Saturday, June 27, 2015

WAO WAKIITIZAMA IKULU, SISI TULITIZAME TAIFA HUKU TUKIWEKA UCHAMA PEMBENI



Dhana ya kulitizama Taifa

Kwa hali ilivyo sasa ninaona jotoridi ikizidi kupanda katika vyama vya siasa hasa ukizingatia michakato ya ndani ya vyama ya kuteua watakaopewa dhamana ya kugombea nafasi za udiwani, ubunge na Urais. Kwa kiasi kikubwa kabisa, naona Wananchi wakigubikwa na mjadala wa nani ni nani na huenda nani atapata nini. Mjadala huu licha ya kwamba ni mzuri sana hasa katika jamii ya kiraia lakini huenda usiwe na tija sasa kwa raia, ushauri wangu kwa raia wenzangu ni kuanza kutizama hali halisi ya nchi yetu, tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi?

Tukijua tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi, itakuwa rahisi sana kujua haiba na wajihi wa mtu ambaye tunamtaka kwa nafasi ya udiwani, ubunge na Urais na hatutajikita katika kujadili watu na kujifunga na ushabiki wa kambi moja dhidi ya nyingine au chama kimoja dhidi ya kingine.

Ifike pahala mjadala wetu kuelekea uchaguzi ili uwe na tija tuutizame kwa msingi kwamba, licha ya kwamba nchi yetu ina changamoto nyingi lakini tuna matarajio fulani kama raia, tuna ndoto za nchi na Taifa tunalolitaka. Tukitizama amani katika Taifa letu, amani ya mtu mmoja mmoja, amani katika jamii zetu, usalama wetu, tukilitizama hili tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Tukiutizama Umoja wa Taifa letu, tumekuwa tukijinasib na kauli kama Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, je tukiutizama kwa jicho la karibu Umoja wa Taifa letu ukoje? Umoja kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, lakini hata Zanzibar, tutizame Umoja kati ya Unguja na Pemba, tuangalie Umoja katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayomaliza muda wake hivi karibuni.

Huku Bara tutizame Umoja kati ya dini mbalimbali lakini pia tutizame Umoja wetu kisiasa, tuna Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Vyama vya Siasa, niwaulize tija ya kuwa na Taasisi hizi muhimu katika kujenga mustakabali wa siasa zetu sasa na baadaye iko wapi? Juzi tu hapa mchakato wa Katiba umekwamishwa kwa makusudi na sikuona Umoja wa kisiasa wa vyama vyote au wanasiasa wote wenye mapenzi mema waliosimamia kweli ili kuokoa mchakato huu wa kihistoria.

Nimeangazia Amani na Umoja wa Taifa, nikijua misingi ya uwepo wake ni Haki na Usawa, je haki za watu na raia wa taifa letu zinalindwa, zinatunzwa, zinahifadhiwa na kutolewa kikamilifu? Bila unafiki na kwa jibu lolote lile unaloona jema, je, haki hizi zinapatikana kwa usawa? Usawa kati ya wasio nacho na walio nacho, usawa kati ya masikini na matajiri, usawa kati ya wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara wadogo-wadogo. Usawa kati ya maeneo ya mijini na maeneo ya pembezoni.

Tunaweza tukajadili usawa wa haki lakini pia usawa wa fursa, hivi ni nani katika Taifa letu ambao wananufaika na mikopo ya mabenki, hivi ni nani katika Taifa letu ambao wananufaika kwa haraka na fursa za ajira. Utasema labda tuangalie tu miongoni mwa vijana upatikanaji wa fursa za ajira ukoje, lakini juzi hapa natizama taarifa ya Habari nasikia katika jiji la Mwanza kuna ongezeko kubwa la wazee wasio na ajira, hii tafsiri yake nini? Tunatoka wapi, tuko wapi na tunataka kuelekea wapi? Tukijikita katika mjadala huuu na kulitizama Taifa hatutakuwa na muda wa kuzongwa na mbwembwe za watangaza nia ambao nia yao na nikiwasikiliza wengi ni kufika ikulu wakati sisi tunataka tufike kule katika nchi ya ahadi ambayo Wananchi, watu na raia wa Taifa letu wanastahili kuwepo.

Kiongozi anayeweza kusimamia Amani na Umoja unaojengwa katika misingi ya Haki na Usawa, ni yule mwenye uthubutu, ni yule asiyeona haya kusimama na watanzania, mwenye hekima, mpole, baba wa wote, ishara ya Umoja wetu, jamii inamuamini na sisi tunajua kwa hakika anajua matatizo yetu na tukimuona tunajua ana dhamira ya kweli kutufikisha katika Tanzania tunayoitaka, kwanza kwa kuijengea misingi imara na pili kutuleta kama Taifa pamoja.

Elimu ya kuhamasisha uandikishaji

Nina uhakika kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura amejiandikisha, ama yuko anajiandikisha au ameshajiandaa tayari kuandikishwa pindi Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakapofika katika eneo lake. Na kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine, kwa makusudi au kwa bahati mbaya wameikosa haki yao ya kikatiba ya kuandikishwa kwenye daftari la wapiga kura, naomba mjitokeze mara moja sasa ili Tume ya Uchaguzi itimize ile ahadi yake kwamba hakuna raia mwenye sifa ya kuandikishwa atakayeachwa kuandikishwa.

Nitoe rai kwa Wananchi wenzangu hasa wale wenye sifa ya kuandikishwa na hawajaandikishwa bado wajitokeze, ili sote tusaidie kuikumbusha Tume ili iwaandikishe wakati muda ungalipo.

Kuhusu uandikishwaji wa wanafunzi walioko shuleni na vyuoni, nimefuatilia hoja za wanafunzi na hoja za Tume ya Uchaguzi, wanafunzi wana hofu juu ya watakapojiandikisha na uhalisia wa watakapopigia kura ifikapo Oktoba 25, hapa kuna hoja. Kama zoezi linavyoendelea kutoka mwanzoni mwa mwaka huu ni hakika kuna wanafunzi wengi watakuwa wameandikishwa wakiwa mashuleni na vyuoni kwao na wakati wa kupiga kura ama watakuwa shuleni na vyuoni au watakuwa likizo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, kutakuwa na fursa ya kubadili eneo la kupigia kura, ambapo mpiga kura kule ambako anajua atakuwepo mwezi Oktoba basi atakwenda na kuboresha taarifa zake na hapo ndipo Tume itahamisha taarifa zake za ukaazi wa awali kwenda eneo jipya atakalopigia kura. Fursa hii ya kubadili taarifa za ukaazi kutoka eneo moja kwenda lingine itakuwepo kati ya tarehe 11 hadi 18 Agosti 2015. Rai yangu, wanafunzi wote zingatieni fursa hii.

