katika mikakati ya maendeleo yetu kiuchumi na sera zetu za kiuchumi ili tuweze kuwapatia watu wetu angalau kiwango cha msingi na chenye utu cha ustawi wa maisha yao. Kama hili lisipofanyika uhuru wetu wa kisiasa bado utakuwa mashakani/hatarini – mwenye kuzidhibiti fedha, wanasema, hudhibiti siasa pia.”

Mwalimu alipata kuyasema haya mwaka 1999 na bado alikuwa ameona mbali sana. Mwalimu alikuwa anatukumbusha kazi kubwa ambayo kipindi kile mwaka 1999 ilikuwa haijakamilika na akiutizamia wakati ujao kwamba bado kazi hiyo ilipasa kukamilishwa – Ukombozi wa Kiuchumi unaotuletea Uhuru wa Kiuchumi kwa Taifa letu la Tanzania.

Kipindi fulani yeye mwenyewe Mwalimu alipata kuamini hakika kwamba uhuru wa Tanzania haungalikuwa mkamilifu mpaka Bara lote la Afrika kukombolewa. Mwalimu akasema mapambano yao ya kulikomboa bara la Afrika yalikamilika mwaka 1994 walipofanikiwa kuufuta ukaburu Afrika Kusini.

Mwalimu Nyerere anaandika Mwaka 1999 kwamba sasa (1999) na kuliko kipindi kingine kabla, anaamini kwa nguvu kubwa kwamba Uhuru wa kisiasa wa Bara la Afrika hautakuwa kamili isipokuwa watu wa Afrika wachukue na kushika kwa mikono yao udhibiti wa uchumi wao badala la kuuacha uchumi wa Afrika katika mikono ya nguvu za kigeni.

Aidha Mwalimu anabashiri na kwa lugha ya kiingereza akisema “This is the Challenge of the new generation of leaders in Africa” akimaanisha kwa kiswahili “Na hii ndiyo changamoto ambayo kizazi kipya cha viongozi wa Afrika wanayo” Tafsiri ni yangu.

Mwalimu anaendelea kusema “Viongozi wa kizazi chake waliweza kutenda kilichowezekana kipindi kile. Viongozi wapya ni lazima wafanikiwe katika utume wao mpya ambao ni ukombozi wa kiuchumi na kushindwa kufanikiwa katika utume huu kutamaanisha kuuachia uhuru wa nchi zao, wa wananchi wao na kukubali hali ilivyo sasa ya utegemezi wa kiuchumi.

Mwalimu Nyerere alikiri kwamba Uongozi wa Afrika unaweza kuwekwa katika mafungu matatu;

Mosi, Viongozi waliopambana kuhakikisha Afrika inakuwa huru, Pili, viongozi waliohangaika na mdororo wa uchumi uliotokana na sera mbovu na zisizotaarifiwa na uhalisia wa Afrika miaka ya 80 na 90. Wapo pia viongozi ambao walidumbukia katika ama rushwa kubwa na kuvuruga Uongozi wa nchi mbalimbali Afrika au matukio ya Mapinduzi ya kijeshi kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi katika nchi hizo. Kwa bahati nzuri kizazi hiki kinaelekea kwisha.

Tatu, ni awamu mpya ya viongozi inayoibuka, hii ni awamu ambayo tutashuhudia kuongezeka kwa viongozi waadilifu na wazalendo wanaochukua Uongozi wa nchi za Afrika. Awamu hii ndio ambayo inakuja kusafisha masalia ya Uongozi usiowajibika na chembechembe za uzembe. Awamu hii itatoa Uongozi bora ambao utaweza kusema HAPANA kwa wale ambao wanacheza na mambo yetu ya ndani katika nchi zetu.

Aidha Mwalimu Nyerere anaendelea kusema viongozi hawa wa awamu mpya wanajua matakwa ya wananchi wao, ni aina mpya ya viongozi wanaotoa aina mpya ya Uongozi. Viongozi hawa wamenia kukamilisha mapambano ya ukombozi – ukombozi wa kiuchumi.

Wajibu Mkuu Mwalimu Nyerere anaeleza wa Maendeleo ya Afrika unabaki kwa waafrika wenyewe. Msaada wowote utakuwa ni nyongeza tu katika jitihada za waafrika wenyewe. Na kama kutakuwa na uhusiano wowote basi lazima mahusiano haya yajengwe katika namna ambayo yatanufaisha waafrika kwa haki na sio katika misingi ya unyonyaji. Mwalimu anamaliza kwa kusema “shime sote tuungane mikono kuiokoa Afrika dhidi ya unyonyaji wowote baadaye”.

