Saturday, May 30, 2015

NIMUONAVYO RAIS WA AWAMU YA TANO: NATEGA KITENDAWILI



Wiki hii joto katika Chama cha Mapinduzi litazidi kuongezeka kadri makada zaidi wanavyopambanua nia zao za kuomba ridhaa ya chama ili washike bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo Oktoba 25 mwaka huu.

Joto hili halitakuwa mahali pamoja, bali kila kona ya Taifa letu, hasa hasa upande wa Tanzania Bara, kule Kaskazini Mashariki, Arusha, Kaskazini kanda ya ziwa, Mwanza, Nyanda za juu kusini, Mbeya na kule kusini mwa Nchi Lindi. Kwa CCM hizi ni ishara njema kwamba kuna watu na kupitia michakato ya kidemokrasia ndani ya chama watu wanajipambanua, lakini chama kisipokuwa makini hii inaweza kuwa dalili isiyokuwa njema, dalili ya mvurugano, dalili ya mpasuko na kugawanyika kwa chama.

Katika Makala hii nataka nieleze kwa sehemu, na kwa mtizamo wangu nimuonavyo Rais wa awamu ya tano ukizingatia nafasi ambayo Marais wa awamu nne zilizotangulia michango yao imekuwa kwa Taifa letu. Ni muhimu kwa wagombea kujitathmini nafasi zao, dhamira zao na mipango yao ili kukidhi mahitaji ya watanzania sasa lakini pia watanzania wanatakiwa pia watambue kila awamu kwa bahati imekuwa na utume wake. Watanzania pia na hasa katika hatua hii wanachama wa CCM wanatakiwa watambue utume unaotakiwa katika awamu ya tano ili waweze kuwapima wagombea kama wana sifa, uwezo, mamlaka, uhalali na dhamira ya kutupatia uongozi wa kutimiza utume wa awamu ya tano.

Ili tuweze kumuona Rais wa awamu ya tano, tuna budi kuelewa utume wa awamu nne zinazotangulia kwa ufupi,-

Awamu ya Kwanza- JK Nyerere

Mwalimu katika nchi yetu ndiye alikuwa na dhamana ya kukata pori na kuianzisha nchi pamoja na sambamba na mashujaa wengine wengi raia wa Taifa letu. Mwalimu alikuwa na kazi ya kwanza kuleta Uhuru wa Tanganyika na baadaye, yeye na Sheikh Abeid Aman Karume kuunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ili kuunda Nchi Mpya Mwaka 1964 ambayo sasa inajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwalimu alikuwa na kazi ya kulijenga Taifa awali, kuwaleta watu pamoja, huku akiheshimu makabila ya watu na mtawanyiko wa makabila katika Tanzania mpya lakini akiupinga na kuutokomeza kwa kiasi kikubwa ukabila.

Kisha akawa na kazi ya kuliunganisha Taifa kuwa kitu kimoja, akatusaidia kukuza utanzania na akasimamia lugha ya Kiswahili kama lugha ya Taifa. Akahakikisha kuna amani na Umoja na ili hayo yaendelee akajenga misingi imara na thabiti ya haki na usawa miongoni mwa watu wetu.

Akajua amani na Umoja utakuja kama haki itatendeka, kutakuwepo usawa wa watu na wa kimaeneo hivyo akaanza kwa sehemu kufanya majaribio ya kujenga na kuimarisha uchumi. Akatizama uzalishaji katika ngazi zote, katika ngazi ya Taifa akawezesha dola kushika hatamu katika uchumi kwa maana ya uzalishaji, kutoa huduma na kukusanya kodi. Katika ngazi za msingi akaanzisha vijiji vya ujamaa, watu wafanye kazi kwa pamoja, wazalishe pamoja na wanufaike pamoja na matokeo mazuri ya kufanya kazi kwa mshikamano. Akailinda nchi dhidi ya maadui wa ndani na wa nje. Alitenda kwa sehemu yake mpaka alipomwachia kijiti Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Awamu ya Pili- Alhaji Ali Hassan Mwinyi

Mhe. Mwinyi alichukua kijiti wakati nchi ilikuwa bado imara kwa maana ya Umoja, mshikamano, Amani na utulivu, lakini kiuchumi nchi ilikuwa imetetereka sana. Uchumi ulioshikiliwa na dola ulikuwa umelemewa na mahitaji wananchi na utendaji wake haukuwa wenye ufanisi mkubwa. Tulikuwa na udhaifu wa ndani kwa maana ya kutokuwajibika miongoni wa watendaji na Wananchi lakini pia tulikuwa na shinikizo kubwa kutoka nje hasa mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa.