Wakati nikiwasihi wanafunzi kuzingatia fursa hii, napenda nieleze pia changamoto zinazoambatana na fursa ya kubadili eneo la kupigia kura. Wanafunzi hawa mwezi wa Agosti ama watakuwa likizo au watakuwa shuleni na watakuwa wameandikishwa katika eneo tofauti na kwao au shule, na tuzingatie Oktoba 25 wanafunzi hawa watakuwa wapi kwao au shule? Kama Tume ya Uchaguzi ikijipanga vizuri mwezi Agosti na iwe zaidi ya wiki moja kama ambavyo wao wamejipangia, basi zoezi la kuboresha taarifa kwa wale watakaotaka kubadili maeneo ya upigaji kura litawezekana.

Bila kusahau kwamba inawezekana kabisa baadhi ya wanafunzi watakuwa shuleni mwezi Agosti na huenda mwezi wa Oktoba wataruhusiwa kwenda kupiga kura makwao, wanafunzi hawa watakuwa wamenyimwa haki ya kupiga kura katika maeneo yao, Tume na Wizara ya Elimu zingatieni hili mapema ili lisituletee lawama baadaye.

Kuhusu watangaza nia wa CCM

Nimeamua kuujadili mchakato wa CCM kwasababu bado ni chama Kiongozi, bado nasisitiza, kila nikipita huku na huko naona mnasemana na kunyoosheana vidole. Nawakumbusha kwamba mbinu za ujanja haziwezi kuwaondoa wajanja. Vitabu vya dini vimeandika, je ufalme mmoja waweza kusimama juu ya ufalme uleule? La hasha, bali ufalme mmoja waweza kuinuka juu ya ufalme mwingine. Najaribu kusema ubaya hauwezi kuushinda ubaya bali ni wema pekee huweza kuushinda ubaya.

Natizama siasa zinavyoendelea nasema, siasa na mikakati ya hila kamwe haiwezi kuwa suluhisho la kuondokana na ubaya kuelekea uteuzi, uchaguzi mkuu na hata serikali itakapopatikana. Wagombea wabaya na ambao wamejivisha ngozi ya kondoo ni wabaya zaidi kuliko wagombea ambao tayari mnaonekana kuwajua kama sio kuwafahamu kwamba wao ni mbwamwitu. Mtaingia katika dhambi kubwa itakayokigharimu Chama cha Mapinduzi kama kwa hekima ya kiMungu mtashindwa kupambanua nani ni mbwamwitu aliyejivisha ngozi ya kondoo na mkaacha kumhukumu anavyostahili na kukimbilia kumhukumu mbwamwitu mnayemjua, hamtakuwa mmetenda haki na kitendo hicho kitawatafuna.

Rai yangu kwa wazee wa CCM, baadhi yenu mnanihuzunisha sana, mimi ni kijana mdogo tu, napenda kujifunza kwenu, lakini matendo ya baadhi yenu yananifanya nijiambie kama Mungu akinipa uhai, aslani sitapenda kuenenda katika njia yenu, mnanichanganya kwa hakika. Hekima yenu iko wapi? Inamaana hamuoni, inamaana na ninyi mmeingia katika mkumbo wa kutokuona na kujitoa ufahamu, je furaha yenu ni kuona nchi ina sintofahamu, nchi iko njiapanda na Chama cha Mapinduzi halkadharika?

Mwalimu Nyerere hakusubiri kualikwa kutoa maoni yake, pale ilipobidi alitoa maoni yake hadharani na Taifa likaponywa. Ninyi nasikia mnasema chinichini eti hamjaalikwa, eti hamshirikishwi, kweli? Ama mnasubiri ratiba au mnasubiri vikao, kweli? Hivi kusema kama mzee ni kusubiri vikao pekee? Au niseme mababa na mababu zangu na ninyi mmeingia katika ule ugonjwa wa Taifa, ule ugonjwa wa kuogopana. Ugonjwa mbaya kabisa, ninyi mnajua wengi wetu na kwa ubinadamu wetu usiofaa hata Mungu hatumwogopi, je leo hii, binadamu wenzetu ni zaidi sana kuliko Mungu? Najua wengine mko madarakani, wengine mmestaafu, lakini mimi mtoto na mjukuu wenu nawaambia kwa hakika msipochukua hatua sasa na hatua ya hekima, mtakuwa na hoja ya kujibu hapa duniani lakini pia mbele ya haki.

Utete wa suala la Zanzibar

Hili la Zanzibar nimelifuatilia kwa ukaribu, ninavyoona ni kama mnalichukulia kama kitu cha mzaha. Naona hatujifunzi kutokana na makosa, naona tunapenda sana utimilifu wa methali kama ile ya asiyesikia la mkuu, huvunjika guu. Eti viongozi wangu, hasa wale mlioko madarakani kwa hamuoni ya Zanzibar na namna ambavyo viashiria vya kuteteresha amani vinavyojidhihirisha? Je mnachukua hatua gani? Je mnataka kutatua tatizo lililoko Zanzibar kwa mbinu za hila au kwa muafaka na kuheshimiana na kulinda maslahi ya watanzania wakaazi wa Zanzibar?


Naona kila mtu yuko kimya, ni kana kwamba kila kitu kiko kawaida, sawa, na najua huwa ni kawaida yenu hasa ndugu zangu wa damu kutoka Zanzibar kujitoa ufahamu kwamba kila kitu kiko sawa. Au na ninyi mnataka mpate utimilifu wa methali za wahenga hasa ile ya mficha maradhi kifo humuumbua? Sasa ukishakufa hata ukiumbuka haitokuwa na mantiki lakini shida ni kwa wale ambao mnatuachia matatizo. Rai yangu tena kwa wazee wa Bara na wa Zanzibar, tizameni matatizo ya Zanzibar na kwa muafaka yatatueni. Na mkumbuke Mgombea Urais wa Muungano, ukomavu, hekima, busara na uelewa wake wa hali tete ya Zanzibar utatusaidia kuishi na matokeo ya baada ya Oktoba katika pande zote za Muungano na kuwa kiungo muhimu cha kuuimarisha Muungano wetu.