Baada ya rejea na nukuu hizi za Mwalimu napenda kujadili CCM MPYA TANZANIA MPYA na ukweli kwamba uhuru wa kiuchumi ni mapambano na asilani hautakuja katika sahani ya fedha. Tafakuri yangu nimeigawa katika vipindi tatu, Mosi, Tulikotoka ni mbali, Pili, Tuliko sasa na Tatu, Tunakokwenda.

Tulikotoka ni mbali

Serikali za Awamu ya Kwanza na ya Pili zimepambana sana kuleta maendeleo ya Taifa la Tanzania, kwanza ya ujenzi wa Taifa Moja Imara na madhubuti linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanganyika na Zanzibar kwa pamoja tumezirithi kutoka kwa wakoloni lakini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ujenzi wake tumeufanya wenyewe. Mwaka 1964 ni mwaka muhimu katika ujenzi wa Taifa na kisha baada ya hapo tunalo zoezi endelevu la kujenga Taifa hili.

Ujenzi wa Taifa la Tanzania haukuwahi kuwa rahisi na umepitia changamoto na mitihani mingi sana. Natafakari katika pande la ardhi ambalo kuna watu wenye lugha na makabila tofauti tofauti zaidi ya 120, na kila kabila likiwa na utamaduni wake, desturi zake na Uongozi wake (Machifu).

Hili Mwalimu Nyerere alianza na viongozi waliofuatia baada yake wakaendelea nalo na leo tunajivuna Tanzania ndio nchi pekee katika Afrika ambayo watu wake wana lugha moja ya Taifa ambayo sio ya kabila mojawapo.

Mitihani ilianza mwaka 1964, wakati wa uamuzi wa kihistoria wa kuunganisha nchi mbili zilizokuwa huru kwa maana ya Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja mpya na huru ilopewa jina “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Wahisani wetu wakubwa wa maendeleo kipindi hicho Ujerumani Magharibi hawakupendezwa na uamuzi huu na wakatishia kuvunja uhusiano nasi.

Kabla hatujatishika tukajitathimini kama Taifa, heshima yetu na umuhimu wa tunu yetu ya UMOJA. Kwa kauli moja tukavunja uhusiano na Ujerumani Magharibi na kurudisha msaada wa fedha ambao tayari ulikuwa umetolewa kwetu. Funzo hapa ni haijalishi tunapitia wakati gani lakini wakati wote tunapaswa kulinda heshima na umoja wa Taifa letu.

Mtihani wa pili ulikuwa mwaka 1965, hii ilikuwa baada ya kikundi cha watu wachache kujitangazia uhuru kule Zimbabwe ya leo (Unilateral Declaration of Independence). Tanzania iliamini katika uhuru wa kweli na wa wengi nchini humo. Tukawaeleza waingereza kwamba tabia ile ni mbaya na haikubaliki na kwa kuwa Uingereza ndiye dada mkubwa katika familia ya Jumuiya ya Madola tukamtaka achukue hatua dhidi ya utawala wa wachache uliojitangazia uhuru chini ya bwana Smith.

Waingereza walisua sua na hata baada ya nchi za Afrika kulaani vikali kitendo kile bado hawakuchukua hatua kali na stahiki. Kati ya Nchi za Afrika huru ni Tanzania na Ghana tu ndio zilizovunja mahusiano na Uingereza, kitendo hiki kililenga kupeleka ujumbe kwamba hatuukubali unyonyaji wa aina yoyote iwe Tanzania au nje ya Tanzania na hasa kwa mataifa rafiki kipindi kile.

Mwaka 1970-75 tukapata ukame mkubwa katika nchi yetu, wakati hali hiyo ikiendelea tukatoka na mikakati ya kupambana na hali hiyo kwa kuanzisha skimu kadhaa za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini. Haikuwa kazi rahisi, ilitaka Chama, Serikali na Umma wa Wananchi kuwa na uelewa wa pamoja wa hali iliyokuwa inatukabili na kusimama imara pamoja ili kukabiliana nayo.

Tukavuka salama, na mwaka 1977 tukaandika historia nyingine kubwa ya kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka mmoja baadaye tukaingia katika Vita dhidi ya Nduli Iddi Amin, vita ya Kagera. Vita hii ilitupa heshima kubwa maana tuliipigana wenyewe na licha ya kwamba Nduli alisaidiwa na mataifa mengine lakini Wananchi wa Tanzania na Jeshi letu la Wananchi (JWTZ) tukamfurushia mbali hadi nje ya mipaka yetu. Vita ya Kagera licha ya heshima kubwa ilituacha katika wakati mgumu sana kiuchumi maana tulitumia karibia hifadhi yetu yote ya fedha za kigeni ambayo hutumika kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje.