Mzee Mwinyi alikuwa na kazi ya kufungua milango ili kila anayeweza kuzalisha basi asaidie kazi ya serikali ya uzalishaji ili chakula na bidhaa ziwafikie watu wa Taifa letu. Kidogo kidogo akaanza kuufanyia marekebisho mfumo wa uchumi wetu kutoka uchumi inaoshikiliwa na dola kwenda kwenye uchumi huria ambao watu na wadau mbalimbali ni washiriki katika kufanya shughuli za uzalishaji na kutoa huduma. Lakini pia akawa mkali kwa wale ambao hawakuwa wawajibikaji, utakumbuka kipindi kile nyimbo maarufu zilikuwa kama vile “usipowajibika ole wako, utakumbwa na fagio la chuma”. Aidha akawapa hamasa Wananchi kwamba kwa hali tuliokuwa nayo kipindi kile ilikuwa budi sote tushikamane, utakumbuka misemo kama “Wananchi sote tujifunge mikanda”.

Ni kipindi hiki Taifa lilianza kuona huduma za kijamii sasa zikianza kutolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali, huduma za ughani katika kilimo, mifugo na uzalishaji mdogomdogo. Ni katika kipindi hiki asasi mbalimbali zilianzishwa na kusajiliwa ili ziisaidie serikali katika kujenga Taifa.

Ikawa ni dhahiri kwamba awamu ya pili ilikuwa ya kujenga mfumo mpya wa uchumi kwa Taifa letu na ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa unaendana na mahitaji ya wakati na dunia. Mzee Mwinyi akaweka misingi ya uchumi huria, tuliyumba yumba kidogo lakini ilikuwa mwanzo. Kubwa zaidi Mzee Mwinyi akaimarisha pia misingi ya demokrasia, katika awamu ya pia tukaondoa mfumo wa demokrasia ya chama kimoja na kwenda katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Mfumo huu uliongeza uwajibikaji, ushiriki wa mpana wa Wananchi katika uongozi wa nchi na uwazi katika shughuli za serikali.

Mzee Mwinyi alitenda kwa sehemu yake mpaka Mhe. Benjamin W. Mkapa alipopokea kijiti.

Awamu ya Tatu- Mhe. Benjamin W. Mkapa

Mhe. Mkapa, alikuwa na kazi moja kubwa, kuimarisha hatua zilizopigwa na awamu ya pili hasa katika kuendelea kuupanga na kuuimarisha uchumi wetu katika mfumo mpya tuliouchukua. Serikali ya Awamu ya tatu chini ya uongozi wa Mzee Mkapa ilijikita katika kuhakikisha kuna “transition” nzuri kutoka uchumi uloshikwa na dola awali kwenda uchumi huria ambao umeshikwa na watu katika sekta binafsi. Kipindi chake kilikuwa na kazi kubwa ya marekebisho ya kimfumo na kitaasisi, wengi wenu mtakumbuka Tume maarufu ya “Parastatal Sector Reform Commission (PSRC)” ambayo ilianzishwa kwa sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992 na kazi kubwa ilikuwa kufanya ubinafsishwaji wa mashirika ya umma.

Mzee Mkapa katika ujenzi wa uchumi huria imara alisimamia uwazi na ukweli hasa kipindi chake cha kwanza, alipiga vita na alichukizwa na rushwa. Hata katika kampeni zake za Urais alitoa ahadi ya kupambana na rushwa, baada ya ushindi mwaka 1996 aliunda Tume ya Kupambana na Rushwa iliyojulikana kama “Tume ya Warioba”. Kwa hakika kulikuwa na matatizo ya hapa na pale tena mengi tu, lakini sote tunakubaliana kwamba Mzee Mkapa alituimarishia uchumi wetu katika mfumo wa soko huria. Uchumi Mkubwa ulikuwa unakuwa mpaka anaondoka kwa asilimia karibu saba. Kazi aliyokuwa ameiacha haijatimia ilikuwa ni kuutafsiri ukuaji wa uchumi mkubwa ambao ulionesha mafanikio makubwa katika maisha ya watu wa Kawaida. Kazi hiyo ilikuwa sasa ni ya Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete Rais wa Awamu ya Nne ambaye alipokea kijiti.

Awamu ya Nne- Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete

Awamu ya nne kama ambavyo ilivyojinasib wakati wa kampeni zake wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kwamba “Maisha bora kwa kila Mtanzania”. Ukiitafsiri kauli mbiu hii utakubaliana nami, uongozi wa awamu ya nne ulikuwa na kazi ya kutafsiri uchumi Mkubwa (Macro) kutokana na tija itokanayo na viwanda na uwekezaji mkubwa kwenda uchumi wa kati (Meso) katika jamii zetu na kisekta kama vile kilimo (Kilimo Kwanza), elimu (shule za Kata) na hata tushuke kiuchumi hadi ngazi ya mtu wa kawaida (micro) hapa ndio tungeona uhalisia wa maisha bora, watu wenye nyumba nzuri, ajira zenye staha, kipato chenye kukidhi mahitaji na watu wanaokopesheka.