Saturday, June 20, 2015

KWA HALI ILIPOFIKA, KUMPATA MMOJA TUNAHITAJI HEKIMA ZAIDI KULIKO VIGEZO NA SIFA



Inaonekana kuna kila dalili kwamba tunaweza kufika arobaini, namaanisha idadi ya watu ambao wanatangaza nia kupitia Chama cha Mapinduzi. Idadi kubwa ikiwa ni pamoja na mawaziri ambao wako katika serikali inayomaliza muda wake, wabunge, na makada wengine wa CCM.

Waumini wa dini nyingi wanajua hata kipindi kile cha agano la kale wakati Nabii Samweli alipokwenda kwa Yese ili kutoka kwa watoto wake achague mfalme wa wayahudi. Yese aliwapitisha watoto wake wote, wale ambao katika macho ya watu walionekana wamejengeka lakini kila alipokuja huyu, Samweli alisema Mungu hakumchagua huyu pia. Naona rundo la watangaza nia kupitia Chama cha Mapinduzi na baada ya mchakato wa kichama ili mmojawao awe mrithi wa Rais Kikwete wakiakisi kwa karibu hadithi ile ya kale ya rundo la watoto wa Yese ambao Mungu alimwambia Samweli hakuona mmoja miongoni mwao.

Naizungumza hadithi hii kwasababu bado kulikuwa na fursa ya kumpata mrithi wa mfalme hata pale ambapo baada ya watoto wote wa Yese kupita, Samweli akasema hakuna mwingine? Watoto wako ni hawa tu? Ndipo Yese akakumbuka kuwa Daudi hakuwepo pale, akasema yuko mdogo wao, yuko machungani, Yese akasema mlete huyo, na Daudi alipoletwa huku akionekana mwekundu kabisa kwa maana mwenye ngozi angavu maana alitumia muda wake mwingi nyikani, hodari na mwenye ujasiri, Mungu akamwambia Sauli huyu ndiye, mpake mafuta awe mfalme wa watu wangu.

Nikiutizama mchakato wa CCM naona rundo la watangaza nia wakiakisi watoto wa Yese, lakini maadamu mpaka leo hii bado tuna siku kama 10 nina uhakika bado tuna watu ambao huenda nao wana maono ya kiuongozi kwa Taifa letu. Rai yangu ni kwamba watu hawa wajitokeze ili michakato ya vyama iwaridhie kama wagombea na huku wakiamini hata Mungu wa Mbinguni akiangalia atasema mtu huyo mnayempendekeza ndiye na atawaongoza salama na kwa uadilifu watu wangu wa Tanzania.

Tusiwatizame watangaza nia sura zao, umaarufu wao, ufuasi wao ambao wameujenga, tusitizame tunanufaika nao sasa kwa kiasi gani, kwa maneno mengine tusitizame masilahi yetu binafsi, tulitizame Taifa kwanza. Nina uhakika michakato katika vyama vya siasa inapaswa kuwa huru na inayozingatia haki ya wanachama kuomba nafasi mbalimbali za uongozi. Rai yangu tena bora watoto wa “Daudi” waendelee kujitokeza na huenda mwishoni tutampata Yule ambaye kwa hakika atakuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano.

Kuhusu Vigezo na Sifa za Mgombea

Kwa jinsi utaratibu ulivyo sasa ni kwamba majina ya watangaza nia yatapelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itayapitia na huenda wengine watakwamia hapo kisha baadaye kwenda Kamati Kuu kwa ajili ya uteuzi wa majina matano.

Haya majina matano yatapelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili yaweze kupigiwa kura na kupatikana majina matatu ambayo yatapelekwa katika Mkutano Mkuu ambao nao utapiga kura ili kumpata mgombea mmoja.

Sifa za wagombea urais katika Chama cha Mapinduzi zinafahamika ambazo watangaza nia watapimwa nazo ili mtangaza nia kwa nafasi ya Urais wa CCM aweze kuchaguliwa katika nafasi hiyo. Mbali ya kupitia taratibu za chama, watangaza nia wanapaswa pia kukidhi vigezo na sifa zifuatazo; Mosi, anapaswa kuwa na uwezo wa kuliongoza Taifa kwa kuzingatia uzoefu alionao katika uongozi wa shughuli za Serikali, umma na taasisi.

Pili, awe mwadilifu, mwenye hekima na busara, tatu, awe na elimu ya kiwango cha Chuo Kikuu au inayolingana na hiyo, nne, awe mwenye upeo na uwezo mkubwa wa kudumisha, kuimarisha na kuendeleza Muungano wetu, umoja, amani na utulivu wetu pamoja na mshikamano wa kitaifa.

Tano, awe mtu wa kuona mbali, asiyeyumbishwa, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara kuhusu masuala nyeti na muhimu ya Taifa kwa wakati unaofaa, sita, awe na upeo mkubwa usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi yetu na Dunia yote kwa jumla.

Saba, asiwe mtu mwenye hulka ya udikteka au ufashisti bali aheshimu na kuilinda Katiba ya nchi, sheria, utawala bora, kanuni na taratibu za utawala bora, nane, awe mtetezi wa wanyonge, kusimamia haki za binadamu, mzingatiaji makini wa maendeleo ya raia wote na asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu wake binafsi.

Tisa, awe mstari wa mbele kuzifahamu, kuzieleza, kuzitetea na kuzitekeleza Sera za CCM na Ilani ya CCM ya Uchaguzi, kumi, awe mpenda haki na jasiri wa kupambana na dhuluma, maovu yote nchini, kumi na moja, asitumie nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali.

Kumi na mbili; awe ni mtu anayekubalika na wananchi, kumi na tatu; awe makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa uongozi, watendaji, asiyevumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ili kuinua nidhamu ya kazi, tija na ufanisi.

Uhalisia wa hali ilivyo

Kwanza ile kusema ni watano tu, tayari ni mgogoro, kama tuna makada wanaokaribia 40 kupata watano inaweza kuwa ngumu kama tutajikita tu kwenye vigezo 13. Nikupe Mfano, kuna ile desturi ya viongozi wakuu ambao wameonesha nia kwamba lazima wawemo katika ile tano ya kwanza, lakini pia lazima tuzingatie uwakilishi wa Bara na Zanzibar, kisha ongeza watu wenye makundi makubwa na kwa bahati mbaya ambayo mpaka sasa yameshaanza kujikita kikanda yaani kimakabila. Halafu kuna hoja ya ujinsia, nina uhakika hii inachukuliwa kama hoja ya kujikosha siku hizi. Utagundua ile tano haitoshi.

Lakini hii ya watano ni desturi tu, bado kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kinaweza kuiagiza Kamati Kuu (CC) kuleta majina zaidi na si matano tu, lakini pia Mkutano Mkuu (Congress) unaweza kusema pia kipindi hiki tunataka majina zaidi ili kutoa haki kwa wagombea wengi zaidi badala ya kuwakata mapema.

Ukilitizama jambo hili vizuri utagundua hekima inahitajika zaidi na hasa hekima kwa viongozi watakaokuwa wanafanya maamuzi. Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete nadhani ndiye mtu ambaye ana mtihani mkubwa zaidi, kwasababu kipindi hiki na kwa uzoefu wa hali, hili ni pori jipya na mbinu za zamani zaweza kuwa sio muafaka katika pori hili nene. Makundi ya sasa ni mabaya zaidi kuliko ya mwaka 1995 na zaidi ya mwaka 2005, maamuzi mabaya ama yatatupeleka katika hali mbaya kuliko 2005 au yatahuisha furaha na imani ya Wananchi kwa Chama cha Mapinduzi.

Tukiwatizama watu tutajiingiza katika mtego wa kuogopana, kuoneana haya, ubinadamu ukiingia, haki itaondoka, na maamuzi hayatokuwa katika maslahi mapana ya chama na Taifa kwa ujumla. Nimeanza kusema sema kwa sauti ya chini, karibia wagombea wote hasa wakubwa wanatumia fedha, ni kweli kwamba hawawezi kutumia mawe, lakini kama tuna nia ya kuwaengua waovu waliozidi ambao sio mmoja kwa hakika lazima tutumie utaratibu safi. Kwa haya maneno tunayoyasikia mitaani ya kutumia mbinu za ujanja ujanja, ni dhahiri kwamba mbinu hizo hazitaweza kuwadhibiti wajanja ambao mpaka sasa ni wengi miongoni mwa watangaza nia.

Tuangalie watu wana matarajio gani kwa serikali ya awamu ya Tano, tutizame kero kubwa ambazo zinakera watu wetu. Kisha mtusaidie kwenye vyama vyenu sio kutuletea watu wenye sifa ya kuwa madiwani, wabunge, mawaziri, mawaziri wakuu, makamu wa Rais, wachambuzi wa sera na kadhalika na mkawafanya hao kuwa ndio mnaowapendeza wachukue nafasi ya Urais wa Nchi yetu. Msifanye makosa kudhani kila mtu anaweza kuwa Rais, msifanye makosa na hapa nizungumzie CCM kudhani kwamba maadamu chama kitambeba basi watu watamkubali, la hasha.

Kizazi cha leo kinajitambua, kinapima, kinapambanua, kinachekecha, tuleteeni mtu ambaye, tukimtizama tupate amani ya nafsi na amani kwamba maslahi yetu kama Taifa yatalindwa kwa manufaa ya Wananchi raia wa Jamhuri yetu.

Hasara ya kuleta bora mtu au mtu mwenye sura nzuri, au mwenye mbinu nzuri za wazi au za siri siri ni kwamba Wananchi wataona mmewachukulia nafuu, na adhabu yake hawataitoa kwa mgombea Urais, watawanyima wabunge, na mkumbuke wakiwanyima wabunge mtakuwa serikali boya.

Tupatieni mgombea ambaye akienda kuwanadi wagombea wenu wa udiwani na hasahasa ubunge Wananchi kwa heshima yake mtu huyo watawapeni wabunge wengi pia. Mkidharau ushauri huu, yatawapata ya serikali za mitaa, Mwenyekiti ni wa CCM na Kikao chote ni UKAWA, kama CCM mnaweza msifike huko. Na ninyi watu wa vyama vyenye mawazo mbadala mnafanya kazi nzuri, narudia tena endeleeni kujenga taasisi zenu na kujiimarisha, kwa mujibu wa Katiba ya Mwaka 1977 na inayotumika sasa, mkipata wabunge wengi, mtakuwa na uwezo wa kutoa Waziri Mkuu, mkifika hapo itakuwa ni hatua kubwa kabisa katika historia ya Taifa letu. Hii tama ya Urais ni ya kusadikika, nimeona niwaseme kidogo, pokeeni na mtafakari.

Naomba mrejee Ibara ya 51 ya Katiba inayosema “(1) Kutakuwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais kwa kufuata masharti ya ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais kwa kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge. (2) Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua Mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye Wabunge wengi zaidi Bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye Wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na Wabunge walio wengi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, naye hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za Wabunge walio wengi.


Karibu msome na tujadiliane kwa hoja na sababu.

Sunday, June 14, 2015

HALI HALISI YA NCHI NA RAIS TUNAYE MTAKA: TANZANIA NJIAPANDA, TAIFA LIFANYE NINI?



Kinyang’anyiro cha Urais-Tanzania iko njia panda

Wengi mtakubaliana name kwamba kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi kimekwenda kwenye kiwango kingine kabi
sa, na hasa ukizingatia mpaka sasa huenda kuna makada zaidi ya 30 ambao wameonesha nia ya kuomba ridhaa ya chama.

Wengi wamekuwa na maswali ya kiuchokozi hapa na pale kwamba unadhani wimbi hili kubwa la wagombea tafsiri yake ni nini? Nimejitahidi mara zote kusema kuna tafsiri zaidi ya moja, mosi ni uhalisia kwamba wana CCM wako huru kuweka mawazo yao hadharani, pili, demokrasia iko pana katika chama kwamba yeyote ambaye anaona anaenea katika nafasi basi anayo fursa ya kujitokeza na kutangaza nia na hatimaye kuomba kukubalika na chama.

Tatu, ni kwamba huenda watu hawajui maana hali ya tafsiri ya urais kama taasisi na Rais kama kiongozi Mkuu wa nchi na majukumu yake, huenda watu wanauona urais kwa maana ya kusafiri kila pahala, kufungua miradi, kutoa hotuba, kutoa maelekezo, kupita kwenye msafara wakati wengine tunasubiri foleni, kutuma watu wakafanye kazi kana kwamba watu hawajui wanalopaswa kutenda.

Wengine wanadhani pia ukiwa Rais kazi ya kuwashughulikia wauza dawa za kulevya, kushughulikia wala rushwa na ufisadi ndio hasa itakuwa kazi yao, hawa nawaona wakitembea na pingu, bakora za mibungo na magereza yanayotembea ili kila watakaye mbaini basi watamfunga papo hapo, wapo watangaza nia ambao nikienda kwenye vichwa vya kwa kutafakari nawaona wakiwaza hivi.

Nne, ni kwamba huenda kuna watu wahuni pia, watu wasio na mapenzi mema na taifa hili, watu ambao wamegeuza nafasi ya urais bidhaa ya mnadani. Hawa wako pale kuhakikisha wanakuwa Rais, haijalishi sote tunajua Urais mtu hupewa kama dhamana na wananchi, lakini wapo ambao tayari wameshajiona marais, hii ni kuwakosea wapiga kura, na zaidi kukikosea heshima Chama cha Mapinduzi. Hawa watu wa namna hii wao hawajali demokrasia kwa maana ya utawala wa watu kwa watu na watu wenyewe yaani kiingereza “democracy”, watu hawa ni genge la wajanja wachache ambao wanataka kushika madaraka ya nchi, maslahi yao ya msingi ni wao wenyewe kiingereza mtindo huu tunaita “mobocracy”.

Kisiasa- Tanzania iko Njiapanda

Wengi wanahoji dira ya Taifa hili ni ipi? Taifa halina dira, ninaposema hivi wengi mtasema kwamba mbona tunayo ile inaitwa “vision 2025”, ni kweli lakini ile ni dira ya Tanzania Bara pekee, na Tanzania Bara si Taifa, utaniambia pia “vision 2020” nakubali lakini hiyo inahusu Zanzibar pekee, sasa na mimi nitakuuliza je iko vision moja ambayo inazungumzia Taifa la Tanzania?

Kwanza nikitizama vision 2020 na 2025 utagundua bado hazina sifa ya kuwa Dira. Dira ni waraka ambao, Taifa kwa mwafaka limesema huko ndiko tunakotaka kwenda. Ukisoma vizuri hizi nyaraka mbili kila moja iko huru, nikimaanisha Ukisoma vision 2025 inazungumza kana kwamba Tanzania Bara ndio Jamhuri na Muungano na vivyo hivyo ukisoma vision 2020 unaona Zanzibar inajizungumza yenyewe kana kwamba ni huru. Kwangu mimi kitendo cha nchi moja kuwa na dira mbili na zisizosomana ni sawasawa kabisa na kuwa na ndege moja yenye marubani wawili wasio na uelewa wa pamoja wa wanakwenda wapi. Juzi juzi hapa kule nchini Ujerumani kitendo cha kuwa na marubani wawili wasio na uelewa wa pamoja ndege inapaswa kwenda wapi kilipelekea ajali mbaya kabisa, rubani mmoja anajua tunatakiwa kuwafikisha salama abiria wakati rubani mwingine ana mipango ya kutoa uhai wa abiria na yeye mwenyewe kwa kuigongesha kwa makusudi ndege kwenye milima.

Mzee Warioba alijaribu kututengenezea dira katika Rasimu ya Katiba Toleo la Pili, lakini Katiba Inayopendekezwa ikasema hata serikali isipofanya chochote katika utekelezaji wake isihojiwe kokote hata mahakamani na mtu yeyote asiwe na mamlaka ya kuhoji juu ya utekelezwaji wa dira hiyo, sasa hapo ni dira au kiini macho?

Taasisi za Mamlaka ya nchi hasa Bunge ni dhaifu, unakumbuka wakati wa Bunge Maalum wengi ya wabunge walitaka mikataba isipelekwe Bungeni, baada ya Bunge maalum wakazinduka wakataka mikataba ya TPDC, wakanyimwa, roho ikawauma sana hata wakatenda kinyume na mamlaka yao na kuelekeza Polisi iwakamate viongozi wa shirika la mafuta, walitenda kwa hasira, kiko wapi leo? Kitendo kile kikawafanya watake mikataba ipitie bungeni kupata ukubalifu, hawa ni wale wale ambao wengi wao walifuta masharti ya rasimu ya Warioba yaliyosema mikataba ya madini iridhiwe na bunge.

Wakati Bunge likiwa na mtanziko wa kimamlaka, hali iko dhahiri shahiri kwamba kuna upungufu wa utamaduni wa kidemokrasia (democratic culture), tumeacha kuwa watu wa majadiliano (dialogue), hatujengi hoja bali tunapiga makelele na kushutumiana wakati wote, Mwalimu Nyerere alipata kusema “argue, don’t shout”. Hatujengi muafaka, hatufanyi maridhiano, hatuna uelewa wa pamoja katika masuala ya msingi, hatuna uhimilivu (tolerance) lakini inaonekana tuna uhimilivu kwa mambo kama rushwa, ufisadi, mauaji ya albino na vikongwe n.k.

Tumeanza kushuhudia roho mbaya ya utengano (negative devisive force), ukabila, ukanda, udini, ubara na uzanzibari n.k. Umeshuhudia hata watangaza nia tayari wameanza kujipanga kikanda hii ni hatari kwa ustawi wa umoja wa kitaifa. Inaanza kuonekana Uongozi si dhamana tena bali mali ya watu fulani. Utumishi wa umma unafanya kazi kwa woga. Maadili ya Taifa, binafsi na ya viongozi ni tatizo kubwa, hata pale sekretarieti ya Maadili ya viongozi inapowafuatilia wale wanaokiuka miiko ya uongozi utagundua nguvu zake zina ukomo mkubwa.

Kuongezeka kwa vitendo vya Rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili, angalia namna ambavyo watangaza nia wanatumia fedha nyingi, swali la kujiuliza ni fedha zao binafsi? Na kama si zao waliowapa wana maslahi gani na nafasi ambayo watangaza nia hawa wanaitafuta? Muungano wetu bado una changamoto nyingi, Serikali 2 hazieleweki, sio tu kwenye Katiba ya 1977 bali hata kwenye Katiba Inayopendekezwa. Watu wa Tanzania Bara wanauona Muungano kama mzigo na watu wa Tanzania Zanzibar wanauona Muungano kama Kero. Kuvurugwa kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ni huzuni nyingine inayoongeza njia panda ya kisiasa

Kiuchumi- Tanzania Njiapanda

Umma wa watanzania hauna mali za pamoja, tulibinafsisha kila kitu na mashirika ya umma yaliyosalia ni hohehahe, mfano ni shirika la ndege la Taifa “Air Tanzania”, shirika la reli (TRL) ni shida nyingine kubwa licha ya kwamba tuna ubia na watu wengine. Tuna shirika la nyumba (NHC), hili linakimbia kwa kasi baada ya maboresho makubwa ya kiutendaji, lakini nawapa indhari kwamba uchumi wa Marekani ulianguka kwa uwekezaji usiotabirika katika makazi na nyumba, tuwe macho.

Sekta binafsi ni dhaifu, sekta binafsi imeingia katika huduma na si uzalishaji, tizama kampuni ambazo zinaonekana vinara ni makampuni ya simu. Haya hayazalishi, haya yanatoa huduma na yanachukua pesa za watanzania masikini zaidi kuliko hata faida ambayo tunanufaika nayo moja kwa moja kama wananchi masikini na wasio na ajira.

Angalia ongezeko kubwa la mabenki, unadhani wanufaikaji ni wakulima na wafanyabiashara ndogondogo ambao kwa kiasi kikubwa wanaangukia katika sifa za watu wasio kopesheka, Tuamke, benki ni nzuri lakini lazima tuwe na uchumi ambao unabeba watu wake.

Hakuna viwanda vya kutosha vya uzalishaji kunakopelekea tatizo la ajira na kupoteza fedha za kigeni (hakuna exports za kutosha), mchele wa mbeya na kwingineko tunao lakini tunaagiza, sukari ya kutoka Mtibwa, Kilombero na Kagera tunayo lakini tunaagiza, tunayo gesi lakini bado tunaagiza mafuta mazito. Halafu dola ya kimarekani ikifika zaidi ya shilingi 2000 tukiuliza tunaambiwa huko duniani dola imeimarika zaidi, kweli?

Sekta binafsi iliyo dhaifu haiwezi kusimamia demokrasia na kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwepo. Na hapa niwaseme kidogo Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwamba wameona Bunge Maalum lilivyoendeshwa na namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imedhoofisha maadili ya viongozi na kuvuruga Dira ya Taifa kwa kuiwekea vikwazo, lakini kwani umesikia wakikemea au wakishauri kitaalamu madhara ya kubomoa misingi ya maadili na uwajibikaji katika Katiba? Nawapa changamoto, na wao wajitafakari.

Mkazo haujawekwa katika uchumi wa kujitegemea unaozingatia ukuaji wa kilimo kinachotoa malighafi kwa ajili ya viwanda ambavyo vinachakata malighafi kuwa bidhaa zilizochakatwa au bidhaa kamili ambazo ziko tayari kurudi na kutumika katia sekta nyinginezo ikiwemo kilimo

Kukosekana kwa uchumi imara unaojitegemea kunazalisha watu masikini wengi zaidi katika Taifa letu. Tuna walipakodi wachache na tuna walaji wengi katika Taifa lakini pia mianya ya wanaokula zaidi yaw engine kinyume cha sheria ni wengi zaidi na kusababisha chakula wanachokusanya wachache wetu ama kinaliwa na wachache wetu kinyume na sheria na matokeo yake hakitoshelezi mahitaji yetu kama Taifa. Tunalo pia Tatizo la kuwa na vyanzo mbadala mbali na hivi vya sasa vya mapato ya Taifa na Serikali, na bado tunalo tatizo la Makampuni ya madini kutokutoa kodi ya mapato kutoka faida zao.

Wengi wanasema wanatoa kodi lakini ni kodi wanazokatwa wafanyakazi wao na sio kodi inayokatwa kutokana na shughuli za ushalishaji wa makampuni. Kwenye gesi ni eneo linguine ambalo ukiachia kwamba limegubikwa na sintofahamu juu ya namna mikataba yake imefungwa hasa katika ngazi ya utafutwaji wa gesi ni kizungumkuti kingine kinachotuweka kwenye njiapanda kama Taifa.

Rais tunayemtaka Awamu ya Tano

Tunataka Rais ambaye anajua tuko njia panda, ana ana uwezo na mamlaka ya kukemea kwasababu na yeye ni mwadilifu “moral authority”. Tunataka kiongozi ambaye anakubalika na jamii na jamii inamwona kama sehemu ya majibu ya changamoto zao. Hatutaki watu wajitembeze kwetu, tunajua tunataka Rais ambaye atasimamia masilahi yetu.


Leo karibu kila mtia nia, nasikia huyu kapata pesa kule, huyu kapata pale, huyu hela za wizi, huyu kapokea hela chafu, huyu kachukua za watu wabaya na kadharika. Watanzania tuache ushabiki, tusimame na tuwe wamoja katika hili. Rais wetu akiletwa na watu maana yake si wetu ni wao. Tafakari

Saturday, June 6, 2015

WATANGAZA NIA WAJIPIME KWANZA KWA HAYA MACHACHE: TUJIREKEBISHE

Kuonesha kila mtu anaweza kutangaza nia ya Urais kwa watu wazima ni kumkosea heshima aliyeko madarakani

Wiki ijayo nitaendelea kujadili hasa kwenye runinga, redioni na kwenye hadhara mbalimbali juu ya mchakato wa ndani ya Chama cha Mapinduzi wa kumpata mtu atakayepewa dhamana na chama ya kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Ninaendelea kusisitiza kwamba, CCM inapasa kuonesha mfano kwa vyama vingine, CCM inatakiwa kutoka katika mchakato wake wa ndani kwa ushindi. Ninaposema ushindi ninamaanisha, mbele ya macho ya watu na kwa wingi wa wale ambao ninaonana nao. CCM haijajijengea taswira nzuri mbele ya watu na hasa vijana wadogo na kwa maneno mengine hii ni fursa adimu na adhimu ya kuuthibitishia umma wa watanzania kwamba imani yao kwa CCM haijawekwa rehani.

Lakini kabla sijaainisha mambo machache ambayo wana CCM wanatakiwa kujipima kwayo ninabudi ya kueleza pia kwamba, licha ya chama kutoa uhuru mpana kwa watu kutangana nia ya uombea Urais, lakini pia jambo hilo linaleta taswira yenye ukakasi kidogo. Inawezekana tuna wana CCM wengi wenye uwezo mkubwa wa hata kupewa utawala wa nchi lakini inabidi kujichunguza na kutafakari ndani ya chama je kuwa na wagombea karibia 20 ni sifa yenye tija au ni sifa za kijinga mbele ya macho ya watu?

Kila kona watu wanasema hata huyu, hata yule? Inaonekana kana kwamba ni mchezo wa gombania goli, maadamu unaweza kubutua mpira mbele basi karibu uwanjani, la hasha. Najua CCM inajua fika na kwa uzoefu kwamba Urais ndio taasisi kubwa kabisa katika Taifa letu. Taasisi ya Urais na kiongozi wake ambaye ni Rais mwenyewe, ni nafasi na wadhifa nyeti kabisa. Taasisi ya Urais na nafasi ya Urais si pahala pa kukimbilia kana kwamba ni mchezo wa “chandimu” au “gombania goli”.

Nimepata kusema hapo awali uongozi wa nchi na hasa uongozi wa juu kabisa wa nchi yetu ni kama cheo cha kiongozi wa dini, ni kama kuhani ni kama nabii, nafasi hiyo ni takatifu. Kwa wale wenye imani ni vema mkajua kwamba hata Mungu anapolitazama Taifa letu ili kulibariki na kutufungulia neema, huzipitisha Baraka na neema hizo kwa yule Kiongozi wetu mmoja ambaye ndiye taswira ya Umoja wetu, huyo ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkichagua mtu ambaye kwa sifa za kibinadamu na kwa muonekano wa haraka haraka wa kibinadamu ni mzuri, Taifa letu litakosa Baraka za Mungu kwa miaka mitano inayokuja.

Nafasi kama hii ya Urais kwa asili yake mtu hutafutwa, huombwa na hata kulazimishwa na wale ambao huwa wameonekana kutoka miongoni mwetu kuenea katika nafasi hiyo aghalabu hukubali kwa kuumia moyo kwasababu wanajua jukumu lilopo mbele yao ni gumu, zito na lenye changamoto nyingi.

Na hapa niwaase viongozi wa dini kwamba wao ndio mabalozi wa Mungu hapa duniani, wawe makini sana hasa kipindi hiki kwasababu iwapo watamwakilisha Mungu sehemu ambazo Mungu asingependa kuwakilishwa itakuwa ni kujichumia dhambi kubwa.

Unajua katika utendaji wa majukumu ya nchi balozi ndiye mwakilishi wa nchi na mwakilishi wa Rais, sasa nikupe mfano, mwaka 1977 tulikuwa na mgogoro na Nduli Idi Amini Kiongozi wa Uganda wakati huo, sasa kama ingetokea balozi wetu kila kukicha yuko kwa Idi Amini anakula na kunywa naye kama marafiki tena kwa utashi wake mwenyewe wala sio kwa maelekezo ya kimkakati kutoka makao makuu kwa maana ya hapa nyumbani. Je balozi kama huyu tungemtendea vipi? Katika kipindi kile cha vita, huyu angekuwa mhaini moja kwa moja na adhabu yake ni kifo. Sasa na ninyi viongozi wa dini ambao mnamwakilisha Mungu katika maeneo ambayo mnajua kabisa asingependa kuwepo, mjue, na ninawaambia leo kwamba mbele za Mungu adhabu zenu zitakuwa zile zimstahilizo anayemuasi Mungu, kibinadamu huwa tunaita mhaini. Kuweni macho!

Na niwaase pia wana CCM watakao kuwa na dhamana ya kupitisha mgombea wao kwamba, msianze kuhukumu watu kwa muonekano wao, msije nanyi mkahukumiwa, hatumpimi mtu kwa habari za kusikia, la hasha, maana najua wako katika watangaza nia ambao wamefanikiwa kuficha ubaya wao, lakini hawana tofauti na wale muwaonao wabaya sasa, watendeeni haki na Mungu atawaheshimu.

Baada ya kusema maneno ya utangulizi sasa naomba kwa sehemu nieleze baadhi ya matarajio ya Tanzania na watanzania kwa Rais wa Awamu ya Tano. Matarajio haya yamejikita katika namna ambavyo Rais wa awamu ya Tano ataweza kwa uwezo na ufanisi mkubwa kushughulika na masuala ambayo kwa muda mrefu sasa yametuvuruga kama Taifa na yametuacha katika sintofahamu juu ya mustakabali wetu kama Taifa sasa na baadaye.

Kusimamia Utawala Katiba na Sheria

Rais wa awamu ya Tano anapaswa kujua kwamba kwa muda mrefu tumekwenda kinyume na Katiba au kwa lugha kali tumekuwa tukivunja Katiba muda mrefu hata tukazoea tabia hiyo na kuifanya mazoea, tabia na utamaduni. Rais wa awamu ya Tano anapaswa kuwa mtu mwenye uhalali wa jamii “social legitimacy” na ambaye kwa uhalali huu atakuwa na mamlaka ya uadilifu yaani “moral authority” ya kuondoa kabisa mazoea, tabia na utamaduni wa kuvunja Katiba na kuenenda kinyume cha sheria za nchi.