Kuna kipindi tulifika tukabaki na akiba isiyozidi wiki mbili ya Mafuta ya Magari, ulikuwa wakati mgumu sana. Huwa nafananisha Uongozi wa Nchi kama Uongozi wa familia inayojitahidi sana kujikwamua kihali na kiuchumi licha ya changamoto mbalimbali. Baba au Mama anaweza kurudi nyumbani na chakula hakuna na ilhali watoto hujua baba au mama lazima awe na uwezo wa kuleta chakula nyumbani. Nadhani Mama na Baba wote wataungana na mimi kwamba hakuna wakati mgumu ambapo watoto wanakutegemea uwawezeshe na hauko katika uwezo wa kuwezesha lakini unapambana uwawezeshe maana hawawezi amini kwamba baba au mama hawezi kuwezesha mahitaji yao.

Miaka ya Themanini (80) ikawa na Changamoto zaidi na ukiongeza na masharti gandamizi ya Taasisi za Kifedha za Kidunia zijulikanazo kwa kiingereza kama “Britton Woods Institutions”. Wakatulazimisha Serikali isifanye tena uzalishaji na iachane na umiliki wa mashirika ya umma, wakalazimisha tushushe thamani ya fedha yetu (shilingi ya Tanzania) na wakatueleza ili tupate misaada kutoka kwao kwanza ni lazima turidhie masharti haya niliyoyataja kwa uchache na tukubali kutekeleza programu za kurekebisha uchumi wetu (Structural Adjustment Programmes – SAPs).

Kibaya zaidi na kwasababu tulikuwa na msimamo wa kuendelea na Mapambano ya kuukomboa Uchumi wetu dhidi ya mikakati ya kinyonyaji ya kibeberu iliyokuwa inatambulishwa na Taasisi hizi za kifedha za kidunia, waliamua pia kutuhujumu waziwazi.

Hujuma ya uchumi wetu ilikuwa kutoka nje na ikiratibiwa kimkakati kabisa na ilikuwa pia kutoka ndani ikiratibiwa kwa ustadi na vibaraka wa mabeberu, watanzania wachache waliokosa uadilifu, uaminifu, uzalendo na mapenzi ya dhati kwa Taifa letu.

Vilikuwepo viwanda zaidi ya 400 na migodi kadhaa, lakini viwanda na migodi inapojiendesha kila baada ya muda huhitaji vipuri, basi kila tulipoagiza vipuri kutoka kampuni za nje walitoa visingizo mbalimbali, mara kampuni zimeuzwa au kampuni ilishafilisika na kadhalika na kadhalika. Hivyo baada ya muda viwanda vingi vilikosa vipuri na kulazimika kusimama na watu kupoteza ajira. Hali kama hiyo ilitokea katika migodi kadhaa na ikailazimu serikali kuweka mpango wa kuifunga migodi hiyo.

Hata pale tulipoamua kampuni yetu ya kizalendo Nyumbu itengeneze vipuri hapa hapa nchini basi mataifa makubwa yalififisha dhamira njema ya kampuni za kizalendo kwa kutoa misaada ili kampuni za ndani zishindwe kufanya biashara, zishindwe kujiendesha na hatimaye kuanguka.

Changamoto ziliongezeka sana kwasababu tulisimamia haki huku tukiendelea kupinga udhalimu. Ililazimu serikali itafute mbinu mbadala ya kujiendesha na ndipo mawazo kama ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Stiegler’s Gorge likaja lakini uwezo wa kujenga hatukuwa nao wakati huo.

Mwalimu alijua huenda katika pwani yetu tunaweza kuwa na gesi au mafuta na akazungumza na nchi fulani za Magharibi ili kuja kufanya utafiti wa uwepo wa mafuta na gesi. Wataalamu wa kimagharibi wakaja na wakafanya utafiti na kusema hakuna dalili yoyote ya mafuta au gesi.

Mwalimu alikuwa mvumilivu na hakuwa mtu wa kukata tamaa, na alizungumza na marafiki zetu wa India ambao walikuja hapa na wakachoronga maeneo machache ya pwani ya Tanzania (Pwani na Lindi) na hatimaye gesi ikapatikana, wakamwambia imepatikana na wakalipua kisima kimoja na kikawaka moto bila kuzimika kwa miezi mitatu. Mwalimu Nyerere akawaambia wakizibe kisima hicho na pasijulikane pahala pale mpaka watakapokuwa tayari hapo baadaye.