Awamu ya nne imekuwa na jukumu la kuendelea kujitahidi kugawa keki ya Taifa katika mazingira na uhalisia tofauti tofauti, kama vile ujenzi zaidi wa barabara, uwekezaji zaidi katika elimu na kilimo. Nchi inapofika katika kiwango cha kuanza kugawa keki ya Taifa huwa inafanya hivyo baada ya kunufaika na ukuaji mkubwa wa kiuchumi na huwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha kwamba ugawaji wa keki unaenda sambamba na jitihada za kuendelea kukuza na kuuimarisha uchumi mkubwa.

Awamu ya nne imeendelea pia kushughulikia pia ujenzi wa demokrasia na kuimarisha mifumo ya udhibiti na kuweka ukomo wa matumizi ya madaraka kwa watumishi na viongozi wa umma, hili mpaka sasa halijakamilika. Mifano ni maboresho mbalimbali ya kitaasisi katika serikali, kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya ambayo ungehakikisha ugawanaji wa keki unawanufaisha wengi na sio makundi ya wajanja wachache, hili halijakamilika.

Utagundua pia katika awamu zote nne, kimsingi tuna kila kitu ambacho kama nchi inahitaji ili kupiga hatua. Kwa mtizamo wangu kilichobaki ni kufanya sasa marekebisho ya mifumo na taasisi na fikra za watu (Wananchi, watumishi na viongozi wetu) na kuhakikisha wote waliopewa dhamana wanatenda hivyo kwa uadilifu na wakijua wakipotoka watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na kamwe hawatakaa juu ya sheria.

Awamu ya Tano- Nimuonavyo Rais huyu (…)

Namuona Rais wa awamu ya akisheheni haiba ya uadilifu, mtu asiyejikweza, mwenye kukubalika na watu, mwenye “moral authority” yaani mtu mwenye uwezo na mamlaka ya kukemea wezi, watu wasio na uadilifu. Mtu ambaye anatambua kwamba mafanikio yote tuliyoyapata katika awamu zote nne hayawezi kutimia pasina kuwa na mifumo ya udhibiti “systems and controls” inayofanya kazi katika taasisi zetu kutoka ngazi ya kitaifa mpaka mtu mmoja mmoja.

Kuna kipindi katika historia za dini kuna kitu kiliitwa “reformation” au matengenezo, tumefika pahala ambapo tunahitaji Kiongozi ambaye atakuja kufanya matengenezo, marekebisho na maboresho kuanzia ikulu hadi katika jamii zetu. Baada ya kipindi cha reformation kupita sasa nitawaona wajenzi wa barabara, wajenzi wa shule, waboresha kilimo na huduma za afya. Kwa sasa tunataka mtu wa kuja kutunyooshea njia, kuturudishia maadili ya Taifa, Maadili ya utumishi na Uongozi wa Umma, kutujengea mifumo na taasisi imara na madhubuti ambazo zitahakikisha kuna uadilifu na uwajibikaji katika sekta ya umma na sekta binafsi.

Rais ajaye nimuonavyo ni yule ambaye anajua watanzania wameshaibiwa sana, vijana wanasema tumeshapigwa sana. Kilimo hakikui kwasababu kuna watu wananufaika na kuagiza mchele kutoka nje. Kilimo cha sukari hakikui kwasababu kuna watu wana mirija ya chuma katika kuagiza sukari kutoka nje. Reli ya Kati inadororora kila siku kwasababu watu wana maslahi na biashara ya maroli. Tunataka Rais ajaye aje na aanzie hapo kutuwekea mifumo ya kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka.

Tunataka Rais ajaye Kiongozi akila rushwa hatasubiri akemewe atajiondoa mwenyewe haraka. Tunataka baba, Kiongozi, mtu ambaye tukimtizama tutakuwa na amani na maisha yetu, tunamtaka mtu ambaye sasa anaonesha kupenda heshima ya Wananchi. Tunamtaka mtu ambaye atarudisha heshima ya cheo cha msingi ambacho ni “Raia”. Tunamtaka mtu asiyejipeleka kwa “wazi” au kwa “kificho”, kwa “kelele” au “kimya kimya”.

Mwisho tunamtaka na nimwonavyo Rais wa Awamu ya Tano, ni mtu mwenye uhalali, mtu anayekubalika katika pande zote za Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mtu ambaye kwasasa Wananchi wanajinasibisha naye, kwasababu anawajua, na wanajua anajua mahitaji yao. Mtu ambaye amesimama nao bega kwa bega na ambaye hajaona aibu kusimamia maslahi yao wakati wowote.

Naomba mnitegulie kitendawili.


3 comments:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. Kwa nionavyo mimi, rais afaaye ni mwigulu nchemba. Ana kila sifa ya kuwa rais wa awamu ya 5.

    ReplyDelete
  3. Maelezo mazuri sana.. Natumaini vijana wengi watakuelewa..

    ReplyDelete