CCM wakitupatia mtu ambaye hana uhalali wa jamii yaani “social legitimacy” na ambaye hana mamlaka ya uadilifu yaani “moral authority” kwa uwazi tumwonavyo sasa na kwa kificho tusivyomjua sasa, mtu huyo kamwe hatoweza kusimamia utawala wa Katiba na Sheria, mtu huyo ataendeleza mazoea yale yale yasiyofaa. Mtu huyo ataendelea kulinda maslahi ya wale wanufaikao na mazoea, tabia na utamaduni wa kuvunja sheria za nchi, mtu huyo hatakuwa Rais wa watanzania na vivyo hivyo watanzania wasitegemee miujiza kutoka kwake.

Suala la Muungano wetu

Matarajio ya watanzania kwa Rais wa awamu ya Tano ni pamoja na kushughulikia na kumaliza kabisa Changamoto za msingi zinazokabili Muungano wetu. Kila mtu anajua kwa tuna manung’uniko kutoka kila upande wa Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Tunataka mtu ambaye ana uhalali, ana mamlaka na anaheshimika na viongozi wastaafu na walioko madarakani kwamba anaweza kuwaitisha na kuwaambia “watanzania wanatatizwa na Changamoto za Muungano wetu na kwa pamoja tunakwenda kuziondoa”. Awe mtu ambaye viongozi wa upinzani na viongozi wa CCM wakimtizama wanasema mtu huyu ninamheshimu na nina imani naye kwamba anaweza kufanya kazi hii.

Naomba niwaume sikio kidogo, tunataka mtu ambaye ataimarisha heshima na nidhamu ya madaraka ya Rais, leo hii wengi wa viongozi wetu hawaheshimiani, hawapendani, hawazungumzi na ukiongea na huyu anamlaumu yule, ukiongea na yule anajifanya kama halioni tatizo vile, na hawakai kwa ujumla wao wakazungumza na kuondoa tofauti zao. Hii inakwenda kwa viongozi wa wastaafu na walioko madarakani, kila mtu anamwonea kinyongo mwenzake. Tunamtaka mtu ambaye ana uhalali wa kuwaita wote na wakaitikia wito. Leo hii tuna nchi mbili na serikali mbili, hili ni baa maana hata ukisoma ibara ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema tofauti.

Muungano umejeruhiwa zaidi miaka mitano iliyopita na hatujaweza kuponya majeraha yake hata kidogo isipokuwa kutoa dawa za kupunguza maumivu, dawa za kupunguza maumivu ndio kushughulika na zinazoitwa “kero za Muungano”. Sasa ufike wakati tumpate mtu ambaye tunaamini ataweza kutoa dawa ya kuponya na kumaliza ugonjwa kabisa ili Muungano wetu uwe na afya ya kudumu miaka 100 ijayo.

Ujenzi wa Amani, Umoja na utulivu (stability) wa kisiasa

Tunamtaka Rais ambaye anajua kwamba amani na Umoja wa Taifa letu msingi wake ni haki na usawa kwa watu na Wananchi wetu. Anapaswa kujua amani ni tokeo la ujenzi endelevu wa amani pamoja jitihada endelevu za kulileta Taifa kuwa kitu kimoja licha ya mtawanyiko mkubwa wa makabila na dini za watu na Wananchi wetu. Matarajio ya watanzania kwa Rais wa awamu ya Tano, ni kuona haki za watu na binadamu raia wa nchi yetu zinaheshimiwa, zinatolewa kwa wakati, zinalindwa na kuhifadhiwa.

Aidha Rais huyu ajaye anategemewa kutoa hamasa na kuwa mfano wa kulinda na kuzitoa haki hizi ili watu na raia wa Taifa letu waweze kunufaika na kufurahia matokeo kuheshimu haki za binadamu. Ili haki itolewe ni lazima usawa uzingatiwe kwa gharama yoyote ile. Haki bila usawa ni kazi bure, Amani bila usawa ni kazi bure kabisa. Rais ajaye anatakiwa kujua tumecheza cheza na haki za raia wetu na kwamba hatujafanya kazi nzuri ya kuzitoa haki hizi kwa usawa kwa watu wetu katika maeneo yote ya nchi na kati ya masikini na matajiri.

Ukicheza na haki za binadamu na watu, kisha ukaondoa usawa kwa kupendelea wachache, jua tunakaribia ukingoni, muda si mrefu, watu na raia wetu watakwenda kuchukua haki zao kwa mikono yao, kwa vigezo vya maeneo ya kijiografia, dini, masikini dhidi ya matajiri na kadharika. Tukifika huko, amani yetu tutakuwa tumeiweka rehani na Umoja wetu mashakani. Leo hii viashiria vyote kwa amani yetu inatetereka viko bayana, tunamtaka mtu ambaye akisimama tu imani zetu za nafsi juu ya Taifa letu zinaanza kukua mara moja, mtu huyo akisimama hata imani ya uchumi inaanza kuimarika na utashangaa kabla ya kuanza kutenda kiuchumi thamani ya shilingi ya Tanzania itaimarika.

Nafasi ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama

Tendeni haki, shaurini viongozi wetu, msijiingize kwenye siasa na kamwe msishiriki kufanya uamuzi wa kisiasa, kazi yenu ni ushauri na ni ushauri tu. Kama mpo wenye tabia mbaya na isiyo na heshima ya kutisha viongozi wetu ninawaasa acheni mara moja. Rais wa nchi hupatikana kwa ridhaa ya Wananchi na si vinginevyo, katika utumishi uliotukuka wa vyombo vya ulinzi na usalama, mnajua ni dhambi na ni kinyume na weledi wenu kujaribu kutengeneza Rais kwa namna na hali yoyote ile.

Najua dhamira njema hutenda haki, na ninyi mmeapa hata kwa kufa ili nchi hii iishi, msiruhusu wachache na wabaya na wenye dhamira mbaya miongoni mwenu kuvuruga zoezi takatifu la kupata Kiongozi wa nchi hii. Wale ambao mtasimamia maadili ya kazi yenu, histoa itasimama kueleza utumishi wenu uliotukuka na wale ambao tama imewazonga, ni suala la muda tu na aibu kuu itawazonga na hatutawadhihaki bali tutahuzunika kwamba tulifanya uamuzi mbaya kuwa nanyi katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Maswali kwa watangaza nia wiki hii


Walikuwa wapi kusimamia waziwazi maslahi ya Wananchi katika mchakato wa Katiba?