Kuna kipindi tulipokuwa tukifanya mashauriano (negotiations) katika masuala ya kiuchumi ili “mabwana wakubwa” ama walegeze kamba au watusaidie, ilitubidi sisi kusafiri kuwafuata, mfano, kule Ulaya katika vikao vya Paris Club, vikao hivi wanakaa matajiri wa dunia na mataifa makubwa. Mzee Cleopa David Msuya alishiriki kule, ilikuwa lazima uwafuate Ulaya mabwana wakubwa kule, na kuna kipindi aliwafuata na aliishia mapokezi, ubeberu bila kugangamala una jeuri, kiburi na dharau sana.

Napenda watu wajua safari yetu imekuwa yenye milima na mabonde lakini kitu kimoja cha kujivuna tumebaki na Taifa moja. Ni wajibu wetu kukumbushana tulikotoka ni mbali na hasa vijana na watoto wetu.

Tulipo sasa

Tanzania iko katika awamu ya Tano ya Uongozi wake tangu kuasisiwa kwake. Baada ya vipindi viwili vya awamu ya Nne, CCM iliamua kufanya Mageuzi Makubwa ambayo yanahakikisha chama hiki kinabaki kuwa Chama cha Wanachama na kinachoshughulika na shida za watu wetu.

Mageuzi ya CCM yanalenga pia kuhakikisha katika kila mawanda haki ya watanzania inapatikana. Taifa hili ni tajiri sana na linaweza kujitosheleza ndani lakini tumeshindwa kwa muda mrefu kujenga uwezo wa ndani ili kutimiza ndoto hii ya kujitegemea ama kwa unyonge au wakati mwingine kwa uzembe wa baadhi yetu.

Chama Cha Mapinduzi baada ya kujitathimini kikatafuta mtu ambaye ataweza kuishika agenda ya Mageuzi ya CCM, na ieleweke Mageuzi ya CCM yatatoa mwelekeo kwa Mageuzi ya Serikali ili sote tuweze kukidhi na kuweka jitihada kubwa ya kutosheleza mahitaji na matarajio ya msingi ya watanzania.

Mtu huyu ambaye ameaminiwa kwanza na wana CCM kisha watanzania ni Ndugu yetu John Pombe Joseph Magufuli, mtanzania kweli kweli na mwenye uchungu wa kuhujumiwa kwetu. Mtu ambaye CCM ilimleta (Ndg. Magufuli) ilipasa awe mtu ambaye hatatuonea soni, hataleta urafiki, hataona haya kutuambia hapa na pale tulikosea.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitafakari na kuamua kutuletea Ndg. Magufuli ili pia aweze kutusimamia kwa haki tena pasina kujiona mnyonge hata mbele ya wabwana wakubwa wa ndani na nje ya nchi.

Leo Afrika nzima inazizima kwamba yuko mwanaume ambaye ameweza kusema imetosha “enough is enough” sio haki na ni unyonyaji kuchukua madini yetu katika namna ambayo haki yetu inapokwa. Ndugu Magufuli ana amini sana katika sekta binafsi na hasa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda sambamba na sekta ya umma, lakini ana amini zaidi katika sekta binafsi inayojiendesha kwa kanuni za maadili ikiwemo kulipa kodi. Ana amini katika uwekezaji kutoka nje, lakini unaotambua kwamba sisi ni Taifa huru na tunayo haki ya kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zetu.

Ndugu Magufuli ana amini kwa hakika uwekezaji kutoka nje unapaswa kujengwa katika misingi ya haki na usawa na kwamba kila upande una wajibu Tanzania na wawekezaji, Tanzania iweke mazingira ya uwekezaji hasa wa viwanda na wawekezaji watende sawa sawa na kanuni za kidunia za maadili ikiwemo kutokuiba kwa ujanja ujanja, kutokwepa kodi, kutosafirisha pesa kwenda nje “capital flight” wakati zinawezwa kutunzwa hapa na kadharika.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemleta ndugu Magufuli wakati muafaka wakati tunamhitaji zaidi mtu kama yeye. Ukisoma Maelezo na Nukuu za Mwalimu Nyerere katika maelezo yangu ya awali juu ya Maono ya Mwalimu Nyerere utaungana nami kusema ile aina ya Uongozi mpya katika bara la Afrika, Tanzania tumekuwa kinara wa kwanza na wengine watafuata ili bara la Afrika lirejeshe heshima yake ya uhalisia na asili.

Wiki ijayo nitaeleza kuhusu tunakokwenda na kwanini Ndugu Magufuli ni zawadi na tumtumie katika kipindi hiki cha mpito na cha kunyooshana nidhamu ili maisha yetu katika miaka mikuu 75 “The Great 75 Years” iwe rahisi na yenye mafanikio makubwa hii ni kati ya Mwaka 2025 na Mwaka 2100. Huu ni wakati wa siasa za Maendeleo na sio siasa za Madaraka.

Makala hii imeandikwa na Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi