Thursday, January 4, 2018

WANA CCM SONGENI MBELE, MAKWAZO HAYANA BUDI KUJA


WANA CCM SONGENI MBELE, MAKWAZO HAYANA BUDI KUJA

CCM Madhubuti inajengwa katika Misingi ya Maadili, Nidhamu ya Chama na Uongozi wa Kiutumishi

Nimeketi na kutafakari sana juu ya mwenendo wa nchi kwa ujumla na nikatizamia baadhi ya mambo ambayo yametendeka katika ulimwengu wa siasa hapa nchini kwa Mwaka 2017, Napata funzo kubwa sana.

Nimejiuliza sana juu ya dhamira yetu kama Taifa, nikajiuliza zaidi juu ya dhamira ya sisi viongozi wa kisiasa wa vyama vyote na kutizama kama dhamira ya Taifa na dhamira ya sisi viongozi wa kisiasa zinawiana.

Kuwiana kwa dhamira hizi ni faida na tija kwa Taifa, maana sote tutakuwa tunajua kama Taifa watanzania wanataka nini? Na kisha tutahakikisha sisi kama viongozi wa kisiasa kwa dhamana zetu na katika vyama vyetu vyote (vyenye uwakilishi na visivyo na uwakilishi katika Mabaraza ya Madiwani na Bunge la Jamhuri) tunasimama kuhakikisha Maslahi ya Taifa yanasimama imara wakati wote.

Dhamira za viongozi wa kisiasa zinapokinzana na matarajio ya wananchi na mahitajio ya wakati, hapo ndipo huibuka msigano wa kimasilahi kati ya viongozi wale wanaosimamia Masilahi ya Taifa na ya muda mrefu na wale ambao wanasimamia masilahi binafsi na ya muda mfupi.

Hitajio la wakati ule na sasa na matakwa ya wananchi katika miaka 10 iliyopita kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 yalikuwa yafuatayo katika kada ya uongozi na kwa uchache nikitaja, kuimarishwa kwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi, kupambana kwa nguvu zote na ubadhirifu au matumizi mabaya ya mali za umma, nidhamu ya watumishi wa umma, maadili ya Taifa, Maadili ya watumishi na viongozi wa umma, viongozi na watumishi hawakuwa tena watumishi wa watu bali mangimeza wasioheshimu watu wala kusikiliza na kushughulika na shida zao.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya tafakuri kubwa kilitambua kwamba hakukuwa na namna nyingine yoyote ya kuendelea kupokea heshima na ridhaa ya wananchi isipokuwa kufanya Mageuzi makubwa ambayo yangeleta Mabadiliko makubwa katika utendaji, usimamizi wa Sera zake kwa Serikali, kuondoa kabisa desturi mbaya, kuongeza na kuimarisha kabisa nidhamu ya chama.

Ilifika pahala Chama kilipoteza heshima yake mbele ya kundi dogo la wanachama ambao walikuwa wana nguvu kuliko Chama chenyewe. Hali hii iliondoa sana imani ya wanachama wa msingi na umma wa watanzania, nidhamu ya Chama inapopotea linaibuka kundi dogo la wanachama masilahi ambao lengo lao ni kujinufaisha kwa mgongo wa Chama, hawa wakiachwa kumea, wanaamua na chama kinalazimika kufuata.

Kazi ya Kwanza ya uongozi wa Awamu ya Tano na vikao vyake vya Maamuzi ilikuwa ni kuvunja desturi hii ya hovyo, Chama kufuata mwanachama, na kurejesha nidhamu ya Chama kwamba mwanachama yeyote lazima afuate nini Chama kinasema na nini kinataka. Hii sio kazi rahisi, maana wapo ambao waliota mizizi na wamenufaika muda mrefu katika desturi hii ya kukitumia Chama kwa faida binafsi.

Kisha Uongozi ukaelekeza Serikali kushughulika kikamilifu na maswala ya ufisadi, rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya ofisi nikitaja machache, na kwa ushahidi leo hii hata tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba rushwa sio tena miongoni mwa kero kubwa miongoni mwa wananchi. Bado tunayo kazi ya kuimaanisha vita hii lakini kwa usaidizi wa wananchi tutashinda.

Kabla ya uchaguzi wa 2015, tulipata ukosoaji mkubwa wa namna tunasimamia haki ya Tanzania katika uvunaji wa rasilimali madini nchini. Na baada ya CCM kuaminiwa tena sote tu mashahidi kwamba kwa mara ya kwanza tumeandika historia kwamba Tanzania itapata 50 kwa 50 gawio la faida katika migodi mikubwa nchini na zoezi la uhakiki wa mikataba gandamizi linaendelea kote nchini.

Ukiacha namna ambavyo Uongozi wa awamu ya tano umejikita katika kurejesha misingi ya uadilifu, uaminifu, kuchapa kazi, unyenyekevu, Uongozi wa Kiutumishi, vita dhidi ya rushwa na kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, kuimarisha makusanyo ya serikali na kuweka nidhamu katika matumizi bado kazi kubwa imefanyika katika masuala ya maendeleo, leo na ndani ya miaka miwili tu, tumenunua ndege sita na moja ikiwa ndege kubwa kabisa na ya kisasa.

Tumeanza ujenzi wa kihistoria wa reli ya kiwango cha kimataifa ambayo gari moshi lake litasukumwa kwa injini za dizeli na Umeme. Gari moshi moja la mizigo litaweza kuvuta mizigo ambayo ingebebwa na malori makubwa mia tano, hata ndio Mapinduzi ambayo watanzania wametamani kuyaona, sasa yanatekelezwa ipasavyo na Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukizungumzia ujenzi wa demokrasia, kama yupo mtu mmoja ambaye amesema muda wote kauli ya “maendeleo hayana chama” ni Ndg. John Pombe Joseph Magufuli. Pale ambapo wewe ni mwakilishi wa wananchi tenda kazi yako ipasavyo, wahudumie watanzania pasina kuwabagua, na zaidi ya yote kipindi hiki ni cha siasa za maendeleo, siasa za masuala, siasa za kushughulika na shida za watu, huu si wakati wa kufanyiana vurumai za kisiasa kama ilivyozoeleka hapo awali.

Licha ya yote haya, bado utaona viongozi wa upinzani ambao walipaswa kutembea kifua mbele kwamba mambo mengi ambayo wananchi waliyasemea sasa yanatekelezwa kwa vitendo na kwa ushahidi, Mfano, leo hii Serikali iko Dodoma ndani ya miaka miwili baada ya tamko Rais Magufuli la kuhamia huko, na mwaka wa tatu 2018 Ndg. Magufuli, Rais wa Nchi yetu, mambo yote yakikaa sawa atahamia Dodoma mapema zaidi kuliko ilivyopangwa awali.

Viongozi wa upinzani ndio wamekuwa mstari wa mbele kutaka kumpunguza mwendokasi Ndg. Magufuli, Rais wetu. Kipindi kile ilifika pahala wakamuita Rais wa Kipindi kile ni dhaifu, leo Ndg. Magufuli mzee wa chuma cha pua, hachengeshi wala “harembi” inapokuja katika kufanya maamuzi.

Mwalimu Nyerere alipata kunukuliwa kuhusu kiongozi ambaye tunamuhitaji, na akasema “awe mtu anayechukizwa na rushwa, na ukimtizama wewe mwenyewe unayemtizama ujiambie kweli huyu anachukizwa na rushwa”. Huyu ndio Magufuli, mtu ambaye akisema sipendi rushwa, sipendi uzembe, sipendi Tanzania ipoteze haki yake katika madini anamaanisha na anatenda na ukimtizama unamwona anamaanisha.

Leo hii badala viongozi wa upinzani kuunga mkono pasina utofauti wa kiitikadi jitihada ambazo wala sio za kiitikadi bali masuala ya kitaifa yenye kubeba mustakabali wa Taifa letu, wao wamekuwa mstari wa mbele kutupinga, kutubeza na kutuvunja moyo.

Siku hizi ni kawaida mtu anayetuhumiwa kwa ufisadi au uhujumu uchumi akikamatwa ili taratibu za mashitaka na za kimahakama zifuate ni jambo la kawaida kuwaona viongozi wa upinzani wakizungumza kuwatetea au kuwaonea huruma watuhumiwa hao.

Si mara moja kiongozi wa Chama cha upinzani nchini amenukuliwa akisema Rais Magufuli amekuwa mkali sana kwahiyo anapendekeza aweke “maneno malaini na matamu”.

Hivi Majambazi na wezi wa Taifa letu wanahitaji lugha ya ukali na kumaanisha au maneno matamu na malaini? Hapo ndipo ulipofika upinzani wa Tanzania.

Kuhusu baadhi ya viongozi wa kiimani kukosoa na kutoa tuhuma pasina kuzingatia haki na wakati uo huo tuhuma na ukosoaji wao wa hadhara ukipigiwa chapuo na viongozi wa upinzani. Mimi naunga mkono viongozi wa kiimani kuikosoa Serikali, lakini nasisitiza, waikosoe kwa haki, kwa staha ya Mamlaka iliyotoka kwa Mungu na zaidi ya yote wakumbuke kuna namna ya kumkosoa Kiongozi Mkuu wa Nchi na kama la kukosoa lipo. Mimi ni mtu mdogo sana ni kondoo tu kiimani, nawakumbusha kwa unyenyekevu habari hii, hata Bwana Yesu alikubali kuzungumza kwa faragha na Nikodemu.

Itakuwa si vema na haki viongozi wetu Maaskofu tukianza kubishana nao hadharani, tu kwa kosa la wao kutokutambua utaratibu, kama kuna ujumbe wa Kiaskofu au kuna ujumbe kutoka kwa Mungu, milango iko wazi kwake mwenyewe (Rais) au kupitia sisi wasaidizi wa Mkuu wa Nchi (iwe kiserikali au kichama) tutafikisha maana sisi huketi mara mojamoja mezani pamoja naye twamjua yu mtu msikivu, mpole, mpenda mashauriano, ni mtu wa maridhiano, ni mtu mpenda haki kweli kweli, ni mtu wa sheria lakini ni mtu wa rohoni hakika. Kwa heshima kubwa nawaacha na changamoto hii.


Mwandishi ni Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)